5 Jul 2012


MOJA ya matokeo yasiyopendeza ya ujio wa mageuzi ya kisiasa katika miaka ya tisini ni ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa hayajamsaidia mwananchi wa kawaida mtaani.
Mageuzi hayo - hasa katika nyanja ya siasa na uchumi, yameendelea kuonekana kama ni kwa ajili ya kikundi kidogo katika jamii huku yakitanua pengo kati ya walio nacho na wasio nacho.
Kwenye siasa, ujio wa vyama vingi haujafanikiwa kwa kiwango cha kutosha kuweka mbele maslahi ya wananchi na badala yake umekuwa kama fursa kwa baadhi ya wanasiasa kujinufaisha.
Utitiri wa vyama vya Upinzani umekuwa turufu muhimu kwa chama tawala kutoyumbishwa au kuwajibishwa vya kutosha; hasa kwa vile Upinzani usio na umoja ni rahisi kudhibitiwa na hata kuhujumiwa na chama kimoja imara na chenye uzoefu wa harakati za siasa. Hapa ninaizungumzia CCM.
Tumeshuhudia baadhi ya vyama vikiibuka nyakati za chaguzi tu, na badala ya kutoa upinzani kwa CCM, vyama hivyo vimekuwa vikigawa kura za wapinzani na hivyo kukinufaisha chama tawala.
Kuna hisia kwamba CCM, kwa kutambua kuwa ushirikiano na/au umoja wa wapinzani ni tishio kwa ustawi na uhai wake, imekuwa ikivisaidia vyama hivyo dhaifu katika nyakati za chaguzi kwa minajili ya kugawa kura za wapinzani.
Pengine hoja hiyo inapewa nguvu na namna baadhi ya vyama hivyo vinavyoendesha kampeni zake ambapo badala ya kuelekeza mashambulizi kwa chama tawala, huwageukia wapinzani wenzao.
Lakini hata kama tuhuma hizo dhidi ya CCM hazina ukweli wowote, kilicho wazi ni kwamba vyama vingi vya upinzani nchini havina maslahi yoyote kwa Mtanzania. Baadhi ya vyama vimegeuka kama kampuni za kifamilia ambapo kiongozi ndio chama ilhali hakuna jitihada zozote za ufunguzi wa matawi mapya au kuongeza idadi ya wabunge au/na madiwani.
Yayumkinika kuhitimisha kuwa adui mkubwa wa vyama vya upinzani ni ubinafsi miongoni mwa baadhi ya viongozi wa vyama hivyo; hususan wale ambao wamegeuza vyama hivyo kuwa mali zao binafsi.
Tukiangalia kwa upana zaidi, tatizo la upinzani dhaifu unaotokana na mgawanyiko (badala ya ushirikiano) miongoni mwa wapinzani linachangiwa pia na ukweli kuwa katika mazingira ya Tanzania yetu, hivi sasa siasa imegeuka kuwa ajira.
Kama ambavyo madhehebu mbalimbali yamevamia na walaghai wanaotumia dini kama chanzo cha mapato yao binafsi, siasa nayo imevamiwa na kundi la wahuni ambao wamebaini kuwa sio tu fani hiyo ni chanzo kizuri cha mapato lakini pia inatoa kinga dhidi ya uhalifu wowote wanaojihusisha nao.
Na ndio maana kila kunapofanyika uchaguzi tunashuhudia baadhi ya wanaowania nafasi za uongozi wakimwaga mamilioni ya fedha ili wachaguliwe. Na kwa kutambua udhaifu wa vyombo vya dola katika kuwabana watoa rushwa kwenye chaguzi, baadhi ya matapeli hao wa kisiasa hufanikiwa kushinda chaguzi hasa kutokana na ukweli kuwa wapiga kura wengi “wana njaa” na wapo radhi kunadi kura zao kwa pishi za mchele na doti za kanga.
Tukiangalia kwenye mageuzi ya kiuchumi, manufaa kwa Mtanzania wa kawaida mtaani yameendelea kuwa haba. Kana kwamba itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea ilikuwa ikiwafunga mkono baadhi ya viongozi kutekeleza imani yao ya ubepari kwa vitendo, mara baada ya kile kinachofahamika kama Azimio la Zanzibar, nchi yetu imeshuhudia matendo kadhaa maovu pengine zaidi ya mkoloni tuliyemtimua mwaka 1961.
Siku zote huwa natoa ‘excuse’ kwa wakoloni kwamba; angalau wao walikuwa na sababu ya kutoihurumia Tanzania yetu kwani hawakuwa Watanzania, na hata nchi hiyo ingetumbukia mtaroni wao wasingeathirika kwani wana makwao. Sasa sijui tuwaelewe vipi Watanzania wenzetu ambao matendo yao ya kuibaka nchi yetu kiuchumi yanazidi kuipeleka nchi yetu mahali pasipostahili.
Hawa hawana ‘excuse’ hasa kwa sababu wengi wao walizaliwa na kukulia Tanzania, na hata nyadhifa walizonazo zimechangiwa na mzigo uliobebwa na Watanzania wenzao kwa njia ya kodi.
Kibaya zaidi, kiasili takriban kila Mtanzania anahusiana na Mtanzania mwingine (kwa wenye uelewa wa historia wanafahamu asili za makabila yetu hususan ya Kibantu). Mtu anayeruhusu madawa ya kulevya yaingie nchini alimradi akaunti yake inazidi kufurika “vijisenti” anapaswa kufahamu baadhi ya watumiaji wa madawa hayo ni watu wanaohusiana nae kikabila kama si kiukoo.
Lakini hata kama hawahusiani, nguvu kazi inayoathiriwa kutokana na matumizi ya madawa hayo inaweza kumwathiri hata mpokea rushwa huyo; kwani sote tunajua kuwa nchi haiwezi kujengwa na 'jeshi la mateja' (watumia madawa ya kulevya).
Kijamii, japo mageuzi hayakuwa ya moja kwa moja, lakini madhara yaliyojitokeza yanaweza kuonekana zaidi katika nyanja za utamaduni, sambamba na kwenye mila na desturi zetu.
Eneo moja ninaloweza kulitumia kama mfano ni katika matumizi ya lugha yetu ya taifa Kiswahili. Binafsi, katika takriban muongo mmoja nilioishi hapa Uingereza sijawahi kuwaona au kuwasikia Waingereza wakiendesha majadiliano/mazungumzo yao kwa lugha ya kigeni.
Na hiyo si kwa Waingereza pekee. Nchi nyingi duniani zimekuwa zikienzi sana lugha zao kwani ni utambulisho muhimu wa utaifa wao.
Sasa akina sie ambao licha ya kuwa na lugha ya taifa Kiswahili tuna lundo la lugha zetu za asili, tunaendelea kuichukulia lugha ya Kiingereza kama kioo cha elimu au ubora wa mtu.
Juzijuzi, nilitoa changamoto kwa Watanzania wenzangu wanaotumia mtandao wa kijamii wa twitter kwamba ni muhimu kwetu kuenzi lugha yetu ya taifa badala ya kuendeleza mijadala yetu kwa Kiingereza.
Japo ninakiri kuwa nyakati fulani nami nimekuwa nikitumia Kiingereza huko twitter(angalau kwa kisingizio kuwa baadhi ya watu wangu wa karibu hapa hawaelewi Kiswahili), kwa kiwango kikubwa nimekuwa nikijitahidi kuenzi lugha yangu ya taifa Kiswahili.
Na kwa sie tulio mbali na nyumbani, kuna wakati tunatamani tuwe kama wenzetu Wachina au Wahindi (kwa mfano) ambao kila wanapokutana wanawasiliana kwa kutumia lugha zao.
Unaingia mtandaoni ukiwa na hamu ya kuwasiliana na wenzio kwa Kiswahili, lakini wao wanakazania lugha nyingine (huku wengine wakikaza misuli ili waimudu lugha hiyo ya kigeni).
Lakini tatizo si kwenye lugha pekee; bali hata kwenye mila na tamaduni zetu. Ukiangalia baadhi ya zinazoitwa kazi za sanaa unaweza kuhisi kuwa ‘mwisho wa dunia’ unakaribia.
Nilishawahi kuandika katika makala moja huko nyuma kuhusu baadhi ya vikundi vya burudani ambavyo sio tu vinatumia majina yenye maana mbaya (kwa mfano ‘Kitu Tigo’), lakini hiyo burudani yenyewe ni laana tupu.
Na kana kwamba ibilisi anazidi kupata wafuasi, burudani za aina hiyo zimetokea kupata umaarufu mkubwa.
Ukiangalia kwenye eneo ambao pengine lingeweza kuwa mkombozi wetu kisanaa, yaani filamu za Kitanzania, hutolaumiwa ukihitimisha kuwa baadhi ya wanaoingia kwenye fani hiyo wapo ‘kibiashara binafsi’ zaidi kuliko kisanii.
Hivi kuna ugumu gani kuwaiga Waafrika wenzetu wa Nigeria ambao sekta yao ya filamu ya Nollywood inatamba ndani na nje ya Afrika; hususan kwa sababu filamu zao zimeelemea zaidi katika uhalisia wa maisha ya Mwafrika, na wengi wa wasanii wanavuma kwa vipaji vyao na si kutengeneza vichwa vya habari visivyopendeza magazetini.
Lakini kwa wengi wa ‘mastaa’ wetu wa filamu, umaarufu wao unaenda sambamba na taarifa za kufumaniwa, kuvaa nguo nusu-utupu na uhayawani mwingine!
January Makamba
Katika kuelekea kuhitimisha makala hii, ningependa kutoa pongezi za kipekee kwa mwanasiasa kijana, January Makamba, ambaye kwa namna fulani anafanya jitihada binafsi za kuleta matokeo chanya ya mageuzi niliyoongelea katika makala hii.

Mwanasiasa huyu wa CCM ni mmoja ya wachache wanaotumia vyema mitandao ya kijamii kuushirikisha umma.
Wiki hii ameandika makala moja nzuri sana kuhusu u-liberali mamboleo ambapo kimsingi anachoongelea kinashabihiana kwa karibu na dhima ya makala hii.
Katika makala hiyo yenye kichwa cha habari ‘Kubadili Dhana’ (Changing the Paradigm), January anachambua jinsi zaidi ya miaka 30 ya dhana hiyo ya u-liberali mamboleo ilivyoshindwa kuzaa matunda ya maana kwa nchi zinazoendelea na hata zile zilizoendelea.
Anaeleza kuwa kushindwa kwa dhana hiyo kunajidhihirisha katika kuyumba kwa uchumi wa soko, kuendelea kutumia jembe la mkono, utajiri kuendelea kuwa mikononi mwa wachache, uhaba wa kidemokrasia, machafuko, kushindwa kukabiliana na maradhi, nk.
Licha ya kuvutiwa na jitihada zake binafsi za kuushirikisha umma; hususan kupitia mitandao ya kijamii, mwanasiasa huyu analeta picha adimu ya mafanikio ya mageuzi ambapo anachepuka nje ya dhana iliyozoeleka ya u-mungu mtu wa viongozi wetu (yaani kiongozi anaonekana jukwaani tu akihutubia huku akitoa maagizo pasipo kusikia mawazo ya wananchi wa kawaida) na ‘kujichanganya’ na wananchi pasipo kujali kaliba zao.
Ukidhani sifa hizo si stahili kwake, jaribu kujiuliza ‘ukiweka kando ‘undugu’ wakati wa kampeni za kuomba kura’ ni lini ulipata fursa ya kuongea na japo diwani wako-achilia mbali Naibu Waziri kama January-kumfahamisha matatizo mbalimbali yanayoikabili eneo analoongoza?
Viongozi wengi hulea dhana potofu kwamba kuwa karibu na wananchi wa kawaida kunawashushia hadhi. Ni katika mazingira ya aina hii ndio maana matendo na kauli za wengi wa viongozi wetu ni kama wanaishi sayari nyingine - hawajui hali halisi mtaani ikoje.
Wengine wanajijengea ukuta wa mawasiliano kati yao na wanaowaongoza ili kukwepa maswali kuhusu ahadi zao hewa walizotoa wakati wanaomba kura.
Nihitimishe kwa kutoa wito kuwa mageuzi ya kweli yanaweza kuletwa na wananchi wenyewe; kwani wao ndio wanaojua nini wanahitaji kwa ajili yao na jamii/nchi yao.



0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.