9 Jul 2012
Naomba nivamie eneo ambalo ninaweza kujiita 'mgeni' (foreign territoty).Hili ni uchambuzi wa muziki,au kwa usahihi zaidi,uchambuzi wa video za muziki.

Nikurejeshe nyuma kidogo.Zamani hizooo,niliwahi 'kuota' kuwa mshiriki wa muziki.Well,sio kuwa mwanamuziki per se bali kujishughulisha na utengenezaji muziki.Nilipokuwa sekondari nilimudu kutunga nyimbo kadhaa kwa kwaya ya shule.Niliweza kutunga aya na sauti lakini tatizo lilikuwa kwenye namna ya uchezaji.Hadi leo,mie na kucheza ni kama kibaka na polisi.Kwa kifupi sijui ku-dance.

Ndoto za kuwa mtengeneza muziki (prodyuza) zilichangiwa zaidi na jinsi ninavyothamini 'michango isiyoonekana.' Hapa ninamaanisha kazi za watu kama watengeneza filamu, watengeneza muziki au hata mashushushu.Hawa ni watu wanaowezesha mengi na pengine laiti wangekuwa wanaonekana na 'products' zilizokwishakamilika basi sifa nyingi zingewaendea wao kuliko ilivyo sasa.

Tunapoona filamu nzuri,sifa nyingi huenda kwa actor au actress.Lakini kimsingi kazi kubwa inayoweza kupelekea filamu ikapata umaarufu hufanywa na mtengenezaji filamu.Kwenye filamu,uzuri wa filamu husika ni mkusanyiko wa jitihada za mwongozaji filamu (yaani director) na mtengenezaji filamu (yaani producer).

Nimeutaja ushushushu.Jamaa hawa ndio kila kitu.Ukiona nchi inakwenda vyema ujue wanafanya kazi yao kwa ufanisi.Ukiona mambo yanayumba basi ujue ndugu zetu hawa wana mushkeli mahala flani.Lakini kimsingi ni kuwa hawaonekani.Kama ilivyo kwa director au prodcuer wa filamu,sifa za kazi husika hulekezwa kwa wengine (kwenye filamu ni actors/actresses) na kwenye mwenendo wa nchi sifa huelekezwa kwa askari au taasisi nyingine za serikali.

Tofauti na filamu na ushushushu ambapo ni mara nyingi ni mkusanyiko wa wengi,kwenye muziki mara nyingi ni jithada za mtu mmoja au wawili. Mara nyingi producer wa muziki ndiye anayebuni ladha ya wimbo kwa maana ya kuunda beatsjapo jukumu la mwisho la ku-flow linabaki kwa msanii husika.Pia inawezekana wimbo ukawa umetungwa na mtu mwingine kisha kumpatia msanii au producer.La msingi hapa ni kuwa producer au mtunzi wa wimbo (kama si msanii mwenyewe) ni watu ambao hawapati sifa za kutosha ukilinganisha na msanii husika.

Kwahiyo moja ya ndoto zangu udogoni ilikuwa kuwa music producer...lakini kama tujuavyo katika maisha sio kila tutakacho ndio tupatacho.Ndoto hiyo 'ilikufa kifo cha asili' baada ya kuelekeza nguvu zangu kwenye  maeneo mengine ya maisha.Lakini hadi leo nina mapenzi ya dhati na muziki hususan wa kufokafoka.

Lengo la makala hii ni kuchambua kazi mbili za wasanii mahiri wa Bongoflava,Fid-Q na Solo Thang,ambao hivi karibuni wametambulisha video zao mpya.

Naomba nisisitize kuwa licha ya mapenzi yangu kwa muziki,mie si mtaalam (expert) wa eneo hilo.Uchambuzi wangu huu ni wa ki-layman (i.e. wa mtu asiye na upeo wa kutosha katika mada husika).

Jingine la kupigia mstari ni desturi iliyojengeka miongoni mwetu kuwa pindi ukionyesha mapungufu ya kitu flani basi wewe ni HATER.Binafsi,nimefika nilipofika kwa sababu siku zote nimekuwa nikipokea na kufanyia kazi maoni mbalimbali hata yale yanayokinzana na imani au mtazamo wangu.Kupewa sifa kuna tatizo moja: hakuwezi kukusaidia kutambua wapi umekwenda kombo.Ofkoz, kazi nzuri lazima isifiwe lakini pengine ili kumsaidia aliyefanya kazi hiyo ni vema kumfahamisha wapi arekebishe au penye mapungufu.Na hiki ndio nitakachofanya katika makala hii.

Video za muziki ninazozichambia ni ile ya SIHITAJI MARAFIKI ya FID-Q na MISS TANZANIA ya SOLO THANG.Kwa kifupi,video zote ni za ubora wa hali ya juu.Wasanii wote wawili wamechagua location za kuvutia wakati wanarekodi video zao.Kadhalika,ubora wa picha ni wa kiwango cha juu.


Wasanii hawa wana sifa moja inayolingana: ni mahiri mno katika uwasilishaji wa ujumbe uliomo kwenye wimbo husika.Wote wana uwezo wa hali ya juu wa kucheza na maneno, neno pekee la Kiingereza unaloweza kulitumia kuwaelezea ni LYRICAL ASSASSINS (Usitishwe na hiyo 'assassins' kwani ni neno tu linalotumiwa kutanabaisha namna msanii anavyoweza 'kucheza na maneno' kwenye tungo husika).

Wakati Solo Thang anamzungumzia Miss Tanzania,Fid-Q anazungumzia marafiki.Ujumbe katika tungo zote mbili haupo wazi sana na inambidi msikilizaji 'asome kati ya mistari' (reading between the lines) kuelewa kinachoongelewa.Usipokuwa makini unaweza kudhani Solo 'anawapaka' warembo lakini kimsingi MISS TANZANIA imebeba ujumbe mzito hususan kwa mabinti warembo wenye kuendekeza tabia zisizopendeza machoni kwa jamii.

Ujumbe wa Solo unapigia mstari mtizamo wa wengi kuhusu urembo kama fani (iwe u-Miss au uanamitindo).Yayumkinika kusema kuwa machoni wa wengi fani hizo mbili hutizamwa 'kwa jicho baya' hasa kutokana na tabia kama za huyo 'Miss Tanzania anayezungumziw na Solo.' Huu ni ukweli i.e. ni mtazamo wa wengi japo si kila Miss au mwanamitindo ana tabia zisizopendeza katika jamii.Inawezekana Solo anamzungumzia Miss Tanzania flani?Jibu la swali hili analo yeye mwenyewe lakini kwa vile ni mahiri mno wa 'kucheza na maneno' yayumkinika kuamini kuwa kuna ujumbe mpana pengine zaidi ya uelewa wetu.

Kwa upande wake Fid-Q, SITAKI MARAFIKI haimaanishi marafiki si muhimu bali kwa kutumia kipaji chake kikubwa cha kuwasilisha ujumbe kwa namna inayohitaji tafakuri,msanii huyo anaweka wazi mtazamo wake kuhusu mahusiano katika jamii,kwa kutumia mfano mwafaka wa marafiki.Nadhani ushaskia msemo  'MARAFIKI WA NINI KAMA MAADUI WANANISAIDIA.' Mara nyingi,marafiki zetu hupenda kututendea mazuri tu tunayotarajia kutoka kwao na pengine kuepuka kutueleza 'hapa umechemka.' Lakini maadui zetu huwa mahiri wa kuonyesha kasoro zetu (hata kama ni kwa uchache) japo kimsingi matarajio yao huwa ni kuonyesha mabaya yetu.Kwa hiyo pasipo kukusudia,maadui zetu wanaweza kuwa na mchango flani chanya katika maisha yetu kwa sababu hawana unafiki katika kunyooshe akidole mapungufu yetu.

Kwa anayezifahamu vema kazi za Fid-Q na Solo Thang ni wazi hatokuwa na wasiwasi kuhusu namna watakavyouwasilisha ujumbe kwenye tungo mpya.Kama nilivyoeleza hapo juu,wasanii hawa wana uwezo wa hali ya juu wa 'kucheza na lugha na maneno.' Uwezo huo unawasiaidia sana katika kuwasilisha ujumbe katika namna inayomwacha msikilizaji 'ameterazika' (ameridhika)

Sasa nigeukia eneo linaloweza kuniingiza matatizoni: mapungufu katika kazi hizo za wasanii hao.Kimsingi si mapungufu bali ni pungufu kwani ni moja tu,na si kubwa sana.Ukiangalia video zote mbili utabaini jambo hili: katika video ya Fid-Q,tangu mwanzo hadi mwisho wa video yake amevaa vazi lilelile.Kwa Solo,kwa kiwango kikubwa katika video hiyo yupo katika T-shirt ileile japo kuna vipande ambapo anaonekana amevaa shati.

Kama nilivyotanabaisha,hii ni kasoro ndogo inayoweza kabisa kufunikwa na ladha ( flavour) ya muziki, ujumbe uliomo katika wimbo,na kiwango cha video.Hata hivyo,kama inavyotanabaishwa kwenye na Andrew Goodwin kwenye Kanuni ya Video ya Muziki (Music Video Theory) vinavyoonekana katika video ya muziki (visuals) vinaweza kuwa na mchango mkubwa sio tu kuiboresha video husika bali pia kuiunganisha na hadhira.

Pengine ili uelewe ninachoelezea hapa nitolee mfano msanii kama Lady Gaga.Mavazi yake ni burudani tosha-japo sio aina ya mavazi unayoweza kumwambia fundi cherahani akutengenezee.Msanii kama Michael Jackson alifahamika sio tu kwa miziki yake bali pia mavazi yake.Kwa sanii wa hip-hop wa Marekani,mavazi ni moja ya vitu muhimu mno,na baadhi ya mapendezeo yao katika mavazi yamepelekea mwamko wa fasheni,kwa mfano mashati ya 'DOGI DOGI' yaliyokuwa yanapendelewa na wasanii wa rap/hiphop wa pwani ya magharibi ya Marekani (West Coast rappers) kwa mfano Snoop Dogg na Ice CubeNadhani sababu pekee iliyowafanya Fid-Q na Solo wasionekane katika mavazi tofaut tofauti katika video zao ni MUDA.Hapa ninabashiri kuwa hawakuwa na muda wa kutosha kurekodi video zao kwa muda mrefu ambao ungewapa nafasi za kubadili mavazi mara kadhaa.Naomba nisistize kuwa kasoro hiyo ndogo haijapoteza hata chembe ladha ya kazi zao bora kabisa.Nimeipigia mstari kasoro hii kwa minajili ya kuwasaidia wasanii hao huko mbeleni wajaribu kutumia muda zaidi katika kurekodi video zao.Kanuni nyepesi ya kurekodi kitu chochote kile ni hii: kadri unavyojipa muda wa kutosha ndivyo unavyomudu kurekodi vitu vingi zaidi ambavyo wakati wa kuhariri utaondoa vile usivyovitaka na kuacha vile unavyovitaka.

Lakini kasoro hiyo ndogo inarekebishika.Ninaamini tulichoshuhudia katika video ya SIHITAJI MARAFIKI na MISSI TANZANIA ni matoleo ya mwanzo tu (iwapo Fid na Solo wana mtizamo kama wangu).Si ajabu kwa msanii kutoa video ya mwanzo kisha kutoa video nyingine rasmi kwa ajili ya wimbo husika.Mfano mzuri ni huu wa kundi la TOK katika wimbo wao Footprints Hii ni version ya awali

Hii ni version rasmi

Pengine kitawachowarahisishia Solo na Fid-Q kutengeneza video 'r(kama wataona kuna haja ya kufanya hivyo) ni ukweli kwamba tayari wana video nzima ya asili,ambapo wakiamua kuongeza chochote inakuwa ni suala la kuongeza tu vipande vipya katika original version.Hili si lazima,as long as wao wameridhika na versions walizoweka hadharani.

Ukiweka kando kasoro hiyo ndogo,Solo Thang ameendelea kuwa mithili ya balozi wetu wa Bongoflava katika anga za kimataifa ambapo anafanyia kazi zake kutoka nchini Ireland.Lakini licha ya kuwa nguli (legend) wa bongoflava na 'wadhifa' huo wa ubalozi wa kimataifa,msanii huyu ni miongoni mwa wachache ambao ni down-to-earth sana na anayejali sana kuishirikisha hadhira,hususan kupitia Twitter na Facebook.Kadhalika,ana blogu yake anayotumia kuwafahamisha wapenzi wa muziki wake kuhusu kazi zake.

Kwa upande wa Fid-Q, mkongwe huyu wa muziki wa kufokafoka huko nyumbani amekuwa mahiri sana katika matumizi ya mitandao ya kijamii kutangaza kazi zake na kuishirikisha hadhira.Huko Twitter ana utaratibu wa kujibu maswali angalau mara moja kwa wiki kwa kutumia hashtag #AskFidQ. Hii inatoa fursa kwa wengi kumuuliza maswali mbalimbali.Kadhalika,anaendesha kitu kinachofahamika kama Hip-Hop Darasa,ambapo pamoja na mambo mengine anatoa elimu kwa kizazi kipya cha Hip-hop huko nyumbani.Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa kipindi chake maarufu mtandaoni cha Fidstyle Friday kitaanza kuonyeshwa kwenye runinga katika kituo cha East Africa Television (EATV).Haya ni maendeleo makubwa.

Basi nimalizie kwa kuwapongeza Fid-Q na Solo Thang kwa kazi zao bora kabisa.Naomba wasitafsiri kasoro ndogo niliyobainisha hapo juu kuwa ni HATING. Sote tunapenda kuona wasanii wetu wakifanikiwa na kuteka anga sio huko nyumbani tu bali Afrika na duniani kwa ujumla.Natambua kuna wataosema "huyu nae,anajifanya anajua kila kitu" lakini lengo langu si kujifanya mjuaji bali kutoa mchango wangu kwa wasanii wetu.

Nimalizie makala hii na video zifuatazo za wasanii hao0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.