Showing posts with label FID-Q. Show all posts
Showing posts with label FID-Q. Show all posts

13 Aug 2016

14026664_162506520845816_426045486_n
Leo ni siku ya kuzaliwa ya mwana-hiphop mahiri na lejendari nchini Tanzania, Fareed Kubanda a.k.a Fid-Q. Na katika kuadhmisha birthday yake, msanii huyu ambaye sio tu amedumu "kwenye fani" kitambo bali pia ni miongoni mwa waasisi wa Swahili Hip-Hop.

 Kwangu, Fid-Q sio tu ni msanii maarufu kabisa huko nyumbani Tanzania na katika Swahii hip-hop duniani, bali ni mmoja wa watu ambao wamkuwa wakinipatia sapoti kubwa katika kazi zangu za uandishi wa vitabu. Na ndio maana kwa kutambua mchango wake huo, alikuwa mtu wa kwanza kupata nakala dhahiri ya kitabu changu kuhusu taaluma ya uafisa usalama wa taifa (ushushushu) kama inavyoonyesha pichani chini.

 Jana niliuliza huko kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuhusu wimbo gani wa Fid-Q unawavutia zaidi mashabiki wake. 



Jibu jepesi lilikuwa "kila wimbo wake unavutia." Nimesikiliza hii track mpya ya 'SUMU.' Imesheheni kauli nyingi za busara. Nitamwomba Fid-Q anitumie mashairi ya wimbo hu ili kuwaletea ninyi wasomaji uchambuzi zaidi ya wimbo huo. Lakini hata bila uchambuzi, kwa kuusikia tu, utaafikiana nami kuwa umeshehenu busara tele.

 Na hiki ndio kinachomfanya Fareed aendelee kuwa mmoja wa wasanii wachache na adimu kabisa Tanzania sio tu kuwa waasisi wa fani bali pia wasiochuja: kuwa na nyimbo zenye ujumbe usiochuja. Kama ingekuwa ni muziki wa bendi basi tungelinganisha na timeless tunes za kina Mbaraka Mwinshehe, Marijan Rajabu, Bitchuka, Shaban Dede, nk ambao tungo zao zilituvutia tangu tukiwa utotoni (kwa tulozaliwa enzi hizo) na ni tamu hadi leo. Na utamu so wa ladha tu bali pia relevance ya ujumbe uliomo. 

 Basi nisiandike 'gazeti,' bali nimtakie Fareed heri ya siku yake ya kuzaliwa, na kumtakia kila la heri na fanaka maishani, na kumshukuru kwa sapoti yake kwa kazi zangu, na kumpongeza kwa kutupatia 'SUMU.' Isikilize hapa chini

4 Nov 2013



Makala hii iliandikwa kwa minajili ya kuchapishwa katika jarida la Raia Mwema toleo la Oktoba 23. Hata hivyo haikuchapishwa kwa madai kuwa ilikuwa inapromoti msanii Fid Q na wimbo wake mpya wa Siri ya Mchezo. Whether uamuzi wa jarida hilo ni sahihi au la, nimeonelea ni vema kuichapisha makala hiyo hapa bloguni

MAKALA YA RAIA MWEMA TOLEO LA OKTOBA 23, 2013

Nianze makala hii kwa kuomba radhi kutokana na kuadimika kwangu katika toleo lililopita. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Uandishi wa makala zangu umekuwa sehemu muhimu ya maisha yangu, na pindi ikipita wiki pasi kuandika chochote (kama ilivyokuwa wiki iliyopita) huwa najisikia kama nimepungukiwa na kitu flani.

Pamoja na kiu yangu kubwa ya kuhamasisha mijadala mbalimbali, kukemea maovu na hata kuhabarishana tu, moja ya hamasa kubwa zinazonifanya niendelee na jukumu hili ni mapokeo ya wasomaji mbalimbali.

Na wiki iliyopita nilipata hamasa kubwa kutoka kwa msanii maarufu wa muziki wa Bongofleva, Fareed Kubanda, au 'Fid Q' kwa jina la kisanii.
Msanii huyo ametoa kibao chake kipya kinachofahamika kama ‘Siri ya Mchezo’ (unaweza kukisikiliza na kusoma mashairi yake hapa). Kilichonivutia kuhusu wimbo huo ni ujumbe mzito wa kisiasa, ambapo ni kitu adimu kwa wasanii wetu kuzungumzia masuala ya kisiasa kwenye tungo zao.

Niliongea na Fid Q kwa kutumia mtandao wa kijamii wa Twitter, ambapo pamoja na mambo mengine alinieleza kitu kimoja kilichonigusa sana. Namnukuu, “Believe or not, nilijaribu kujivisha viatu vyako wakati ninaandika hii track.”

Ni nani hatofarijika kuambiwa na msanii mwenye jina kubwa kama Fid Q kuwa alipata hamasa kutoka kwao wakati anaandika mashairi ya wimbo ambao kwa hakika utavuma?

Lakini licha ya hamasa, furaha na heshima hiyo kutoka kwa msanii huyo, kuna kitu cha ziada ambacho kimsingi ndicho kinabeba dhima ya makala hii: nafasi ya wasanii wetu katika kuhamasisha mabadiliko chanya kwa jamii.

Kwa muda mrefu wasanii wetu, hususan wa muziki ‘wa kizazi kipya’ (Bongofleva) wamekuwa wakilaumiwa kwa aidha kutumika vibaya na wanasiasa au kutotilia maanani matatizo mbalimbali yanayoikabili Tanzania yetu.

Imezoeleka kwamba ukifika wakati wa uchaguzi ndipo wanasiasa wetu hukumbuka kuwa kuna vijana wanaendesha maisha kwa kujishughulisha na sanaa ya muziki. Kama ilivyo kwa makundi mengine ya jamii, wanasiasa hao pasi haya huwavuta karibu wasanii na kisha kuwatumia kwenye kampeni zao. Wakishapata madaraka, wanawatelekeza kama inavyotokea kwa wengi wa wapigakura majimboni.

Lakini wakati ni rahisi kuwalaumu wasanii kwa kile kinachotafsiriwa na wengi kama ‘kutojali matatizo yanayoikabili Tanzania yetu,’ Fid Q alinieleza kuwa tatizo mojawapo ni ukiritimba wa vyombo vya habari ‘vya asili’ (yaani traditional media, kwa maana ya radio, televisheni na magazeti). Sio siri kwamba wamiliki wa vyombo hivyo huchelea sana kuwaudhi watawala kiasi kwamba si ajabu kwa wimbo unaokemea maovu flani yanayowahusu watawala ukanyimwa fursa radioni au kwenye runinga.

Tukirejea kwenye wimbo huo wa Siri ya Mchezo, yayumkinika kubashiri kuwa Fid Q anafungua mlango wa kile kinachofahamika kimuziki kama ‘political rap’ yaani muziki wa kufokafoka uliobeba ujumbe wa kisiasa. Aina hiyo ya muziki ilikuwa maarufu sana huko Marekani kwenye miaka ya 1970 hadi 1980, ambapo ulilenga kuzungumzia masuala mbalimbali ya kisiasa na kijamii. Kimsingi, muziki huo ulikuwa ni kama nyenzo ya wasanii kupambana na udhalimu, sambamba na kuhamasisha jamii, hususan vijana, kushiriki katika harakati za kujenga jamii bora.

Katika wimbo huo, Fid Q anamkumbuka mmoja wa wasomi lulu kwa taifa letu, marehemu Profesa Chachage Chachage ambaye wakati wa uhai wake alijitahidi sana kutuelimisha kuhusu soko huria na athari zake. Kadhalika, msanii huyo anasononeka kuhusu hatma ya taifa letu akidadisi “tutarithi nini...” katika zama hizi ambapo utajiri wetu unanufaisha wachache (hususan wageni na vibaraka wao) huku mamilioni ya Watanzania wakibaki masikini.

Kadhalika, msanii huyo anawanyooshea kidole wahujumu wa uchumi, kabla ya kutoa angalizo muhimu kuwa “taifa la kondoo huendeshwa na serikali ya dubu/mbwa mwitu wenye siri...

Vilevile, Fid Q anatahadharisha kuhusu siasa inavyotumika kama kitega uchumi, na kusikitishwa na jinsi ukoloni mamboleo ulivyotupatia uhuru wa bendera huku ukituonyesha “kufuru za wenye hela.”

Katika lugha ya kisanii, msanii huyo analalamika kuwa Tanzania imegeuka kama mwanamke asiyefuata maadili, ‘anayetembea’ na kila mtu, mpaka wanamwita “cha wote,” na ambaye anatumia pombe kama njia ya kukimbiza matatizo yake. Kimsingi, hapa anazungumzia jinsi nchi yetu ilivyogeuka ‘shamba la bibi’ ambapo kila mwenye ‘fursa’ anajichumia.

Msanii huyo anakwenda mbali zaidi na kukemea dhana kuwa wawekezaji wa kigeni watatuletea maendeleo, na anasema “maendeleo ni ndoto, ile mwekezaji ashaipuuza,” na kutahadharisha kwamba uwepo wa wawekezaji hautufanyi tufikie viwango vya maendeleo katika nchi zao, akihoji “je kukaa karibu na moto ni kuota au kujiunguza?”

Fid Q pia anazilaumu taasisi za kisiasa kwa ‘kuwafelisha’ wananchi, kama ambavyo tunashuhudia vyama vyetu vya kisiasa vikiwa ‘bize’ kulumbana huku walalahoi wakizidi kutaabika.

Pia anakumbusha kuwa “hakuna utumwa mbaya kama kujiona uko huru” na kutahadharisha kuwa jitihada za kusaka ukweli zitakumbwa na vizingiti, akisema, “Kuusaka ukweli  ni  sawa na kumenya kitunguu/
kila ganda litakutoa machozi na utabaki macho juu/
Ukishafika kwenye kiini  niambie nini utagundua.
.?”

Anahitimisha tungo hiyo aliyomshirikisha msanii mwingine maarufu Juma Nature kwa kutahadharisha kuhusu wanasiasa matapeli ambao “wamejivisha u-Noah, safina zao zikatoboka; wakajivisha u-Mussa, fimbo zao hazikugeuka nyoka; sasa wamejivisha u-Mungu mtu...” Kadri tunavyoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 tutashuhudia kila aina ya utapeli wa kisiasa ambapo baadhi ya wanaosaka urais wataahidi mambo ambayo hata wenyewe hawayaamini.

Lengo la makala hii sio kuchambua wimbo huo bali kupigia mstari umuhimu wa alichofanya msanii Fid Q kutumia kipaji chake cha muziki kuuzindua umma hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa kupata Katiba mpya, sambamba na hekaheka za uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Nimalizie makala hii kwa kumpongeza msanii huyo, na kutoa wito kwa kila Mtanzania kutumia nafasi aliyonayo kuwa chachu ya mabadiliko stahili kwa nchi yetu. Hatuwezi kuendelea kuwa watu wa kulalamika tu ilhali tuna uwezo wa kubadilisha yote yanayokwaza ustawi wa taifa letu.


Inawezekana, timiza wajibu wako

9 Jun 2013


Huiwezi kuuzungumzia muziki wa Bongoflava pasi kumtaja Mike Mhagama. Huyu alikuwa mtangazaji wa kituo cha kwanza binafsi cha redio nchini Tanzania, Radio One. Mike,ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani, alitoa mchango mkubwa sana kuutambulisha muziki wa Bongoflava- na kama sijakosea ni miongoni mwa waasisi wa neno 'Bongoflava' (sina hakika sana).

Ninakumbuka enzi hizo, kukosa kipindi cha DJ Show (kama sijakosea) ilikuwa kama dhambi flani kwa mtu anayependa muziki. Ama kwa hakika zama hizo kulikuwa na raha ya kuskiza redio, burudani iliyokuwa ikitolewa licha ya kuwa na ladha nzuri lakini pia iliendeshwa ki-professional.

Kama ambavyo wengi tumeguswa na kinachoonekana kama 'bifu' (uhasama) wa wasanii wawili nguli wa Bongofleva, Hamisi Mwinjuma a.k.a @MwanaFA na Judith Wambura a.k.a @LadyJaydee, Mike nae ameonyesha kuguswa na suala hilo japo yupo mbali na nyumbani.

Katika 'Timeline' yake huko Twitter, mtangazaji (@MikeMhagama) huyo wa zamani ameandika (ninamnukuu)

Screenshot_2013-06-09-21-09-01-1.png

Mike alikuwa anajibu rai yangu kwa wasanii Fareed Kubanda a.k.a @FidQ Ambwene Yesaya a.k.a AY (@AyTanzania) na Joseph Haule a.k.a @Profesa_Jay wafanye jithada za upatanishi kati ya Mwana FA na Jide. Kadhalika nilipendekza kuwa kikao hicho kinaweza pia kuhudhuriwa na watangazaji walio-present Kilimanjaro Tanzania Music Awards 2013 Jokate (@JokateM) na Millard Ayo (@MillardAyo)

Hadi wakati ninaandika makala hii raia hiyo ilikuwa haijajibiwa.Hata hivyo,ninapenda kumpongeza Mike Mhagama kwa angalau kuonyesha kuguswa na 'bifu' hiyo na kutamani kuisuluhisha. Si vigumu kuelea kwanini Mike ameguswa. Kama miongoni mwa waasisi na waliopromoti Bongoflava tangu inazaliwa hadi ilipofikia, lazima atakuwa anahuzunishwa na ugomvi huu.

Kwa upande mwingine, mhariri na mmiliki wa tovuti ya Bongo Celebrity, ambayo maarufu zaidi ya burudani kuliko zote za Watanzania,  Jeff Msangi, naye ameandika makala nzuri inayohusu suala hilo la bifu ya FA na JIDE. 

Makala hiyo ni hii hapa chini 

LADY JAYDEE Vs MwanaFA: BEEF,BIASHARA, PERSONAL AU?

Yapo mambo ambayo mara nyingi sisi hapa BC huwa tunayaacha yapite. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na Beef baina ya watu fulani fulani hususani wale ambao BC inawachukulia kama Celebrities na hivyo kuleta maana halisi ya BongoCelebrity.
Nakumbuka wakati BC inaanza (miaka mingi sasa) nia ilikuwa ni kuyatizama maisha ya watu wetu maarufu (celebrities) katika jicho chanya zaidi. Tulielewa kwamba watu wanapenda zaidi kusikia umbea. Tulifahamu kwamba habari mbaya huenea kwa kasi ya aina yake kulinganisha na habari njema. Pamoja na kuelewa hivyo,tumejikita kwenye nia. To stay positive and ask everyone to stay positive and pay attention to more positives than negatives.
Sasa kama wewe ni mtumiaji au mtembeleaji mzuri wa mitandao ya kijamii kama vile Twitter,Facebook, Instagram etc, bila shaka leo umekumbana na maendeleo ya mpambano wa maneno kati ya Lady Jaydee na MwanaFA.Kuna kashfa, kuna kuitana majina. Kuna ushabiki ambao naamini mwisho wake sio mzuri….
Hawa wote ni wasanii wakongwe. Ni mifano ya kutizamwa na wengi hususani wasanii wachanga ambao wanataka kufikia mafanikio ambayo hawa tayari wameyafikia. Kinachoendelea, ingawa ni kweli kinaleta msisimko fulani (hususani kwa watu wanaofurahia wakati wengine wakiumizana), hakina mantiki yenye mlengo chanya. Ni ushindani wa siku moja (June 14-siku ambayo wote wana show). Tarehe 15 June kutakuwa na nini?
Kuna njia kadhaa za kuangalia kitu kinachoendelea. Ni beef? Ni biashara? Au ni mambo binafsi? Kama ni beef la ukweli,basi kuna haja ya mtu kuingilia kati na kuwapatanisha. Kama wasanii naamini issues zao zinafanana. Matatizo ya kudhulumiwa au kutolipwa ipasavyo, ni matatizo yao wote. Sio tatizo la JayDee au MwanaFA peke yake. Hakuna haja ya beef. Kuna haja ya kuungana na kupigania kitu kimoja; Haki.
Kama malumbano haya ni kibiashara zaidi, basi tutaona tarehe 14 June kama njia inayotumiwa ni sahihi au la. Kuna tofauti kubwa kati ya beef za kupromote biashara katika nchi za wenzetu kama Marekani (50Cent na Kanye West) na Tanzania yetu.Mazingira yanatofautiana…
Kama kinachoendelea ni masuala binafsi…then we don’t have a business to be into other people’s businesses. Wanaweza kuyamaliza…



CHANZO: BONGOCELEBRITY.COM Ni matumaini yangu-na pengine yenu wasomaji- kuwa hatimaye wasanii wetu, Mwana FA na Jide, watakaa pamoja na kufikia mwafaka wa kumaliza tofauti zao.Labda baadhi ya video hizi walioshirikiana zinaweza kuwakumbusha kuwa wamtoka mbali
Katika wimbo huu 'Nangoja Ageuke' wa FA a AY kuna cameo ya Lady Jaydee



9 Jul 2012




Naomba nivamie eneo ambalo ninaweza kujiita 'mgeni' (foreign territoty).Hili ni uchambuzi wa muziki,au kwa usahihi zaidi,uchambuzi wa video za muziki.

Nikurejeshe nyuma kidogo.Zamani hizooo,niliwahi 'kuota' kuwa mshiriki wa muziki.Well,sio kuwa mwanamuziki per se bali kujishughulisha na utengenezaji muziki.Nilipokuwa sekondari nilimudu kutunga nyimbo kadhaa kwa kwaya ya shule.Niliweza kutunga aya na sauti lakini tatizo lilikuwa kwenye namna ya uchezaji.Hadi leo,mie na kucheza ni kama kibaka na polisi.Kwa kifupi sijui ku-dance.

Ndoto za kuwa mtengeneza muziki (prodyuza) zilichangiwa zaidi na jinsi ninavyothamini 'michango isiyoonekana.' Hapa ninamaanisha kazi za watu kama watengeneza filamu, watengeneza muziki au hata mashushushu.Hawa ni watu wanaowezesha mengi na pengine laiti wangekuwa wanaonekana na 'products' zilizokwishakamilika basi sifa nyingi zingewaendea wao kuliko ilivyo sasa.

Tunapoona filamu nzuri,sifa nyingi huenda kwa actor au actress.Lakini kimsingi kazi kubwa inayoweza kupelekea filamu ikapata umaarufu hufanywa na mtengenezaji filamu.Kwenye filamu,uzuri wa filamu husika ni mkusanyiko wa jitihada za mwongozaji filamu (yaani director) na mtengenezaji filamu (yaani producer).

Nimeutaja ushushushu.Jamaa hawa ndio kila kitu.Ukiona nchi inakwenda vyema ujue wanafanya kazi yao kwa ufanisi.Ukiona mambo yanayumba basi ujue ndugu zetu hawa wana mushkeli mahala flani.Lakini kimsingi ni kuwa hawaonekani.Kama ilivyo kwa director au prodcuer wa filamu,sifa za kazi husika hulekezwa kwa wengine (kwenye filamu ni actors/actresses) na kwenye mwenendo wa nchi sifa huelekezwa kwa askari au taasisi nyingine za serikali.

Tofauti na filamu na ushushushu ambapo ni mara nyingi ni mkusanyiko wa wengi,kwenye muziki mara nyingi ni jithada za mtu mmoja au wawili. Mara nyingi producer wa muziki ndiye anayebuni ladha ya wimbo kwa maana ya kuunda beatsjapo jukumu la mwisho la ku-flow linabaki kwa msanii husika.Pia inawezekana wimbo ukawa umetungwa na mtu mwingine kisha kumpatia msanii au producer.La msingi hapa ni kuwa producer au mtunzi wa wimbo (kama si msanii mwenyewe) ni watu ambao hawapati sifa za kutosha ukilinganisha na msanii husika.

Kwahiyo moja ya ndoto zangu udogoni ilikuwa kuwa music producer...lakini kama tujuavyo katika maisha sio kila tutakacho ndio tupatacho.Ndoto hiyo 'ilikufa kifo cha asili' baada ya kuelekeza nguvu zangu kwenye  maeneo mengine ya maisha.Lakini hadi leo nina mapenzi ya dhati na muziki hususan wa kufokafoka.

Lengo la makala hii ni kuchambua kazi mbili za wasanii mahiri wa Bongoflava,Fid-Q na Solo Thang,ambao hivi karibuni wametambulisha video zao mpya.

Naomba nisisitize kuwa licha ya mapenzi yangu kwa muziki,mie si mtaalam (expert) wa eneo hilo.Uchambuzi wangu huu ni wa ki-layman (i.e. wa mtu asiye na upeo wa kutosha katika mada husika).

Jingine la kupigia mstari ni desturi iliyojengeka miongoni mwetu kuwa pindi ukionyesha mapungufu ya kitu flani basi wewe ni HATER.Binafsi,nimefika nilipofika kwa sababu siku zote nimekuwa nikipokea na kufanyia kazi maoni mbalimbali hata yale yanayokinzana na imani au mtazamo wangu.Kupewa sifa kuna tatizo moja: hakuwezi kukusaidia kutambua wapi umekwenda kombo.Ofkoz, kazi nzuri lazima isifiwe lakini pengine ili kumsaidia aliyefanya kazi hiyo ni vema kumfahamisha wapi arekebishe au penye mapungufu.Na hiki ndio nitakachofanya katika makala hii.

Video za muziki ninazozichambia ni ile ya SIHITAJI MARAFIKI ya FID-Q na MISS TANZANIA ya SOLO THANG.Kwa kifupi,video zote ni za ubora wa hali ya juu.Wasanii wote wawili wamechagua location za kuvutia wakati wanarekodi video zao.Kadhalika,ubora wa picha ni wa kiwango cha juu.


Wasanii hawa wana sifa moja inayolingana: ni mahiri mno katika uwasilishaji wa ujumbe uliomo kwenye wimbo husika.Wote wana uwezo wa hali ya juu wa kucheza na maneno, neno pekee la Kiingereza unaloweza kulitumia kuwaelezea ni LYRICAL ASSASSINS (Usitishwe na hiyo 'assassins' kwani ni neno tu linalotumiwa kutanabaisha namna msanii anavyoweza 'kucheza na maneno' kwenye tungo husika).

Wakati Solo Thang anamzungumzia Miss Tanzania,Fid-Q anazungumzia marafiki.Ujumbe katika tungo zote mbili haupo wazi sana na inambidi msikilizaji 'asome kati ya mistari' (reading between the lines) kuelewa kinachoongelewa.Usipokuwa makini unaweza kudhani Solo 'anawapaka' warembo lakini kimsingi MISS TANZANIA imebeba ujumbe mzito hususan kwa mabinti warembo wenye kuendekeza tabia zisizopendeza machoni kwa jamii.

Ujumbe wa Solo unapigia mstari mtizamo wa wengi kuhusu urembo kama fani (iwe u-Miss au uanamitindo).Yayumkinika kusema kuwa machoni wa wengi fani hizo mbili hutizamwa 'kwa jicho baya' hasa kutokana na tabia kama za huyo 'Miss Tanzania anayezungumziw na Solo.' Huu ni ukweli i.e. ni mtazamo wa wengi japo si kila Miss au mwanamitindo ana tabia zisizopendeza katika jamii.Inawezekana Solo anamzungumzia Miss Tanzania flani?Jibu la swali hili analo yeye mwenyewe lakini kwa vile ni mahiri mno wa 'kucheza na maneno' yayumkinika kuamini kuwa kuna ujumbe mpana pengine zaidi ya uelewa wetu.

Kwa upande wake Fid-Q, SITAKI MARAFIKI haimaanishi marafiki si muhimu bali kwa kutumia kipaji chake kikubwa cha kuwasilisha ujumbe kwa namna inayohitaji tafakuri,msanii huyo anaweka wazi mtazamo wake kuhusu mahusiano katika jamii,kwa kutumia mfano mwafaka wa marafiki.Nadhani ushaskia msemo  'MARAFIKI WA NINI KAMA MAADUI WANANISAIDIA.' Mara nyingi,marafiki zetu hupenda kututendea mazuri tu tunayotarajia kutoka kwao na pengine kuepuka kutueleza 'hapa umechemka.' Lakini maadui zetu huwa mahiri wa kuonyesha kasoro zetu (hata kama ni kwa uchache) japo kimsingi matarajio yao huwa ni kuonyesha mabaya yetu.Kwa hiyo pasipo kukusudia,maadui zetu wanaweza kuwa na mchango flani chanya katika maisha yetu kwa sababu hawana unafiki katika kunyooshe akidole mapungufu yetu.

Kwa anayezifahamu vema kazi za Fid-Q na Solo Thang ni wazi hatokuwa na wasiwasi kuhusu namna watakavyouwasilisha ujumbe kwenye tungo mpya.Kama nilivyoeleza hapo juu,wasanii hawa wana uwezo wa hali ya juu wa 'kucheza na lugha na maneno.' Uwezo huo unawasiaidia sana katika kuwasilisha ujumbe katika namna inayomwacha msikilizaji 'ameterazika' (ameridhika)

Sasa nigeukia eneo linaloweza kuniingiza matatizoni: mapungufu katika kazi hizo za wasanii hao.Kimsingi si mapungufu bali ni pungufu kwani ni moja tu,na si kubwa sana.Ukiangalia video zote mbili utabaini jambo hili: katika video ya Fid-Q,tangu mwanzo hadi mwisho wa video yake amevaa vazi lilelile.Kwa Solo,kwa kiwango kikubwa katika video hiyo yupo katika T-shirt ileile japo kuna vipande ambapo anaonekana amevaa shati.

Kama nilivyotanabaisha,hii ni kasoro ndogo inayoweza kabisa kufunikwa na ladha ( flavour) ya muziki, ujumbe uliomo katika wimbo,na kiwango cha video.Hata hivyo,kama inavyotanabaishwa kwenye na Andrew Goodwin kwenye Kanuni ya Video ya Muziki (Music Video Theory) vinavyoonekana katika video ya muziki (visuals) vinaweza kuwa na mchango mkubwa sio tu kuiboresha video husika bali pia kuiunganisha na hadhira.

Pengine ili uelewe ninachoelezea hapa nitolee mfano msanii kama Lady Gaga.Mavazi yake ni burudani tosha-japo sio aina ya mavazi unayoweza kumwambia fundi cherahani akutengenezee.Msanii kama Michael Jackson alifahamika sio tu kwa miziki yake bali pia mavazi yake.Kwa sanii wa hip-hop wa Marekani,mavazi ni moja ya vitu muhimu mno,na baadhi ya mapendezeo yao katika mavazi yamepelekea mwamko wa fasheni,kwa mfano mashati ya 'DOGI DOGI' yaliyokuwa yanapendelewa na wasanii wa rap/hiphop wa pwani ya magharibi ya Marekani (West Coast rappers) kwa mfano Snoop Dogg na Ice Cube



Nadhani sababu pekee iliyowafanya Fid-Q na Solo wasionekane katika mavazi tofaut tofauti katika video zao ni MUDA.Hapa ninabashiri kuwa hawakuwa na muda wa kutosha kurekodi video zao kwa muda mrefu ambao ungewapa nafasi za kubadili mavazi mara kadhaa.Naomba nisistize kuwa kasoro hiyo ndogo haijapoteza hata chembe ladha ya kazi zao bora kabisa.Nimeipigia mstari kasoro hii kwa minajili ya kuwasaidia wasanii hao huko mbeleni wajaribu kutumia muda zaidi katika kurekodi video zao.Kanuni nyepesi ya kurekodi kitu chochote kile ni hii: kadri unavyojipa muda wa kutosha ndivyo unavyomudu kurekodi vitu vingi zaidi ambavyo wakati wa kuhariri utaondoa vile usivyovitaka na kuacha vile unavyovitaka.

Lakini kasoro hiyo ndogo inarekebishika.Ninaamini tulichoshuhudia katika video ya SIHITAJI MARAFIKI na MISSI TANZANIA ni matoleo ya mwanzo tu (iwapo Fid na Solo wana mtizamo kama wangu).Si ajabu kwa msanii kutoa video ya mwanzo kisha kutoa video nyingine rasmi kwa ajili ya wimbo husika.Mfano mzuri ni huu wa kundi la TOK katika wimbo wao Footprints Hii ni version ya awali

Hii ni version rasmi

Pengine kitawachowarahisishia Solo na Fid-Q kutengeneza video 'r(kama wataona kuna haja ya kufanya hivyo) ni ukweli kwamba tayari wana video nzima ya asili,ambapo wakiamua kuongeza chochote inakuwa ni suala la kuongeza tu vipande vipya katika original version.Hili si lazima,as long as wao wameridhika na versions walizoweka hadharani.

Ukiweka kando kasoro hiyo ndogo,Solo Thang ameendelea kuwa mithili ya balozi wetu wa Bongoflava katika anga za kimataifa ambapo anafanyia kazi zake kutoka nchini Ireland.Lakini licha ya kuwa nguli (legend) wa bongoflava na 'wadhifa' huo wa ubalozi wa kimataifa,msanii huyu ni miongoni mwa wachache ambao ni down-to-earth sana na anayejali sana kuishirikisha hadhira,hususan kupitia Twitter na Facebook.Kadhalika,ana blogu yake anayotumia kuwafahamisha wapenzi wa muziki wake kuhusu kazi zake.

Kwa upande wa Fid-Q, mkongwe huyu wa muziki wa kufokafoka huko nyumbani amekuwa mahiri sana katika matumizi ya mitandao ya kijamii kutangaza kazi zake na kuishirikisha hadhira.Huko Twitter ana utaratibu wa kujibu maswali angalau mara moja kwa wiki kwa kutumia hashtag #AskFidQ. Hii inatoa fursa kwa wengi kumuuliza maswali mbalimbali.Kadhalika,anaendesha kitu kinachofahamika kama Hip-Hop Darasa,ambapo pamoja na mambo mengine anatoa elimu kwa kizazi kipya cha Hip-hop huko nyumbani.Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa kipindi chake maarufu mtandaoni cha Fidstyle Friday kitaanza kuonyeshwa kwenye runinga katika kituo cha East Africa Television (EATV).Haya ni maendeleo makubwa.

Basi nimalizie kwa kuwapongeza Fid-Q na Solo Thang kwa kazi zao bora kabisa.Naomba wasitafsiri kasoro ndogo niliyobainisha hapo juu kuwa ni HATING. Sote tunapenda kuona wasanii wetu wakifanikiwa na kuteka anga sio huko nyumbani tu bali Afrika na duniani kwa ujumla.Natambua kuna wataosema "huyu nae,anajifanya anajua kila kitu" lakini lengo langu si kujifanya mjuaji bali kutoa mchango wangu kwa wasanii wetu.

Nimalizie makala hii na video zifuatazo za wasanii hao



25 Nov 2011


23 Oct 2011





Kwa Freestyles za wiki zilizopita bonyeza hapo kulia kwenye nembo ya Cheusi Dawa TV (FID-Q)

23 Jul 2011



Kalapina on politics, Freemasons, war, peace, Rostam, Drugs etc.
More from Kalapina and kikosi http://www.reverbnation.com/tunepak/3387426

Click the banner titled CHEUSI DAWA TV (FID-Q) (see the sidebar) for previous episodes of Fridstyle Friday and much more!

18 Jun 2011


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.