18 Oct 2012


KWA mara nyingine, wiki iliyopita Tanzania imeshuhudia ‘sura mbaya’ (ugly face) ya imani ya kidini. Kwa mujibu wa taarifa zenyewe, kilichoanza kama mchezo wa watoto kilisababisha vurugu kubwa zilizopelekea makanisa zaidi ya matano kuchomwa moto, sambamba na uharibifu wa mali kadhaa.
Inaelezwa kwamba chanzo cha vurugu hizo ni kitendo cha mtoto mmoja kuikojolea Kuran Tukufu baada ya ‘mabishano ya kitoto’ na mtoto mwenzie. Habari zinasema mtoto aliyefanya kitendo hicho alitaka kuthibitisha ukweli wa ‘tishio’ alilopewa na mtoto mwenzie kuwa iwapo atakikojolea Kitabu hicho Kitukufu, basi atageuka nyoka!
Sote tuliwahi kuwa watoto katika hatua za mwanzo za maisha yetu, na kwa kutumia uzoefu huo kama ‘watoto wa zamani’ tunaweza kukumbuka vitu vya ajabu, vya kukera, vya kuchekesha, na vya kila aina ambavyo twaweza kuvihitimisha kwa msemo huu wa Waingereza: ‘kids will always be kids’ (watoto wataendelea kuwa watoto).
Kwamba binadamu, pasipo kujali umri wake, anaweza kukojolea Kitabu Kitukufu cha dini fulani, ni jambo lisilopendeza hata kidogo. Na kwa hakika, kitendo cha aina hiyo, kitamchukiza kila muumini wa dini husika. Lakini kama ilivyo katika maeneo mengine ya maisha ambapo umri unaangaliwa kama kigezo muhimu cha kuhukumu tendo, ukweli kwamba aliyekojolea Kuran Tukufu ni mtoto wa miaka 14, ulipaswa kupewa uzito na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislam ambao waliamua kuchukua sheria mkononi kwa kufanya vurugu kubwa ikiwa ni pamoja na kuchoma moto makanisa.
Licha ya kuguswa na tukio hilo la kusikitisha kama Mtanzania na Mkristo, lakini pia nimeguswa kwa vile linahusiana na eneo ambalo nimekuwa nikihangaika nalo kitaaluma kitambo sasa. Miaka michache iliyopita, nilikuja huko nyumbani kukusanya data kwa ajili ya utafiti wa kitaaluma kuhusu harakati za vikundi vya Kiislam nchini Tanzania. Kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu, utafiti huo bado haujakamilika japo katika hatua niliyofikia unaweza kutoa majibu fulani kuhusu kinachoendelea huko nyumbani hivi sasa.
Nilipata fursa ya kuzungumza na makundi makuu mawili ya waumini wa dini ya Kiislam. Wale tunaoweza kuwaita ‘wenye msimamo mkali’ na wale wa ‘wenye msimamo wa kawaida.’ Naomba nisisitize kuwa matumizi ya maneno ‘msimamo mkali’ na ‘kawaida’ ni kwa minajili ya mjadala tu. Ninatoa tahadhari hii mapema kwa kuchelea uwezekano wa shutuma kuwa ninawagawa Waislam katika makundi, ambayo kama ilivyothibitika katika utafiti wangu, wengi wao hawapendi mgawanyo wa aina hiyo kwani wanaamini wote ni Waislam.
Moja ya mambo yaliyojitokeza katika mahojiano yangu na ‘makundi’ yote mawili ni manung’uniko (grievances) ambayo yamedumu kwa muda mrefu. Manung’uniko hayo yameshamiri zaidi kwenye suala la usawa katika elimu na ajira. Wahojiwa wengi walionyesha kuwa na hisia ya kubaguliwa kati yao na Wakristo katika upatikanaji wa fursa za elimu na ajira. Kimsingi, ukimnyima mtu fursa ya elimu, unatengeneza mazingira ‘mazuri’ ya kumkwaza kupata ajira.
Takwimu mbalimbali nilizokusanya katika utafiti huo, zinaweza kusapoti madai hayo. Lakini la muhimu zaidi hapa si sapoti ya takwimu hizo, bali mazingira yaliyopelekea uwepo wa hali hiyo. Kutokana na ufinyu wa nafasi ninalazimika kutoa maelezo ya jumla kwani kupitia kipengele kimoja hadi kingine kunahitaji zaidi ya makala moja.
Kwa kifupi, moja ya sababu zilizopelekea ‘ubaguzi’ katika upatikanaji wa fursa za elimu na ajira kati ya Waislamu na wasio Waislam (hususan Wakristo) ni mfumo wa utawala wa kikoloni. Kama tunavyofahamu, wakoloni walikuwa Wakristo, na tunafundishwa kwenye somo la historia kuwa miongoni mwa ‘watangulizi wa ukoloni’ walikuwa wamisionari wa Kikristo.
Moja ya mbinu zilizotumiwa na wamisionari kutengeneza mazingira mazuri ya kutawala jamii za Kiafrika ni ‘kusilimisha,’ japo neno hilo lina maana zaidi kwenye Uislam. Ninalitumia hapa kwa maana ya kuwatoa watu kutoka katika imani yao ya awali na kuwaingiza katika imani mpya.
Lakini historia inatufundisha kuwa Uislam ulifika huko nyumbani karne kadhaa kabla ya Ukristo. Kwa bahati mbaya au makusudi, walioleta Uislam walikuwa wafanyabiashara kutoka Arabuni na Mashariki ya Mbali, na hawakuwekea mkazo sana kusambaza dini yao.
Yayumkinika kuhitimisha kwamba kushindwa kwa watangulizi hao wa Uislam kueneza dini hiyo miaka kadhaa kabla ya ujio wa Wamisionari na hatimaye wakoloni, kulichangia kurahisisha kusambaa kwa Ukristo kwa ama ‘kusilimisha’ Wapagani (ninatumia neno hili kumaanisha dini za asili za Kiafrika) na Waislam.
Tukifupisha historia, mkoloni alitumia Ukristo kama moja ya njia za kuzitawala jamii zetu. Ni katika mazingira hayo, stadi mbalimbali zinaonyesha kuwa kwa namna fulani baadhi ya Wakristo walichelea kuunga mkono mapambano dhidi ya mkoloni kudai uhuru wetu hasa kwa vile wakoloni walifanikiwa kwa kiasi fulani kuulinganisha ukoloni na Ukristo (yaani kumpinga mkoloni ni sawa na kumpinga Yesu/Mungu).
Kwa kutumia Ukristo kama njia ya kurahisisha utawala wao, wakoloni pia walitumia dini hiyo kama chombo cha kuwatenganisha watawaliwa. Kimsingi, kuna aina ya mwafaka wa kitaaluma kuwa si kwamba wakoloni waliwathamini sana Wakristo wa Kiafrika, bali waliwaona kama nguzo muhimu katika kuigawa jamii, na hivyo kuwarahisishia kiutawala jamii husika.
Ingawa kuna wamisionari waliokuja Afrika kwa minajili ya kidini halisi, wengi wao waliendelea kushirikiana na utawala wa kikoloni katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utoaji elimu. ‘Ushirika’ huu wa wamisionari na wakoloni katika utoaji elimu, unaweza kuelezewa kama mwanzo wa ujenzi wa tabaka la Wakristo wenye elimu na ‘wasio Wakristo’ (hususan Waislam) wasio na elimu.
Kadhalika, baadhi ya Waislam walichelea kujiunga na taasisi za elimu za wamisionari/wakoloni kwa kuhofia kuingizwa katika dini hiyo (Ukristo). Tukiweka hali ilivyokuwa kabla ya uhuru, mazingira yaliyojitokeza baada ya kuondoka mkoloni, yameendelea kwa kiasi fulani kurutubisha ‘ubaguzi’ huo wa elimu na ajira.
Baada ya kupata uhuru, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikiri hadharani kuwa kuna umuhimu wa kurekebisha hali ya kutokuwapo usawa wa kielimu kati ya Wakristo na Waislam. Licha ya jitihada zake kubwa, hadi anaondoka madarakani ‘usawa’ huo haukuweza kufikiwa kwa kiwango cha kuridhisha.
Kuna maelezo mengine hapa. Shule za seminari za Wakristo ambazo kimsingi ni maalum kwa ajili ya ‘kuzalisha’ viongozi wa makanisa, zilikuwa ‘zikizalisha’ kundi la wasomi wa Kikristo ambao kwa sababu moja au nyingine, hawakuishia kuwa viongozi wa kanisa, bali wakachukua ajira serikalini au kwenye taasisi nyingine. Kwa upande mwingine, shule za kidini za Waislam ziliegemea zaidi kwenye utoaji elimu ya kidini, na katika mazingira hayo, tofauti na ilivyo kwa seminari, ‘hazikuzalisha’ wasomi wa kutosha kuingia kwenye ajira serikalini (naomba nieleweke kwa makini hapa).
Kwamba utawala wa Mwalimu Nyerere uliwapendelea Wakristo na kuwabagua Waislam, ni jambo ambalo halijathibitika kitaaluma. Hoja hiyo ni miongoni mwa masuala yanayojenga manung’uniko kwa baadhi ya Waislam. Kwamba baadhi ya Wakristo, hususan waliotoka seminari na kujiunga na ajira serikalini, waliwabagua Waislam na kuwapendelea Wakristo, ni jambo ambalo halijathibitika kitaaluma ingawa linawezekana kinadharia na kimantiki.
Kimsingi, tatizo si ubaguzi wa msomi/mwajiri Mkristo dhidi ya mwanafunzi/msaka ajira Muislam, bali mfumo ambao ulijengeka wakati wa ukoloni na umeendelea kuwepo. Unatoa nafasi (on merit) kwa Wakristo zaidi ya Waislam. Kama mwajiri anataka kujaza nafasi kwenye ofisi yake, anapaswa kuangalia, pamoja na mambo mengine, sifa za kitaaluma za waomba kazi. Sasa kwa vile mfumo wa elimu tuliorithi kwa mkoloni, na kama nilivyobainisha hapo juu, unatengeneza wasomi wengi wa Kikristo kuliko wa Kiislam, ni dhahiri kutarajia ‘ubaguzi’ wa nafasi za ajira.
Majuzi tumefanya sensa. Watawala wetu wamegoma kujumuisha kipengele cha dini kwa madai mbalimbali. Lakini kwa kufanya hivyo, watawala wanajinyima fursa ya kuelewa, kwa mfano uwiano wa ajira kati ya Wakristo na Waislam. Na cha muhimu hapo si kuelewa tu, bali pia kutafuta namna ya kurekebisha hali hiyo. Na hili ni tatizo la msingi linalofanya ‘tatizo la dini’ kuendelea kuwapo. Kuna hisia kwamba kwa kujaribu kulizungumzia suala hili kwa uwazi, kutazua tafrani kubwa kuliko mwafaka. Lakini sote tunajua kuwa ugonjwa hautibiki kwa kujidanganya kuwa haupo mwilini!
Je; kilichotokea Mbagala ni hasira tu za baadhi ya Waislam waliochukizwa na kitendo cha ‘mtoto wa Kikristo’ kukojolea Kuran Tukufu? Binafsi, naamini kuna sababu za ndani zaidi ya ‘hasira’ hizo na zinazosababisha ‘hasira’ hizo. Je; udini ni tatizo kubwa katika Tanzania yetu ingawa halizingumzwi vya kutosha? Binafsi, ninaamini jibu la swali ilo, ni ndiyo. Kama ni ndiyo, kwanini tunalikwepa tatizo hili?
Jibu linaweza kupatikana kwenye tatizo jingine ‘lisilozungumzika’ la kero za Muungano wa ‘Tanganyika’ na Zanzibar. Kwa kifupi, hadi sasa hakuna utashi wa kisiasa na kijamii kulikabili tatizo hili. Kwenye Muungano, kila Rais anachelea kuvunjikiwa na Muungano, ambao Baba wa Taifa ‘alishatoa radhi’ kwa atakayeuvunja. Kwenye hili la udini, viongozi wetu wanakwepa kulikabili kwa kuchelea kuonekana wadini. Kibaya, baadhi yao walitumia udini kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliopita. Je; yawezekana udini ni turufu muhimu kwa baadhi ya wanasiasa mufilisi?
Makala hii itaendelea wiki ijayo.




0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.