15 Nov 2012


Nianze makala hii kwa kujipongeza kutokana na ‘ubashiri wangu sahihi’ kuhusu Uchaguzi wa Rais wa Marekani. Kama mnakumbuka, katika makala ya kwanza kwa mwaka huu nilijaribu kubashiri mwenendo wa masuala mbalimbali kwa ‘mwaka mpya’ 2012, na moja ya ubashiri huo ulikuwa huu:

“Kwa kuzingatia uchambuzi wa watu mbalimbali na kwa kadri ninavyofuatilia siasa za Marekani, dau (bet) langu ni ushindi ‘kiduchu’ kwa Obama dhidi ya Mitt Romney, mgombea ninayetabiri atapitishwa na Republican (iwapo upepo wa kisiasa hautobadilika.)”

Well, Romney alifanikiwa kushinda kuwa mgombea wa Republican na hatimaye kuchuana na Obama kwenye uchaguzi moja ya chaguzi zilizokuwa na ushindani mkali kabisa, na hatimaye Obama akafanikiwa kutetea kiti chake cha Urais (nami nikafarijika kuona ‘utabiri’ wangu umetimia.)

Tukiachana na hilo, makala hii anahitimisha mfululizo wa makala zangu kuhusu vurugu za kidini huko nyumbani. Katika kuhitimisha, nitazungumzia maeneo manne: vikwazo vya ndani ya Uislam kupata ufumbuzi wa manung’uniko yao; baadhi ya migongano ya kiimani kati ya Waislam na Wakristo, na ‘utata’ wa Kikatiba kuhusu migongano hiyo; na mwisho, mapendekezo ya nini kifanyike kukabiliana na vurugu za kidini huko nyumbani.

Vikwazo vya ndani ya Uislam kupata ufumbuzi wa manung’uniko yao:
Maeneo mawili yanayothibitika kitaaluma kuwa ni msingi wa manung’uniko ya Waislamu wengi ni upatikanaji (access) wa nafasi ya elimu na ajira. Sote twatambua kuwa ukimnyima mtu elimu unamnyima fursa ya ajira (angalau kwa ajira zinazohitaji ujuzi.)

Tukiweka kando ‘lawama’ kuhusu ‘mfumo wa kibaguzi, ni muhimu kwa Waislam wenyewe kutambua kuwa lawama pekee haziwezi kuleta ufumbuzi utakaoleta angalau usawa katika fursa za ajira na elimu. Tukumbuke kuwa hata mkoloni hakuamua kutupa uhuru kwa kumchukia au kumlaumu tu.

Kadhalika Nduli Idd Amin (ambaye hivi karibuni baadhi ya ‘Waislam wenye msimamo mkali’ walibadili mtizamo wao na kumwona kama shujaa katika namna ileile ya kifo cha gaidi la Kimataifa Osama bin Laden kiliombolezwa na watu hao kama shujaa wao) hakuondoka kwa vile tulimwita kila aina ya jina baya.
Kama Waislam wanaafikiana kuwa mfumo ‘wa kibaguzi’ uliwanyima fursa ya elimu na hivyo kuwatengenezea mazingira magumu ya kupata ajira zinazohitaji elimu, basi ni muhimu kwao kuwekeza vya kutosha kwenye elimu.

Na moja ya njia bora inaweza kuwa kuziwezesha shule za kidini (pengine kuanzia madrasa) zitoe pia elimu ‘ya kidunia.’ Nilishaeleza huko nyuma kwenye mfululizo wa makala hizi jinsi shule za seminari za Kikristo zilivyochangia kuzalisha wasomi Wakristo.

Huu ni ‘ukweli mchungu’: kama mtoto wa Kikristo akitoka shule anaenda twisheni kuongeza maarifa ya ‘elimu ya kidunia’ ilhali mwenzie wa Kiislam akitoka shule anaenda madrasa kuongeza elimu ya kidini, ni wazi mmoja wao anajitengenezea mazingira mazuri ya kufaulu huku mwingine anajikwaza. Hapa simaanishi watoto wasiende madrasa bali ikiwezekana, shule za kidini (ikibidi hata kuanzia madrasa) zijumuishe pia elimu ya kidunia.

Kwa uelewa wangu, misikiti si mahala pa ibada pekee bali pia sehemu ya kumpatia muumini elimu itakayomwezesha kumtumikia Muumba wake ipasavyo. Pengine kuna umuhimu kwa kasi ya ujenzi wa misikiti kuendana na kasi ya ujenzi/uanzishwaji wa taasisi za kielimu, au ikibidi kutumia misikiti hiyo kama sehemu za ‘mapambano ya kuziba pengo la kielimu linalowakabili Waislam wengi.’

Pendekezo jingine ambalo lipo nje ya uwezo wa Waislamu ni kwa serikali kuangalia uwezekano wa kile kinachofahamika katika lugha ya Kiingereza kama ‘affirmative action’ (yaani upendeleo wenye lengo la kuleta uwiano kwa kundi flani katika jamii katika eneo flani.) Sitaki kuamini kuwa kama takwimu zikiwekwa wazi kuonyesha pengo lililopo kielimu na kiajira kati ya Wakristo na Waislamu, kisha serikali ikaridhia kutaka kupunguza pengo hilo kwa njia za uwazi, Wakristo watapinga hatua hiyo. Cha muhimu ni kufanya jitihada hizo kwa uwazi. Affirmative action imeweza kufanikiwa kwa kiasi fulani katika nchi za Magharibi kuleta uwiano kati ya, kwa mfano, ‘wazungu’ (Whites) na makundi madogo katika jamii (minorities), kwa mfano Watu Weusi (Blacks).

Baadhi ya migongano ya kiimani kati ya Waislamu na Wakristo, na utata wa Kikatiba unaotokana na migongano hiyo:
Kuna migongano kadhaa ya kiimani kati ya Waislamu na Wakristo lakini nafsi hainiruhusu kuitaja/kuizungumzia yote. Hapa nitazungumzia eneo moja tu, ambalo binafsi ninalitafsiri kama ‘nyeti’ zaidi.
Kwa Wakristo, Yesu ni Mungu na pia mwana wa Mungu (yaani Utatu Mtakatifu wa Mungu.) Kwa Waislamu, ile kusema tu Mungu ana mtoto (achilia mbali mtoto huyo ni Nabii Issa bin Mariam, yaani Yesu) ni kufr. Hakuna njia ya mkato katika migongano huu, hasa kwa vile dini hizi mbili zinaongozwa na Maandiko Matukufu/Matakatifu tofauti, yaani Kuran Tukufu kwa Waislam na Biblia Takatifu kwa Wakristo. Laiti Waislam wangekuwa wanatumia Biblia kuchunguza imani ya Wakristo kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, na laiti Wakristo wangekuwa wanatumia Kuran kuchunguza kwanini kusema Mungu ana mtoto ni kufr, labda kungepatikana mwafaka wa namna flani.

Lakini kama ilivyo kwa sie wanafunzi wa stadi za siasa kuwekea mkazo zaidi kwenye siasa na sio Fizikia, ndivyo ambavyo Waislam wanawekea mkazo kwenye Kuran na Wakristo kwenye Biblia. Na huo ni wajibu kwa kila muumini.

Hata hivyo, kama ambavyo sie wanafunzi wa siasa kuna nyakati tunalazimika kuyaelewa maeneo mengine ya kitaaluma in relation to siasa, ndivyo ambavyo baadhi ya Waislam wanafanya jitihada ya kuuelewa Ukristo in relation to Uislam, na baadhi ya Wakristo kuuelewa Uislam in relation to Ukristo. Hata hivyo hao ni wachache.

Na kwa bahati mbaya (au makusudi), jitihada hizo za kusaka uelewa wa dini nyingine ‘zimetekwa’ na dhamira ‘mbaya’ ya ‘kutaka kumwelewa adui vizuri ili kumkabili vizuri pia.’ Kwa wanaofuatilia mihadhara ya ‘kashfa’ ya kidini watakuwa wameshuhudia namna wengi wa wahubiri wanavyotumia Biblia au Kuran kuonyesha kwanini Ukristo au Uislam sio dini sahihi.

Lakini ili kuepusha ‘overgeneralization’ (kuhitimisha mambo jumla jumla) ni muhimu kufahamisha kuwa wapo wanazuoni wachache wa Kiislamu wanaoisoma Biblia kwa minajili ya uelewa tu wa kidini (na si kupambana na Ukristo).Kadhalika, katika stadi za kidini za Kikristo kuna wachache wanaoisoma Kuran kwa minajili ya uelewa tu wa kidini.

Mgongano wa kiimani kati ya Waislam na Wakristo kuhusu “Yesu ni Mungu na pia Mwana wa Mungu” ulijidhihirisha zaidi katika kesi iliyomkabili mhadhiri mmoja wa Kiislam, Ustaadh Khamis Dibagula, ambaye mwaka 2000 alihukumiwa kwenda jela huko Morogoro kwa ‘kashfa’ ya kudai “Yesu si Mungu” kama wanavyoamini Wakristo.

Kipengele cha 19 cha Katiba yetu kinatoa uhuru wa kuamini dini yoyote (japo kinakumbushia umuhimu wa kufanya hivyo bila kuathiri sheria za nchi). Na kipengele cha 18 kinatoa uhuru wa kutoa maoni (pasipo kuathiri sheria za nchi.) Kwahiyo basi Kipengele cha 19 cha Katiba kilimruhusu Dibagula kuamini “Yesu si Mungu/Mwana wa Mungu”, na kipengele cha 18 kilimruhusu kueleza imani yake hiyo waziwazi.

Kwahiyo, kwa upande mmoja Katiba iliruhusu kutoa maoni ambayo kwa upande mwingine ni kashfa. Hili ni eneo hatari ambalo ninachelea kuingia kwa undani zaidi kwani hata huo migongano wa kisheria uliopelekea Dibagula kufungwa na hatimaye kuachiwa huru ni suala ambalo Waingereza wanaliita legal minefield (yaani uwanja wa kisheria uliotegwa mabomu).

Kwa kifupi, ufanisi wa Katiba katika suala hilo unategemea zaidi busara za waumini, hususan utashi kuwa “nikasema hili-japo ni sahihi katika imani yangu-nitakuwa ninamkwaza flani.” Lakini, kusema ni jambo moja na kuamini ni jambo jingine. Katiba inaweza kuzuwia kusema hadharani kuwa “Yesu si Mungu/Mwana wa Mungu” lakini haiwezi kuzuwia wanaoamini kuwa “Yesu si Mungu/Mwana wa Mungu.”

Na kwa vile sheria zinazotokana na Katiba yetu ndizo zilizomfunga Dibagula kwa ‘kashfa’ lakini baadaye zikamwachia huru, hatua hiyo inajenga taswira gani kuhusu Katiba yetu kama chombo kinachopaswa kulinda uhuru wa kuabudu na wa maoni?
Nini kifanyike?
  1. Tuukabili ukweli kuwa tuna matatizo. Badala ya kuwa na sensa zinazokwepa kutupa ufahamu wa uwiano wa kielimu na ajira kati ya Wakristo na Waislam, ni muhimu kuwa na njia za wazi za kufahamu ukubwa wa tatizo la inequality katika maeneo mbalimbali, na hili si kwa Waislam pekee bali hata makundi mengine ya jamii.
  2. Jitihada za makusudi zinahitajika kushughulikia matatizo hayo. Ugonjwa hauponi kwa kujidanganya kuwa haupo. Badala ya kuruhusu wanasiasa watumie manung’uniko ya Waislam kama mtaji wao wa kura (mfano ahadi feki za CCM kwa Waislamu kuhusu Mahakama za Kadhi na kujiunga na OIC), harakati za kiraia zikiongozwa na wanazuoni na wanataaluma wenye mtizamo wa kuleta maelewano badala ya mifarakano ziimarishwe.
  3. Jitihada za ndani na nje ya Uislam zinahitajika katika kuhamasisha maendeleo ya kielimu kwa Waislam. Malalamiko pekee hayawezi kuleta ufumbuzi. Kadhalika, ushirikiano kati ya Waislam na serikali na taasisi nyingine za kidini na kijamii ni muhimu iwapo itakubalika kuwa na affirmative action.
Mwisho, ninatambua tofauti zetu za kiimani. Busara inahitajika katika kudumisha imani zetu na wakati huo kutoa fursa kwa wenzetu kubaki na imani zao. Tuliweza huko nyuma, na tunaweza sasa na hata milele kuwa Watanzania kwanza kisha ndio tuangalie huyu Muislam au Mkristo, Mchagga au Mndamba, mwanamke au mwanaume, nk.

Adui yetu mkubwa ni umasikini unaotishia uhai wa nchi yetu bila kujali huyu ni Hamisi na yule ni John. Mafisadi wanaotafuna raslimali zetu na kuficha mabilioni huko Uswisi, visiwa vya Jersey, nk hawafanyi hivyo kwa vile wanawapenda Wakristo na kuwachukia Waislam (au kinyume chake), bali wanamnyonga kila Mtanzania pasi kujali dini yake.

Kama ambavyo umasikini wetu ni mtaji mzuri kwa maharamia wa kisiasa kununua kura ndivyo ambavyo utengano wetu wa kidini unavyokuwa turufu kubwa kwa wanasiasa mufilisi ambao kimsingi dini zao si Uislam au Ukristo bali ulafi wa kuifilisi nchi yetu hadi tone la mwisho.
UMOJA NI NGUVU UTENGANO NI UDHAIFU

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.