23 Nov 2012


NIANZE makala haya na nukuu ya bandiko la Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kuhusu ushindi wa hivi karibuni wa Rais Barack Obama wa Marekani. Nape aliweka bandiko hilo kwenye mtandao wa Jamii Forums, Novemba 7, mwaka huu akisema:
“Ushindi wa Obama dhidi ya Romney, ni fundisho zuri kwa upinzani nchini kwetu kama wataamua kujifunza, mafunzo muhimu sana kwa washindani wa kisiasa ni pamoja na; Mosi, kiwango cha utekelezaji wa ahadi mbalimbali na mipango (Ilani ya Uchaguzi) kwa wananchi ina nguvu kubwa katika kuwafanya wapigakura kuamua nani wa kumpa kura wakati wa kupiga kura...kupigia kura mabadiliko au la...
Pili, kelele nyingi na wingi wa wapiga kelele si kigezo cha kupata kura nyingi siku ya kupigiwa kura...mikakati na ukaribu na wapigakura ambao huonyesha ni kiasi gani Chama kiko karibu na kuzijua changamoto zinazowakabili wapigakura, ni moja ya misingi mikubwa...
Tatu, kutumia muda mwingi kuponda mafanikio yaliyopatikana kwenye kipindi cha mshindani wako...hasa aliyeko madarakani, hakusaidii kukufanya upate kura, bali wenye akili zao wataona unawadharau na kuwaona wajinga kama vile hawaoni yaliyofanyika...ndicho kilichommaliza Romney...
Nne, lakini ushindi kwa Obama ni dalili njema za kukubalika kwa fikra za kijamaa kwa Taifa kubwa na la kibepari duniani...sasa tizameni upya itikadi zenu...”
Katika makala haya, nitamjibu Nape hoja kwa hoja kwa minajili ya kuwafumbua macho Watanzania wenzangu juu ya hatari ya baadhi ya wanasiasa kama Nape kuteka mafanikio ya wanasiasa wa nchi nyingine na kuyalinganisha na ubabaishaji wao ambao wao wanaamini ni mafanikio.
Kimsingi, mwanasiasa huyo amepotoka katika hoja zote nne. Ingawa ni kweli kwamba CCM na Serikali yake wamejaribu kutekeleza baadhi ya ahadi zao (kwa mfano ujenzi wa barabara kadhaa), moja ya ahadi za msingi iliyotolewa na mgombea wa chama hicho mwaka 2005, Rais Jakaya Kikwete, kuhusu maisha bora kwa Watanzania imeendelea kuwa kiini macho.
Kwa mtizamo wangu, kikwazo kikubwa kwa ahadi hiyo ya Rais Kikwete, ni ufisadi ambao yayumkinika kuhitimisha kuwa umeshamiri zaidi tangu Awamu ya Nne iingie madarakani. Na ufisadi usingepaswa kuwa kikwazo kwani moja ya matamko ya awali ya Rais Kikwete baada ya kuingia madarakani ilikuwa kuwapa ‘deadline’ mafisadi, akidai kuwa asingekuwa na huruma nao na kwamba tabasamu lake lisitafsiriwe vibaya.
Hadi leo hakuna fisadi mmoja aliyejali ‘deadline’ hiyo, na badala yake tunashuhudia ufisadi mpya ukiibuka kila kukicha. Kwa makusudi, Nape anajaribu kulinganisha utekelezaji wa ahadi za Obama wakati anaingia madarakani na porojo za CCM.
Wakati Obama amefanikiwa kutekeleza ahadi ya kumteketeza aliyekuwa gaidi wa kimataifa, Osama bin Laden, na pia kutekeleza ahadi yake ya kuyaondoa majeshi ya Marekani huko Iraki, licha ya ‘deadline’ ya Rais Kikwete kwa mafisadi kubaki historia tu, ahadi nyingine kuwa angemaliza kero ya mgao wa umeme, imeendelea kuwa ndoto tu.
Katika hoja ya pili, Nape anadai CCM inazijua changamoto zinazowakabili wapigakura wa Tanzania. Yupo sahihi. CCM inatambua kero za Watanzania, hususan kushamiri kwa rushwa nchini, lakini chama hicho kimetokea kuwa hifadhi ya wala rushwa.
Ushahidi wa karibuni kwamba CCM ni kichaka kinachohifadhi mafisadi ni kusuasua kwa Serikali yake kuwashughulikia majambazi walioficha fedha zetu huko Uswisi. Anachokiita Nape kuwa ni wingi wa kelele, akimaanisha za vyama vya upinzani, kwa hakika ni kilio cha Watanzania walio wengi, ukiondoa mafisadi. Kelele hizo anazozungumzia Nape ndizo zilizopelekea kuibua ufisadi mkubwa kama wa EPA, Richmond na kadhalika na sasa hili suala la fedha zilizoibwa na mafisadi na kufichwa Uswisi.
Katika hoja ya tatu, Katibu Mwenezi huyo wa CCM anadai kuwa kudharau mafanikio ya utawala uliopo madarakani, ni sawa na kuwatusi wapigakura. Kimsingi, sijawahi kuwasikia CHADEMA au chama kingine cha upinzani kikiponda jitihada za Serikali ya CCM katika masuala ya maendeleo ya nchi. Na ndiyo maana Rais Kikwete alipokuwa ziarani mkoani Arusha, alimwagiwa sifa na baadhi ya wapinzani hao hao ambao Nape anadai wanaponda kila kitu.
Kile anachotafsiri Nape kwamba ni kuponda kila kitu, kwa hakika ni usikivu wa vyama vya upinzani kwa kero za wananchi na kisha kuziongelea hadharani. Sawa, ujenzi wa barabara ni moja ya ‘priorities’ zetu, lakini miundombinu bora kwenye jamii iliyogubikwa na ufisadi, ni sawa na kuwa na ndoo inayojazwa maji ilhali imetoboka.
Rais Kikwete anajenga, mafisadi wanabomoa, na pasipo kuwadhibiti mafisadi hao, ni wazi kwamba jitihada zake zitaishia kuwa moto wa karatasi tu.
Hoja ya nne ya Nape inanifanya nijiulize kama alikuwa anafanya utani mbaya au ni uthibitisho kwamba hata Katibu Mwenezi wa Taifa wa CCM haelewi chama chake kinafuata itikadi gani. Nape anaweza kuwa mjamaa, na anaweza kuwa anatamani chama chake kirejee kwenye itikadi hiyo, lakini haihitaji kuwa na uelewa wa siasa za nchi yetu kutambua kuwa CCM iliyokumbatiwa na mafisadi, si tu haifuati siasa za ujamaa, bali haiwezi kurejea kwenye itikadi hiyo kamwe.
Wakati Nape ana haki ya kulinganisha ‘mafanikio’ ya CCM na chama chochote kile (haki hiyo imebainishwa katika Katiba yetu: freedom of expression), ukweli ni kwamba kitakachokimaliza chama hicho tawala ni mitizamo kama hiyo fyongo ya Nape kuwa kelele za wapinzani ni zao binafsi na si vilio vya Watanzania.
Wakati niliweza kubashiri kwa usahihi ushindi wa Obama, ninachelea kufanya hivyo kwa uchaguzi wetu mkuu wa mwaka 2015 kuhusu nafasi ya wapinzani kuing’oa CCM. Hiyo si kwa sababu CCM ina mafanikio kama Obama na chama chake cha Democrats (yaliyopelekea kumbwaga Romney na Republicans kwa ujumla), bali ukweli kwamba upinzani una kazi kubwa ya kujiimarisha kati ya sasa na 2015 kama kweli una nia ya kuing’oa CCM, ambayo kimsingi inafanya kila jitihada kung’olewa madarakani haraka iwezekanavyo.


1 comment:

  1. Ludovick Chahally ndani ya Karlstad city and Jonkoping in Sweden.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.