28 Aug 2013


Majaji wanaowalinda wauza 'unga' wabainika

* Gazeti hili sasa limeamua kuwataja kwa majina
* Mahakimu nao wanawaachia mapapa kienyeji
* Kigogo ofisi ya DPP, Mahakama Temeke, Kinondoni balaa


Na Waandishi Wetu, Dar na Zanzibar
Mahakama kupitia baadhi ya majaji na mahakimu wasio waadilifu imebainika kuwa kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Pamoja na Mahakama, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), nayo imelaumiwa kwa kufuta kesi katika mazingira ambayo hata mtu ambaye hakusoma sheria, anaweza kuyatilia shaka. 
Wakati vyombo hivi vikikwamisha vita hii, lawama zimekuwa zikielekezwa kwa polisi na vyombo vingine vya usalama, ambavyo watendaji kazi wake wanafanya kazi usiku na mchana. 
Juhudi zote zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama zinagonga mwamba mahakamani kwa msaada wa ofisi hiyo ya DPP.
Wakati kesi nyingine zikifutwa, nyingine hazisikilizwi, kiasi cha kusababisha zirundikane mahakamani tangu mwaka 2005. Kesi chache zinazohusu watuhumiwa wakubwa wa kuuza ‘unga’ zinamalizwa haraka kwa utaratibu wa ofisi ya DPP kuwasilisha nia ya kutoendelea na mashtaka mahakamani (nolle prosequi) au wasimamizi hao wa utoaji haki kutoa hukumu zinazoacha wengi vinywa wazi na kuwakatisha tamaa polisi.
Katika hali ya kushangaza, majaji na mahakimu wamekuwa wakikiuka wazi Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya Na, 9 ya Mwaka 1995 inayozuia mtu yeyote aliyekamatwa na dawa zenye thamani kuanzia Sh milioni 10 asipewe dhamana, lakini hilo halizingatiwi. JAMHURI haikubahatika kufahamu bayana nini kinawapofusha majaji na mahakimu wakati ‘mapapa’ wanapofikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuuza unga, lakini ni wazi kuwa kuna mtandao mkubwa wa kulindwa kwa watuhumiwa hao wenye ukwasi mkubwa.
Wakati polisi wanafanya kazi ya hatari usiku muda wote, wakipambana na wauaji, wahongaji na watu wanaouza dawa za kulevya, kesi za mapapa zinamalizwa kienyeji mahakamani.
Moja ya kesi inayotia shaka ni Na. 47 ya Mwaka 2011. Kesi hii ilifunguliwa dhidi ya watuhumiwa Fredy William Chonde, Kambi Zuberi Seif; ambao ni Watanzania na Abdulghan Peer Bux na Shaaban Malik ambao ni raia wa Pakistani.
Hawa walikamatwa eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam wakiwa na kilo 175 za heroin, ambako kesi dhidi yao ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini humo. Wakati kesi inaendelea Kisutu, mawakili wa vigogo hawa walikwenda Mahakama Kuu wakafungua shauri la kuomba wapewe dhamana chini ya Jaji Pendo Msuya, wakitambua kuwa sheria inazuia.
Bila kuchukua jalada wala kuwasiliana na Mahakama ya Kisutu, huku Jaji Msuya akijua fika kuwa kilo 175 ambazo thamani yake ni zaidi ya Sh bilioni tano, na watuhumiwa hawapaswi kupewa dhamana; yeye kwa mamlaka aliyonayo kama Jaji aliamua kuwapa dhamana watuhumiwa hawa. Baada ya kupata dhamana, Wapakistani walirejeshewa pasipoti zao na wakakimbia nchi. Hawajakamatwa hadi leo.
“Cha kusikitisha kesi iliendelea bila kujua kuwa watuhumiwa wamekwishapewa dhamana na hadi Aprili 8, mwaka huu 2013 kesi hiyo ilitajwa… baadaye Mahakama ikapewa taarifa kuwa watuhumiwa walishapewa dhamana na Mahakama Kuu ndiyo maana hawaonekani mahakamani. Tulishangaa sana,” kilisema chanzo chetu kutoka Mahakama ya Kisutu.
Kesi nyingine iliyomalizwa kienyeji ni ya Mwinyi Rashid Mkoko. Vyanzo vya JAMHURI vinaonesha kuwa huyu na familia karibu yote wanatuhumiwa kufanya biashara ya dawa za kulevya. Ndugu zake waliokamatwa kwa nyakati tofauti na baba yao, ambako mmoja alidhulumiana, na ‘mzigo’ na wauza unga, hali iliyofanya wamuue kwa kumpiga risasi.
Katika familia hii, Rashid Ismail Mkoko ndiye aliyeuawa na wauza unga wenzake eneo la Ilala, Dar es Salaam. Huyu alipata kukamatwa kuhusiana na dawa za kulevya, ila pia kwa kosa la mauaji. Shuhuda wa tukio la Rashid Ismail Mkoko anasimulia kama ifuatavyo:“Huyu ndiye wa kesi ile ambayo kijana aliyemtuma mzigo Pakistan pipi zilipasukia tumboni akafia gesti kule Tabata, Dar es Salaam. Mmoja wa ndugu wa kijana huyu aliyefariki, alimpigia simu akamwambia ‘si unajua alikuwa na mzigo wako ndiyo umemuua? Sasa mbona umetususa? Hata maji ya kunywa hutupatii msibani?’
“Mkoko akamwambia nitakuja jioni. Na kweli jioni iliyofuata akampigia simu kuwa anakwenda hapo nyumbani msibani. Alipofika akampigia simu, akamwambia njoo tuonane. Huyu ndugu wa kijana aliyefariki akatoka nje, akaenda kwenye gari kuonana na Mkoko.“Alipofika Mkoko akamuuliza ndiye wewe uliyenipigia simu jana, yule ndugu wa marehemu akajibu ‘ndiyo’, basi Mkoko alichofanya akatoa bastola akampiga risasi ya usoni yule kijana…akafariki papo hapo, Mkoko akaondoka.

“Polisi walimkamata wakamfikisha mahakamani. Mahakama ikamwachia kwa mizengwe. Ila Mungu si Athumani, ikatokea naye akadhulumu wauza unga wenzake huko Ilala, nao wakamuwinda wakampiga risasi akafa mwaka juzi.
“Huyu alikuwa muuza dawa za kulevya mkubwa. Mdogo wake Mwinyi Rashid Mkoko, naye anauza dawa. Tulimkamata na heroin gramu 250 zenye thamani ya Sh milioni 11, ikafunguliwa kesi Temeke Na. PI 26 chini ya Hakimu Mkwawa, lakini ajabu wakati kesi inaendelea kutajwa Temeke hadi leo, huyu Mwinyi Mahakama Kuu imekwishamwachia huru bila vielelezo vyovyote,” kilisema chanzo chetu kutoka mahakamani.Uchunguzi wa JAMHURI umeonesha kuwa awali mawakili wa Mwinyi waliwasilisha ombi la dhamana kwa Jaji Munisi, ambaye aliwaelekeza mawakili wa Serikali kuwa badala ya kumshtaki Mwinyi kwa kukutwa na dawa za kulevya, waiondoe kesi mahakamani na kuifungua upya kama kesi ya kusafirisha dawa za kulevya. Kwa kawaida tuhuma za aina hiyo huwa hazina dhamana.Mawakili walivyopata mwanya huo, wanajua jinsi walivyozungumza na wanasheria wa Serikali. Kesi hiyo badala ya kuiondoa kama alivyoelekeza Jaji Munisi wakaihamishia kwa Jaji Dk. Fauz Twalib, ambaye katika hukumu yake ya Julai 30, 2012 alikiri kuwa mbele yake halikufikishwa jalada la kesi hiyo na wala hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza kwani yeye si hakimu, ila akasema kwa kuwa Mahakama ya Temeke haina mamlaka ya kusikiliza kezi za dawa za kulevya kama cocaine, basi akatoa fursa ya kumsikiliza mtuhumiwa.“Kwa kasi ya aina yake, siku hiyo hiyo ya Julai 30, 2012 baada ya Jaji Dk. Fauz kutoa hukumu hiyo ya ajabu, mawakili wa Serikali ambao ni upande wa mashitaka wakawasilisha nolle chini ya Section 91 ya CPA (Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka), hivyo Mwanasheria wa Serikali Mpembo kwa niaba ya DPP akawasilisha hati hiyo, na Jaji Fauz akaifuta kesi dhidi ya Mwinyi.“Kisichoeleweka na kufahamika ni nini kilitokea na nini kiliendelea siku hiyo hiyo kutoa hukumu, na siku hiyo hiyo Mpembo akawasilisha nolle na kesi ikafutwa siku hiyo hiyo. Hapa kuna maswali mengi. Mwinyi amekimbilia Zanzibar. Yupo anaponda raha, kesi bado ipo Temeke na hakuna kinachoendelea,” kimesema chanzo chetu.Baba yao Mwinyi na Rashid, naye kwa nyakati tofauti anadaiwa kukamatwa na polisi akituhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Mtoto wake mwingine, Abubakar Mkoko, yeye alitolewa dawa za kulevya tumboni, lakini Mahakama ikampiga faini ya Sh milioni 1 na kumwachia huru.Kesi nyingine inayowakosesha usingizi polisi ni ile ya Dhoulkefly Awadh Abdallah Na. 238 ya Mwaka 2010. Kesi hii ilimhusisha Abdallah na mkewe Asha Seif Kiluvya. Asha ndiye aliyekamatwa na dawa za kulevya. Hata hivyo, katika mazingira ya kutatanisha, ofisi ya DPP ilipeleka nolle prosequi mahakamani Asha akaachiwa huru, na sasa anashitakiwa Abdallah ambaye hakukutwa na kitu chochote.Kioja kinginge kilifanywa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kinondoni anayetajwa kwa jina la Msongo. Kesi hii ilianza mwaka 2005 na kumalizika mwaka 2008. Mshitakiwa alikuwa Yusufu Hassan Yossye, mkazi wa Kinondoni A, Mtaa wa Togo, aliyekutwa na gramu 1,244 za heroin ambazo alikamatwa nazo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Aliwekwa chini ya ulinzi kwa lengo la kumfanya atoe ‘pipi’ kwa njia ya haja kubwa. Katika hukumu ambayo inatia shaka Hakimu Msongo aliandika hivi:“Katika ushahidi wote uliotolewa, hakuna ubishi kuwa ni kweli amekutwa na dawa za kulevya. Pia ushahidi unaonesha kuwa mshitakiwa alitoa madawa hayo kwa njia ya haja kubwa. Hata hivyo, upande wa mashitaka umeshindwa kueleza ni dalili zipi zilipelekea (zilisababisha) kushukiwa kuwa mshitakiwa ana madawa ya kulevya. Na pia hawakushirikishwa watu au wataalamu wa afya ya binadamu.“Upande wa mashitaka katika ushahidi wao umeonesha walipishana kutoa idadi [ya pipi alizotoa kwa haja kubwa]. Kutokana na hilo, ushahidi hautoshelezi na mshitakiwa namwachia chini ya Kifungu cha 235 cha CPA (Kanuni ya Mwenendo wa Mashitaka) katika mashitaka yote mawili.” Hukumu hii ilitolewa na Hakimu Msongo Mei 2, 2008. Yossye alikuwa akishitakiwa kwa kukutwa na dawa; na pia kwa kuwaambia polisi uongo kuwa hakuwa na dawa, lakini baadaye akazitoa kwa njia ya haja kubwa.Katika Mahakama ya Kisutu, mwanamke mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Pilly, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa na zawadi ya kinyago ambacho ndani yake kilikutwa na dawa za kulevya, lakini Mahakama ya Kisutu wakati inatoa taarifa ilimwachia huru Pilly kwa maelezo kuwa wakati polisi wanamkamata, hakuwapo mwanamke, hivyo ni kosa mhalifu mwanamke kukamatwa na polisi mwanaume. Akaachiwa huru!
Kesi nyingine ni ya Kwaku Sarfo, raia wa Ghana, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere mnamo Novemba 14, 2010. Thamani ya dawa ilikuwa Sh milioni 390. Kesi ilipelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Samora kwa Hakimu Mkazi Luago.“Tulishangaa, kwamba kwanza Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi hii, lakini pia baada ya kupita siku 60; bila mamlaka kisheria, Hakimu Luago akaifuta. Hakimu huyu ni kero. Amehamishiwa Lindi akagoma kwenda. Hatujui anapewa jeuri na nani. Tungeomba Rais Kikwete na mhimili wa Mahakama waingilie kati suala hili vinginevyo nchi inateketea,” kimesema chanzo chetu.Uchunguzi umebaini kuwa kati ya kesi 423 zilizofikishwa Mahakama Kuu kati ya mwaka 2005 na 2013 hadi leo kesi iliyokwisha ni moja tu ya Shaaban Mintanga, ambayo nayo imeisha kutokana na mashahidi muhimu kufariki dunia kabla kesi haijasikilizwa. Kati ya mashahidi waliofariki dunia ni Mkemia Mkuu, Dk. Ernest Mashimba, aliyefariki Septemba 2010.
Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alikiri matukio hayo kuwapo na akasema: “Mimi mamlaka yangu ni kukamata, na kuwafikisha mahakamani. Sasa huko kama mmekuta hali iko hivyo, ambayo ni kweli kimsingi inasikitisha na kukatisha tamaa, inabidi muwaulize huko mahakamani au kwa DPP wao ndiyo waeleze nini kinatokea.”
JAMHURI haikufanikiwa kuzungumza na Msajili wa Mahakama Kuu kwani mara zote kila mwandishi wetu alipofika aliambiwa yuko kwenye vikao kwa wiki nzima, na hata alipoacha ujumbe wa maandishi haukujibiwa.
Baada ya juhudi za kumpata Msajili wa Mahakama Kuu kugonga mwamba, JAMHURI iliwasiliana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, ambaye Kamisheni ya Dawa za Kulevya iko chini yake. Yeye alisema ni kweli tatizo hilo lipo, na kwamba kuna mengi zaidi ya hayo.
“Mimi nasema sheria zinapaswa kubadilishwa, na Serikali tayari imeanza mchakato. Mtu akipatikana na pipi za dawa za kulevya zikatolewa tumboni mwake, nataka sheria irahisishwe na kuwezesha ashitakiwe na kufungwa maisha ndani ya siku saba.
“Hali ilivyo sasa ambapo unapaswa kuhifadhi ushahidi kwa miaka hadi 10 ukiendesha kesi moja, ushahidi unapoteza ubora. Wakati mwingine mtuhumiwa anashindwa kesi anatozwa faini ya Sh 500,000. Hatuwezi kupambana na dawa za kulevya tukashinda vita hii kwa utaratibu huo.
“Sasa Serikali imejipanga, ipo kwenye mchakato wa kuanzisha mahakama maalum ya kudhibiti dawa za kulevya na kwa kweli katika hili tunataka mchakato uwe mfupi kadiri inavyowezekana. Ndani ya muda mfupi kadiri inavyowezekana tupitishe sheria hii ili sheria iwe kali itoe adhabu itakayowazuia wengine kufanya biashara hii,” alisema Lukuvi.
Hivi karibuni, Tanzania imeanza kuzungukwa na sura ya kuwa Taifa la wauza dawa za kulevya baada ya Watanzania wengi kukamatwa ndani na nje ya nchi wakiwa na dawa hizo. Taarifa za uhakika zilizoifikia JAMHURI zinasema Rais Jakaya Kikwete ametoa maelekezo ya dhati kuhakikisha linafanyika jambo kubwa litakalowezesha kukamata mtandao wa wauza dawa za kulevya na kumaliza tatizo hili nchini.
Kwa mwezi mmoja sasa, JAMHURI imekuwa ikichapisha orodha ya wauza unga ‘dagaa’ na ‘mapapa’ hapa nchini, ambako hadi sasa gazeti hili limekwishatangaza

hadharani majina ya wauza unga 504 katika matoleo manne yaliyotangulia.
CHANZO: Jarida la Jamuhuri

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube