4 Nov 2013



Makala hii iliandikwa kwa minajili ya kuchapishwa katika jarida la Raia Mwema toleo la Oktoba 23. Hata hivyo haikuchapishwa kwa madai kuwa ilikuwa inapromoti msanii Fid Q na wimbo wake mpya wa Siri ya Mchezo. Whether uamuzi wa jarida hilo ni sahihi au la, nimeonelea ni vema kuichapisha makala hiyo hapa bloguni

MAKALA YA RAIA MWEMA TOLEO LA OKTOBA 23, 2013

Nianze makala hii kwa kuomba radhi kutokana na kuadimika kwangu katika toleo lililopita. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Uandishi wa makala zangu umekuwa sehemu muhimu ya maisha yangu, na pindi ikipita wiki pasi kuandika chochote (kama ilivyokuwa wiki iliyopita) huwa najisikia kama nimepungukiwa na kitu flani.

Pamoja na kiu yangu kubwa ya kuhamasisha mijadala mbalimbali, kukemea maovu na hata kuhabarishana tu, moja ya hamasa kubwa zinazonifanya niendelee na jukumu hili ni mapokeo ya wasomaji mbalimbali.

Na wiki iliyopita nilipata hamasa kubwa kutoka kwa msanii maarufu wa muziki wa Bongofleva, Fareed Kubanda, au 'Fid Q' kwa jina la kisanii.
Msanii huyo ametoa kibao chake kipya kinachofahamika kama ‘Siri ya Mchezo’ (unaweza kukisikiliza na kusoma mashairi yake hapa). Kilichonivutia kuhusu wimbo huo ni ujumbe mzito wa kisiasa, ambapo ni kitu adimu kwa wasanii wetu kuzungumzia masuala ya kisiasa kwenye tungo zao.

Niliongea na Fid Q kwa kutumia mtandao wa kijamii wa Twitter, ambapo pamoja na mambo mengine alinieleza kitu kimoja kilichonigusa sana. Namnukuu, “Believe or not, nilijaribu kujivisha viatu vyako wakati ninaandika hii track.”

Ni nani hatofarijika kuambiwa na msanii mwenye jina kubwa kama Fid Q kuwa alipata hamasa kutoka kwao wakati anaandika mashairi ya wimbo ambao kwa hakika utavuma?

Lakini licha ya hamasa, furaha na heshima hiyo kutoka kwa msanii huyo, kuna kitu cha ziada ambacho kimsingi ndicho kinabeba dhima ya makala hii: nafasi ya wasanii wetu katika kuhamasisha mabadiliko chanya kwa jamii.

Kwa muda mrefu wasanii wetu, hususan wa muziki ‘wa kizazi kipya’ (Bongofleva) wamekuwa wakilaumiwa kwa aidha kutumika vibaya na wanasiasa au kutotilia maanani matatizo mbalimbali yanayoikabili Tanzania yetu.

Imezoeleka kwamba ukifika wakati wa uchaguzi ndipo wanasiasa wetu hukumbuka kuwa kuna vijana wanaendesha maisha kwa kujishughulisha na sanaa ya muziki. Kama ilivyo kwa makundi mengine ya jamii, wanasiasa hao pasi haya huwavuta karibu wasanii na kisha kuwatumia kwenye kampeni zao. Wakishapata madaraka, wanawatelekeza kama inavyotokea kwa wengi wa wapigakura majimboni.

Lakini wakati ni rahisi kuwalaumu wasanii kwa kile kinachotafsiriwa na wengi kama ‘kutojali matatizo yanayoikabili Tanzania yetu,’ Fid Q alinieleza kuwa tatizo mojawapo ni ukiritimba wa vyombo vya habari ‘vya asili’ (yaani traditional media, kwa maana ya radio, televisheni na magazeti). Sio siri kwamba wamiliki wa vyombo hivyo huchelea sana kuwaudhi watawala kiasi kwamba si ajabu kwa wimbo unaokemea maovu flani yanayowahusu watawala ukanyimwa fursa radioni au kwenye runinga.

Tukirejea kwenye wimbo huo wa Siri ya Mchezo, yayumkinika kubashiri kuwa Fid Q anafungua mlango wa kile kinachofahamika kimuziki kama ‘political rap’ yaani muziki wa kufokafoka uliobeba ujumbe wa kisiasa. Aina hiyo ya muziki ilikuwa maarufu sana huko Marekani kwenye miaka ya 1970 hadi 1980, ambapo ulilenga kuzungumzia masuala mbalimbali ya kisiasa na kijamii. Kimsingi, muziki huo ulikuwa ni kama nyenzo ya wasanii kupambana na udhalimu, sambamba na kuhamasisha jamii, hususan vijana, kushiriki katika harakati za kujenga jamii bora.

Katika wimbo huo, Fid Q anamkumbuka mmoja wa wasomi lulu kwa taifa letu, marehemu Profesa Chachage Chachage ambaye wakati wa uhai wake alijitahidi sana kutuelimisha kuhusu soko huria na athari zake. Kadhalika, msanii huyo anasononeka kuhusu hatma ya taifa letu akidadisi “tutarithi nini...” katika zama hizi ambapo utajiri wetu unanufaisha wachache (hususan wageni na vibaraka wao) huku mamilioni ya Watanzania wakibaki masikini.

Kadhalika, msanii huyo anawanyooshea kidole wahujumu wa uchumi, kabla ya kutoa angalizo muhimu kuwa “taifa la kondoo huendeshwa na serikali ya dubu/mbwa mwitu wenye siri...

Vilevile, Fid Q anatahadharisha kuhusu siasa inavyotumika kama kitega uchumi, na kusikitishwa na jinsi ukoloni mamboleo ulivyotupatia uhuru wa bendera huku ukituonyesha “kufuru za wenye hela.”

Katika lugha ya kisanii, msanii huyo analalamika kuwa Tanzania imegeuka kama mwanamke asiyefuata maadili, ‘anayetembea’ na kila mtu, mpaka wanamwita “cha wote,” na ambaye anatumia pombe kama njia ya kukimbiza matatizo yake. Kimsingi, hapa anazungumzia jinsi nchi yetu ilivyogeuka ‘shamba la bibi’ ambapo kila mwenye ‘fursa’ anajichumia.

Msanii huyo anakwenda mbali zaidi na kukemea dhana kuwa wawekezaji wa kigeni watatuletea maendeleo, na anasema “maendeleo ni ndoto, ile mwekezaji ashaipuuza,” na kutahadharisha kwamba uwepo wa wawekezaji hautufanyi tufikie viwango vya maendeleo katika nchi zao, akihoji “je kukaa karibu na moto ni kuota au kujiunguza?”

Fid Q pia anazilaumu taasisi za kisiasa kwa ‘kuwafelisha’ wananchi, kama ambavyo tunashuhudia vyama vyetu vya kisiasa vikiwa ‘bize’ kulumbana huku walalahoi wakizidi kutaabika.

Pia anakumbusha kuwa “hakuna utumwa mbaya kama kujiona uko huru” na kutahadharisha kuwa jitihada za kusaka ukweli zitakumbwa na vizingiti, akisema, “Kuusaka ukweli  ni  sawa na kumenya kitunguu/
kila ganda litakutoa machozi na utabaki macho juu/
Ukishafika kwenye kiini  niambie nini utagundua.
.?”

Anahitimisha tungo hiyo aliyomshirikisha msanii mwingine maarufu Juma Nature kwa kutahadharisha kuhusu wanasiasa matapeli ambao “wamejivisha u-Noah, safina zao zikatoboka; wakajivisha u-Mussa, fimbo zao hazikugeuka nyoka; sasa wamejivisha u-Mungu mtu...” Kadri tunavyoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 tutashuhudia kila aina ya utapeli wa kisiasa ambapo baadhi ya wanaosaka urais wataahidi mambo ambayo hata wenyewe hawayaamini.

Lengo la makala hii sio kuchambua wimbo huo bali kupigia mstari umuhimu wa alichofanya msanii Fid Q kutumia kipaji chake cha muziki kuuzindua umma hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa kupata Katiba mpya, sambamba na hekaheka za uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Nimalizie makala hii kwa kumpongeza msanii huyo, na kutoa wito kwa kila Mtanzania kutumia nafasi aliyonayo kuwa chachu ya mabadiliko stahili kwa nchi yetu. Hatuwezi kuendelea kuwa watu wa kulalamika tu ilhali tuna uwezo wa kubadilisha yote yanayokwaza ustawi wa taifa letu.


Inawezekana, timiza wajibu wako

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.