1 Feb 2014

MOJA ya matukio makubwa duniani yaliyojiri wiki iliyopita ni kongamano la uchumi lililofanyika huko Davos, Uswizi. Kongamano hilo la kila mwaka huwakutanisha wadau mbalimbali wa uchumi wa dunia. Rais Jakaya Kikwete amekuwa akihudhuria takriban kila mwaka.
Kati ya yaliyojitokeza katika kongamano hilo ni 'ndoto' ya binadamu tajiri kabisa duniani, Bill Gates, ambaye alidai kuwa anatarajia itakapofika mwaka 2030, miaka 16 kutoka sasa, dunia haitakuwa na nchi masikini hata moja.
Kwanza ni muhimu kutambua mchango wa bilionea huyo katika miradi na misaada mbalimbali kwa nchi masikini kama yetu. Akishirikiana na mkewe, Melinda, kupitia taasisi yao ya Bill and Melinda Gates Foundation, wamefanya mengi mazuri kiasi kwamba makala hii haitoshi kuyaorodhesha yote. Kwa kifupi, tajiri huyu amekuwa akiutumia utajiri wake kuwasaidia wasiojiweza huku akiamini kwa dhati kuwa kuna siku umasikini utakuwa historia.
Kinachompa Bill Gates matumaini kuwa takriban muongo mmoja na nusu kutoka sasa dunia haitakuwa na nchi masikini ni kile kile ambacho Watanzania wengi hushindwa kukielewa, takwimu za uchumi. Tajiri huyo anadai kuwa takwimu zilizopo zinaonyesha maendeleo ya kuridhisha kwa nchi masikini.
Kwa huko nyumbani, mara kadhaa wananchi hushindwa kuamini kama viongozi wao ni 'wazima' au wapo ndotoni wanapoelezea kukua kwa uchumi ilhali hali ya maisha ikizidi kuwa ngumu. Tatizo la viongozi wetu, na pengine kwa Bill Gates pia, ni kuzifanya takwimu kuwa sawa na watu. Ndio, takwimu hizo hutokana na vigezo fulani vinavyohusisha watu lakini hiyo haina maana kwamba takwimu ni watu. Namba ni namba na watu ni watu.
Japokuwa nami ni 'mchovu' (dhaifu) linapokuja suala lolote linalohusiana na namba, ikiwa ni pamoja na takwimu, miongoni mwa machache ninayoyaelewa ni kwamba takwimu nyingi huwa kiwakilishi tu cha hali halisi.
Nitoe mfano halisi, ni rahisi kuhitimisha kuwa Tanzania imepiga hatua kimaendeleo kwa kuhesabu idadi ya magari yanayosababisha foleni jijini Dar es Salaam. Na huko nyuma, Rais Kikwete aliwahi kunukuliwa akijigamba kuwa foleni kubwa za magari barabarani jijini Dar es Salaam ni uthibitisho wa maisha bora kwa Mtanzania. Tatizo ni kwamba asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi maeneo ya vijijini, ambapo kwa baadhi ya maeneo, magari sio tu ni anasa wanayomudu wachache bali pia ni ndoto kuyamiliki.
Kwa hiyo, pengine Jiji la Dar es Salaam licha ya kupiga hatua katika idadi ya magari na majengo ya kuvutia, sio kiwakilishi kizuri cha hali halisi ya Watanzania walio wengi wanaoishi vijijini. Na japo kuna jitihada za kuleta matumaini zinazofanywa na viongozi wetu kuhamasisha maendeleo maeneo ya vijijini, ukweli ni kwamba kuna tofauti kubwa kati ya maisha ya mijini na vijijini.
Kila linapofanyika kongamano hilo la Davos, wachambuzi mbalimbali wa uchumi wa dunia wamekuwa wakihoji ufanisi wake katika kuzinusuru nchi masikini, hususan za Afrika. Kimsingi, moja ya ajenda kubwa za kongamano hilo ni misaada kwa nchi masikini. Yayumkinika kuhitimisha kuwa misaada inaonekana kama mwarobaini wa tatizo la umasikini kwa nchi masikini.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanakwenda mbali zaidi na kuhoji kuhusu hao 'wenye roho nzuri' wanaohamasisha misaada kwa nchi masikini. Kimsingi, kongamano la Davos linatafsiriwa na baadhi ya wachambuzi kama sehemu muhimu kwa matajiri kukutana na fursa mpya za kupanua biashara zao kwa mgongo wa misaada. Kwamba ninakupa msaada wa magari ili nipate soko la viwanda vyangu vya vipuri za magari.
Lakini hata tukiangalia wasifu wa 'manabii wa kupambana na umasikini kwa njia ya misaada,' baadhi yao ni wakwepa kodi katika nchi zao, kwa kuficha fedha zao kwenye 'mbingu za kodi' (tax havens) au katika offshore accounts.
Uingereza ni moja ya mataifa yanayoongoza duniani kwa kutoa misaada, na Waziri Mkuu Donald Cameron, amekuwa akishutumiwa vikali hususan na wenzake katika chama tawala cha wahafidhina (Conservative Party), kwamba asilimia kubwa ya misaada hiyo inaishia katika akaunti za watawala wabadhirifu katika nchi masikini.
Na kwa hakika kama kuna jambo moja ninashindwa kabisa kuwaelewa hawa 'wazungu' ni jinsi wanavyomwaga fedha zao kama misaada kwa nchi masikini lakini hawasumbuliwi na jinsi sehemu kubwa tu ya misaada hiyo inavyotumika kinyume cha malengo na matarajio.
Hivi inaingia akilini kweli kuona msafara wa kiongozi wa nchi tajiri ukiwa na magari machache ya 'bei ya kawaida' huku ule wa kiongozi wa nchi masikini ukisheheni magari lukuki ya thamani kubwa kabisa? Yaani kwa haraka haraka unaweza kudhani 'tajiri ndiye masikini na masikini ndiye tajiri' kwa kuangalia tofauti ya 'lifestyles' zao.
Tukirejea kwenye dhana ya misaada kama mwarobaini wa tatizo la umasikini, ni wazi kuwa nchi tajiri zitaendelea kumwaga misaada na japo sehemu fulani ya misaada hiyo itatumika kama wanavyotaka watoa misaada, kiwango kikubwa kitaishia kwenye akaunti za mafisadi, kuongeza idadi ya magari na mahekalu yao ya thamani, pasi kusahau udhaifu wao mkubwa, yaani kuongeza idadi ya 'nyumba ndogo' zao.
Akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha New York, Marekani, Cameron alisema jambo la muhimu si kiwango (quantity) cha misaada bali kile alichokiita 'kamba ya dhahabu', akimaanisha kwamba maendeleo yatapatikana tu kwa kamba ya dhahabu inayounganisha serikali imara, kutokuwepo ufisadi, uwepo wa haki za binadamu, utawala wa sheria na taarifa za wazi.
Na alichotanabaisha Waziri Mkuu huyo wa Uingereza sio sayansi ya roketi (rocket science) kwani hata katika mazingira ya kawaida tu, ukimpatia msaada wa fedha mtu ambaye mara tu baada ya kupata fedha hizo anakwenda baa kunywa pombe, ni wazi msaada huo hautoleta matokeo yanayokusudiwa. Ni sawa na kujaza maji kwenye pipa lililotoboka.
Majuzi nimesoma gazeti moja lenye habari kuwa Rais Kikwete ameiomba Uingereza msaada wa mabehewa mitumba. Sawa, sisi ni masikini kwa hiyo inatulazimu wakati mwingine tuishi kwa kutegemea misaada. Lakini tuwe wa kweli, hivi kama tulishindwa kuyamudu mabehewa yetu wenyewe katika reli ya kati na Tazara, miujiza gani itayafanya mabehewa hayo 'ya bure' kutoka kwa Waingereza yasalimike?
Inaweza kuonekana kama mzaha lakini sitashangaa kusikia Mwingereza katuletea mabehewa lakini miezi kama si wiki chache baadaye, viti vya mabehewa hayo vimeng'olewa na kugeuzwa viti katika 'pub' ya kigogo fulani (kwa taarifa yako msomaji mpendwa, viti katika nyingi ya treni za hapa ni kama vya kwenye ndege, ukikaa unatamani safari isifike kikomo).
Nihitimishe makala hii kwa kusisitiza kwamba mimi si mpinzani wa misaada kwa nchi masikini kama Tanzania lakini ningependa kuona misaada hiyo ikizaa matunda yanayokusudiwa. Ni muhimu kwa nchi na taasisi wahisani wakaanzisha mkakati wa makusudi wa kusisitiza, na ikibidi kulazimisha, udhibiti dhidi ya majambazi wanaodhulumu wananchi wenzao kwa kuchota misaada ya wafadhili kwa manufaa yao binafsi. Ni suala la akili tu, vinginevyo uwe na fedha za kuchezea, unapotoa msaada unalazimika kufuatilia ili kuona unakidhi malengo yaliyokusudiwa.
Na kwa akina sisi ambao 'tumelemazwa kwa misaada,' ni muhimu kutambua kuwa japo Bill Gates 'anaota' kwamba mwaka 2030 dunia haitakuwa na nchi masikini, kuna uwezekano mkubwa katika miaka michache tu ijayo, nchi na mashirika wahisani wakapunguza misaada yao kwetu kutokana na mtikisiko wa uchumi wa dunia, ambao hauonyeshi dalili ya kuondoka hivi karibuni.
Tukiendelea na matumizi ya anasa, usimamizi mbovu na ufisadi katika rasilimali zetu, sambamba na kutojijengea uwezo wa kujitegemea wenyewe badala yake kutumaini misaada, tunaweza kuumbuka huko mbele.
Penye nia pana njia.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube