26 Jun 2014

Serikali imetangaza  kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa MAJENEZA
KWA kila anayefuatilia makala zangu kwa karibu hatashindwa kubaini kuwa moja ya vyanzo vya mada za makala hizo ni kwenye mijadala mbalimbali ya mitandao ya kijamii, hususan twitter. Mara kadhaa nimekuwa nikipata cha kuandika katika makala hizi kutokana na mijadala hiyo inayohusu masuala mbalimbali.
Na kwa hakika, mitandao ya kijamii imekuwa na umuhimu wa kipekee kwangu hasa katika jitihada zangu za kukuza uelewa nje ya mazingira ya kitaaluma. Lakini pengine faida kubwa zaidi imekuwa katika kutengeneza marafiki muhimu kutoka nyanja mbalimbali za maisha. Nimefahamiana na wanasiasa, wasanii, wasomi, wanahabari na wengineo. Wakati kwa bahati mbaya au makusudi, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii huko nyumbani (Tanzania) wameigeuza kuwa sehemu za kutafutia umaarufu kama sio kuwabughudhi wenzao, kwangu mitandao hiyo imekuwa fursa ya kutengeneza ‘mduara wa watu muhimu’ sambamba na ‘kisima cha kuchota elimu ya bure.’
Lengo la makala hii sio kuzungumzia umuhimu wa mitandao ya kijamii japo ningependa kuwahamasisha ‘wanaoikwepa’ watumie hamasa hii kuijaribu, na nina uhakika wataafikiana nami juu ya umuhimu wake. Makala hii inalenga kuzungumzia kinachoendelea huko Mashariki ya Kati, hususan nchini Iraq.
Nimeanza makala hii na umuhimu wa mitandao ya kijamii kwa sababu majuzi nilifanya maongezi na dada mmoja ambaye kwa asili ni Mkenya lakini ameishi sehemu mbalimbali duniani kutokana na wazazi wake kuwa wanadiplomasia. Nilifahamiana naye huko twitter hasa baada ya kuvutiwa na ‘tweets’ zake kuhusu masuala mbalimbali ya kimataifa. Kumbe pasi kufahamu, naye pia alikuwa akiguswa na ‘kelele’ zangu kuhusu maovu mbalimbali yanayoikabili Tanzania yetu.
Binti huyo ana uelewa mkubwa kuhusu siasa za Mashariki ya Kati, na kwa hakika ‘darasa’ alilonipatia kuhusu mapigano  yanayoendelea nchini Iraq kati ya waumini wa madhehebu ya Sunni na Shia lilinifungua upeo wangu zaidi ya nilivyokuwa nikielewa kupitia vyanzo vingine mbalimbali. Kikubwa zaidi, aliweza kwa ufanisi mkubwa kunifahamisha madhara ya kinachoendelea katika eneo hilo la Mashariki ya Kati na athari zake kwa nchi za Afrika Mashariki, hasa kwa sababu, kwa mujibu wa uelewa wake, uhusiano wa kidiplomasia kati ya baadhi ya mataifa ya eneo hilo na nchi za Afrika Mashariki umekuwa wa kimkakati (strategic) zaidi kuliko tunavyodhani (nitaongelea suala hili katika makala zijazo).
Lakini kubwa zaidi ni mjadala wetu kuhusu chanzo cha ukosefu wa amani nchi Iraq na jinsi kinachotokea huko kinavyoweza kulinganishwa na hali ilivyo katika nchi zetu, Kenya kwake na Tanzania kwangu.
Kwa mujibu wa taarifa za kiintelijensia za Marekani, Waziri Mkuu wa Iraq, Nouri al-Maliki, alikwishaonywa miaka miwili iliyopita kuhusu hisia miongoni mwa waumini wa madhehebu ya Sunni nchini humo kuwa wanatengwa. Hata hivyo, si Maliki wala serikali yake waliochukua hatua stahili kushughulikia tatizo hilo. Kimsingi, kuna lawama kadhaa zinazoelekezwa kwa Serikali ya Maliki kwa kushindwa kwake kujifunza kuhusu siasa za upatanishi (reconciliatory politics) kati ya Watutsi na Wahutu nchini Rwanda na Weusi na Makaburu nchi Afrika Kusini.
Miaka michache iliyopita nilipokuja huko nyumbani kwa ajili ya utafiti wa vitendo (fieldwork) kuchunguza kuibuka kwa ‘Uislamu wa msimamo mkali’ nchini Tanzania, moja ya hoja iliyojitokeza mara kwa mara ni hisia miongoni mwa Waislamu wengi kwamba wanatengwa. Nilizungumzia suala hili katika makala zilizopita lakini kwa sasa nadhani kuna umuhimu wa kuliangalia kwa kurejea kinachojiri nchini Iraq.
Kimsingi hisia hizo za kutengwa ni zaidi ya miongoni mwa baadhi ya Waislamu pekee. Hebu msomaji mpendwa angalia tofauti kati ya mbunge anayelipwa zaidi ya shilingi milioni 10 kwa mwezi na mlalahoi ambaye hana uhakika wa mlo wake wa siku inayofuatia. Unaweza pia kuangalia sekta ya afya ambapo watawala wetu wakipatwa na mafua tu wanakwenda ng’ambo kuangalia afya zao ilhali inafahamika kuwa hali ni mbaya sana katika takriban kila hospitali zetu.
Kilichonisukuma zaidi kuzungumzia suala hili ni taarifa kwamba katika jitihada zake za kuongeza mapato kwa ajili ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha, Serikali imeanzisha kodi ya nyongeza ya thamani (VAT) kwenye majeneza. Hivi kweli Serikali yetu imeishiwa kabisa mbinu za kukusanya mapato hadi ifikie hatua ya kukifanya kifo kiwe ghali kiasi hicho?
Ndio, tatizo la waumini wa madhehebu ya Shia na Sunni nchini Iraq ni la kidini zaidi, lakini ukweli unabaki kuwa uwepo wa hisia za kubaguliwa, kutengwa, kunyanyaswa au kupuuzwa na watawala kunaweza kuzua balaa kubwa katika nchi husika.
Ikumbukwe kuwa pamoja na kuandamwa na tuhuma kuhusu ufisadi wa kampuni ‘feki’ ya Richmond kulikosababisha kujiuzulu, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amekuwa akikumbushia mara kwa mara kuhusu kile Anachokiita ‘bomu la wakati,’ yaani tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana. La muhimu hapa sio kama ‘kelele’ zake ni za uchungu wa dhati au anasaka tu ‘kura za vijana,’ bali ukweli kwamba ukosefu wa ajira ni tatizo ambalo lisipopatiwa ufumbuzi wa haraka linaweza kuzua matatizo makubwa huko nyumbani.
Ninachojaribu kubainisha hapa ni jinsi mazingira ya baadhi ya wananchi kuhisi wanatengwa yanavyojengeka kama ilivyokuwa nchini Iraq. Sina maana wala kutabiri kuwa kinachojiri nchini humo kitatokea Tanzania, na Mola aepushe hilo, lakini ni vema kwa watawala wetu kutambua kuwa mazingira hayo ni kile Waingereza wanakiita ‘recipe for disaster.’
Tuna makundi mbalimbali katika nchi yetu yanayohisi kutengwa na watawala wetu. Haiingii akilini kwa Serikali kuamua kutoza VAT kwa majeneza badala ya kwa mfano, kupunguza safari mfululizo za Rais Jakaya Kikwete nje ya nchi ambazo zinatafuna mamilioni ya fedha za walipakodi. Ndio, Rais lazima asafiri lakini sio mara kwa mara, zaidi hata ya viongozi wa nchi tajiri kama Marekani ambazo zinamudu gharama za Rais kuwa ziarani hata kila siku ya mwaka.
VAT kwenye majeneza ni mkakati fyongo wa kuongeza mapato sio tu kwa vile karakana zinazotengeneza majeneza zinalipa kodi za uendeshaji biashara bali pia sio ubinadamu kuwa na ‘kodi ya kifo’ ilhali tungeweza kuokoa fedha nyingi tu kwa Serikali yetu kuwa na matumizi yanayoendana na umasikini wetu.
Nimalizie makala hii kwa kuwasihi watawala wetu wafumbue masikio na macho yao na kujifunza yanayojiri katika sehemu nyingine duniani kama huko Iraq kuhusiana na athari za mazingira ambapo makundi fulani katika kujiona yanatengwa, yanabaguliwa, yanadharauliwa au yanakandamizwa. Watanzania walio wengi hawatendewi haki na watawala wetu ambao ni wepesi wa kutoa ahadi zisizotekelezeka wakati wanaomba kura lakini wepesi wa kuchukua uamuzi unaowafanya watawaliwa kuhisi watawala hao wanaishi sayari tofauti kabisa (kwa mfano uamuzi wa VAT kwa majeneza).
Wito wangu kwa Rais Kikwete ni kuwaagiza watendaji wake waachane na ‘kodi hiyo ya laana’ ya VAT kwa majeneza. Ninarejea kumkumbusha kuwa amebakiwa na takriban miezi 18 tu madarakani kutengeneza legacy nzuri ya kukumbukwa na kuenziwa na Watanzania atakapostaafu hapo mwakani. Kadhalika, ninamsihi atumie muda huu uliobaki kufanya jitihada zaidi kuleta usawa kati ya makundi mbalimbali katika Tanzania yetu, hususan pengo linalozidi kukua kati ya wenye nacho na wasio nacho.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/ipo-siku-watawaliwa-hawa-wataamua-%E2%80%98liwalo-na-liwe%E2%80%99#sthash.eJ7DR5WJ.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube