26 Jul 2014




 Mara ngapi unakutana na tweet, au post kwenye Facebook, au picha Instagram ikiambatana na maneno 'I am happy'? Nina hakika ni takriban kila siku. Si dhambi kutamka hadharani kuwa una furaha, lakini uzoefu waonyesha kuwa wenye furaha za dhati wala hawahitaji kuishawishi dunia kuwa wana furaha: ukiwa na furaha ya kweli itaonekana tu bila hata kuitangaza.

Hebu tuangalie tabia 20  za watu wenye furaha ya dhati lakini wala hawana muda wa kujitangaza kuwa wana furaha, kwa vile furaha hujionyesha nyenyewe pasi haja ya matangazo.

1.  Hawana muda na drama za watu wengine: Kamwe usianzishe drama, na kamwe usiruhusu drama za watu wengine zikuhusu. Wengi wa watu wenye furaha hawajali nini kinachosemwa dhidi yao na watu 'wasio muhimu' kwao. Kwa hakika, watu wenye furaha huwashukuru wanaowasema vibaya kwani ni fundisho kwao kuhusu wasivyostahili kuwa ,yaani kutostahili kutokuwa na furaha.

2. Hupendelea kutoa/kusaidia kila wanapoweza: Nadhani ushaskia usemi 'kutoa ni moyo si utajiri. Watu wenye furaha ni wepesi kutoa/kusaidia, lengo kuu likiwa kusambaza furaha waliyonayo.

3. Wanathamini mahusiano yao muhimu: Mara nyingi watu wenye furaha wana marafiki wengi kwa sababu wanathamini marafiki, na marafiki hao in return wanatambua kuthaminiwa kwa urafiki wao.Hata hivyo, umuhimu wa marafiki hao hutegemea mchango walionao kwa furaha ya wenye furaha hao.Ni vema kuepuka watu watakapa mawazo fyongo.

4. Wanatenga muda kwa ajili ya kujipenda wenyewe pia: huwezi kupenda wengine wakati hujipendi mwenyewe. Ushakskia msemo 'charity begins at home.' Na Maandiko Matakatifu yanausia kuwa huwezi kumpenda Mungu usiyemuona ilhali huwapendi wanadamu unaowaona. Kadhalika,huwezi kuwapenda wengine ilhali wajichukia mwenyewe.Tenga muda ujipende.And by the way, kama mwenyewe hujipendi nani atakuwa na muda wa kukupenda?

5. Huthamini ufanisi kuliko umaarufu: Kamwe usi-confuse ufanisi na umaarufu.Kuwa maarufu kwamaanisha unapendwa kwa kipindi flani tu,lakini kuwa na ufanisi kunamaanisha unaleta tofauti chanya katika maisha ya wengine, na kuleta tofauti chanya katika maisha ya wengine kunamfanya mtu kuwa na furaha zaidi kwani inatambulisha umhimu wake kwa wengine.

6. Wanasema 'hapana' pale inapobidi: kuna msemo wa Kiswahili kwamba mkono hujikuna pale unapofiki.Huwezi kutaka kumridhisha mtu kwa kujiumiza mwenyewe. Na ni vema kusema 'hapana' ya dhati kuliko 'ndio' ya uongo. Kumbuka,kuwa mkweli ni kiungo muhimu cha kukufanya uwe mwenye furaha.

7. Wanajua kushukuru/kuthamini: Shukrani ni mfalme wa furaha, wanasema Waingereza (gratitude is the king of happiness).Watu wenye shukrani huwa na furaha maishani kwani ni nadra kwao kuwa na kinyongo au hasira. Shukrani ninayoonglea hapa ni pamoja na kuridhika na yale tuliyojaaliwa au tulofanikiwa kuwa nayo. Kwa mfano rahisi kabisa ni kumshukuru Mungu kwa kuamka ukiwa hai.

8. Hujenga matumaini: Watu wenye furaha huyaangalia maisha kwa mtizamo chanya. Kisaikolojia,ukiliangalia jambo kwa mtizamo hasi waweza kufanya matokeo ya jambo hilo kuwa hasi pia.Kumbuka kwamba mtizamo wetu ni sehemu muhimu ya kinachotusukuma au kutuzuwia kufanya/kutofanya vitu katika maisha yetu.

9. Hawajihusishi na kila fanikio au anguko: Watu wenye furaha hawachukulii kila anguko kuwa ndo mwisho wa kila kitu na kamwe hawavimbishwi vichwa na mafanikio. Hawaruhusu anguko (failure) kuwakaa moyoni na hawaruhusu mafanikio/sifa kuwalevya kichwani.

10. Hujenga mikakati ya kukabiliana na nyakati ngumu: Sote twatambua kuwa si kila leo ni kama jana, na si kila kesho ni kama juzi. Siku huwa tofauti,na ndo maana leo kuna mvua kesho kuna jua kali. Cha muhimu ni kuwa na mikakati madhubuti ya kukabiliana na matatizo.Na moja ya njia nzuri ni kujifunza kutoka kwa wengine.Twaweza kujifunza kwa kujali experiences za wengine ma kusoma pia.

11. Huchukulia kukataliwa kama kinga dhidi ya mabaya: Kuna namna njema ya kudili na kukataliwa- kuangalia kukataliwa kama kinga ya kukuepusha na jambo bayana. Sio kila kukataliwa kunamaanisha wewe si bora,wakati mwingine kunamaanisha kwamba alokukataa ameshindwa kutambua jinsi gani ulivyo bora.Ukikataliwa, amini kwamba kuna jema zaidi lipo njiani kwa ajili yako.

12. Wanaweka mkazo katika wakati uliopo: Kuendelea kunung'unika kuhusu mabaya yaliyopita hakusaidii kubadili hali ilivyo sasa. Cha muhimu ni kujifunza kutoka kwa mabaya hayo na kujitahidi kuhakikisha kuwa hakujitokezi tena. Kwa kujifunza kutokana na mabaya yaliyopita,watu wenye furaha wanatengeneza mazingira bora ya muda uliopo na kuweka 'bima' kwa ajili ya wakati ujao. 

13. Wanawekeza nguvu na muda kwa mambo ya msingi: Ukipanda upupu utavuna upupu. Mawazo chanya huzaa matokeo chanya, mawazo hasi huzaa matokeo hasi.Hilo halina ubishi. Kesho ni matokeo ya bidii za leo, na kwa kuwekeza nguvu na muda kwa mambo bora sasa, kehso ina uhakika wa kuvuna matokeo bora ya jitihada hizo za leo.

14. Wanaji-commit katika vipaumbele vyao: Ushaskia msemo'mshika mawili moja humponyoka.' Huwezi kuchanganya shule na mapenzi na ukafainikiwa katika vyote viwili.Lakini ili uweze kuwa na mafanikio ni muhimu kutambnua vipaumbele vyako, na si kutambua tu bali pia kufahamu mbinu za kuvifikia. Na ukishavitambua na kufahamu namna ya kuvifikia,yalazimu kuwekeza mtaji wa kutosha (sio lazima fedha bali nguvu, akili na muda) kuhakikisha unavifikia.

15. Wanaangalia kutopendezwa kama sehemu ya kuboresha uwezo wao: Kuna nyakati utafanya hili lakini huotfanikiwa. Lakini badala ya kubaki na hasira au manung'uniko ni vema kutumia fursa hiyo kujiuliza kipi kilikwenda mrama hadi ukashindwa kufanikiwa.Na kwa kufanya hivyo,unatengeneza mazingira mazuri ya kupata matokeo bora kwa kitu kilekile kilichoshindikana hapo awali.

16. Wanajali afya zao: Mwili wenye afya ni kama koti la akili yenye afya: Pasipo afya bora ni vigumu mno kuwa na furaha.Na katika hali ya kawaida tu, ukiwa unaumwa na kichwa, huwezi kuwa na furaha. Watu wenye furaha huwekeza vya kutosha katika kula vizuri,kufanya mzoezi,kuepusha vitu vinavyoweza kuathiri afya zao na pia kujali mapumziko.

17. Hutumia fedha kupata uzoefu badala ya vitu wasivyohitaji: Watu wenye furaha wapo makini katika matumizi yao, hasa kuepuka manunuzi ya vitu wasivohitaji na badala yake kufanya manunuzi ya vitu muhimu kwa maisha yao. Kuna kitu kinaitwa manunuzi ya uzoefu (experiential purchase),yaani kununua uzoefu, kwa mfano kutumia fedha kwenda likizo ya kujifunza kitu flani kinachoweza kukubailishia maisha yako, au kutumia fedha kujiunga na kozi flani itakayokuongezea ujuzi, na vitu kama hivyo.

18. Wanathamini furaha japo kidogo: Ili uweze kuwa na furaha kubwa shurti uweze kuthamini furaha ndogo,kwani hata wahenga walisema haba na haba hujaza kibaba.Kidogo unachopata katika dakika moja,kitakuwa kingi kikipatikana katika saa nzima,na kingi zaidi katika siku,na kwa mwezi,mwaka au miaka kitakuwa kingi kabisa. Furaha ni ku-enjoy vitu vidogo wakati tunafukuzia vitu vikubwa.

19. Wanatambua hali ya vitu kutodumu milele: Ni hivi, kwa vile kitu kizuri hakikudumu, haimaanishi kuwa kilikuwa kibaya. Kila kitu kina muda na wakati wake.

20. Huishi maisha wanayotaka kuishi: Tatizo la watu wengi wasio na furaha ni kuhangaika kuishi maisha ya wengine.Hakuna ubaya katika kutamani jinsi flani anavyoishi lakini ni vema kutambua wewe sio yeye, na kinachompa furaha yeye si lazima kukupe furaha wewe pia.Ndege wanaweza kuruka angani, na pengine nawe ungependa kuwa na uwezo huo,lakini wewe si ndege. Wanachofokiria watu wengine kuhusu wewe,hususan usiowajua- hakijalishili. cha muhimu ni ndoto zako,malengo yako na matarajio yako. Jitahidi kuzungukwa na watu ambao sio wanaotaka uwe wao wanavyotaka bali wanaojali na kuthamini wewe unavyota kuwa au ulivyo.Tengenezeza marafiki wa kweli na dumisha mawasiliano nao. Na la muhimu kabisa ni kutambua kwamba furaha ni chaguo lako mwenyewe, kama ilivyo kwa kutokuwa na furaha.





0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.