26 Jul 2014

Januari Makamba
KAMA nilivyotabiri katika jarida hili wiki iliyopita, wanasiasa kadhaa wemejitokeza kutangaza nia yao ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Nilitabiri hivyo baada ya tangazo la Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, January Makamba, kwamba kwa zaidi ya asilimia 90 anatarajia kugombea urais.
Pasi kujali kama atafanikiwa katika dhamira yake hiyo au la, January ataingia kwenye kumbukumbu za Uchaguzi Mkuu wa mwakani kama mwanasiasa aliyefungua rasmi mbio za kuingia Ikulu.
Hata kama uamuzi wake huo utamgharimu, kwa maana ya kuwapa wapinzani wake muda wa kutosha ‘kumdhuru kisiasa,’ ukweli unabaki kuwa amewatendea jema wapiga kura, angalau ndani ya CCM, kupata fursa ya kuwafahamu mapema wenye nia ya kugombea urais hapo mwakani.
Hadi wakati ninaandika makala hii, wanasiasa waliotangaza hadharani ni pamoja na Steven Wassira, Profesa Mark Mwandosya, Ali Karume na Frederick Sumaye. Hata hivyo, ni January pekee ambaye ameonekana kuwa ‘serious’ zaidi, kwa maana ya ‘kuendelea na moto uleule’ tangu siku ‘alipotangaza nia.’ Akitumia mitandao ya kijamii, hasa twitter, mwanasiasa huyo kijana amekuwa akifanya jitihada za kutosha kuthibitisha kuwa tamko lake hilo ni la dhati, na kwa hakika anataka kumrithi Rais anayemaliza muda wake, Jakaya Kikwete.
Majuzi, alinieleza (kwa ‘tweet’) kwamba, “tutaporuhusiwa kufanya kampeni mapema mwakani tutakuwa katika nafasi nzuri ya kuonyesha kwa mapana Tanzania mpya inapatikanaje.”
Inafahamika kwamba ili wapigakura wafikie uamuzi wa kumuunga mkono au hata kumpinga mgombea, sharti kwanza wamwone kuwa ana dhamira ya dhati na si anawahadaa tu. Watu hawawezi kupoteza muda wao japo kumjadili - kwa mema au mbaya - mwanasiasa wanayedhani ‘anapima upepo tu.’ Yayumkinika kuhitimisha kuwa kwa kiasi fulani, January anafanikiwa kuwaaminisha wananchi (angalau kwenye mitandao ya kijamii) kuwa hatanii.
Lengo la makala hii si kumjadili January au ‘wagombea’ wengine bali kuamsha tafakuri kuhusu nafasi ya mwananchi wa kawaida  katika hatma ya/mwelekeo wa taifa letu wakati tunajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu mwakani.
Ninaandika makala hii nikitambua bayana kwamba hatma ya uchaguzi huo inategemea sana maendeleo ya kikao cha Bunge Maalumu la Katiba, ambayo hadi sasa bado ni tete.
Kwa upande mmoja, licha ya kutamani kuona vikwazo vilivyojitokeza dhidi ya ufanisi wa Bunge hilo – hususan, uamuzi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia – vikiondoka, bado ninabaki na mtizamo kuwa Katiba mpya haitoweza kutupatia dira njema ya kulifikisha taifa letu panapostahili. Tatizo la msingi si kitakachokuwamo katika Katiba hiyo bali utekelezaji wake.
Kwa Watanzania wengi ‘wa kawaida,’ Katiba mpya inahusu muundo wa Muungano wa ‘Tanganyika’ na Zanzibar. Japo hicho ni kipengele kimoja tu katika mapendekezo kuhusu Katiba hiyo, kwa makusudi kabisa, wanasiasa wetu wameligeuza suala hilo kuwa ndio msingi wa Katiba hiyo.
Muundo wa Muungano ni suala la kiutawala, na kwa kiasi kikubwa linawahusu wanasiasa kuliko wananchi wa kawaida.
Nitoe mfano. Majuzi, nilialikwa futari na dada zangu wa Kizanzibari wanaoishi hapa Glasgow. Katika muda wote niliokuwa hapo, hakukuwa na kitu chochote cha kunitofautisha mie m-Bara na hao ndugu zangu wa Kizanzibari (labda ni tofauti ya lafidhi tu). Na hata ule mtizamo ‘fyongo’ kuwa Zanzibar ni taifa la Kiislam ilhali Bara imeelemea kwenye Ukristo haukujitokeza kwa aina yoyote ile.
Tukio hilo lilikuwa mjumuiko wa Watanzania pasi kujali mie ni wa Ifakara (Bara) na wenzangu ni wa Michenzani (Zanzibar). Na hapa ndipo wanasiasa wetu wanapokoroga mambo: kuchimba tofauti kati ya wananchi si kwa minajili ya kuwaunganisha bali kuzitumia kudumisha utawala wao.
Laiti Bunge la Katiba lingewekeza nguvu katika kumwangalia mwananchi badala ya namna wao wanasiasa watakavyofanya kazi- chini ya serikali mbili au tatu, au hata moja - basi kwa hakika huenda hata hao akina UKAWA wasingekuwapo.
Na hata kama Bunge la Katiba lingeelemea kuhusu masuala ya ‘kisiasa’ au utawala, bado kuna mambo mengine ya muhimu zaidi ambayo yanapuuzwa kwa makusudi.
Nina mfano. Kwa mujibu wa taarifa nilizonazo, inasemekana kuna ‘vita baridi’ inayoendelea ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa kuhusu mrithi wa Mkurugenzi Mkuu wa sasa.
Vyanzo vyangu vya uhakika vinaeleza kwamba ‘sintofahamu’ hiyo inachangiwa na utaratibu mbovu unaompa Rais madaraka ya kumteua mtu yeyote yule anayeona anafaa na halazimiki kuzingatia ushauri wa taasisi hiyo kuhusu nani anayefaa kuiongoza.
Haya ni masuala nyeti ambayo pengine si mwafaka sana kuingia kwa undani ila kilicho wazi ni kwamba mapendekezo kuhusu Katiba mpya ‘hayana jipya’ ku-address kilio cha baadhi yetu kwamba muundo wa Idara ya Usalama wa Taifa unahitaji mabadiliko makubwa, na ya haraka’ ili si tu iiondoe katika minyororo inayofanya kuwa taasisi ya kisiasa bali pia kuiwezesha kulitumikia taifa letu kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande mwingine, Katiba iliyopo na hiyo tunayohangaika kuitengeneza haimlindi mwananchi dhidi ya “kinachoendelea hivi sasa” huko serikalini wakati tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
Kwa mujibu wa taarifa nilizonazo, vitendo vya ufisadi vinazidi kushika kasi katika taasisi mbalimbali za umma kwa mwendo wa ‘chukua chako mapema.’ Na inaelezwa kuwa hali itazidi kuwa mbaya itapofika muda wa viongozi wa kisiasa katika taasisi hizo kwenda majimboni kupigania nafasi zao.
Kuna mzalendo mmoja kwenye taasisi fulani nyeti amenihabarisha kwamba tutasikia ‘mengi mno’ baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu ujao, na kusisitiza kwamba “ufisadi tunaousikia sasa ni sawa na tone la maji tu kwenye bahari” akimaanisha kuna mengi yanayoendelea ‘nyuma ya pazia.’
Je, Katiba tuliyonayo na hiyo tunayohangaika kuitengeneza inampa nguvu zipi mwananchi wa kawaida kudai haki yake? Labda sheria zipo lakini sote twafahamu kwamba tatizo letu si sheria bali utekelezaji wake.
Ni rahisi kwa baadhi ya wasomaji kuhitimisha kwamba “Bwana Chahali tumekuzowea, hujui kusifia bali kukosoa na kutabiri majanga tu.” Sihitaji kujitetea kwa sababu, kwanza, kukosoa si dhambi au kosa la kisheria, na pili, ni vema kulaumiwa lakini hatimaye ukaokoa taifa lako kuliko kusifiwa na baadaye kuwa sehemu ya anguko la taifa lako.
Wenzetu huku nchi za Magharibi sasa wameanza taratibu ‘kuupa kisogo utawala (governance)’ kwa kuwekeza katika kinachoitwa ‘algorithmic regulation.’ Nitajadili suala hili kwa kirefu katika makala zijazo ila kwa kifupi, ‘utaratibu’ huu mpya unaelemea katika kutumia mifumo ya teknolojia badala ya urasimu (bureaucracy) wa wanasiasa na watendaji- ambao ni binadamu, na sote twafahamu mapungufu ya kawaida ya binadamu.
Ni kwamba kwa vile serikali na taasisi zake inajua nini inachohitaji kutoka kwa wananchi, na wananchi wanajua wanachohitaji kutoka kwa serikali yao, kwa kuzingatia wajibu na haki, basi teknolojia inatumika ipasavyo kuondoa urasimu unaochelewesha au kukwaza michakato  hiyo. Ninafahamu hii ni kama ndoto kwa akina sisi ambao kwa baadhi yetu suluhisho jepesi la kurahisisha urasimu ni rushwa au ushirikina, lakini twaweza kuanza na kutambua umuhimu wetu kama wananchi kwa taifa letu.
Kupiga kura, kulipa kodi, ‘kumkaba koo’ kiongozi au mfanyabiashara fisadi, nk ni sehemu muhimu ya uhai wetu, na ni masuala tunayopaswa kuyafanya wenyewe pasi kusubiri mwongozo wa serikali au watawala.
Na ndio maana, kwa mfano, juzi nilipopata barua-pepe kutoka kwa rafiki yangu akinishawishi nifikirie kuhusu alichokiita ‘kuokoa jimbo letu,’ sikupata shida kumwelewesha kwamba kuna njia mbadala, na pengine bora zaidi, ya kuutumikia umma zaidi ya kuwa kiongozi, nayo ni kuwa ‘political civilian’ (mwananchi mwanasiasa), ambapo, kwa kifupi, ni kuwajibika kama mwanasiasa/kiongozi ilhali ni mwananchi.
Nimalizie makala hii kwa kuhamasisha umuhimu wa kuangalia nafasi zetu kama wananchi katika kuleta mabadiliko kusudiwa kwa ajili ya ustawi na hatma ya nchi yetu.
Uwezo tunao, sababu tunayo ila kinachohitajika ni nia tu. Kama inawezekana kumweka madarakani kiongozi aliyekughilibu kwa ahadi nyingi tamu lakini akashindwa kutelekeza, basi kwa hakika unaweza kujiweka madarakani wewe mwenyewe, si kwa kuwa mbunge au rais bali raia anayetambua wajibu wake katika kujenga na kudumisha taifa analostahili kuishi.
INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.