19 Sept 2014

ALHAMISI, Septemba 18, 2014, mamilioni ya Waskochi watapiga kura ya kuamua hatma ya taifa lao, aidha liwe taifa huru au liendelee kuwa ndani ya ‘Muungano wa Falme ya Uingereza.’
Pengine kabla ya kuelezea kwa undani kuhusu kura hiyo, ni muhimu kutoa ufafanuzi kuhusu nchi hii ambayo kwa wengi inaitwa tu Uingereza japo ina ‘mkanganyiko’ fulani katika majina yake halisi kwa Kiingereza. Jina halisi la nchi hii kama ilivyo sasa ni the United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland. Hivyo ndivyo ilivyo kwenye hati za kusafiria za nchi hii.
Great Britain ni muungano wa mataifa matatu: England ambayo mji mkuu wake ni London, Wales ambayo mji mkuu wake ni Cardiff na Scotland ambayo mji mkuu wake ni Edinburgh (ambao Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipata elimu yake ya chuo kikuu). Ukiunganisha Great Britain na Ireland ya Kaskazini (ambayo mji mkuu wake ni Belfast), ndio tunapata kitu kiitwacho The United Kingdom (of Great Britain and Northern Ireland) au kwa kifupi UK.
Ni muhimu kubainisha pia kwamba ‘kuna Ireland mbili,’ Ireland ya Kaskazini ambayo ni sehemu ya United Kingdom, na Jamhuri ya Ireland (Republic of Ireland), yenye mji mkuu wake Dublin, ambayo ni taifa linalojitegemea na sio sehemu ya UK.
Baada ya ufafanuzi huo, turejee kwenye ‘kura ya uhuru’ Alhamisi. Baada ya kipindi kirefu cha majadiliano na makubaliano, hatimaye wakazi wa Uskochi watapiga kura yenye jibu la ‘ndio’ au ‘hapana’ kwa swali ‘Je, unataka Uskochi kuwa nchi huru?’
Hadi wakati ninaandika makala hii kura za maoni zinaashiria mchuano mkali kabisa, ambapo moja ya kura hizo ilionyesha ‘wanaotaka uhuru’ (kambi inayojulikana kama ‘Yes’ inayoongozwa na Waziri Mkuu- hapa anaitwa First Minister- Alex Salmond, na chama chake cha Scottish Nationalist Party-SNP) inaongoza kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya kambi ya ‘No’ ya wanaotaka Uskochi iendelee kuwa sehemu ya UK, inayoongozwa na ‘Waziri wa Fedha’ (Chancellor of the Exchequer) wa zamani, Alistair Darling. Hata hivyo, kura nyingine ya maoni inaonyesha kambi ya No inaongoza kwa idadi hiyo hiyo ya pointi.
Binafsi nitakuwa miongoni mwa wapiga kura hao. Na pengine suala hili linapaswa kuwasuta wanasiasa wetu walioamua kwa makusudi kuwanyima Watanzania wenzao kadhaa haki ya uraia, kwa kukataa suala la uraia pacha. Ni hivi, kwa hapa, haki ya kupiga kura inawapa haki raia wa nchi za Jumuiya ya Madola, ikiwemo Tanzania, kupiga kura. Kwa hiyo, pamoja na ‘sababu nyingine,’ kinachonipa haki ya kupiga kura hiyo ni asili yangu kama Mtanzania, nchi iliyowahi kuwa koloni la Uingereza.
Japo ningetamani sana kubashiri matokeo ya kura hiyo ya kesho, matukio kadhaa ya hivi karibuni yananifanya nishindwe kufanya hivyo. Awali, kwa uelewa wangu wa stadi za siasa na chaguzi, nilitarajia matokeo kuwa ‘Uskochi kuendelea kubaki sehemu ya UK,’ wazo lililopewa nguvu na kura mbalimbali za maoni hadi wiki chache zilizopita.
Na pengine mtizamo huo, ambao wachambuzi wengi wa siasa walikuwa nao pia, ulichangia viongozi wa vyama vikuu vya siasa hapa Uingereza, wanaounga mkono Uskochi kuendelea kuwa sehemu ya UK, chama tawala cha Conservative na washiriki wake wa Liberal Democrats na chama cha upinzani cha Labour, wasihangaike kuhamasisha kura ya ‘hapana.’ Hata hivyo, wiki iliyopita ilishuhudia ujio wa Waziri Mkuu David Cameron (akiwakilisha Conservatives), Naibu Waziri Mkuu Nick Clegg (akiwakilisha Liberal Democrats) na Ed Milliband (kiongozi wa Labour) hapa Uskochi kupiga kampeni dhidi ya kura ya ‘ndiyo.’
Ujio huo ulichangiwa zaidi na kura ya maoni ya taasisi ya kura za maoni inayoheshimika hapa Uingereza, ya YouGov, iliyoonyesha kambi ya ‘Ndiyo’ ikiwa mbele kwa asilimia 51 na kambi ya ‘hapana’ ikiwa na asilimia 49. Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kabisa kwa kambi ya ‘ndiyo’ kuongoza katika kura za maoni. Na pengine kuashiria kuwa uwezekano wa ‘uhuru wa Uskochi’ si suala la kufikirika tu bali linawezekana, asilimia hiyo 51 katika kura za maoni ilikuwa imepanda kwa takriban asilimia 30 ndani ya mwezi mmoja.
Ningependa kutumia nafasi hii kukiri kwamba kamwe sijawahi kushuhudia siasa ikifanya kazi kama ilivyo sasa tunapoelekea kwenye ‘siku ya hukumu’ hapo kesho (Alhamisi). Wenyewe wanasema ‘siasa imerejea kwenye siku zake za nyuma’ au kwa kimombo ‘old school politics.’ Wanasiasa wameonekana mitaani wakijumuika na wanaounga mkono au kupinga ‘uhuru wa Uskochi,’ huku mijadala mbalimbali ikifanyika katika hali unayoweza tu kulinganisha na mijadala ya maisha yetu ya kila siku, ila kwa umuhimu mkubwa kabisa.
Japo nina furaha ya kuwa miongoni mwa watakaopiga kura kuamua hatma ya taifa hili, ninajisikia uchungu kuona hali ikiwa tofauti kabisa huko nyumbani, ambapo sasa tunashuhudia Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, akitumia ubabe dhidi ya ushauri wa Rais Jakaya Kikwete na Kituo cha Demokrasia Tanzania kuwa mchakato wa kupata Katiba mpya usogezwe mbele. Sitta ameziba kabisa masikio yake dhidi ya kelele kutoka kila kona kuwa Bunge la Katiba lisitishwe na taifa lijipe muda kujipanga vizuri kushughulikia suala hilo muhimu kwa mustakabali wa taifa letu.
Ndiyo, pengine Sitta anataka kuchapa kazi kwa kinachoitwa ‘kasi na viwango,’ lakini japo kasi kwa mwendesha gari la mashindano ya Formula One ni mkakati mzuri wa ushindi, kwa barabara za mtaani ni sawa na kuikaribisha ajali. Kichwani mwangu ni kama namsikia Sitta akijigamba siku moja, ‘mie ni mtu wa viwango na kasi, na mmeshuhudia wenyewe jinsi nilivyoweza kuhakikisha Bunge la Katiba linakamilisha kazi yake ndani ya muda tuliojipangia.’ Japo ninashindwa kutabiri matokeo ya kura ya kesho, sipati tabu kubashiri kuwa ‘kiburi cha Sitta’ sio tu kitaharibu mchakato mzima wa kupata Katiba mpya bali pia chaweza kuwa ndio anguko lake kisiasa.
Nikiangalia jinsi ajenda ya ‘uhuru wa Uskochi’ ilivyoanza hadi kufikia leo siku moja kabla ya kupiga kura, nadhani sitaonekana mtu wa ajabu nikiyumkinisha kuwa ‘kuna kitu fulani walichojaaliwa hawa wenzetu lakini sisi tumenyimwa...au tumejinyima.’ Nikisikiliza hoja za kambi zote mbili- wanaotaka uhuru na wanaopinga- mkazo unawekwa zaidi kuhusu hatma ya taifa hili (Uskochi au UK kwa ujumla) na vizazi vijavyo. Kwa kiasi kikubwa, japo kura zitapigwa kesho, lakini mtizamo wa wengi ni wa muda mrefu kabisa.
Ningetamani sana Sitta asome makala hii na ajifunze jinsi mwafaka wa kitaifa unavyopatikana kwa njia za demokrasia halisi, kwa maana ya wanaotaka uhuru wa Uskochi na wanaopinga kujadiliana kistaarabu na hatimaye kupewa fursa ya kuhitimisha mjadala huo kwa sanduku la kura. Mchakato huu umechukua muda mrefu, japo si kwa gharama kubwa kulinganisha na ‘vurugu-mechi’ yetu ya kusaka Katiba mpya.
Na japo hoja ya ‘uhuru wa Uskochi’ imekuwa ajenda ya muda mrefu ya chama cha SNP, kampeni ya ‘kudai uhuru’ imeendeshwa kwa utaifa badala ya itikadi za kichama. Na wengi wanaounga mkono suala hilo wametamka bayana kuwa wanafanya hivyo kwa mustakabali wa Uskochi na sio kuiunga mkono SNP. Kadhalika, wanaopinga suala la ‘uhuru’ wamekuwa wakieleza bayana kwamba hawafanyi hivyo kwa minajili ya kuviunga mkono vyama vya Conservatives, Labour au Liberal Democrats.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanadai kuwa hata kama kambi ya ‘hapana’ itashinda na Uskochi kuendelea kuwa sehemu ya UK, wazo la kudai uhuru halitokufa, huku baadhi wakitabiri kuwa Uskochi inaweza kuwa huru ndani ya miaka 10 ijayo. Sababu ni nyingi lakini kubwa zaidi ni utawala wa chama cha kihafidhina cha Conservatives ambao sera zake zimeonekana kuwachukiza Waingereza wengi.
Lakini kama ilivyo huko nyumbani ambapo kila Rais baada ya Mwalimu Julius Nyerere anahofia kuvunjikiwa na Muungano wetu wakati wa utawala wake- kinachoitwa ‘kuogopa mzimu wa Nyerere’- kwa hapa pia mtihani unaomkabili Waziri Mkuu Cameron ni kutoingia katika historia kama mtu aliyeongoza Uingereza na kushuhudia Uskochi ikijitenga.
Laiti Uskochi ikipata uhuru wake, kuna dalili kuwa ‘moto’ huo ukasambaa sehemu nyinginezo duniani, ambapo tayari kumesikika ‘kelele kama hizo’ huko Hispania na kwingineko. Lakini pengine la muhimu zaidi kwa hatma ya Muungano wetu ni ukweli kwamba Uskochi ni makazi ya Wazanzibari wengi (na kwa ufahamu wangu wengi wao kesho watapiga kura ya ‘ndiyo’ kama ilivyo kwa wapiga kura wengine wengi wenye asili ya nje ya Uskochi). Je, kwa kuona ‘mchango wao’ katika kupatikana uhuru wa Uskochi hawawezi kuhamasika kuchochea Wazanzibari wenzao huko Zanzibar kuhusu ‘uhuru wa nchi yao’?
Nimalizie makala hii kwa kukiri kwamba nina msisimko kama ilivyo kwa Waskochi wengine kuhusu siku ya kesho na umuhimu wake kwa hatma ya taifa hili ambalo kwangu limekuwa ‘nyumbani mbali na nyumbani’ (home away from home) kwa zaidi ya miaka 12 sasa. Yawezekana makala hii ikawa ya mwisho kuiandika nikiwa katika Uskochi iliyo sehemu ya UK. Lakini kubwa zaidi ni kupata fursa adimu ya kushuhudia historia ikijiandika- iwe kwa Uskochi kujitenga au kubaki sehemu ya UK. Na kubwa zaidi kama mwana-stadi za siasa, ni kushuhudia jinsi siasa inayofanya kazi katika hali ambayo nimekuwa nikiisoma vitabuni tu.
Japo kura ni siri, kesho nitapiga kura ya 'ndiyo’ ili Uskochi iwe nchi huru, hasa kutokana na imani yangu kwamba ina uwezo na sababu za kuwa huru. Kwa hiyo basi, nihitimishe kwa kusema kwa ki-Skochi ‘AYE FOR ALBA’ yaani ‘Yes for Scotland’ au ‘Ndiyo kwa (uhuru wa) Uskochi’

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube