4 Sept 2014


NIANZE kwa kuomba samahani kwa kutoonekana kwenye toleo lililopita. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.
 
Pili, ninaomba kwa niaba ya wakazi wa Wilaya za Kilombero na Ulanga, kutoa shukrani za dhati kwa Rais Jakaya Kikwete kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwapatia daraja linalounganisha Wilaya hizo mbili zilizopo mkoani Morogoro.
 
Kama mzaliwa wa Ifakara, ninatambua vema adha zilizokuwa zikiwakabili wakazi wa Wilaya hizo hususan, msimu wa masika ambao Mto Kilombero ulikuwa ukifurika na kusababisha usafiri wa pantoni kuwa wa matatizo.
 
Pamoja na hilo ni pongezi kwa wakazi wa Kilombero na Ulanga nilizopewa na Msaidizi wa Rais (Hotuba), Togolani Mavura, kwa kile alichokieleza kuwa ni ukarimu wa hali ya juu uliofanywa wakati wa ziara ya Rais Kikwete katika wilaya hizo.
 
Kupitia mtandao wa twitter, Mavura ‘alinifanya nitokwe na udenda’ aliponisimulia jinsi walivyoridhishwa na ladha ya samaki wa aina mbalimbali wanaopatikana maeneo hayo.
Baada ya samahani na pongezi hizo nielekee kwenye mada ya wiki hii. Wiki iliyopita binti wa Kitanzania alifariki katika tukio ambalo siwezi kulielezea kwa undani kwa vile ninaamini lipo mikononi mwa vyombo vya dola.
 
Hata hivyo, kwa kifupi, siku chache kabla ya kufariki, binti huyo, mkazi wa jijini Dar alinyanyaswa vikali katika mtandao wa kijamii wa twitter. Japo hakujapatikana taarifa iwapo manyanyaso hayo yana uhusiano na kifo chake, katika mazingira ya kawaida tu, kumnyanyasa mtu kisha akafariki siku chache baadaye ni jambo lisilopendeza.
 
Sasa kwa vile binti huyo alinyanyaswa mtandaoni kabla ya kifo chake, zilipopatikana taarifa kuwa amefariki, watumaji kadhaa wa mtandao huo ‘waliamsha sauti zao’ dhidi ya vitendo vya unyanyasaji mtandaoni. Hili ni tatizo kubwa japo halifahamiki sana, pengine kutokana na ukweli kwamba idadi ya Watanzania wanaotumia mitandao ya kijamii bado ni ndogo.
 
Kadhalika, yayumkinika kuhisi kwamba kwa watumiaji wageni wa mitandao hiyo, suala la unyanyasaji linaweza kuonekana kama ‘utaratibu’ wa kawaida tu katika ‘maeneo’ hayo, hasa kutokana na ukweli ni nadra kuona mtu akikemewa kwa kumnyanyasa mwenzie.
 
Binafsi, niliguswa na matukio hayo – unyanyasaji ulifonywa kwa binti huyo na kifo chake- na niliona kuwa hiyo ni fursa nzuri ya kuhamasisha mapambano dhidi ya unyanyasaji mtandaoni, ambao kwa Kiingereza unafahamika kama ‘cyber bullying.’
 
Kwa upande mmoja tatizo hilo linachangiwa na watumiaji wenyewe wa mitandao hiyo ambao aidha kwa uoga ama kutojali huwapa uhuru wanyanyasaji mitandaoni ‘uwanja huru’ wa kufanya watakavyo.
 
Pengine tatizo hilo ni la kitaaluma zaidi, kwani baadhi ya stadi za tabia za binadamu zinatanabahisha kuwa ni hulka ya angalau baadhi ya wanadamu kufarijika wanapoona wenzao wakitaabika.
 
Stadi hizi zinaeleza kwamba hata inapotokea ajali, baadhi ya wanaokimbilia kwenye eneo la tukio hawafanyi hivyo kwa minajili ya kwenda kutoa msaada kwa majeruhi bali kufahamu “wangapi wamekufa” kana kwamba kifo ni habari njema.
 
Pengine maelezo haya yanaweza kukufahamisha kwanini matukio ‘mema’ kama harusi, mahafali, nk hayana ‘mvuto’ mkubwa kama ajali, ugomvi, na mingineyo ‘yasiyopendeza.’
 
Na hilo linaweza kueleza vizuri kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii, na hususan, katika madhila aliyopitia binti huyo kabla ya kukutwa na mauti.
 
Kuna watu wengi tu walioshuhudia jinsi alivyokuwa akinyanyaswa lakini hawakuchukua hatua dhidi ya wanyanyasaji. Ninatambua umuhimu wa busara ya ‘kutoingilia yasiyokuhusu’ lakini kwa yeyote atakayesoma ‘tweets’ zake (ambazo bado zipo katika mtandao huo wa kijamii) hatoshindwa kubaini kuwa alikuwa katika wakati mgumu, na alihitaji msaada wa haraka.
 
Pengine msomaji waweza kuhoji kwanini sikuingilia kati. Ukweli ni kwamba mimi na marehemu tulikuwa ‘hatufuatani’ (not following each other) kama ilivyokuwa kwa hao waliokuwa wakimyanyasa. Na kwa taratibu za mtandao huo wa kijamii, ni vigumu kuona kinachotokea katika ‘ukurasa’ (timeline) wa mtu ‘usiyefuatana naye.’
 
Japo haipendezi kuona hadi mtu adhurike au apoteze maisha ndipo jamii ishituke kuhusu ‘jambo baya,’ ukweli ni kwamba kifo cha binti huyo kiliamsha kelele za wengi kukemea kuhusu unyanyasaji mtandaoni.
 
Cha kusikitisha, siku moja tu baada ya tukio hilo, kundi la vijana wanaosifika kwa unyanyasaji kwenye mitandao ya kijamii walianzisha ‘vita’ dhidi ya wote waliokuwa wakihamasisha mapambano dhidi ya unyanyasaji mtandaoni. Pengine kilichowasukuma vijana hao kuanzisha harakati yao hiyo mpya kilikuwa ni kile Waingereza wanakiita ‘guilt consciousness,’ yaani hali ya kujiskia unawajibika kwa ‘baya’ lililomtokea mwenzako.
 
Wengi wa vijana hawa walishiriki kumnyanyasa marehemu, na pengine kwa upeo mdogo wa kufikiri, waliona njia pekee ya ‘kuosha dhambi zao’ ni kuwaandama wanaokemea unyanyasaji mtandaoni.
Stadi mbalimbali kuhusu unyanyasaji (pamoja na huo wa mtandaoni) zinabainisha kuwa katika mazingira ya kawaida mnyanyasaji ni mtu mwenye mapungufu, na hutumia unyanyasaji kama fursa ya ‘kusawazisha’ (compensate) mapungufu yake. Kimsingi, unyanyasaji ni ugonjwa wa akili, ambapo mhusika hupata furaha kuona fulani anateseka kwa maneno au vitendo vya mnyanyasaji huyo.
 
Kuna tatizo jingine kubwa. Mitandao ya kijamii imetoa fursa kwa watu wa aina mbalimbali katika jamii kukutana pamoja. Katika mazingira ya kawaida, hiyo ni nafasi nzuri, kwani hata mtu ‘aliyekwepa umande’ aweza kuwa ‘rafiki wa kimtandaoni’ na msomi mwenye shahada kadhaa.
Nilipata kuandika huko nyuma jinsi kuwapo kwangu katika mitandao hiyo ya kijamii, hususan twitter, kulivyoniwezesha kufahamiana na mawaziri, wanasiasa, mabalozi, wasanii maarufu na hata watu wa kawaida ambao vinginevyo nisingeweza kufahamiana nao.
 
Fursa hiyo inaweza kutumiwa vibaya pia, ‘mtu asiye na chochote’ anaweza kuwa karibu na ‘watu muhimu’ na akiutumia vibaya ukaribu huo kwa kudhani kuwa ‘naye ni muhimu pia.’
Lakini baya zaidi, mitandao hiyo inatengeneza ‘wafuasi’ (followers), na kuna baadhi ya watumiaji wa mitandao hiyo wanaoweza kutafsiri visivyo wingi wa wanaowa-follow kuwa ni dalili ya kukubalika kwao katika jamii.
 
Mtu anaweza kujidanganya, kwa mfano, “mie na matusi yangu yote haya lakini nina followers elfu kadhaa. Kwa hakika matusi ni mtaji.” Na huwezi kumlaumu. Kwanini watu wenye akili timamu wamfuate mtu mwenye matusi au mnyanyasaji mtandaoni?
 
Inakuja sababu nyingine: kumfuata (following) mtu ‘maarufu’ (hata kama ni maarufu kwa matusi) kunaongeza uwezekano wa mtu kupata wafuasi wengi pia.
 
Nimekuwa nikilipigia kelele suala hili la unyanyasaji mtandaoni kwa muda mrefu, hasa ikizingatiwa kwamba nami ni miongoni mwa Watanzania wa mwanzo kabisa ‘kukumbatia’ teknolojia ya mawasiliano mtandaoni (nilianzisha blogu mwaka 2006 na kujiunga na twitter mwaka 2008).
Na kuwa kwangu huko kwa kipindi chote hicho nimeshuhudia mengi ikiwa ni pamoja na kuwa mhanga wa manyanyaso ya mtandaoni.
 
Labda kwa vile suala hili la unyanyasaji mtandaoni linawagusa Watanzania wachache, kwa maana ya idadi ya wanaotumia mitandao ya kijamii, mamlaka husika hazijafanya jitihada za kutosha kulishughulikia.
 
Mfano mzuri, karibuni hapa wakati tunahamasisha mapambano dhidi ya tatizo hilo, wahusika wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) walikuwa kimya japo baadhi yao wapo kwenye mtandao huo wa kijamii.
 
Kadhalika, ‘kelele’ za wengi kuhusu suala hilo zilikosa kuungwa mkono na watu muhimu kama wanasiasa, wanaharakati na hata wengi wa wasanii wetu (ambao baadhi yao licha ya kuwa wahanga wa manyanyaso mtandaoni pia wanashuhudia mashabiki wao wakinyanyaswa). Huu ni usaliti wa wazi.
 
Hata hivyo, kwa upande wa wasanii ninawapongeza wawili, mmoja akiwa Lady Jaydee ambaye alieleza hadharani anavyofahamu jinsi tatizo hilo lilivyosambaa, na msanii mwingine maarufu ambaye siwezi kumtaja kwa vile aliwasiliana nami kwa faragha.
 
Nimalizie makala hii kwa kusema ya kuwa nimejaribu kufuata mafundisho ya Uislam katika kukabiliana na jambo baya kama hili. Katika dini hiyo, inafundishwa kwamba “ukiona jambo baya aidha lichukie au likemee au liondoe-hata kwa nguvu ikibidi.” Sasa, nimeuchukia unyanyasaji mtandaoni vya kutosha, nimeukemea vya kutosha, ila kwa hakika sijafanya jitihada za kuuondoa, kwa nguvu ikibidi. Na hilo ndilo nina furaha ya kulitangaza.
 
Kwa kuanzia, nimefungua ‘ukurasa’ katika mtandao wa picha wa Instagram kuwawezesha wahanga wa unyanyasaji mtandaoni kutumia mbinu ileile maarufu ya ‘cyber bullies’ ku-screenshot. Mhanga ata-screenshot alivyonyanyaswa mtandaoni na kui-post kisha tuiachie jamii imwelimishe mnyanyasaji haja ya kuacha vitendo hivyo. Hii sio ‘mob justice’ bali matumizi ya nguvu ya umma kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.
 
Jingine, ninatarajia kufungua kesi dhidi ya mnyanyasaji mmoja maarufu, lengo likiwa si kumkomoa bali kufikisha ujumbe kwa wote wenye vitendo kama hivyo. Kimsingi, tatizo si hawa wanyanyasaji bali tabia wanayoiendekeza. Hatutibu joto la homa kwa kumnywesha mgonjwa maji ya baridi bali twampatia dawa ya homa. Lengo langu ni kuhamasisha nguvu ya umma kupambana na maovu.
 
Nani anajua, labda mafanikio katika hili yaweza ‘kuigwa’ pia katika mapambano dhidi ya maovu mengine katika jamii kama vile ufisadi.
 
INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.