12 Oct 2014

Kama mtu mwenye uelewa kiasi kuhusu utendaji kazi wa Idara yetu ya Usalama wa Taifa, nimekuwa 'nikipiga kelele' mara kwa mara kuhusu haja ya mageuzi ndani ya taasisi hiyo nyeti. Kwa bahati mbaya sio tu kelele hizo ni vigumu kueleweka kwa Watanzania wengi, uwezekano wa kusikilizwa ni mdogo hasa ikizingatiwa kuwa asili ya taasisi hiyo ni kutekeleza majukumu yake kwa siri, na kama hiyo haitoshi, mara nyingi wahusika wa taaluma hiyo inayopaswa kuhusisha matumizi ya hali ya juu ya akili, hawapendi kusikia ushauri wa 'walio nje' kama akina sie.

Mageuzi ninayoyapigia kelele ni ya kimfumo. Kubwa zaidi ni haja ya uwepo wa mazingira ya uwajibikaji pale watu wanapoboronga. Moja ya dhana zinazotawala fani ya ushushushu ni ile isemayo 'kushamiri kwa matishio ya usalama katika nchi husika ni dalili kuwa taasisi ya ushushushu katika nchi husika ina mapungufu.' Sasa huhitaji uelewa wa fani hiyo kutambua kushamiri kwa matishio kadhaa ya usalama katika Tanzania yetu, kubwa zaidi likiwa ufisadi. 

Labda waweza kujiuliza, iweje ufisadi uwe tishio la usalama? Jibu jepesi ni kwamba ufisadi unatoa fursa kwa maadui wa ndani na nje wa taifa kutimiza azma zao kwa urahisi. Kwa mfano, laiti kukiwa na ufisadi kwenye mipaka ambapo wahusika wanaruhusu kirahisi tu wageni kuingia nchini pasi kuzingatia taratibu zilizopo, ni rahisi kwa magaidi kutumia mwanya huo. 

Ufisadi unaweza kutuletea tapeli la kimataifa kuwekeza kwenye maeneo yanayofahamika kiusalama kama 'vituo muhimu' (vital installations) kama vile viwanja vya ndege na bandarini.

Sasa tukichukulia mfano wa ufisadi, sio tu umeshamiri vya kutosha lakini ndo wazidi kuongezeka. Kuna wanaojiuliza je TISS (Idara yetu ya Usalama wa Taifa) ipo likizo ndefu, wahusika wapo katika usingizi fofofo au kazi imewashinda? Mie sina jibu la moja kwa moja lakini nadhani tatizo la TISS ni la kimfumo zaidi kuliko kiutendaji, japo utendaji wao nao una walakini.

Lakini kabla ya kuingia kwa undani katika mada hii, nirejee kwenye kichwa cha habari. Majuzi, mkuu wa taasisi yenye jukumu la ulinzi wa viongozi wakuu wa Marekani, Secret Service, Bi Julia Pierson alilazimika kujiuzulu wadhifa huo baada ya mtu mmoja kuingia uzio wa Ikulu ya nchi hiyo na kutishia usalama wa Rais Barack Obama. Kwa wenzetu tukio hilo lilikuwa na uzito mkubwa sana, na lilitawala sana katika vyombo vya habari.


Hata hivyo, kwa vile wenzetu wanaendesha mambo kwa uwazi, mwanamama huyo aliitwa mbele ya kamati moja ya bunge la juu la nchi hiyo na kupewa fursa ya kuieleza, ambapo watunga sheria waliafikiana kwamba anapaswa kujiuzulu.
Tukirejea huko nyumbani, ukweli usiopingika ni kwamba licha ya vikwazo vya kimfumo vinavyoikabili TISS, ksingizio  cha 'taasisi hii yafanya kazi kwa siri na hakuna anayepaswa kuhoji' kinatoa fursa kwa wazembe kupata kinga katika utendaji wao mbovu. Ndio, kazi za TISS ni za siri lakini so far usiri huo haujafanikiwa kuwawezesha kukabiliana ipasavyo na matishio ya kiusalama, la wazi likiwa ni ufisadi.

Miongoni mwa mapendekezo yangu (yapo mengi) kuhusu haja ya mageuzi ni kama ifuatavyo.

Kwanza, uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu unapaswa kufanywa kwa uwazi zaidi, ikiwezekana kuidhinishwa na Bunge. Hiyo itazuia uwezekano wa Rais kumpatia wadhifa huo mtu yeyote yule bila kuzingatia uadilifu na uwezo wake kikazi. Kwa kumpa Rais 'blank cheque' ni rahisi kwake kumchagua mtu wake, au mshkaji wake kwa minajili ya kumlinda au kuwa kibaraka wake badala ya kulitumikia taifa kiufanisi.
Pili, ni muhimu TISS kama taasisi iwajibike kwa umma, na si kwa Rais pekee (maana huyo Waziri Katika Ofisi ya Rais mwenye jukumu la kuisimamia TISS anakwazwa na mazingira yalivyo, sambamba na 'uoga' wa kawaida). Ifike mahali, watendaji wakuu wa TISS waweze kuitwa Bungeni, kwa mfano, kuhojiwa kuhusu masuala mbalimbali yanayoihusu taasisi hiyo.

Kiutendaji, ni muhimu kwa taasisi hiyo kupewa uhuru wa kioperesheni utakaoiwezesha kuondokana na hali iliyopo sasa ambapo kwa kiasi kikubwa imekuwa kama tawi la usalama la chama tawala. Sambamba na hilo ni haja ya kuitengenezea mazingira yatayoiwezesha kuhakikisha mapendekezo yake kwa Rais yanafanyiwa kazi hata pale Rais anapoyapuuza. Ikumbukwe kuwa licha ya Rais kuwa 'mkuu halisi wa TISS,' yeye bado ni mwananchi kama wananchi wengine ambao TISS inawajibika kuhakikisha sio tu usalama wao bali hawawi tishio kwa usalama huo. Rais anapopuuza ushauri unaotishia usalama wa taifa basi TISS ijengewe mazingira ya kuhakikisha kuwa ushauri wake unafanyiwa kazi.

Nimalizie kwa kutumaini kuwa 'kelele' hizi zitasikika kwa wahusika. Tujifunze kwa wenzetu waliotatutangulia na wahusika wasione aibu kusikia ushauri wa wenye uelewa hata kama wapo nje ya 'uwanja wa mapambano.'

Endelea kutembelea blogu hii kwa habari mbalimbali, ikiwa ni pamoja na hizi za ushushushu (bonyeza hapo kwenye menu ya INTELIJENSIA upelekwe moja kwa moja)





1 comment:

  1. Sasa nimepata mahali ambapo nilikuwa natamani sana kujua mambo ya ushushushu kiundani,kwakwel chahali umeniweza nilikuwa siijui hii blog,nimefika mahala pake

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube