22 Oct 2014

Watanzania tuna sifa moja kuu isiyopendeza ya usahaulifu wa haraka. Kuna wanaodai si usahaulifu as such bali kutojali, lakini bottom line ni kwamba haichukui muda mrefu kwa jambo linalotokea Tanzania bila kujali ukubwa au athari zake kwa taifa hilo kusahaulika haraka. 

Ni kwa mantiki hiyo ndio ninajikuta nikijiuliza ni Watanzania wangapi wanakumbuka ujio wa Rais wa China huko nyumbani, ulioambatana na utiaji saini wa mikataba kumi na kitu ambayo hadi leo imebaki kuwa siri ya namna flani. Mengi yamesemwa kuhusu mikataba hiyo lakini kilicho wazi, kwa kwa kuzingatia uzoefu wetu huko nyuma, mnufaika mkubwa wa mikataba hiyo ni Wachina na pengine kikundi kidogo cha wenzetu waliovuna teni pasenti kwenye akaunti zao.

Ndio maana niliposikia kuwa Rais Jakaya Kikwete anaelekea China nikabaki najiuliza: HIVI KAMA RAIS WA CHINA ALIKUJA KWETU NA IKASAINIWA MIKATABA KADHAA NA TUKAFICHWA, JE MIKATABA ITAKAYOSAINIWA WAKATI WA ZIARA YA KIWEKTE HUKO CHINA TUTAFAHAMISHWA? Jibu la wazo ni BIG NO. Hatutojua kitu.

Wakati natafakari hayo, nikakutana na habari hii ambayo ni tamko la Katibu Mkuu wa Chadema Taifa Dkt Willibrod Slaa ikitoa tuhuma nzito kuhusiana na ziara hiyo ya Kikwete China. Soma taarifa hiyo hapo chini na angalia kwa makini maneno ya rangi nyekundu.


Kamati Kuu ilikuwa na jumla ya agenda kumi na moja, mengine tutayatoa kwa umma kadri muda unavyokwenda.
Kwa leo tutazungumzia masuala mawili ambayo yana sura ya utekelezaji, tena wa muhimu na haraka; Mchakato wa Katiba Mpya na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa;
Katiba;
 
Tunawataka Watanzania wanaopenda nchi yao sasa waache kulia lia, waache kunung’unika pekee, waache kulalamika. Tuingie kazini. Sasa ni wakati wa kuingia kazini.  
Wenzetu tangu siku ya kupokea rasimu ambapo Kikwete si kama rais wa nchi, bali kama Mwenyekiti wa CCM alianza kuipigia chapuo debe Katiba Inayopendekezwa. Sasa tuingie kazini…
Kikwete kama mwenyekiti wa CCM akitumia kofia ya rais wa nchi, baada ya kupokea rasimu ameendelea kuipigia chapuo, anawaambia wananchi wasome Katiba inayopendekezwa waelewe, sisi tunamwambia aache kuwadanganya Watanzania. Katiba si sawa na novel kwamba kila mtu anaweza kuisoma tu na kuelewa, ingelikuwa ni rahisi namna hiyo tusingekuwa na haja ya kuwasomesha akina Lissu (Tundu). 
Tunahitaji wananchi wetu wasaidiwe tafsiri hasa ya katiba yenyewe na maana yake, hadi yale mambo ya ndani kabisa. Ndiyo kazi ambayo CHADEMA tunaanza kuanzia kesho kuzunguka nchi nzima, ambapo timu ya kwanza itaongozwa na BAWACHA. Ujumbe utakuwa ni Katiba Mpya na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tunataka kuwafafanulia Watanzania kwa kina. 
Wakati bado tunapigania Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka kesho, moja ya ujumbe wetu kuanzia sasa ni kuwataka Watanzania kujiandaa kufurika vituoni kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambalo litaanza kuandikishwa siku 21 kabla ya uchaguzi wenyewe. 
Watanzania wafurike kwa wingi. Wajiandikishe. Kuiondoa CCM kunahitaji vitendo. Tuingie kazini. 
Kwa mtindo huo huo wa kuingia kazini sasa kwa vitendo, tutatembea nchi nzima sasa kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi sana siku ya Desemba 14, kupiga kura kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji… 
Tunawaagiza vile vile viongozi wetu katika ngazi zote za chama, kuanzia kanda, mikoa, wilaya, majimbo, kata, matawi na hadi misingi kuwaongoza Watanzania wote; 1. Kujiandikisha, 2. Kupiga kura na 3. Kusimamia taratibu za kikanuni… 
Tumeshabaini na kila Mtanzania sasa anajua kuwa kuwa Rais Kikwete si mtu wa kuaminika tena…ni mtu anayebadilika badilika na wala haoni haja ya kuomba samahani… 
Na sasa tumezidi kubaini kuwa Kikwete amefikia mahali pa kugeuka kuwa procurement officer na tumenasa nyaraka ambazo zinaonesha kuwa katika kujigeuza ofisa manunuzi huko yanafanyika maandalizi ya kufanya mapambano na wananchi badala ya kuandaa maridhiano.
Nyaraka…Rais amegeuka kuwa Ofisa Manunuzi, Ofisa Mawasiliano TCRA 
Tumepata taarifa za ziara yake ya kwenda China. Siwezi kusema atakwenda tarehe ngapi maana mimi si kazi yangu kutangaza tarehe za ziara za Kikwete ambazo sasa hata tumechoka kuhesabu maana zimeshakuwa nyingi mno zaidi ya 300+ ndani ya miaka kumi. 
Kilichotushtua si Kikwete kwenda ziara, maana siku hizi wala si habari tena, kilichotushtua ni hicho kinachompeleka huko China…ukimsikiliza Kikwete kwenye mazungumzo anapenda kuonekana mtu anayeoenda amani, mshikamano lakini si kweli.  
Amejigeuza Ofisa Manunuzi. Kwa miezi kadhaa sasa kumekuwa na jitihada za kupata helkopta tatu mpya…zingelikuwa ni kwa ajili ya Jeshi letu la Wananchi nisingekuwa na shida, shida inakuja namna zinavyotafutwa. Zinatafutwa kwa utaratibu ule ule wa kifisadi uliotumika kununua ndege ya rais wakati ule na hata rada. 
Tena anamtumia kampuni moja hivi ambayo tumekuwa tukiituhumu katika ufisadi. Sasa sisi tunahoji, hivi ni kwa nini Serikali ya CCM inashindwa kwenda kiwandani na kufanya order ya manunuzi kiwandani moja kwa moja hadi itumie taratibu za kifisadi au mafisadi kufanya kazi hizi… 
Kikwete anajua kuwa ninajua. Maana ameshalalamika kwa watu wake wa vyombo vya dola kwamba taarifa hizi zimefikaje kwa Dokta Slaa…
Wametumia fedha zetu za mikopo kutoka Ujerumani…ndege zinanunuliwa Ufaransa…anatuma fisadi kwenda kufanya manunuzi hayo badala ya Serikali… 
Kinachoonekana na taarifa na sisi hapa tunahoji je ni kweli ndege hizo zinataka kutumika kwa manufaa ya CCM? 
Rais pia ameomba kwenda Beijing kufuatilia mitambo ya Police Surveillance System…wanataka mitambo hiyo ifike hapa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015…ujumbe huu umeandikwa na mtu anaitwa Mbelwa…Kairuki. Waandishi wa habari mtakuwa mnajua huko Wizara ya Mambo ya Nje. Anamwandikia Waziri wa Mambo ya Nje…ujumbe huu umeandikwa tarehe 7/10/2014… 
Sasa hizo ndege anayotaka kununua iko mji mwingine huko China si ule aliopangiwa katika ziara yake, sasa imeagizwa irushwe hadi pale atakapokuwa ili eti Rais mwenyewe aweze kuiona…nimeangalia kwenye budget component hiyo kitu hakuna. Kwa kawaida vitu vya kijeshi huwa havitajwi kwenye bajeti, lakini kwenye randamana ungeweza kuona mpango wa kununua kitu kama hicho. Hakuna. 
Sasa kinachoonekana ni kwamba kwa sababu wamejua mwaka 2015 wanaondoka madarakani, wanaanza kujiandaa kwa mapambano badala ya maridhiano. 
Nataka kumwambia Rais Kikwete kwamba nchi haiongozwi kwa misuli, haiongozwi kwa kutunishiana misuli. Wanataka kufanya kama walivyofanya majuzi kutunga Katiba Mpya kwa mitutu ya bunduki. 
Sasa tena uchaguzi unakaribia wanaanza maandalizi ya mitutu…tunamwambia Kikwete sisi tutakuwa wa mwisho kuona nchi hii inaingia katika vurugu. Ndiyo maana ili kuepusha mambo mabaya yasitokee kila taarifa kama hii tukiipata tutapiga kelele. Silaha kubwa ya mnyonge ni kupiga kelele. 
Katika mwendo huo huo wa Rais Kikwete kugeuka kuwa Ofisa Manunuzi, sasa amejigeuza kuwa Bwana TCRA, wanapanga kukutana na Kampuni ya HUAWEI ya China ili wanunue mtambo utakaowekwa ikulu kwa ajili ya kunasa simu za akina Dokta Slaa… 
Mitambo hiyo inapelekwa ikulu badala ya…ingepelekwa Usalama wa Taifa ningeelewa, ingepelekwa kwenye Jeshi letu ningeelewa, lakini ikulu? Tunasisitiza hatuna tatizo kama mambo haya ya ndege, helkopta au mitambo ya mawasiliano yangekuwa yanafanywa kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi, lakini ni tatizo kubwa kama rais ndiye anakuwa Ofisa wa Manunuzi au Ofisa wa Mawasiliano, TCRA. 
Sasa wanatafuta na kuhangaika kutafuta kila njia ya kubaki madarakani. 
Tunamuonya Rais Kikwete kuwa hizo pesa anazotaka kuchezea kwa yeye kuwa Ofisa Manunuzi si za mfukoni mwake. Aache kuchezea fedha za Watanzania. Tulimuonya pia hivi hivi wakati alipochezea fedha za Stimulus Package. Kama anataka kutukamata atukamate lakini sisi tutasema. Haya ndiyo mambo ya madhara ya katiba inayopendekezwa, kama ambavyo tumeshasema vizuri mapema.


























































0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.