30 Jan 2015

l


Angalia dakika ya 3,14  hadi dakika ya 3,19, baadhi ya waandamanaji wanasema "TUUENI..."
Angalia pia kuanzia dakika ya 3.21 ambapo polisi wanaanza kurusha risasi (sina hakika kama ni risasi za moto au bandia) lakini kitu cha kukiangalia kwa makini ni ukweli kwamba ukiacha watu wachache wanaoonekana kutishwa na milio hiyo ya risasi, idadi kubwa tu ya watu inaonekana kutotishika. Hali hiyo inaendelea hata baada ya 'king'oling'oli' cha polisi kinapooanza kulia na hatimaye polisi kutembeza kipigo cha kinyama.

Licha ya kuumia mno kuona Polisi wakitumia nguvu kubwa katika tukio ambalo lingeweza kabisa kumalizwa kwa amani pasipo haja ya kurusha risasi japo moja au kuwapiga na hatimaye kuwakamata waandamanaji akiwemo Mwenyekiti wa CUF Prof Lipumba, kilichonipa hofu ni jinsi taratibu wananchi wanavyoanza kuota 'usugu' dhidi ya unyanyasaji wa polisi. 

Inapofika mahala wananchi wanaashiria bayana kuwa wapo radhi kuuawa, na kuwaambia polisi waziwazi kuwa TUUENI, basi kwa haki tumeshafika mahala pabaya. Na kama nilivyobainisha hapo juu, na kama inavyoonekana kwenye video hiyo, imefika mahala wananchi wameanza kuzowea sauti za risasi sambamba na mabomu ya machozi.

Hii ina maana gani? Wakati tayari wananchi wameshaonyesha kuzowea unyanyasaji na unyama wa polisi wetu na kuwa tayari kwa lolote lile, yayumkinika kubashiri kuwa kuna siku sio tu wananchi wataweka kando uoga na kuendeleza 'usugu' huo nilioueleza hapo juu bali pia wanaweza kujibi mashambulizi.

Uchambuzi mwepesi ni kwamba wakati polisi hawana njia nyingine zaidi ya hizi wanazotumia kila siku: kutumia nguvu kuvunja maandamano ya amani, wananchi wanapata nguvu mpya kwa kuondoa uoga na kuwaacha polisi wafanye watakalo. Upo uwezekano wa wananchi hao kutoishia hapo tu bali badala ya kuwaachia polisi wawaonee, WANAWEZA KUJIBU MASHAMBULIZI. Na kwa mwenendo ulivyo, hatuko mbali na hali hiyo.

Ni vigumu kubashiri ni lini polisi wetu watathamini haki za binadamu na uhai wa wananchi wasio na hatia. Ni vigumu zaidi kutarajia mabadiliko kutoka kwa mwana-CCM yoyote yule atakayemrithi Kikwete baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.Na ndio maana hujaskia yeyote kati ya waliotangaza nia ya kuwania Urais kupitia CCM akilaani unyama huo wa polisi. Walaani kwanini ilhali wao wana kinga ya kudumu dhidi ya polisi? Japo Rais kutoka chama cha upinzani anaweza kutugeuka, lakini katika mazingira ya kawaida ya kibinadamu angalau yeye naye atakuwa ameshaonja unyama wa polisi wetu na ni rahisi kwake kuchukua hatua kuliko hao wasioguswa na polisi.

Kwako msomaji, nakusihi uiangalie video hii kwa makini zaidi ya hayo niliyotanabaisha hapo juu. Jiulize, kama wanaweza kumfanyia LIPUMBA hivyo, watashindwa kukufanyia wewe, familia yako, nduguzo au jamaa zako? Sikiliza malalamiko ya huyo mwanamama katika dakika ya  6.24 na uyafanyie kazi.

TANZANIA ISIYO NA UNYAMA WA POLISI INAWEZEKANA

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube