1. Hivi karibuni ndugu zetu, viongozi wenzetu wa Dini ya Kikristo chini ya “mwamvuli” wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, wametoa Tamko la kuitaka Serikali isitishe Mchakato wa Mahakama ya Kadhi kwa kuondoa muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 02 wa Mwaka 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislamu, Sura ya 375(The Islamic Law(Restatement) Act, Cap.375) na ambao unatarajiwa kujadiliwa katika Mkutano wa 18 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoendelea hivi sasa Dodoma, ikiwa ni ahadi ya Serikali iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Pinda mwishoni mwa Mkutano wa Bunge Maalum la Katiba.


2. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imelipitia Tamko hilo la Jukwaa la Wakristo Tanzania kwa umakini mkubwa na baada ya tafakuri ya kina juu ya kadhia hii, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inaweka bayana yafuatayo:-3. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imesikitishwa sana na Tamko la Maaskofu chini ya Jukwaa la Wakristo Tanzania kuingilia kwa hila madaraka ya Bunge na kutaka kuifanya Serikali iliyotoa ahadi kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ionekane imewadanganya Waislamu ili Waislamu waichukie Serikali yao. Ikumbukwe kwamba Ahadi ya Marekebisho ya Sheria kuitambua Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara ni Ahadi ya Serikali. 4. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawanasihi na kuwaomba Maaskofu wawaachie “uhuru” Wabunge Waumini wa Dini ya Kikristo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waujadili muswada huo bila ya shinikizo la kiimani la kuukataa.5. Mbinu zozote za kuwashawishi Wabunge kiimani kutekeleza Maazimio ya Maaskofu chini ya Jukwaa la Wakristo Tanzania, huo ni “udini” ambao ni hatari sana kwa Umoja na Mustakabali wa Taifa letu.6. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawakumbusha Maaskofu kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina Vyombo vya Uchunguzi na Utafiti vyenye uwezo wa kubaini maeneo yanayovunja Umoja wetu wa Kitaifa, na hata mambo yanayopingana na Katiba ya nchi yetu tuliyo nayo sasa na ile inayopendekezwa. Kamwe Maaskofu si sehemu ya vyombo hivyo. Ni vizuri wakaendelea kuongoza Ibada na kazi hizo za Uchunguzi wakawaachia walioaminiwa kuzifanya.7. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inachukua fursa hii kuwakumbusha Maaskofu na Watanzania kwa ujumla kwamba “Hofu” ya kuwepo Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara ni hofu “bandia”, kwani kesi zinazohukumiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kiislam zinazohusiana na Ndoa ya Kiislamu, Talaka, Miirathi, Wasia, Waqfu na Malezi ya Watoto zinapatiwa uamuzi (hukumu) katika Mahakama zilizopo na kwa miaka kadhaa na wala Maaskofu hawajapata kudai ziondolewe kwa kuwa ni za kidini. Ieleweke kuwa wanachoomba Waislamu ni kubadilishiwa Hakimu ili aje Kadhi ambaye ana taaluma na uelewa mpana wa Sheria ya Kiislamu. Je, ni vipi kasoro ya Dini ionekane baada ya kuletwa Kadhi atakayezipatia hukumu za kesi hizo na isionekane sasa wakati zipo Mahakamani kwa Hakimu anayezikosea hukumu hizo?8. Kuhusu hofu ya Maaskofu kwamba, kwa kuwa baadhi ya Taasisi za Kiislamu hazikubaliani na Mamlaka ya Mufti wa Tanzania kwenye masuala yao, na hivyo kuijumlisha hoja hiyo kama hoja ya kutaka muswada huo uondolewe kwa ujumla wake, tunapenda kuwakumbusha na kuwataka viongozi wa kikristo wayaache mambo ya ndani ya waislamu yashughulikiwe na waislamu wenyewe. Kadhalika wakumbuke kauli yao “ Ya Kaizari mpe Kaizari, na ya Mungu mpe Mungu” na hivyo basi waiache Serikali na Bunge kutekeleza majukumu yao bila ya kuingiliwa kiimani. Viongozi wa Kikristo watambue kuwa Waislamu wanajua migongano na mifarakano iliyopo ndani ya makanisa lakini waislamu hawajathubutu kuyaingilia mambo ya ndani ya wakristo kwa namna yoyote na wamewaachia Wakristo watatue matatizo yao wao wenyewe. Viongozi wa Kikristo waache kuwadanganya Waislamu kwa “huruma ya mamba” na ikiwa kweli Viongozi hawa wa Kikristo ni wasikivu wa sauti ya Baadhi ya Taasisi za Kiislamu wangefanyia kazi madai ya uwepo wa “Mfumo Kristo” yaliyotolewa hadharani na Taasisi hizo.9. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania itashangazwa sana iwapo Serikali itaamua kuuondoa Bungeni Muswada unaolenga kuitambua Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara kwa kisingizio cha kupingwa na baadhi ya Taasisi za Kiislamu na chembilecho itadhihirika wazi kuwa Serikali imeuondoa Muswada huo kutokana na shinikizo la Jukwaa la kikristo, kwa kuwa ni Serikali hii iliyoamua kuendelea na mchakato wa SENSA mwaka 2012 pamoja na kupingwa na baadhi ya Taasisi za Kiislamu. 10. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawaomba Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wazingatie viapo vyao vya kuitumikia nchi hii na watu wake kwa uadilifu na bila ya kuathiriwa na shinikizo la kiimani lililotolewa na Maaskofu kupitia Jukwaa la Wakristo Tanzania waupokee Muswada huo na waupime kwa hoja na kutoa majibu yenye hoja, na kamwe wasikubali wagawanywe kiimani kwani jaribio la kuligawa Bunge kiimani ni jambo la hatari linalotishia kuligawa Taifa la Tanzania.11. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania haina pingamizi na dhamira ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwafahamisha “wenye hofu” na uwepo wa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara kuwa Mahakama hiyo haina madhara yoyote kwa Umoja, Mshikamano na Mustakabali wa Taifa la Tanzania. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inaahidi kumpa ushirikiano wowote atakaouhitaji katika utoaji wa elimu hiyo.12. Mwisho, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawaomba Waislamu wote nchi nzima kuwa watulivu na kuendelea kuiombea nchi yetu isiingie katika machafuko yoyote.Wabillahit Tawfiiq
SHEIKH KHAMIS MATAKA KATIBU MKUU.