Showing posts with label LIPUMBA. Show all posts
Showing posts with label LIPUMBA. Show all posts

4 Mar 2020Kuna njia mbalimbali za kufanya uchambuzi wa kiintelijensia, njia zinazotegemea vigezo mbalimbali, kigezo muhimu zaidi kikiwa tukio husika na/au "key players" (kwenye ushushushu tunawaita "subjects") katika tukio hilo.

Katika kufanya uchambuzi wa kiintelijensia kuhusu tukio la jana ambapo Rais Magufuli alikutana na viongozi wakuu watatu wa upinzani, Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT-Wazalendo, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, na Ibrahim Lipumba wa CUF, nitatumia kanuni ijulikanayo kama 'Linchpin,' ambayo ni mwafaka zaidi pale ambapo "ukweli mzima" upo bayana (au "vipande vya ukweli).Kanuni hii ya Linchpin ilibuniwa na Naibu Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), Douglas MacEachin, na inahusu "matukio ya ghafla/ya kushangaza," ambapo aliitumia kanuni hiyo kueleza tukio la ghafla na Iraki kuivamia Kuwait mwaka 1990. 

Katika kanuni hii, uchambuzi wa kiintelijensia unatathmini tukio/matukio husika kwa kuzingatia "ukweli uliopo/unaofahamika," kitu tofauti kidogo na mbinu nyingine za uchambuzi wa kiintelijensia zinazoanza na hisia au dhana (kama ile ya ACH -Dhana Zinazoshindana -nilioutumia majuzi kuchambua tukio la Membe kufukuzwa uanachama wa CCM)

Kwa vile lengo la makala hii sio kutoa darasa la "mbinu za uchambuzi wa kiintelijensia," bali kutumia kanuni ya Linchpin kueleza "tukio la ghafla," la Jiwe kukutana na Maalim Seif, Mbatia na Lipumba, ni vema nikahamia kwenye uchambuzi husika.

Kwa kutumia kanuni hiyo, kuna "ukweli " (facts) kadhaa ambao ni msingi wa uchambuzi huu. Ukweli mkubwa zaidi ni kitu nilichokiongea wiki iliyopita baada ya mwandishi Erick Kabendera kuachiwa baada ya kuwekwa jela kwa uonevu kwa zaidi ya miezi sita.Awali nilieleza kuhusu hilo la "Jiwe kukaliwa kooni na mabeberu" katika chapisho langu hili


Kwahiyo ukweli mmoja - na muhimu zaidi - uliopelekea "tukio hilo la ghafla" ni shinikizo la mabeberu. Shinikizo ambalo wiki iliyopita lilipelekea mwandishi Kabendera kuachiwa, na wiki hii limepelekea Jiwe kukutana na viongozi hao watatu wa upinzani.

Nimetanabaisha kuwa huo ni "ukweli muhimu zaidi" kwa sababu kuna ukweli mwingine japo sio wenye uzito sana. 

Uamuzi wa Jiwe kukutana na akina Maalim Seif jana ni sawa na "kuua ndege wawili kwa JIWE moja." Kwa upande mmoja amefanikiwa kutuliza shinikizo la mabeberu ambao wameweka bayana msimamo wao kuwa wanaweza kutochangia bajeti ijayo endapo ukandamizwaji wa demokrasia na haki za binadamu utaendelea. Amewatuliza mabeberu kwa kuwaonyesha kuwa "demokrasia ipo" na ndio maana ameweza kukutana na sio kiongozi mmoja tu wa upinzani bali watatu kwa mkupuo.

Nimesema "ameua ndege wawili kwa jiwe moja." Na "ndege" wa pili ni Membe. Mkutano wake huo na akina Maalim Seif unafikisha salamu muhimu kwa Membe aliyefukuzwa uanachama wa CCM wiki iliyopita, kwamba "hao unaotaka kujiunga nao ndo hawa niko nao hapa Ikulu kwangu."

Kama nilivyoeleza katika uchambuzi kuhusu tukio hilo la Membe kufukuzwa uanachama wa CCM, kuna uwezekano mkubwa wa mwanasiasa huyo kujiunga na ACT-Wazalendo. Na kwa vilekufukuzwa kwake CCM ni matokeo ya uoga wa Jiwe kuhusu upinzani kwenye nafasi ya urais, Membe "kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo" ni worst nightmare kwa Jiwe. 

Naomba nirudie kusisitiza kuwa uoga huo wa Jiwe hauna msingi kwa sababu Membe hana uwezo wa kumwangusha Jiwe kwa sababu nilizowahi kutanabaisha katika makala hii.Kwahiyo Jiwe akiweza kumzuwia Membe kisaikolojia asiwaamini Wapinzani itakuwa ni nafuu kubwa kwake na uoga wake.

Ukweli mwingine kuhusu mkutano huo kati ya Jiwe na viongozi hao wa upinzani ni "busara ya kisiasa" inayosema "kuwa karibu na marafiki zako, lakini kuwa karibu zaidi na maadui zako."

Ukweli mchungu kuhusu wanasiasa wetu - wa CCM na hao wa upinzani - ni huu: wote wapo katika "tabaka tawala" (ruling class). Hapana, simaanishi kuwa akina Seif, Mbatia na Lipumba ni sehemu ya utawala wa Jiwe bali ukiangalia kwa undani wasifu wa viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, unaweza kubaini kuwa "wote ni wale wale."

Na ukiangalia wasifu wa Maalim Seif, Mbatia na Lipumba hutoshindwa kubaini kuwa ni watu ambao tumekuwa tukiwasikia "miaka nenda miaka rudi" lakini "wakiwa upande wa pili," kwa maana "sio upande wetu" watu wa tabaka la chini. Kwa kuazima neno la mtaani, hawa ni "vigogo."

Ukweli mwingine ni kwamba mkutano huo wa Jiwe na akina Maalim Seif "ndio siasa ilivyo." Kuna kitu kwenye siasa kinaitwa "realpolitik" ambacho kwa tafsiri isiyo rasmi ni "siasa ilivyo kimatendo kuliko kinadharia/kiitikadi." 

Sasa kwenye "siasa halisi" iwe ya kitaifa au ya kimataifa, "hakuna marafiki au maadui wa kudumu bali maslahi tu." Na ndio maana licha ya msimamo wake msimamo wake mkali dhidi ya vikundi vya kigaidi, na kauli maarufu kuwa "we don't negotiate with terrorists," majuzi Marekani ilifikia makubaliano na kundi la kigaidi la Taliban.

Na jana ilifahamika kuwa Rais wa nchi hiyo Donald Trump aliwapigia simu viongozi wa kundi hilo, kitu ambacho kabla ya tukio hilo kilikuwa sio rahisi kukifikiria.Baada ya kuangalia "ukweli"(facts) huo unaojenga msingi wa uchambuzi huu, kanuni ya Linchpin inawezesha kujenga picha ya matarajio yanayohusiana na tukio/watu husika. Hapa ninamaanisha kuwa hadi kufikia hapa, yawezekana kueleza nini kinaweza kujirihivi karibuni au huko mbeleni.

Moja ni hiyo sintofahamu inayoweza kumkumba Membe baada ya kumuona Maalim Seif akiwa Ikulu na Jiwe. Ikumbukwe tu Lowassa alipoonekana Ikulu bila kutarajiwa "waumini"wake walimtetea na kuamini porojo zake kuwa kaambiwa arudi CCM lakini amegoma. Baadaye ukweli ukadhihirika baada ya Waziri Mkuu huyo wa zamani kurejea CCM.

Simaanishi kuwa Maalim Seif atakubali kurudi CCM. La hasha. Kinachoweza kutokea ni Jiwe kujaribu tena "kuua ndege wawili kwa JIWE moja." Anaweza kumfarakanisha Maalim Seif na Zitto na hapohapo kupunguza tishio kubwa kwake kutoka kwa Zitto kama Zitto, na Zitto akiwa na Maalim Seif.

Ikumbukwe tu kuwa japo Lowassa alikuwa kama 'mungu-mtu' huko Chadema, kitendo chake cha kuonekana Ikulu na Jiwe kiliwafanya hata baadhi ya "waumini" wake waanze kuwa na hofu nae.

Sina uhakika hali ikoje huko ACT-Wazalendo baada ya Maalim Seif kukutana na Jiwe, lakini ni siri ya wazi kuwa Jiwe na Zitto "picha haziivi," na wala sio jambo la kushangaza kuona Zitto hakualikwa kwenye mkutano huo.Na wala  sina hakika kama angekubali mwaliko wa Jiwe.

Kuhusu Mbatia na Lipumba, hakuna haja ya kupoteza muda kuwajadili maana "wapo kama hawapo." 

Moja ya maswali muhimu kuhusu Malim Seif kwenda Ikulu kukutana na Jiwe ni je alipata ridhaa ya Zitto na chama kwa ujumla? Na je tukio hili linaweza kuzua mpasuko huko ACT-Wazalendo? Pengine kukusaidia kuelewa vema "siasa za ACT-Wazalendo," pitia uchambuzi wangu huu nilioufanya mara baada ya Maalim Seif kujiunga ACT-Wazalendo.

Huhitaji kuwa na uelewa mkubwa wa siasa za Tanzania yetu kubaini kuwa mnufaika mkubwa wa mkutano huo kati ya Jiwe na viongozi hao watatu wa upinzani ni Jiwe mwenyewe. 

Hilo lipo wazi. Lisilo wazi ni "yanayoweza kujiri" kutokana na mkutano huo. Je Maalim Seif anaweza kuangaliwa kama "msaliti" kwa kukubali "kukutana na dikteta ambaye majuzi tu akiwa Zanzibar alikuwa anamwaga sumu kwa Dkt Shein kuhusu jinsi ya kumdhibiti Maalim Seif?"

Kwa upande mwingine, kama kweli Jiwe alikuwa na nia njema ya kukutana na viongozi wa upinzani basi pengine wa kwanza kabisa kupewa kipaumbele cha kukutana nae angekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ambaye majuzi tu alimuomba Jiwe kuwe na MARIDHIANO. Lakini ni vema "kuweka akiba ya maneno" kwani haitokuwa jambo la kushangaza tukimuona Mbowe Ikulu kama alivyoongozana na timu yake Mwanza kwenye sherehe za Uhuru Desemba 9 mwaka jana. 

Nihitimishe uchambuzi huu kwa kutahadharisha kuwa intelijensia sio sayansi timilifu (intelligence is not exact science) licha ya uchambuzi huu kuongozwa na kanuni ya Linchpin ambayo ina ufanisi mkubwa penye uwepo wa ukweli kuhusu tukio/mtu husika.


30 Jan 2015

l


Angalia dakika ya 3,14  hadi dakika ya 3,19, baadhi ya waandamanaji wanasema "TUUENI..."
Angalia pia kuanzia dakika ya 3.21 ambapo polisi wanaanza kurusha risasi (sina hakika kama ni risasi za moto au bandia) lakini kitu cha kukiangalia kwa makini ni ukweli kwamba ukiacha watu wachache wanaoonekana kutishwa na milio hiyo ya risasi, idadi kubwa tu ya watu inaonekana kutotishika. Hali hiyo inaendelea hata baada ya 'king'oling'oli' cha polisi kinapooanza kulia na hatimaye polisi kutembeza kipigo cha kinyama.

Licha ya kuumia mno kuona Polisi wakitumia nguvu kubwa katika tukio ambalo lingeweza kabisa kumalizwa kwa amani pasipo haja ya kurusha risasi japo moja au kuwapiga na hatimaye kuwakamata waandamanaji akiwemo Mwenyekiti wa CUF Prof Lipumba, kilichonipa hofu ni jinsi taratibu wananchi wanavyoanza kuota 'usugu' dhidi ya unyanyasaji wa polisi. 

Inapofika mahala wananchi wanaashiria bayana kuwa wapo radhi kuuawa, na kuwaambia polisi waziwazi kuwa TUUENI, basi kwa haki tumeshafika mahala pabaya. Na kama nilivyobainisha hapo juu, na kama inavyoonekana kwenye video hiyo, imefika mahala wananchi wameanza kuzowea sauti za risasi sambamba na mabomu ya machozi.

Hii ina maana gani? Wakati tayari wananchi wameshaonyesha kuzowea unyanyasaji na unyama wa polisi wetu na kuwa tayari kwa lolote lile, yayumkinika kubashiri kuwa kuna siku sio tu wananchi wataweka kando uoga na kuendeleza 'usugu' huo nilioueleza hapo juu bali pia wanaweza kujibi mashambulizi.

Uchambuzi mwepesi ni kwamba wakati polisi hawana njia nyingine zaidi ya hizi wanazotumia kila siku: kutumia nguvu kuvunja maandamano ya amani, wananchi wanapata nguvu mpya kwa kuondoa uoga na kuwaacha polisi wafanye watakalo. Upo uwezekano wa wananchi hao kutoishia hapo tu bali badala ya kuwaachia polisi wawaonee, WANAWEZA KUJIBU MASHAMBULIZI. Na kwa mwenendo ulivyo, hatuko mbali na hali hiyo.

Ni vigumu kubashiri ni lini polisi wetu watathamini haki za binadamu na uhai wa wananchi wasio na hatia. Ni vigumu zaidi kutarajia mabadiliko kutoka kwa mwana-CCM yoyote yule atakayemrithi Kikwete baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.Na ndio maana hujaskia yeyote kati ya waliotangaza nia ya kuwania Urais kupitia CCM akilaani unyama huo wa polisi. Walaani kwanini ilhali wao wana kinga ya kudumu dhidi ya polisi? Japo Rais kutoka chama cha upinzani anaweza kutugeuka, lakini katika mazingira ya kawaida ya kibinadamu angalau yeye naye atakuwa ameshaonja unyama wa polisi wetu na ni rahisi kwake kuchukua hatua kuliko hao wasioguswa na polisi.

Kwako msomaji, nakusihi uiangalie video hii kwa makini zaidi ya hayo niliyotanabaisha hapo juu. Jiulize, kama wanaweza kumfanyia LIPUMBA hivyo, watashindwa kukufanyia wewe, familia yako, nduguzo au jamaa zako? Sikiliza malalamiko ya huyo mwanamama katika dakika ya  6.24 na uyafanyie kazi.

TANZANIA ISIYO NA UNYAMA WA POLISI INAWEZEKANA

20 Jul 2013Na katika video hii, Lipumba anakiri kuwa alimsaidia JK katika kampenzi za uchaguzi mkuu uliopita...kwa kigezo cha dini

26 May 2013MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameibua suala zito akikihusisha chama chake na “kumnusuru” Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita.

Tanzania Daima limefahamishwa kuwa Profesa Lipumba alitoboa siri hiyo katika Msikiti wa Idrissa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, alikokwenda kuswali swala ya Ijumaa, miezi kadhaa iliyopita.

Kwa mujibu wa video ya tukio hilo, ambayo gazeti hili lina nakala yake, Profesa Lipumba alikaribishwa kuzungumza na waumini hao mara baada ya utangulizi uliotolewa na Imamu wa msikiti huo, Sheikh Ali Basaleh, aliyemtaka awaeleze Waislamu hali ya kisiasa nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano wa kiimani, Profesa Lipumba alianza kwa kuzungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, na ushindani mkali wa kisiasa uliokuwapo.

Alisema hawaoni matunda ya jitihada walizofanya kumnusuru Rais Kikwete asishindwe, kwani hata chini ya uongozi wake, Waislamu wameendelea kutothaminiwa.

“Ninyi masheikh mnajua vizuri zaidi hali ya kisiasa ilivyokuwa, kwamba ilibidi zifanyike juhudi za makusudi ili kuokoa jahazi. Lakini pamoja na kuliokoa jahazi, hali halisi inaonyesha mpaka sasa hakuna matunda yoyote yaliyopatikana, na tupo katika mtihani mgumu zaidi,” alisema.

Katika hali ambayo inasemekana ushindi wa Rais Kikwete ulipatikana kwa mbinu, huku wengine wakiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa ilimnusuru mgombea wa CCM, kauli hii ya Profesa Lipumba inadokeza kwamba anajua mkakati zaidi wa kazi ya Tume ya Uchaguzi.

Katika hali isiyo ya kawaida, Profesa Lipumba anaonekana kuhamasisha Waislamu kujipanga akisema “wenzetu wameanza kujipanga” kuelekea 2015.

“Kwahiyo kama Waislamu tunataka kupata haki zetu, kama tunataka kuishi kama raia wa daraja la kwanza katika nchi yetu, lazima tujipange kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015; na sisi tuanze kujipanga kwa sababu wenzetu wameanza kujipanga, vinginevyo tutaendelea kubaki maskini na raia wa daraja la nne katika nchi yetu wenyewe.

“Mwaka 2010 wakati mshindi wa uchaguzi wa rais alipotangazwa, mimi nilikwenda kwenye hafla ya kutangazwa matokeo, na nilikwenda makusudi tu, siyo kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, ila nilikwenda makusudi kwa kujua hali ya kisiasa ilivyokuwa wakati huo.

“Huku nilikutana na Sheikh Basaleh. Nilipokutana naye, alinipongeza; sijui kama yeye anakumbuka, akaniambia ‘umeweka mbele imani yako na umekuwa mwelewa wa mambo.’”

Hata hivyo, licha ya Profesa Lipumba kuwaambia Waislamu wajipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu, hakusema wajipange kupitia chama kipi.

Lakini alisisitiza kwamba uchaguzi ujao ni zaidi ya siasa au rais yupi anafaa, bali maslahi, hasa ya rasilimali nyeti zinazopatikana katika ukanda wa Pwani ya Mashariki, eneo ambalo alisema linakaliwa zaidi na watu wenye imani ya Kiislamu.

Katika moja ya kauli zake, Profesa Lipumba alisema kwamba kuna chama kimoja kinataka kuchukua madaraka ya nchi, lakini kinasaidiwa na mataifa ya magharibi, yasiyoenzi wala kuthamini imani ya Kiislamu.

Kwa muda sasa, zimekuwapo tetesi kwamba CCM imekuwa inafanya siasa za udini dhidi ya vyama vya upinzani, hasa inapoona maslahi yake yapo hatarini.

Mwaka 2010 makada kadhaa wa CCM walitumia mitandao ya simu kuchonga (spoofing) ujumbe wa simu ulioshambulia mgombea mmoja wa upinzani, ukimhusisha na imani yake.

Kauli ya Lipumba imethibitisha pia minong’ono iliyokuwapo muda mrefu kuwa baadhi ya kura za Profesa Lipumba zilipotelea kwa Rais Kikwete.

Katika uchaguzi huo, Lipumba alitangazwa kushika namba ya tatu, nyuma ya Rais Kikwete na Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA.

Alipoulizwa kuhusu ziara yake msikitini na kauli aliyotoa, Profesa Lipumba alikiri kwamba alikwenda kuzungumzia hali ya kisiasa nchini. Hata hivyo alisema inawezekana video hiyo imechakachuliwa kwa kuungaunga vipande vya matamshi wanavyovitaka badala ya hotuba nzima.

Hata hivyo, video iliyotazamwa na waandishi wa habari hii, ambayo nakala yake imetunzwa na gazeti hili, haionekani kukatwakatwa.

Katika tukio hilo, Sheikh Baseleh ndiye anayeanza kuzungumza huku akisoma kipande cha gazeti lililomnukuu Waziri wa Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu, akizungumzia mchakato wa katiba, kwamba Tume ya Katiba “haitazingatia maoni ya wachache”, na kwamba mambo ya dini yasiingizwe kwenye katiba.

Katika ufafanuzi wake, Sheikh Basaleh anasema Dk. Nagu alizungumza mambo haya mbele ya waumini wa Kanisa la Chang’ombe kwenye uzinduzi wa kwaya; na kwamba miongoni mwa mambo ambayo yanaitwa ya kidini yasiyotakiwa kuingizwa kwenye katiba ni Mahakama ya Kadhi Mkuu.

Baadaye anamkaribisha Profesa Lipumba, ambaye naye katika hotuba yake, pamoja na mambo mengine, anakosoa msimamo wa serikali kutaka Waislamu waanzishe mahakama yao ya kadhi, akisema mahakama ni chombo cha dola ambacho hakipaswi kuwa nje ya mfumo wa serikali.

Mara baada ya Profesa Lipumba kuhitimisha hotuba yake, Sheikh Basaleh alimkaribisha Sheikh Musa Kundecha, ambaye naye alisisitiza kauli ya Profesa Lipumba kuwataka Waislamu wajipange kwa ajili ya 2015.

Vile vile alifafanua kuwa “wachache” waliozungumzwa na Dk. Nagu ni Waislamu, kwani zilishatoka taarifa katika kituo cha TBC kuwa idadi ya wasiokuwa Waislamu nchini ni asilimia 52.

“Mimi sijaiona hiyo video ila nimeisikia tu kuwa ipo inauzwa mitaani na makanisani, lakini inawezekana waliorekodi wamenichakachua maana imekuwa siku nyingi kidogo tangu niende kuongea pale Msikiti wa Idrissa. Yamewezekana wameungaunga vipande wanavyovitaka ili kunipaka matope mimi na CUF kuwa tuna udini,” alifafanua Profesa Lipumba.

Alipotakiwa akutane na waandishi wa habari hii ili waiangalie kwa pamoja video hiyo ili kujua ukweli kama ni video halisi au ya kuchakachua, Profesa Lipumba alisema waandishi waende kumwona Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma, Abdul Kambaya.

Alipopigiwa simu, Kambaya hakutoa ushirikiano kwa waandishi. Badala yake aliwashambulia kuwa wana ajenda ya siri dhidi ya CUF, akisema wanafuatilia na kuona makosa ya viongozi wa CUF tu na kufumbia macho vitendo vya wanasiasa wengine wanapokwenda makanisani.

“Nyie waandishi wa Tanzania mmezidi, yaani ninyi mnaona matendo ya viongozi wa CUF tu, wengine wakienda makanisani mbona hawafuatiliwi? Mbona hamumfuatilii Lowassa akienda makanisani? Au mbona hamsemi Dk. Slaa akienda kanisani? Sasa Profesa akienda msikitini kuongea na Waislamu wenzake kuna kosa gani? Sasa ninyi andikeni chochote,” alifoka na kukata simu.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro alipotakiwa kuzungumzia video hiyo, alikataa katakata na kuwashauri waandishi wawasiliane na ama Profesa Lipumba mwenyewe au Kambaya.

Itakumbukwa kuwa kumekuwepo tuhuma dhidi ya Rais Kikwete na CCM kuwa mwaka 2010 waliendesha propaganda chafu za udini zenye lengo la kuwagawa Watanzania hususan Wakristo na Waislamu kwa manufaa yao ya kisiasa.

Mwelekeo huo wa kisiasa wa Rais Kikwete na CCM unadaiwa kutokana na hatua ya viongozi wa Kanisa Katoliki nchini kupitia Idara ya Uchungaji kutoa waraka maalumu uliowataka Watanzania kuchagua viongozi waadilifu.

Waraka huo haukuifurahisha CCM, ambayo imekuwa inagubikwa na tuhuma nyingi za ufisadi. Makada na viongozi wa CCM walijaribu kuupinga kwa kuupotosha, wakisema unaingiza mambo ya dini katika siasa.

Kanisa Katoliki lina utaratibu wa muda mrefu wa kutoka nyaraka kuelekeza waamini na wananchi juu ya mambo ya msingi katika jamii.

Katika hali hiyo, Rais Kikwete na CCM wanadaiwa kukimbilia kwa viongozi wa Kiislamu na kuwaomba wawaunge mkono kwa kuwajaza maneno ya uongo, kwamba Wakatoliki walikuwa wamewaagiza waumini wao kupigia kura wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Inadaiwa waliwafitinisha zaidi kwa kuwaeleza kuwa aliyekuwa mgombea kiti cha rais wa CHADEMA katika uchaguzi huo, Dk. Willibrod Slaa ambaye ameshawahi kuwa Padri, alikuwa ametumwa na Kanisa Katoliki ili kuendeleza utawala wa Kikristo nchini.

Propaganda hizo hazikuishia kwa viongozi na waumini wa Kiislamu tu, bali zilielekezwa pia kwa viongozi na wafuasi wa CUF ambao walirubuniwa na kushawishiwa kumpigia kura “Muislamu mwenzao” Rais Kikwete, huku wakiahidiwa kuwa mwaka 2015 Waislamu wa CCM nao watampigia kura mgombea wa CUF kwa hoja kuwa CCM watakuwa wamesimamisha mgombea Mkristo.

Licha ya madai hayo ya udini kuwa wazi kwa muda mrefu, lakini wakati wote Rais Kikwete na CCM wamekuwa wakikanusha tuhuma hizo na kuziita kuwa uongo na uzushi.


CHANZO: Tanzania Daima

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube