29 Jan 2015

Enzi hizo: Rais Kikwete akiwa na James Rugemalira

RAIS Jakaya Kikwete anapaswa kuwajibika binafsi katika kashfa ya ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Tegeta Escrow. Saed Kubenea anaandika…(endelea)

Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mabere Marando amesema, Rais Kikwete, ndiye aliyeruhusu kiasi cha Sh. 321 bilioni kuchotwa katika mazingira yaliyosheheni udanganyifu.

“Fedha zile zimechukuliwa kwa maelekezo ya Rais Kikwete ili kumuwezesha chama chake kufanikishe kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” ameeleza Marando.

Hata hivyo, Marando anasema, “Tumeambiwa na watu waliokaribu na chama hicho, kuwa ni sehemu ndogo sana ya fedha iliyoibwa zilizofikishwa CCM. Nyingi ya fedha hizo zimechukuliwa na familia ya rais mwenyewe.”

Taarifa zinasema, familia ya Rais Kikwete imepata zaidi ya Sh. 9 bilioni, kutoka katika mgawo wa fedha zilizohifadhiwa katika akaunti ya Escrow.


“Kikwete anajua kila kitu. Yule singasinga – Harbinder Singh Sethi – alitokea Ikulu. Mpango wa uchotaji wa fedha za umma ulipangwa Ikulu na ulitekelezwa kwa maelekezo ya rais,” ameeleza.


Taarifa zinasema, anayejiita na kuitwa na serikali kuwa ni “mmiliki mpya wa IPTL/PAP,” Harbinder Singh Sethi, alichotewa fedha hizo baada ya kufikishwa Ikulu na baadaye akakutanishwa na gavana wa BoT, Prof. Benno Ndullu; na kutoka hapo alikwenda kukwapua mabilioni hayo ya shilingi hata bila kumfahamisha James Rugemalira – mbia mwenzake.

Sakata la ukwapuaji wa fedha katika akaunti ya Escrow ndilo lililomtupa nje ya ofisi, aliyekuwa waziri wa nishati, Prof. Sospeter Muhongo.

Taarifa zinasema, Prof. Muhongo, ni miongoni mwa wanaotajwa kunufaika na fedha za Escrow zilizopitia benki ya Stanbic. Mwingine ambaye jina lake lilitajwa bungeni na mmoja wa wabunge wa upinzani, ni Albert Marwa.

Marando anasema, “Pamoja na kujiuzulu kwa Prof. Muhongo, bado haitoshi bila kuhojiwa au kuwajibishwa kwa gavana Ndullu, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Katibu Mkuu wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwalile na maofisa wa ikulu na hata rais mwenyewe ambaye ndiye aliyeruhusu fedha hizo kutolewa.”

Akiongea kwa kujiamini, Marando anasema, “Wizi huu ulianzia Ikulu na umefanyika kwa baraka za Ikulu na mbele ya macho ya rais. Umewashirikisha baadhi ya maofisa wake na hata familia yake.”

Dk. Likwalile ndiye aliyewasilisha kwa gavana wa BoT kwa ajili ya utekelezaji, maagizo ya Rais Kikwete kuwa fedha katika akaunti ya Escrow zilipwe kwa PAP.

Alikuwa akirejea maagizo kutoka kwa Rais Kikwete kwa kunukuu barua ya tarehe 13 Novemba 2013, ambayo ilisainiwa na Katibu wa Rais, Bw. Prosper Mbena.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.