19 Feb 2015


WIKI iliyopita kuliibuka video ‘ya kutisha’ ambayo msemaji katika video hiyo alidai kuwa yeye na wenzake ni kundi ambalo limekuwa likivamia vituo vya Polisi na kupora silaha.
Kadhalika, msemaji huyo ambaye licha ya kujitambulisha kama Abu (magaidi wengi hupendelea jina hilo japo si kila Abu ni gaidi) hakubainisha jina la kikundi chake.


Vilevile, msemaji huyo aliyeficha sura yake kwa kifunika-uso (balaclava) na miwani nyeusi ya jua (sunglasses) alidai kuwa kundi lake limefanikiwa kupora silaha katika vituo vya Polisi huko Ushirombo, Ikwiriri na Tanga, na walifanya hivyo pasipo kutumia silaha yoyote.
La kuogofya zaidi, msemaji huyo alidai kwamba tayari wana mtaji wa ‘roho tano za polisi,’ akimaanisha wameshauwa polisi watano.


Japo nina ujuzi wa wastani tu kuhusu masuala ya ugaidi, zaidi kwa kufuatilia habari zinazohusu suala hilo na harakati za vikundi vya kigaidi duniani, nikiri kwamba nilipoiona video hiyo kwa mara ya kwanza niliamini. Sababu kubwa ya kuiamini ni kwamba tishio lililomo kwa video hiyo lilionekana halisi.


Hata hivyo, baada ya kuiangalia mara kadhaa, nilijikuta nikipatwa na maswali kadhaa. Miongoni mwa maswali hayo ni:


Kwanini msemaji anaonekana kama anafikisha ujumbe kwa Inspekta Jenerali wa Polisi ‘kwamba hawezi kazi’ kwa vile ameshindwa kuwakamata ‘magaidi’ hao? Kwa uchambuzi wa haraka, katika hilo ni kama ‘magaidi’ hao wana lengo la kumchafua tu IGP.


Katika video hiyo, ‘magaidi’ hao wanamtaja Rais kwa kumuita ‘Mheshimiwa Rais.’ Hii si lugha ya kawaida kwa magaidi halisi.Kwa sababu pamoja na mambo mengine, malengo yao huendeshwa na chuki kwa utawala uliopo madarakani. Licha ya kumuita Rais ‘Mheshimiwa,’ msemaji anaonekana kumshawishi ‘Mheshimiwa Rais’ kuwa hana polisi, na kwamba hawajaona jeshi dhaifu kama la polisi. Hapa tena inaonekana lengo la msemaji au kikundi hicho ni kulichafua jeshi la polisi.

Ni kawaida kwa vikundi vya kigaidi wanapotoa tishio kama hilo la kwenye video hiyo kutaja madai yao. Labda kama video hiyo ni mwanzo wa mfululizo wa video, ingetarajiwa msemaji huyo kueleza kuwa lengo lao ni nini na madai yao ni yapi.
Linaloshabihiana na hilo ni video hiyo kutotajwa mlengwa wa ‘hasira’ zao ni nani. Pamoja na msemaji kutumia maneno ya Kiarabu na kutamka ‘ujumbe kwa vijana wa Kiislamu’, hakuna mahala katika video hiyo ambapo wanazungumziwa wasio- Waislam (kwa mfano Wakristo) wala serikali au taasisi zake au taasisi binafsi au mtu/kundi la watu.
Pamoja na maswali hayo, haimaanishi kuwa ujumbe huo ni wa ‘kizushi’ tu. Kama nilivyeoeleza awali, tishio lililomo katika video hiyo linaonekana kuwa halisi. Tatizo ni katika uwasilishaji wake kama nilivyoonyesha hapo juu. Hata hivyo, kasoro hizo zaweza kuwa ni za kiufundi tu.
Kinachochanganya zaidi ni ukweli kwamba takriban siku moja baada ya kuibuka video hiyo, zilipatikana habari za mapambano makubwa kati ya jeshi la polisi likisaidiwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) na kikundi kimoja kwenye Mapango ya Amani huko Tanga.
Mkanganyiko zaidi ni kuhusu utambulisho wa kikundi hicho. Wakati baadhi ya vyombo vya habari vimeliita kundi hilo ‘magaidi wa Al-Shabaab,’ vingine vimedai ni kikundi chenye uhusiano (affiliated) na magaidi hao wa Somalia, huku vyombo vingine vya habari vikieleza kuwa kundi hilo ni genge tu la wahuni (thugs), kama maelezo ya Kamanda Chagonja wa polisi yalivyotanabaisha.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika vyombo mbalimbali vya habari, baadhi ya wakazi wa eneo husika wamedai kuwa kundi hilo ni la kigaidi, huku wakililaumu jeshi la polisi kwa kuficha ukweli, na kuhoji iweje nguvu kubwa kiasi hicho itumike kukabiliana na genge la wahuni tu.
Taarifa zinadai kuwa polisi mmoja aliuawa katika mashambulio hayo na wengine kadhaa kujeruhiwa. Hata hivyo, Kamanda Chagonja alinukuliwa akidai kuwa ‘wahuni’ hao walifanikiwa kutoroka.
Wakati kiongozi huyo mwandamizi wa jeshi la polisi akieleza kuwa genge hilo si la magaidi, huhitaji uelewa wa fani ya uchunguzi wa kipelelezi kujiuliza “amejuaje ilhali hawakufanikiwa kumkamata japo mhusika mmoja wa kundi hilo?”
Nadhani moja ya matatizo ya mwanzo kabisa katika sakata hili la Amboni na lile la video ya ‘magaidi’ ni ukweli kwamba jeshi la polisi haliaminiki kabisa na linachukiwa na Watanzania wengi.
Sababu za kuchukiwa zipo wazi; ukiukwaji wa hali ya juu wa haki za binadamu, sambamba na ukandamizwaji demokrasia kwa uonevu wa waziwazi dhidi ya vyama vya upinzani na viongozi na wanachama wao, pamoja na rushwa iliyokithiri ndani ya chombo hicho cha dola, kama ilivyothibitishwa na utafiti mmoja wa hivi karibuni.
Hadi wakati ninaandika makala hii kumeshajitokeza madai kuwa matukio hayo mawili ni mkakati wa jeshi la polisi kuandaa mazingira ya kuvibana vyama vya upinzani. Baadhi ya watu wanadai kuwa jeshi la polisi linaweza kuwa linaandaa mkakati wa kupiga marufuku shughuli za kisiasa za wapinzani, kama vile mikutano ya hadhara na maandamano, kwa kigezo cha ‘tishio la ugaidi.’
Baadhi ya wananchi wanayahusisha matukio hayo na ‘hadithi’ ya aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Omari Mahita, alipotoa tuhuma nzito siku moja kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kuwa chama cha CUF kimeingiza makontena ya visu na majambia kwa minajili ya kuvuruga uchaguzi huo.
Pengine kilichonichekesha wakati ninatafakari kuhusu matukio haya mawili, ni bandiko la mwanachama wa mtandao mahiri wa kijamii, Jamii Forums, aliyehitimisha kuwa, ninamnukuu, “Chagonja na sinema ya mwaka: Unajivamia, unajiteka, unajitorosha, unajisaka, na hatimaye unatangaza kujitafuta kwa udi na uvumba. Matukio yote haya hayana majina ya waathirika. Kweli siasa zimefika mahali pake. Tutashuhudia mengi 2015”
Huwezi kuwalaumu wanaohisi matukio hayo mawili ni ‘mchezo mchafu tu’ hasa ikizingatiwa kuwa licha ya polisi kutoaminiwa na kuchukiwa, chama tawala CCM ni mahiri kwa ‘uzushi’ dhidi ya wapinzani wake.

Ninaamini wengi mwakumbuka kuhusu tuhuma lukuki dhidi ya Chadema, kutoka chama cha Kikristo, cha Wachagga, na hatimaye cha kigaidi. Tumeshuhudia pasi aibu CCM ikijaribu kuwahusisha wapinzani na maafa yaliyofanywa na jeshi la polisi, hadi kufikia hatua ya kudai kuwa Chadema ndio waliomuuwa mwandishi Daudi Mwangosi aliyeuawa kikatili na jeshi la polisi.
Kwa hiyo tupo njia panda. Yawezekana kabisa kuwa tukio la video yenye tishio la kigaidi ni ya magaidi kweli na kundi lililokuwa limejificha Mapango ya Amboni kuwa ni la kigaidi halisi, lakini rekodi za polisi na CCM zinaleta ugumu katika kuamini kipi ni cha kweli na kipi ni usanii tu.
Hilo lina madhara makubwa kwa sababu kama kweli matukio hayo ni ya kigaidi, kinachohitajika si nguvu za vyombo vya dola pekee bali ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwa wananchi. Lakini hali ilivyo sasa hasa kuhusu jeshi la polisi ni mbaya, japo watawala wetu hawaonekani kujali.
Na iwapo matukio hayo ni ya kigaidi kweli, tuna matatizo mawili makubwa: mipaka yetu ipo ‘porous’ sana (inapenyeka kirahisi, na ushuhuda ni jinsi ‘unga’ unavyoingizwa na kutoka kirahisi kana kwamba ni bidhaa halali inayoingizwa na kutolewa nchini kihalali). Na tatizo la pili ni rushwa.
Japo ni vigumu kuzuwia ugaidi kwa asilimia 100, nchi ilivyotapakaa rushwa inafanya mapambano dhidi ya ugaidi kuwa magumu mno kwa vile rushwa inawawezesha magaidi kununua fursa ya kufanya hujuma zao kirahisi.
Nimalizie makala hii kwa kutoa wito kwa mamlaka husika kuyachukulia matukio hayo mawili kwa uzito mkubwa, sambamba na kumsihi Rais Jakaya Kikwete kuupa uzito uhasama kati ya wananchi na polisi.
Kadhalika, pamoja na kutokuwa na imani nalo, ninalisihi jeshi la polisi kujaribu kuwa wazi katika kuripoti matukio mbalimbali yanayohusu usalama wa raia na nchi kwa ujumla.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.