Hii ni mara ya pili kwa serikali ya Kenya kuchukua hatua
hiyo, ambapo mwaka jana ilitangaza amri hiyo ya kuzuwia magari yaliyosajiliwa
Tanzania kuchukua, kushusha au kubadilishana abiria katika uwanja wa kimataifa
wa Jomo Kenyatta.
Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Utalii, Biashara na
Masuala ya Afrika Mashariki wa nchi hiyo, Phyllis Kandie, hatua hiyo mpya
inafuatia kupita kwa muda wa wiki tatu zilizoombwa na Waziri mwenzie wa
Tanzania, Lazaro Nyalandu, ili yafanyike majadiliano kuhusu suala hilo, lakini muda
huo ulipita pasi ofisa yeyote wa Tanzania kujitokeza.
“Wiki hizo tatu zimepita bila wenzetu wa Tanzania kujitokeza
kwa ajili ya majadiliano. Kwahiyo tumeendelea mbele kutekeleza makubaliano ya
pande mbili,” alisema Waziri Kandie akirejea Mkutano wa Tano wa Kisekta wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhusu mwafaka wa utalii na wanyamapori.
Suala hili lilionekana kutawala mijadala mwishoni mwa wiki
katika mitandao ya kijamii hususan Twitter na Facebook, huku Mbunge wa Kigoma
Kusini (Chadema) Zitto Kabwe akitoa wito kwa Tanzania kulipiza kisasi kwa
kuzuwia ‘maziwa ya Rais Uhuru Kenyatta.’ Namnukuu, “Naona ndugu zetu wa Kenya
wameamka. Mjadala umeisha! Mnaendelea na ban yenu, we respond in kind. Rais
wenu atafute pa kuuza maziwa yake (akimaanisha maziwa chapa Brookside
yanayodaiwa kutengenezwa na kiwanda kinachomilikiwa na Rais Uhuru Kenyatta).”
Baadaye, mwanasiasa machachari wa Kenya, Seneta Mike Sonko,
naye aliingilia kati mjadala huo na kudai angekwenda Tanzania kumtaka Zitto
aombe radhi “kwa kumtisha na kumtapeli Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Uhuru Kenyatta.”
Kwa mtizamo wangu, wakati ninadhani Kenya wanapaswa kuwa
wastahimilivu katika kusaka ufumbuzi wa suala hilo, ninawaona watendaji wetu
serikalini kama wahusika wa moja kwa moja kwa ‘uzembe’ wao. Kwa upande mmoja,
maelezo ya Waziri Kandie kwamba maafisa wa serikali yetu hawakufanya lolote
katika muda wa wiki mbili waliiomba wapewe kushughulikia suala hilo,
yanaashiria uzembe wa wazi. Busara ndogo tu zinatosha kueleza kuwa kama pande
mbili zenye mgogoro zimeafikiana kukutana baada ya muda flani, kisha pande moja
‘ikapuuzia,’ hiyo inatoa fursa kwa upande mwingine kuchukua hatua inazoona
zinafaa.
Kwa vile sie tumeruhusu nchi yetu kuwa ‘uwanja wa wazi’ kwa
wafanyabiashara halali na hata haramu (kama wauza mihadarati) haimaanishi
majirani zetu nao wafuate ukosefu huo wa busara. Ni katika mazingira kama haya,
licha ya nchi yetu kuwa pekee kwa ‘uzalishaji’ wa madini ya Tanzanite, ni India
na Kenya zinazoongozwa kwa mauzo ya madini hayo duniani.
Kwa upande mwingine, tatizo hili la sasa la Kenya kupiga
marufuku magari ya uchukuzi wa watalii yenye usajili wa Tanzania ni matokeo ya
uzembe mwingine mkubwa wa kupuuzia kurejea uhai wa shirika letu la ndege na
kuboresha viwanja vyetu vya ndege hasa ule wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Haiingii akilini kabisa kwa nini nchi yetu yenye umri wa
zaidi ya nusu karne isiwe na shirika lake la ndege lenye uwezo wa kutoa huduma
za kimataifa, ilhali wenzetu Kenya sio tu wana shirika lao la ndege bali ni
Kenyan Airways ni miongoni mwa mashirika ya ndege makubwa duniani.
Sie tunaendekeza ngonjera kila kukicha. Mara ATCL imepata
mwekezaji kutoka Uarabuni, mara China inakuja kuwekeza...alimradi ni mwendelezo
wa porojo tu zinazoambatana na ufisadi. Ripoti mbalimbali zimeonyesha jinsi
gani ATCL ilivyouawa ikiwa hai na jitihada za ufisadi zinavyokwamisha kufufuka
kwake. Kama ilivyo kwa ufisadi kwenye maeneo mengine, waliofisadi shirika hilo
wakati wa uhai wake, na wanaofisadi likiwa mfu bado wapo mtaani, hali
inayowashawishi mafisadi watarajiwa kuendeleza uhalifu.
Mara kadhaa utasikia viongozi wetu wakienda ng’ambo
kutangaza vivutio vya utalii nchi mwetu. Sawa hilo ni jambo la manufaa, lakini
sambamba na hatua hiyo ilipaswa viongozi hao kuwekeza vya kutosha katika
kuboresha miundombinu ya utalii, ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege. Majuzi
tu nilitumiwa video inayoonyesha jengo la wageni maalum katika Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar, likiwa linavuja ‘chapa chapa’
kutokana na mvua.
Ni muhimu kutambua kwa hawa wenzetu huku Ulaya, kwa mfano,
likizo zinazoambatana na kutembelea nchi za nje ni moja ya mambo muhimu mno
maishani. Baada ya kujituma vya kutosha, na kuhifadhi fedha zao, wanafikia
uamuzi wa kutembelea sehemu flani kama watalii. Na hawa sio kama sie wa
kuvumilia mgao wa umeme milele; they never settle for less (hawakubali kupewa
pungufu ya kile wanachostahili). Sasa mtalii anapofika Tanzania mara ya kwanza
na kukuta ukumbi wa kupokelea wageni unavuja kama umeezekwa kwa nyasi, ni wazi
tushampoteza mtalii huyo. Na pia wenzetu wana kawaida ya kutoa ‘reviews’ kuhusu
maeneo ya utalii. Kwa maana hiyo ‘kumuudhi’ mtalii mmoja kwaweza kupelekea
kupoteza watalii tarajiwa kadhaa.
Nimekuwa nikizungumzia suala hili mara kadhaa: sie hatuna
uhaba wa sera na mipango mizuri. Ukisikia hotuba za bajeti za mawaziri wetu, au
wanapopiga porojo kwenye mikutano ya ndani na nje ya nchi, hutoonekana wa ajabu
ukidhani ni mawaziri kutoka ‘nchi ya dunia ya kwanza.’ Utasikia maelezo matamu
na mikakati ya kimapinduzi lakini tatizo ni kwenye utekelezaji. Na kikwazo
kikubwa cha utekelezaji wa sera au mipango hiyo ni kutanguliza mbele maslahi
binafsi badala ya maslahi ya taifa. Vitambi vyao, mahekalu yao, idadi ya magari
yao, na hata ustawi wa ‘nyumba ndogo’ zao vinakuwa na umuhimu mkubwa kuliko
maendeleo ya taifa letu au urithi kwa vizazi vijavyo.
Wakati mjadala kuhusu zuio hilo la magari yetu kuingia
nchini Kenya ukiendelea, kulijitokeza mawazo kuwa rafiki wa kweli wa Tanzania
sio katika Ushirikiano wa Afrika Mashariki bali Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika (SADC). Ukweli ni kwamba hakuna rafiki atakayekuwa na faida kwetu
kama sie wenyewe hatujithamini wala kufanya jitihada za kuonekana wa maana kwa
nchi nyingine. Ni muhimu kukumbuka kwamba Mwalimu Nyerere alitufundisha kuwa
ili tuendelee twahitaji ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Hakutaja
marafiki, kwa sababu nchi yenye maendeleo lazima itapata marafiki. Raslimali
tunazo ‘bwerere,’ na watu wapo takriban milioni 50. Uongozi bora na siasa safi
je? Hapo ndio tunapokwama.
Basi nimalizie makala hii kwa kutarajia kuwa tatizo hilo
kati ya nchi yetu na majirani zetu wa Kenya litamalizwa karibuni. Hata hivyo,
ufumbuzi wa kudumu haitoishia kwa Kenya kuruhusu magari ya ukuchuzi wa watalii
yenye usajili wa Tanzania bali sie wenyewe kuhakikisha kuwa tunafufua shirika
letu na ndege na kuliwezesha kufanya safari za kimataifa kama ilivyo kwa Kenyan
Airways, sambamba na kuboresha viwanja vyetu vya ndege, hususan KIA ili tuache
utegemezi kwa viwanja vya ndege vya nchi jirani, kwa mfano huo wa Jomo
Kenyatta.
Viongozi wetu wakiacha porojo, uzembe na kutafuta visingizio
visivyo na kichwa wala miguu, basi hakuna cha kutukwamisha kufanikiwa.
0 comments:
Post a Comment