5 Mar 2015

"NI wajinga wa kisiasa pekee wanaoweza kudharau mchango wa Marehemu Komba katika siasa za Tanzania. Nimeona kuna watu wanabwabwaja sana!" Hii ni kauli ya Profesa Kitila Mkumbo aliyoitoa Jumapili iliyopita, katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
MSOMI huyo ambaye pia ni mwanasiasa alitamka hivyo kufuatia mpasuko mkubwa uliojitokeza (angalau katika mtandao wa intaneti) kufuatia taarifa za kifo cha mwanasiasa maarufu na Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM) Kapteni John Komba, kilichotokea Jumamosi jijini Dar es Salaam.
Japo inafahamika kwa idadi ya Watanzania wanaitumia mtandao wa intaneti ni ndogo sana kulinganisha na idadi ya Watanzania wote, kwa kiasi fulani mada zinazotawala mtandaoni huweza kuakisi hali halisi iliyopo 'mtaani.' Ni kwa mantiki hiyo, ninashawishika kuhisi kuwa mpasuko uliojitokeza mtandaoni kufutia kifo cha Kapteni Komba waweza pia upo mitaani pia.
Mpasuko huo ulichukua sura ya makundi mawili, moja likionekana kufurahia kifo cha mwanasiasa huyo huku likifanya marejeo ya kauli zake mbalimbali hasa ile ya wakati wa Bunge Maalum la Katiba kuwa angeingia msituni iwapo pendekezo la muundo wa Muungano wa serikali tatu lingepitishwa.
Kundi jingine lilikuwa la waombolezaji, wananchi walioguswa na kifo hicho, huku wakilaani vikali 'jaribio lolote la kumlaumu marehemu.' Katika kundi hili, kulijitokeza 'mapadri na mashehe' walionukuu Biblia Takatifu na Kuran Tukufu kukumbushia umuhimu wa kuenzi marehemu na kuheshimu kifo.
Lakini ndani ya makundi hayo kulijitokeza 'waliouma na kupuliza,' yaani kwa upande mmoja wakionyesha jinsi walivyokwazwa na baadhi ya kauli za marehemu Komba hususani zilizokua zinachochea chuki na uhasama wa kisiasa na kijamii, lakini upande mwingine wakidai kuwa 'si vizuri kumsema vibaya marehemu.'
Kama nilivyotanabaisha hapo juu, sina hakika hali ikoje huko mitaani lakini yayumkunika kuhisi kuwa idadi ya waombolezaji ni kubwa kuliko ya 'wanaomwandama marehemu.' Idadi kubwa ya waombolezaji yaweza kusababishwa zaidi na 'uoga wetu wa kawaida kwa kifo' kuliko kuguswa na kifo husika.
Japo sote twatambua kwa uhai wetu una kikomo kwa njia ya kifo, na japo hatuna la kufanya kubadili ukweli huo mchungu, twaendelea kukiogopa kifo huku vifo vya watu wa karibu au tunaowafahamu vikitukumbusha tena na tena kuwa kifo kipo.
Kwa namna flani ya kusikitisha, kuna nyakati vifo huwa nafasi ya kushuhudia unafiki wa baadhi yetu kama wanadamu. Ni mara ngapi tumeshuhudia, kwa mfano, baadhi ya vijana wakiteketeza uhai wao kwa matumizi ya madawa ya kulevya, lakini jamii ikiwatelekeza, na kisha kumwaga lundo la rambirambi pale wanapofariki? Sawa, rambirambi ni ishara ya kuguswa na kifo, lakini ina faida gani hasa pale upendo ungeweza kuepusha kifo hicho?
Kwa upana zaidi, kuna haja gani kumpenda mtu baada ya kufariki ilhali alipokuwa hai alichukiwa? Upendo huo wa ghafla ni nini zaidi ya unafiki kwani wakati mwafaka tunapohitaji upendo ni tunapokuwa hai.
Kilichojitokeza baada ya kifo cha marehemu Kapteni Komba, ambapo baadhi ya wenzetu wameonekana 'kufurahia,' ni mwendelezo wa chuki katika Tanzania yetu, huku baadhi ya wanasiasa wa CCM wakiwa ndio wahusika wakuu.
Sawa, sio vema kuzungumzia 'mabaya' ya marehemu Komba, kwa mfano, lakini kwa bahati mbaya au makusudi, ukiweka kando umahiri wake katika nyimbo za maombolezo ya kifo cha Baba wa Taifa, marehemu Julius Nyerere, kumbukumbu muhimu ya hivi karibuni ni lugha kali aliyoitumia wakati wa Bunge Maalum la Katiba.
Yeye, pamoja na 'waeneza chuki' wengine walifikia hatua inayoweza kutafsiriwa kama kumtakia kifo Jaji Joseph Warioba kwa vile tu Tume aliyoongoza kukusanya maoni ya Katiba ilipendekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu.
Lakini ishara kuwa chuki inazidi kutawala katika Tanzania yetu zilianza kujitokeza kwa wazi zaidi pale Rais Jakaya Kikwete alipolazwa nchini Marekani kwa matibabu ya tezi dume. Wakati idadi kubwa tu ya Watanzania ilijitokeza kumtakia Rais wetu uponyaji wa haraka, kulikuwa na kundi dogo ambalo halikuficha hisia zao, kiasi cha baadhi yao kutaka Rais asirudi akiwa hai. Kwa lugha nyingine, wenzetu hawa walikuwa wanamwombea kifo Rais wao.
Kwa bahati mbaya au makusudi, hakuna jitihada zilizofanyika japo kuanzisha mjadala tu kuhusu ustawi wa chuki katika nchi yetu. Na matokeo yake, leo hii twashuhudia baadhi ya wenzetu wanaoonekana kufurahia kifo cha mwanasiasa wetu mahiri.
Ni rahisi kuitazama chuki hii kama ujinga, kama alivyotanabaisha Profesa Kitila, lakini binafsi ninaamini hili ni swali gumu lisilostahili majibu rahisi. Kwa mtizamo wangu, moja ya sababu za chuki hiyo inaweza kuwa ni pengo la kitabaka kati ya watawala na watawaliwa, sambamba na pengo linalozidi kukua kati ya wenye nacho na wasio nacho.
Lakini chuki hiyo inachangiwa pia na jeuri ya watawala wetu, kusahau kuwa 'kesho kuna kifo,' kuropoka kila baya hasa kwa wapinzani wao kisiasa, na kuwadharau wananchi ambao kimsingi ndio waajiri wa watawala hao.
Kauli za baadhi ya wanasiasa mahiri kwa 'kusema ovyo' kama ile ya 'vijisenti' ya Mbunge wa Bariadi (CCM) Andrew Chenge, hii ya majuzi ya 'shilingi milioni 10 za kununulia mboga (labda ni tembo mzima)' ya Profesa Anna Tibaijuka, ile ya Profesa Muhongo kuwa 'Watanzania hawawezi kuendesha biashara ya gesi na mafuta bali wanamudu biashara ya matunda tu,' na nyinginezo nyingi, zinachangia kushamiri kwa hasira za baadhi ya wananchi kwa baadhi ya viongozi wao.
Tuna wanasiasa kama LivingstonLusinde, maarufu kama 'kibajaji’, Nape Nnauye, William Lukuvi, Stephen Wassira na Mwigulu Nchemba (japo huyu amekuwa na nafuu sasa), ambao wakizungumzia vyama vya upinzani wanaweza kumwaminisha msikilizaji kuwa wapinzani ni viumbe hatari kuliko magaidi wa Al-Shabaab, Boko Haram au ISIS.
Wanajitahidi sana kupamba mbegu za chuki, na kwa hakika wamefanikiwa kwa kiasi fulani. Lakini uongozi wa juu wa chama hicho tawala haujawahi kukemea kauli hizo za chuki, yayumkinika kuhisi kuwa ujenzi wa chuki ni miongozi wa sera zisizo rasmi kwa chama hicho, kama ilivyo ufisadi.
Ni muhimu kwa watawala wetu kujifunza kitu katika chuki hii inayolitafuna taifa letu. Kinachotufanya tuendelee kumlilia Baba ya Taifa hadi leo ni matendo yake ya kuigwa mfano wakati wa uhai wake.
Yawezekana kama binadamu mwingine, Mwalimu aliwahi kuwakwaza baadhi ya Watanzania, lakini 'hukumu ya jumla' kwa matendo yake wakati wa uhai wake ni kwamba aliweka mbele maslahi ya taifa kuliko maslahi yake binafsi. Tunamkumbuka na kumlilia kwa sababu tunaona ombwe kubwa lililotokana na kifo chake.
Sasa, japo 'marehemu hasemwi vibaya,' sidhani kama kuna atakayeshangaa sana kuona kifo cha mwanasiasa mahiri kwa matusi, vijembe, mipasho na mambo mengine mabaya kikipelekea furaha katika sehemu flani ya jamii. Ndio, dini zetu zinasisitiza kuwaenzi marehemu, lakini dini hizo pia zinasisitiza umuhimu wa heshima wakati wa uhai wetu.
Na pia licha ya ukweli si kila Mtanzania ni mcha-Mungu, wingi wa wacha-Mungu katika nchi yetu umeshindwa kuzuwia mauaji ya albino, ufisadi na 'dhambi'nyingine lukuki.
Nimalizie makala hii kwa kutoa salamu zangu za rambirambi kwa familia ya marehemu Kapteni Komba, ndugu, jamaa, marafiki na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla.
Njia mwafaka ya kumwenzi marehemu ni kudumisha mema yake, na kujifunza katika mapungufu yake. Kadhalika, kifo hiki kinapaswa kutuamsha na kuanza mjadala wa kitaifa kuhusu kudidimia kwa upendo, umoja na mshikamano wetu.
Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Kapteni Komba mahala pema peponi. Yeye ametangulia tu, sote twaelekea huko.

1 comment:

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.