1 Apr 2015


Pengine kabla ya kueleza kwanini naunga mkono muswada wa kudhibiti uhalifu wa mtandaoni (The Cyber Crime Bill),ni vema nikaeleza background yangu kidogo ili kutanabaisha sio tu ninavyothamini uhuru wa habari bali pia nilivyonufaika nao.

Nilianza uandishi kwenye vyombo vya habari mwaka 1996,mwaka mmojabaada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.Aliyenishawishi kuingia kwenye fani hiyo ni mwanahabari mkongwe, Albert Memba.Nikiwa mwaka wa pili, na yeye mwaka wa kwanza chuoni hapo, Memba aligundua kuwa 'utani wa busara' niliokuwa nikifanya eneo la 'kijiweni' (nyuma ya ukumbi wa mihadhara ya Sanaa -ATB,mkabala ya Maktaba Kuu ya chuo hicho) ungeweza kunipatia fursa katika gazeti 'lisilo serious.'

Nikafuata ushauri wake na kuanza kuandika 'unajimu wa utani' katika gazeti la 'udaku' la SANIFU lililokuwa linamilikiwa na kampuni ya Business Times, wachapishaji wa gazeti la Majira.Sanifu ni gazeti la kwanza kabisa la udaku Tanzania. Gazeti hilo lilinipa safu (column) niliyoipa jina 'nyota za Ustaadh Bonge.' Nyota hizo licha ya kutumia alama za unajimu kama 'Mshale' (Sagittarius), Ng'e (Scorpio),nk hazikuwa na ukweli wowote zaidi ya burudani. Kwa mfano, ungeweza kukutana na utabiri 'wa kisanii' kama huu: "Wiki hii utakumbwa na nuksi itakayokuletea ulaji mbeleni.Mwanao atagongwa na gari la ubalozi wa Marekani,lakini hatoumia.Ubalozi huo utakufidia kwa kukupatia viza ya kuishi Marekani.Usimzuwie mwanao kucheza barabarani."

Sio siri, watu wengi tu walivutiwa na 'Nyota za Ustaadh Bonge' na hii ilipelekea mie kupewa jina la utani la Ustaadh Bonge kwa muda wote niliokuwa hapo Mlimani (UDSM), na hadi leo, baadhi ya marafiki zangu wananiita Bonge.

Baada ya gazeti la Sanifu 'kufa' nilijiunga na gazeti jingine la udaku la Komesha, na baadaye Kasheshe, magazeti yaliyokuwa yanamilikiwa na kampuni ya IPP. Huko nako niliendeleza safu ya 'Nyota za Ustaadh Bonge.'

Hatimaye niliamua kuachana na magazeti ya udaku na kuhamia kwenye magazeti yenye 'serious news.' Nikafanikiwa kupata safu kwenye gazeti la KULIKONI,na safu hiyo ndio iliyopelekea jina la blogu hii yaani KULIKONI UGHAIBUNI ambalo lilikuwa jina la safu yangu katika gazeti hilo.Lengo la awali la blogu hii niliyoianzisha mwaka 2006 lilikuwa kuwapatia fursa wasomaji wa gazeti la Kulikoni walio nje ya Tanzania kusoma makala zangu kwa vile gazeti hilo halikuwepo mtandaoni.

Ni katika uandishi wa makala katika gazeti la Kulikoni ndipo nilipojitengenezea matatizo makubwa baada ya kuandika makala moja mwishoni mwa mwezi Oktoba 2006 ambapo nilikemea jitihada za aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa, kukwamisha mjadala wa sakata ya Richmond. Makala hiyo ilipelekea Press Secretary wa Lowassa, Said Nguba, kunikaripia vikali hadharani. Mwendelezo wa sakata hilo hatimaye ulipelekea mwisho wa ajira yangu serikalini mwaka 2008.

Baadaye nikapewa safu katika gazeti la MTANZANIA,ambapo safu yangu ilijulikana kama MTANZANIA UGHAIBUNI. Lilipoanzishwa jarida la RAIA MWEMA, nikafanikiwa kupata safu, ambayo niliita RAIA MWEMA UGHAIBUNI, ambayo imedumu kwa miaka kadhaa hadi hivi leo.

Kwahiyo kwa kuangalia background hii utabaini kuwa sio tu nimeutumia vema uhuru wa habari bali pia nimenufaika nao vya kutosha.Nitakuwa mtu wa mwisho kuwa kikwazo cha uhuru huo kwani nami ni mnufaika mkubwa.

Nirejee kwenye mada halisi ya makala hii.Sababu kuu zinazonifanya niunge mkono muswada wa kudhibiti uhalifu wa mtandaoni ni TATU:

Kwanza, KITAALUMA/KITAALAM: Kwa zaidi ya miaka 10 huko nyuma, nilisomea na hatimaye kufanya kazi katika sekta ya usalama. Japo kimsingi kwa sasa si mwajiriwa katika taasisi ya usalama, nina interest kubwa kuhusu stadi na taaluma hiyo, ndani na nje ya Tanzania. Licha ya kujihusisha na usalama kwa maana ya intelijensia, pia nina interest kubwa kuhusu usalama wa mtandaoni hususan uhalifu wa mtandaoni (cybercrime). 

Sambamba na hilo, nimekuwa nikiutumia sana mtandao kwa minajili ya kupashana habari.Licha ya blogu hii, nimekuwa nikiweka mabandiko katika mitandao mingine ya kijamii kama vile Tumblr, Google+, Facebook, Instagram, Pinterest na hata Jamii Forums. Kutokana na uwepo wangu mkubwa mtandaoni, nimelazimika kufuatilia kwa karibu umuhimu wa usalama mtandaoni ikiwa ni pamoja na njia na nyenzo za kujikinga na wahalifu wa mtandaoni, sambamba na kuhabarisha masuala mbalimbali yanayohusiana na suala hilo.

Vilevile, kwa miaka ya hivi karibuni nimepata interest mpya ya software hususan za simu, kwa maana ya maendeleo na matumizi ya apps mbalimbali, pamoja na masuala ya teknolojia kwa ujumla.Katika hilo, nimelazimika pia kufuatilia usalama wa software mbalimbali, za kompyuta na simu.

Kwahiyo, uzoefu wangu mdogo kitaaluma/kitaalam unanituma kuunga mkono umuhimuwa muswada huo hasa kwa vile suala la kompyuta kwa ujumla bado ni geni kwa Watanzania wengi, na hiyo inaota fursa kwa wahalifu wa mtandaoni kufanya hujuma zao kirahisi.Lakini pia hali hiyo inapelekea matumizi yasiyofaa ya teknolojia hiyo ngeni.

Kiintelijensia, kama ilivyosikika hivi karibuni, kuna jitihada za makundi ya kigaidi ya ISIS na Al-Shabaab kufanya hujuma eneo la Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania. Kwa bahati mbaya, mtandao umekuwa nyenzo muhimu ya vikundi vya kigaidi, hususan ISIS, katika harakati zao za kidhalimu. Na hivi karibuni tumesikia matukio mbalimbali yanayoelezwa kuwa ya kigaidi huko nyumbani. Hatuwezi kupuuzia taarifa hizi kwa sababu ugaidi, kama ilivyo kifo au tukio la wizi/ujambazi, hausubiri kualikwa.Unatokea tu. Kwahiyo ni muhimu kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kudhibiti matumizi ya kompyuta kwa minajili ya kufanya uhalifu. Naomba kusisitiza kuwa huu ni mtizamo wa kitaalam (kiinteliujensia) zaidi, na pengine si rahisi sana kueleweka.

Pili, KIJAMII: Ni ukweli usiopingika kuwa Tanzania yetu inaweza kuwa inashika nafasi ya juu kabisa katiika matumizi yasiyofaa ya mtandao.Ninaamini kuwa wengi wetu tumeshuhudia utitiri wa blogu za ngono mtandaoni. Ashakum si matusi, uki-Google 'picha za uchi' utakumbana na mlolongo wa mambo yasiyoendana na mila na desturi zetu.

Kama kuna sehemu inayotoa ushahidi mkubwa wa matumizi mabaya ya mtandao kwa Tanzania yetu basi ni INSTAGRAM.Huko imekuwa 'dunia uwanja wa fujo.' Kama si mzoefu wa matusi basi dakika chache tu katika mtandao huo utakutana na kila aina ya matusi. Wenyewe wameanzisha 'timu' za kusapoti au kupinga watu flani maarufu, na kwa hakika lugha inayotumika huko inachefua. Busara pekee hazitoshi kuwadhibiti watu hawa.Dawa pekee ni kuwa na sheria, sio tu ya kuwakumbusha umuhimu wa kuzingatia maadili bali pia kuwazuwia kuendeleza maovu yao.Ifike mahala, kabla mtu hajabandika picha za uchi ajiulize mara mbili iwapo hatochukuliwa sheria.

Matumizi ya simu za kisasa zenye kamera yamechangia 'kumfanya kila mwenye simu kuwa paparazi,' na katika hili, tumekuwa tukishuhudia picha zisizofaa kabisa mitandaoni.Hivi ni mara ngapi tumekwazwa na picha za maiti kwenye mitandao ya kijamii? Ni mara ngapi tumeitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya uhuni wa kubandika picha zisizofaa mtandaoni? Naam, serikali imesikia kilio chetu kwa kuleta muswada wa kuzwia uhalifu wa mtandaoni ili kupata sheria itakayosaidia angalau kupunguza kadhia hiyo inayokera wengi.

Pia kuna blog zisizo za picha za ngono lakini zinazosababisha utengano mkubwa katika jamii. Ukimtkana mtu kwa mdomo unaweza kusahau na hata huyo aliyetukanwa anaweza kusahau, lakini mtandao wa kompyuta (internet) hausahau kitu. Uki-Google jina langu, moja ya mambo utakayokutana nayo ni 'ugomvi' wangu wa zamani sana na gazeti moja huko Tanzania uliotokana na mimi kulilaumu kwa kutumia picha za uongo kuhalalisha habari waliyochapiusha.Japo ugomvi huo uliisha miaka mingi iliyopita na wahusika ni marafiki zangu kwa sasa, na tumeshasdahau yaliyopita, lakini internet bado inakumbuka.

Sasa blogu zinazoendekeza matusi, kuchafuana, uzushi na vitu kama hivyo sio tu zinawathiri wahanga kwa muda huo wa tukio lakini zinaweka kumbukumbu ya milele mtandaoni...kwa sababu mtandao hausahau kitu. Tuendelee kuvumilia uhuru huu usio na ukomo wa kumchafua mtu yeyote kwa vile tu mlikorofishana? 

Baba wa Taifa aliwahi kutuusia kuwa "Uhuru bila utii ni ujinga" na "uhuru usio na mipaka ni uwendawazimu." Sasa pasipo sheria ya kudhibiti ujinga na uwendawazimu huu unaotokana na dhana fyongo kuwa 'hakuna anayeniona ninapobandika mabaya mtandaoni' tutaendelea kuumizana.

Tatu, sababu BINAFSI: Japo sitaki kuwa mbinafsi kwa maana ya 'kuunga mokono muswada huu kwa sababu mie pia ni mhanga' lakini pia sitaki kuwa mnafiki kwa kukwepa ukweli kwamba nimeshawahi kuwa mhanga wa matumizi mabaya ya uhuru mtandaoni. Mfano mmoja halisi ni kilipotokea kifo cha binti mmoja aliyekuwa miongoni mwa watumiaji mahiri wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Marehemu Betty Ndejembi (Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi). Kwa vile kabla ya tukio hilo la kusikitisha nilikuwa nikihamasisha upinziani dhidi ya unyanyasaji mtandaoni, kifo cha marehemu Betty kilinipa changamoto mpya, hasa ikizingatiwa kuwa siku chache kabla ya kukutana na mauti, binti huyo alinyanyaswa vya kutosha huko Twitter. Kwahiyo haikuwa jambo la kushangaza nilipoungana na baadhi ya wanaharakati kutumia hashtag #StopCyberbullying.

Lakini kwa sababu ambazo hadi leo sizielewi, lilijitokeza kundi katika mtandao huo sio tu kupambana na jitihada hizo za kukemea unyanyasaji mtandaoni bali pia kunichafua kwa maana ya jitihada kuonyesha kuwa eti nami ni mnyanyasaji pia huko mtandaoni. Kama kuna kitu kiliniuma na kinaendelea kuniuma hadi leo ni pale mmoja wa watu hao aliponiita MUUAJI. Yaani kuhamasisha mapambano dhidi ya unyanyasaji mtandaoni ni sawa na UUAJI? Ningeweza kumburuza mtu huyo mahakamani kwa kosa la kunidhalilisha (defamation) lakini ukosefu wa sheria halisi inayohusu unyanyasaji mtandaoni (cyberbullying) ungeweza kuniathiri.

Ni rahisi kuzungumzia 'uhuru usio na ukomo' kwa jamii iwapo hujawahi kuwa mhanga wa matumizi ya uhuru huo. Naomba nisieleweke vibaya.Siungi mkono muswada huo kwa vile tu mie ni mhanga huko nyuma, au utakomoa watu flani, lakini pia kuna sababu nyingine muhimu kama nilivyobainisha hapo juu.

MWISHO, japo ninatambua umuhimu wa wananchi kushirikishwa katika utungaji wa sheria zinazowahusu, na pia ninaafikiana na hoja ya kutoharakisha miswada inayohitaji ushirikishwaji wa umma, ninaunga mkono muswada huo kwa sababu UNAHITAJIKA SASA. Na kwa hakika umechelewa sana. Hatuwezi kuendelea kuvumilia matumizi mabaya ya mtandao wa kompyuta kwa kisingizio cha uhuru wa habari. Hatuwezi kuendelea kuvumilia picha za ngono na maiti zikiwekwa hadharani kama mapambo.Jamii yeyote yenye kuzingatia maadili inapaswa kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo kama hivyo. Hatuwezi kuwatengenezea mazingira mazuri magaidi kwa kisingizio cha 'umbeya si dhambi.' Madhara ya kutochukua hatua ni makubwa kuliko kuchukua hatua.

Mie ninaweza kuwa mhanga wa sheria hiyo (ikipitishwa) hasa kwa vile ni mtumiaji mkubwa wa mtandao, na pia mkosoaji wa serikali ninapoona inastahili kukosolewa. Ni kweli kwamba sheria hiyo ikipitishwa inaweza kudhuru hata watu wasio na hatia.Lakini katika hili, tatizo si sheria bali CORRUPTION. Tunapozungumzia corruption hatumaanishi tu kuhonga au kuhongwa fedha, bali hata kupindisha sheria kwa maslahi binafsi au kukomoana.Sasa katika hilo, tuna tatizo katika nyingi ya sheria zetu.Ni wangapi wanaporwa viwanja kutokana na corruption katika sheria na sekta ya ardhi? Ni wangapi wapo gerezani muda huu kwa sababu tu walishindwa kuhonga polis au hakimu? Ni vigumu kwa sheria yoyote kuwa na ufanisi katika mfumo corrupt.Ni jukumu letu sote kupambana na corruption ili sheria zenye maslahi kwa jamii zisiishie kuathiri wasio na hatia.

Muswada huu ni kwa maslahi ya kila Mtanzania. Kama wewe si mhalifu wa mtandaoni, sheria hii haitokudhuru. As to itatumika vibaya na serikali, tatizo hapo sio sheria husika bali corruption.Kuna sheria nyingi tu na pengine kali zaidi ya hii tarajiwa, kwa mfano Sheria ya Usalama wa Taifa 1970, Sheria ya Idara ya Usalama wa Taifa 1996 na Sheria ya Kuzuwia vitendo vya Ugaidi ya mwaka 2002, zinazoweza kutumika vibaya kutokana na corruption. Sina hakika wangapi miongoni mwa wanaopinga muswada wa Cybercrime wameshakuwa wahanga wa 'matumizi mabaya' ya sheria hizo kali kuliko hii tarajiwa.

Hofu yetu dhidi ya matumizi mabaya ya sheria isiwe sababu ya kutokuwa na sheria kabisa. Tusielemee kwenye hofu yetu tu bali tutambue kuwa takriban kila siku kuna victims kadhaa kutokana na ukosefu wa sheria ya kudhibiti uhalifu wa mtandaoni.

ANGALIZO: Huu ni mtizamo wangu binafsi na unaweza kuonekana fyongo kwa mwingine.Twaweza kujadiliana pasipo haja ya 'kupigana.'

MUNGU IBARIKI TANZANIA1 comment:

  1. kitu ambacho mfumo wa kiutawala na kiuongozi ktk tanzania kimefanikiwa ni kuwa ni watu ambao tunajua kusoma na kuandika tu lakini kutambua kilichoandikwa ni nini limekuwa tatizo.Hivi majuzi tasisi moja ambayo ilifanya utafiti ilitoa matokea kuwa tunaongoza ktk kukosa uelewa ukilinganisha na mataifa mengine
    Katika mjalada wa kuwa na sheria hii au la tulikimbilia kusema imearakishwa na kuangalia vifungu vinavyotugusa kama watumiaji binafsi bila ya kuangalia umuhimu wa kuwa na sheria hii.
    Suala hili kwa wkt mmoja unaweza kurusha lawama kwa mtu mmojammoja au kwa jamii ambayo imeweza kutengeneza tabaka mbalimbali za watz kuanzia kwenye kipato,elimu nk kiasi mtu anaangalia maslahi yake binafsi badala ya kuangalia jamii kwa ujumla.
    Katika sheria hii nilikuwa nahoji hivi nyanya yangu itamwathiri vipi mpaka nione ni mbaya hata kama naye anatumia simu kwa kuwasiliana na ndugu zake? Nilichoona ni endapo kati ya ndugu zake watatumia vibaya hadi kuingia matatani au itumiwe na wenye madaraka kuwakomoa hata hivyo nikaona nao no uozo na wala siyo rushwa kama tulivyozoea kuita!

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube