21 May 2015

ANGALIZO: Makala hii ilipaswa kuchapishwa gazetini wiki iliyopita lakini nilichelewa kutimuma gazetini.Pia, kwa kiasi kikubwa, kichwa cha habari cha makala hii gazetini kinatofautiana na kilichomo ndani ya makala (na ndio maana kipo tofauti na hapa bloguni.Samahani kwa hilo)
HIVI karibuni, Uingereza ilifanya uchaguzi wake mkuu ambapo chama kilichokuwa madarakani kwa kushirikiana na chama kingine cha Liberal Democrats cha Conservatives kilipata ushindi wa kishindo.
Moja ya mambo yanayoweza kukumbukwa kwa muda mrefu kuhusu uchaguzi huo ni jinsi matokeo ya mwisho yalivyokuwa tofauti kabisa na ubashiri wa kura mbalimbali za maoni. Kimsingi, matokeo hayo ambayo hayakutarajiwa kabisa yamepelekea baadhi ya wachambuzi wa siasa kuhoji ufanisi wa kura za maoni katika kubashiri matokeo ya chaguzi.
Na katika hatua nyingine, kunatarajiwa kuundwa tume huru ya uchunguzi kudadisi kwanini kura za maoni zilibashiri matokeo tofauti sana na matokeo halisi (na hii inaonyesha jinsi ‘wenzetu’ walivyo makini hata katika tatizo dogo tu).
Hadi siku ya uchaguzi, kura mbalimbali za maoni zilikuwa zikibashiri kuwa vyama vya Conservatives na Labour vingepata matokeo yanayokaribina na kufungamana, na hivyo kupelekea kitu kinachofahamika kama ‘hung parliament.’
Pengine ni vema nitumie fursa hii kuelezea kidogo kuhusu uchaguzi mkuu hapa jinsi ulivyo.Hapa hatuna rais, na japo mkuu wa nchi ni Malkia, mtendaji mkuu wa serikali ni Waziri Mkuu.
Malkia, kama zilivyo tawala za kifalme hapigiwi kura. Na uongozi wake wa nchi ni wa kiheshima (ceremonial) kuliko kiutawala.
Katika uchaguzi mkuu kama huo uliofanyika majuzi, wapiga kura wanachagua wabunge wa vyama mbalimbali na idadi ya viti itakavyopata chama katika uchaguzi ndivyo vitaamua nafasi yake katika kuunda serikali.
Namba ya ushindi inayohitajika ili chama kiunde serikali ni viti 326 kati ya viti vyote 650. Iwapo vyama vyote havitofikia idadi hiyo, basi hali inakuwa kama ilivyotokea katika uchaguzi mkuu uliopita, ambapo Conservatives walipata viti 307, Labour viti 258 na Liberal Democrats viti 57. Matokeo hayo ndiyo yanayojulikana kama ‘hung parliament.’
Kutokana na hali hiyo, chama cha Conservatives kiliamua kufanya ushirikiano na chama cha Liberal Democrats na kuunda serikali ya ushirikiano, kwa kimombo coalition government. Kwahiyo katika miaka mitano iliyopita, serikali ya hapa ilikuwa inaongozwa na ushirikiano wa vyama hivyo, ambapo Waziri Mkuu alikuwa David Cameron kutoka Conservatives na Naibu wake Nick Clegg wa Liberal Democrats.
Turejee kwenye kura za maoni. Hadi siku ya uchaguzi, kura nyingi za maoni zilibashiri kuwa Conservatives na Labour wangefungana kwa asilimia takriban 34 (kwa mujibu wa kampuni ya kura za maoni inayoheshimika sana hapa ya YouGov).
Kutokana na hali hiyo, na kwa vile ilitarajiwa kuwa Liberal Democrats wangepata matokeo mabaya (kulikuwa na hofu kuwa kiongozi wa chama hicho, Clegg, angepoteza jimbo lake), chama tawala cha hapa Uskochi, Scottish Nationalist Party (SNP) kilionekana kama ndicho kingeamua hatma ya nani kati ya Conservatives na Labour aunde serikali.Kura za maoni zilikuwa zikibashiri kuwa SNP ingepata majimbo 58 kati ya yote 59 ya hapa Uskochi.
Dalili za kwanza kwamba kura za maoni ‘zilipotea njia’ zilijitokeza sekunde chache tu baada ya vituo vyote vya kupigia kura kufungwa (saa nne usiku). Kwa kawaida ya hapa (na katika nchi nyingine zenye mfumo wa uchaguzi kama huu wa hapa), mara baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa, kunatangazwa kitu kinachojulikana kama exit poll.
Hii ni kura ya maoni inayofanywa kwa kuuliza sampuli ya wapigakura (katika uchaguzi huo wa majuzi, sampuli ilikuwa ya watu 22,000) wamekipigia kura chama gani au mgombea gani.
Matokeo ya sampuli hiyo hutumika kubashiri matokeo ya uchaguzi mzima kwa ujumla.
Sasa, exit poll iliyotangazwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ilibashiri kuwa Conservatives ingepata viti 316, Labour 239, Liberal Democrats 10, SNP 58 pamoja na ubashiri wa matokeo ya vyama vinginevyo.

Hiyo ilikuwa tofauti kabisa na ubashiri wa kura za maoni kadhaa kabla na siku ya uchaguzi zilizoonyesha Conservatives wangepata takriban viti 280, Labour takriban 270, 18 kwa Liberal Democrats na 55 kwa SNP.
Je, kwanini kura zile za ubashiri zilibashiri tofauti sana na exit polls na hatimaye matokeo ya jumla? Ni vigumu kupata jibu rahisi lakini inaelezwa kuwa huenda moja ya sababu ni watoa maoni wengi katika kura za maoni kusema tofauti na walivyotenda, yaani majibu ya wengi yalikuwa tofauti na jinsi walivyopiga kura. Hata hivyo, sababu halisi zinatarajiwa kufahamika baada ya tume huru iliyoundwa kuchunguza kasoro hiyo kumaliza kazi yake.
Matokeo ya mwisho yalikuwa kama ifuatavyo: Conservatives viti 331, Labour viti 232, SNP viti 56, Liberal Democrats viti 8 na vyama vinginevyo viti 23. Kwa matokeo hayo, Conservatives walifanikiwa sio tu kupata idadi ya viti 326 vinavyohitajika kuunda serikali pepe yake, bali pia ilipata viti vitano Zaidi. Kwahiyo, David Cameron amerejea madarakani na chama chake cha Conservatives kinaunda serikali pasi kuhitaji ushirikianoi na chama kingine ukilinganisha na ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita.
Tukiweka kando ‘ubashiri fyongo’ wa kura za maoni, moja ya matukio ya kihistoria katika uchaguzi huo ni mafanikio makubwa ya SNP, chama ambacho katika uchaguzi mkuu uliopita kiliambulia viti 6 tu lakini safari hii kimesomba viti 56, ikiwa ni viti vitatu tu pungufu ya kuomba viti vyote 59 vya Uskochi. Mafanikio ya SNP yamekuwa habari mbaya mno kwa Scottish Labour na Scottish Liberal Democrats ambavyo pamoja na Scottish Conservatives wameambulia viti vimoja vimoja. Kibaya zaidi, hata kiongozi wa Scottish Labour Jim Murphy alibwagwa katika uchaguzi huo, na hatma yake kisiasa ipo mashakani.
Baada ya uchaguzi huo kumalizika, kiongozi wa Labour Ed Miliband alitangaza kujiuzulu, sambamba na Nick Clegg wa Liberal Democrats.Awali, kiongozi wa chama cha kibaguzi cha UKIP, Nigel Farage, aliapa kuwa akishindwa katika jimbo alilokuwa anagombea angejiuzulu.
Alishindwa, lakini chama hicho kimemwomba aendelee kuwa kiongozi wake. Tofauti na matarajio ya awali, na ‘mvuto’ wake katika sera dhidi ya wahamiaji na uwepo wa Uingereza katika umoja wa Ulaya, chama hicho kiliambulia jimbo moja tu.

Wengi wa wachambuzi wa siasa za hapa wanatarajia kuwa miaka mitano ya Cameron na Conservatives kuwa sio rahisi. Changamoto kubwa zaidi ni kuzuia Uskochi kudai kura nyingine ya maoni kuhusu uhuru wake, na kwa upande mwingine ni sokomoko la Uingereza kujitoa katika Jumuiya ya Ulaya.
Kwa hilo la ‘uhuru wa Uskochi,’ wachambuzi wengi wanatafsiri ushindi mkubwa wa SNP kama ‘idhini isiyo rasmi’ kwa chama hicho kudai tena kura ya maoni (referendum) ya uhuru, baada ya iliyofanyika mwaka jana kushindwa kuamua Uskochi iendelee kubaki katika ‘muungano wa Uingereza’ kwa tofauti ya kura chache tu.
Licha ya ukweli kuwa matokeo hayo ya ‘kura ya maoni ya uhuru wa Uskochi’ imepeleka umaarufu mkubwa kwa SNP, huku ikivuna idadi kubwa kabisa ya wanachama wapya, kauli za Cameron wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa majuzi dhidi ya chama hicho tawala Uskochi, zinaelezwa kutafsiriwa na wengi wa wapigakura wa hapa (Uskochi) kama ‘chuki dhidi ya taifa lao,’ na hivyo kuamua kukisapoti ‘chama chao’ (SNP) kwa wingi. Sapoti hiyo inaweza kuwa na umuhimu mkubwa iwapo SNP itaamua kudai kura nyingine ya maoni ya ‘uhuru wa Uskochi.’
Kwa upande wa hatma ya Uingereza katika Jumuiya ya Ulaya, Cameron ameshaahidi kutekeleza azma yake ya kuitisha kura ya maoni iwapo nchi hii iendelee na uanachama wake au ijitoke, kabla ya mwisho wa mwaka keshokutwa. Huu utakuwa mtihani mkubwa sana kwa Cameron na Conservatives kwa ujumla.
Wakati wahafidhina ndani ya chama hicho wakipigania kwa udi na uvumba Uingereza ijitoke, kuna idadi kubwa tu ya Waingereza wanaodhani wazo hilo ni baya na hatari kwani linaweza kuiathiri nchi yao kiuchumi na kisiasa za kimataifa.
Je kuna lolote Watanzania twaweza kujifunza kutoka katika uchaguzi huo mkuu wa Uingereza? Yapo mengi, lakini machache ni pamoja na mfumo imara kabisa, tofauti na wetu unaoonekana kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu (Tume yetu ya Uchaguzi inataka wananchi wasisikie maneno ya pembeni, lakini mazingira yaliyopo yanapelekea hofu iwapo uchaguzi mkuu utafanyika kweli hapo Oktoba).
Kingine ni nafasi ya sera za vyama katika kushawishi wapiga kura. Moja ya sababu zinazotajwa kupelekea Labour kufanya vibaya ni sera zake zilizoonekana kuwatenga wafanyabiashara wadogowadogo na kutowapa kipaumbele watu wa tabaka la kati. Kwa uapnde mwingine, inaelezwa kuwa ushindi wa Conservatives ulichangiwa zaidi na mvuto wa sera zake za kiuchumi kwa wapigakura.
Kadhalika, jingine ambalo vyama vyetu vya siasa huko nyumbani vyaweza kujifunza ni uchaguzi wa mgembea anayekubalika.Kwa kiasi kikubwa, kampeni za Labour ziligubikwa na hofu ya uwezo binafsi wa Ed Miliband kumudu Uwaziri Mkuu.
Nimalizie makala hii kwa kuwapongeza Waingereza kwa kuendesha Uchaguzi Mkuu kwa ufanisi mkubwa, kuanzia mwenendo wa kampeni ambapo kwa asilimia kubwa ulihusu sera badala ya ‘madongo,’ idadi kubwa ya wapigakura iliyojitokeza (asilimia 66.10) na uungwana wa walioshindwa matokeo kuyakubali matokeo, sambamba na Miliband na Clegg kujiuzulu kutokana na vyama vyao kufanya vibaya.
Wakati nina matumaini hafifu kuona kura ya maoni ikifanyika kabla ya uchaguzi mkuu wetu hapo Oktoba, ninajipa moyo kuwa serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wataongeza bidii ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unafanyika kama ilivyopangwa.
Kutokana na kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu, na hali yetu mbaya kiuchumi, ni muhimu kwa watawala wetu kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, tujibane na kidogo tulicho nacho (tukitarajia wafadhili watatumbukiza fedha zao katika ‘bakuli’ letu) ili tuwezeshe uchaguzi huo kufanyika kwa ufanisi na amani.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube