21 May 2015

WAZIRI mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, ameanza kuwaandaa wafuasi wake kwa uwezekano wa kujiunga na mojawapo ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Raia Mwema limeelezwa.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka katika kambi ya mgombea huyo zinaeleza kuwa amepiga marufuku mazungumzo yoyote ya kutafuta mbadala wake ndani ya CCM na kutaka nguvu yote ielekezwe kwake.

Gazeti hili limeelezwa kuwa wapo watu walio ndani ya kambi yake wanaoamini kwamba anahitajika mwanasiasa mwingine ndani ya kundi hilo ambaye anaweza kuvaa viatu vya Lowassa endapo CCM itaamua kumkata au kuendeleza adhabu yake ya kutofanya shughuli za siasa aliyopewa na chama chake.

Hata hivyo, kundi hilo linadaiwa kuwa na wakati mgumu kwa madai kwamba Lowassa hataki kusikia chochote kuhusu suala hilo.

“Anasema yeye ndiyo Plan A, Plan B na Plan C. Kama, kwa sababu yoyote ile, CCM itaamua kumpitisha mgombea mwingine na si yeye, yuko tayari kujiunga na Ukawa lakini si kubaki ndani ya chama.

“Hili ndilo jambo linalotusumbua sana kwa sasa. Hakuna vita ambayo ina mpango mmoja tu. Lazima muwe na mpango zaidi ya mmoja. Huku Pwani wanasema ukienda kuteka maji wakati wa ukame, ni muhimu uwe na ndoo na kidumu cha kushika mkononi.

“Kwenye kutembea na ndoo mtu unaweza kujikwaa na maji yote yakamwagika na kile kidumu cha mkononi ndiyo kikakuokoa. Sasa huyu bwana hataki kusikia habari ya kidumu.
“Anataka twende kutafuta maji na ndoo moja tu ambayo ni yeye. Hili linatupa shida kidogo kwa sasa,” alisema mbunge mmoja wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni mtu wa karibu na mtarajiwa huyo.

Katika kambi ya Lowassa, kuna majina ya wanasiasa vijana ambao wanatajwa kuwa tayari kuvaa viatu vyake endapo CCM itaamua tofauti na matarajio yao.

Miongoni mwa wanasiasa wanaotajwa kuwa katika kambi ya Lowassa na ambao kambi inayotaka Plan B inawapendekeza ni Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.

Miongoni mwa wanaotajwa, Dk. Nchimbi anaelezwa kuwa na nguvu zaidi kutokana na ukweli kwamba ndiyo mwenye ushawishi zaidi ndani ya chama kutokana na ukweli kuwa amekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa zaidi ya miaka 10.

Kimsingi, kwa upande wa Tanzania Bara, hakuna mwana CCM aliyedumu katika Kamati Kuu ya chama hicho kwa muda mrefu kuliko Nchimbi miongoni mwa waliomo sasa, ukimwondoa Rais Jakaya Kikwete.


Anasema Mbunge huyo: “ Tunajaribu kumshawishi Lowassa akubali kuwa akikosa yeye, basi apatikane mtu ambaye ataweza kuyafanya yale aliyopanga kuyafanya kupitia CCM. Kwa sasa, hili hajakubaliana nalo,” kilisema chanzo hicho cha gazeti hili ambacho hakikutaka kuwekwa jina lake wazi.

Hata hivyo, kwa vile Ukawa si chama cha siasa, kama Lowassa ataamua kuhama CCM, ni lazima ajiunge na mojawapo ya vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na National League (NLD).

Akizungumzia taarifa hizo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kwa sasa hawataki kujihusisha na mambo ya ndani ya CCM na badala yake wanaangalia namna ya kukishinda kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.

“Sisi sasa hivi lengo letu kubwa ni kuijenga Ukawa kitaasisi na kuifanya iwe tishio katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.

“Kamanda, sitaki kuzungumza kama tutampokea au hatutampokea Lowassa kama akiamua kuhamia Ukawa. Mambo ya CCM waachie CCM wenyewe. Mimi nakuhakikishia kuwa wakati wa uchaguzi ukifika; CCM wamweke Lowassa, au Membe, sijui Makongoro Nyerere ama yeyote mwingine, Ukawa itashinda tu kwenye uchaguzi huo,” alisema Mbowe kwa kujiamini.

Juhudi za kuwapata wenyeviti wenza wengine wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, James Mbatia na Emmanuel Makaidi hazikufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni juzi Jumatatu.

Kwa sasa, Lowassa na wanasiasa wengine watano ndani ya CCM wako katika kifungo cha muda usiojulikana walichowekewa na chama chao kutokana na madai ya kukiuka taratibu za chama hicho.

Wanasiasa wengine walio katika kifungo hicho ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe; Ngeleja na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Ilivyokuwa chaguzi mbili zilizopita
Taarifa hizi za uwezekano wa Lowassa kuhamia Ukawa hazitofautiani na zile zilizoibuka mwaka 2005 wakati ilipodaiwa kuwa Kikwete angehamia Chadema endapo CCM isingempitisha.

Wakati huo, zilikuwapo taarifa kuwa CCM ilikuwa na mpango wa kumwondoa Kikwete kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na kutokidhi vigezo vya kimaadili vya chama hicho.
Hata hivyo, Kikwete hatimaye alipitishwa na chama chake kuwania urais na kushinda kwa kishindo.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2010, baadhi ya wanachama wa CCM walitajwa kutaka kujiunga na Chama cha Jamii (CCJ) na mmoja wao, Fred Mpendazoe, aliachia ubunge wake kabla ya wakati ili kuanza kazi ya kukijenga chama hicho.

Wakati huo, CCJ ilidaiwa kuwa na mkono wa wana CCM waliokuwa wakipinga kukithiri kwa ufisadi ndani ya chama hicho.

Miongoni mwa majina mazito yaliyokuwa yakihusishwa na kujiunga na CCM yalikuwa ni Samuel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe.

CHANZO: Raia Mwema

WAKATI HUOHUO,

BALOZI wa kudumu wa Umoja wa Afrika (AU), huko Marekani, Mtanzania Amina Salum Ali, ametangaza  kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, 2015.

[aminaali.jpg]
Balozi Amina ametangaza uamuzi wake huo mapema leo  jijini Dar es Salaam.

Itakumbukwa ya kuwa Balozi Amina ambaye alidumu kwa muda mrefu kama waziri kwenye serikali ya Rais mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Salmin Amour Juma, almaarufu kama (Komandoo), aliwahi kutupa karata yake kuwania urais wa Zanzibar, kabla ya kujitoa.

Huyu anakuwa mwana mama wa kwanza kwenye historia ya chama cha Mapinduzi CCM, kutangaza kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Hali kadhalika, Balozi Amina rekodi yake ya kwanza ni kuwa mwanamke wa kwanza kuwa balozi wa kudumu wa AU huko Marekani.

Mbali na kuwahi kuwa waziri, Balozi aAmina ndiyo muasisi wa taasisi ya Zanzibar Women Welfare Trust, inayojishughulisha na kupambana na afya ya akina mama na watoto hususan kwenye eneo la maambukizi ya VVU.0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.