28 May 2015

HATIMAYE kipenga cha kuanzisha mbio za kumrithi Rais Jakaya Kikwete kimepulizwa rasmi, kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo majuzi chama hicho tawala kilitangaza ratiba ya kupata wagombea wake katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Lakini kabla ya hatua hiyo, kuna matukio makuu mawili yanayohusiana na mbio hizo za urais yaliyotokea hivi karibuni. Kwanza, Ikulu ilitangaza kuwasafisha watendaji kadhaa wa serikali ambao walipoteza nyadhifa zao huko nyuma kutokana na kashfa za Operesheni Tokomeza na Akaunti ya Tegeta Escrow. Huhitaji kuwa na ujuzi wa uchambuzi wa siasa za Tanzania kutambua kuwa hatua hiyo inaweza kuhusishwa na harakati za urais baadaye mwaka huu.
Pengine hatua hiyo ya Ikulu iliyowashangaza wengi inaweza kuwa imetumia fursa ya wabunge wa chama hicho waliovalia njuga sakata hilo kubanwa na harakati zao binafsi za kutaka kurejea tena bungeni baada ya Uchaguzi Mkuu ujao. Ni dhahiri kuwa mbunge anayetegemea ridhaa ya CCM kumpitisha agombee tena anajikuta katika wakati mgumu kuikosoa serikali ya chama hicho, kwani inaweza kupeleka mizengwe dhidi yake huko mbeleni.
Lakini kwa upande wa pili, wahusika waliosafishwa kuhusu kashfa hizo wametengenezewa mazingira mazuri ya kuingiza majina yao katika ‘kapu’ la wenye dhamira ya kugombea urais. Na hata kama hawatataka kugombea urais, basi kikwazo cha kuondolewa madarakani kutokana na kashfa hizo hakipo tena iwapo wataamua kugombea ubunge tu.
Japo binafsi ninaamini baadhi ya watendaji waliowajibishwa kutokana na kashfa hizo walikuwa majeruhi tu, hususan aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki (ukifuatilia kwa makini utabaini kuwa kuna watu wengi wenye imani kama hiyo yangu), wengine wanaonekana kusafishwa kwa vile tu ‘huwezi kumsafisha huyu na kumuacha yule.’
Tukio la pili lilikuwa hatua ya CCM kuwafungulia makada wake walioadhibiwa kwa kukiuka taratibu za kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho. Adhabu hiyo ilikuwa mzaha tangu ilipotangazwa. Mzaha sio tu kwa sababu wengi wa walioadhibiwa waliendelea na ‘kampeni’ zao waziwazi, lakini pia mantiki nzima ya adhabu ilikuwa fyongo. Licha ya kuwa chama hicho tawala kina taratibu zake za kupata wagombea katika nafasi mbalimbali, kuwanyima wanachama wake uhuru wa kutangaza nia ya kuwania uongozi ni sawa na udikteta.
Ukifuatilia kwa makini, utabaini kuwa hatua ya baadhi ya makada wa chama hicho kutangaza nia ya kumrithi Rais Kikwete hapo Oktoba imewasaidia Watanzania kuwaelewa wanasiasa hao kwa kiasi kikubwa. Katika nchi za wenzetu waliokomaa kidemokrasia, wenye dhamira ya kuwania urais hutangaza takriban mwaka kabla ya Uchaguzi Mkuu, kama tunavyoshuhudia huko Marekani. Kwa vile urais si suala la mgombea au chama pekee bali wananchi wote kwa ujumla, kuna umuhimu mkubwa kwa wanaotaka kuongoza nchi kufahamika mapema ili wapiga kura wawapime kama kweli wanafaa na kustahili kushika nyadhifa wanazowania.
Tukiweka kando matukio hayo mawili, mwishoni mwa wiki iliyopita, Halmashauri Kuu ya CCM ilikutana huko Dodoma, na kama ilivyotarajiwa, suala la Uchaguzi Mkuu lilitawala kikao hicho muhimu. Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Kikwete alitoa wito kwa chama hicho kuchagua mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama.
Kadhalika, Rais Kikwete aliwaonya wana-CCM wenzake kwamba zama za kudhani kuwa mgombea yeyote atakayepitishwa na chama hicho atakuwa rais zimepitwa na wakati.
Hebu tuzichambue kidogo kauli hizo mbili. Kuhusu CCM kupata mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama, nadhani tatizo ni ‘nini kinamfanya akubalike?’ Wengi tunaifahamu vema CCM na utamaduni uliojengeka wa ‘kununua kukubalika.’ Japo wenyewe wanaweza kupinga, lakini ni ukweli usiofichika kuwa ni rahisi mno kwa kugema damu kwenye jiwe kuliko kupitishwa kugombea uongozi katika chama hicho kama huna fedha za kutosha. Na uthibitisho wa hilo upo katika takriban kila chaguzi za ndani katika chama hicho hadi kwenye uongozi wa chipukizi.

Na pengine ushahidi mkubwa zaidi ni katika ‘kukubalika’ kwa mmoja wa makada wa chama hicho ambaye licha ya kulazimika kujiuzulu kutokana na kashfa moja kubwa huko nyuma, uwezo wake mkubwa kifedha umesababisha makundi mbalimbali ya kijamii kumuunga mkono huku walalahoi kadhaa wakimchangia fedha za kulipia fomu ya kuwania urais. Je, huyu anakubalika ndani na nje ya CCM kwa sababu ya uwezo wake kiuongozi au uwezo wake kifedha?
Lakini changamoto kubwa kwa Rais Kikwete ni nguvu yake ndani ya chama hicho. Baadhi yetu tunaofuatilia kwa karibu mwenendo wa siasa za nchi yetu tunadhani kuwa uenyekiti wa Kikwete umebaki kuwa wa heshima zaidi kuliko wenye nguvu ya kufanya matakwa yake sio tu yasikilizwe bali pia yatekelezwe. Kuna wanaodai kuwa baadhi ya makada wa chama hicho wana nguvu zaidi ya mwenyekiti Kikwete, na hilo linaweza kukwamisha matakwa yake kuona CCM inapata mgombea stahili.
Kuhusu zama za mgombea atakayepitishwa na CCM kuwa rais ‘moja kwa moja,’ bado mazingira yaliyopo yanakipendelea chama hicho tawala. Kitakachoweza kuiangusha CCM si mabadiliko ya kimazingira bali mazingira ndani ya chama hicho. Kuna kitu kinafahamika kama ‘tactical voting’ ambacho majuzi tu kilimwokoa aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu wa hapa Uingereza, Nick Clegg, kushindwa ubunge katika jimbo lake wakati alikuwa akikabiliwa na upinzani mkali na kulikuwa na dalili kuwa angeangushwa. Sasa, kwa vile chama tawala cha Conservatives kilikuwa kinamhitaji Clegg, ambaye alikuwa kiongozi wa chama cha Liberal Democrats kilichounda serikali ya pamoja na Conservatives baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, wafuasi wake walimpigia kura kwa wingi na ‘kumtosa’ mgombea wa chama chao, kwa malengo ya kumsaidia Clegg ashinde.
Kwa hiyo, endapo CCM watampitisha mgombea ambaye wanachama wengi hawamtaki, wakati wa kura, tactical voting inaweza kuvinufaisha vyama vya upinzani. Lakini ili wapinzani waweza kunufaika basi sharti nao wawe na mgombea ambaye ana sifa zaidi ya huyo ‘mbovu’ wa CCM. Ni muhimu kutambua kuwa ili wapigakura bila kujali itikadi zao ‘waitose’ CCM, lazima waaminishwe kuwa chama au mgombea mbadala ni bora zaidi ya CCM au mgombea wake.
Nimalizie makala hii, ambayo ninatarajia kuiendeleza siku zijazo kwa kadiri tunavyojongea kwenye Uchaguzi Mkuu, kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa uchaguzi huo si kwa ajili ya manufaa ya chama au mgombea fulani. Wanufaika au waathirika wa uchaguzi huo ni wananchi.
Na uzoefu umekwishatuonyesha jinsi ‘mahaba kwa chama au mgombea’ yalivyosababisha miaka mitano ya kujilaumu kwa kukubali utapeli wa kisiasa. Ni muhimu kuweka mbele maslahi ya nchi na kumchagua mtu atakayeweza kuikwamua Tanzania kutoka katika lindi la umasikini unaochangiwa zaidi na ufisadi.
INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/kikwete-ni-mwenyekiti-wa-heshima-ccm#sthash.lZwwRU9T.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube