10 Jun 2015

WIKI iliyopita ilitawaliwa na hekaheka za Uchaguzi Mkuu ambapo makada kadhaa wa chama tawala CCM walijitokeza kutangaza nia ya kuwania urais endapo watapitishwa na chama chao.
Kama nilivyoandika katika makala yangu iliyopita, uamuzi huo wa kuwania nafasi hiyo ni haki kwa kila Mtanzania mwenye sifa stahili. Hata hivyo, wingi wa makada wa CCM waliokwishatangaza nia ya kuwania urais, sambamba na idadi ya makada wanaotarajiwa kutangaza nia zao hivi karibuni, imezua maswali makuu mawili.
Kwanza, je utitiri huu wa wagombea ni matokeo ya kukua kwa demokrasia ndani ya CCM au nchini kwa ujumla? Swali hili linaendana na dhana halisi ya demokrasia ambapo wingi wa wagombea, wanachama au vyama vya siasa hutafsiriwa kama ishara za kukua au kustawi kwa demokrasia. Hata hivyo, mara kadhaa dhana hii imethibitika kuwa fyongo, ambapo nchi kadhaa zina idadi kubwa tu ya vyama vya siasa lakini mara nyingi vyama hivyo huwa ni kwa maslahi ya viongozi na sio kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi. Licha ya vyama vya siasa, nchi kadhaa zina idadi kubwa ya wabunge, kama ilivyo Tanzania yetu, lakini kwa kiasi kikubwa idadi hiyo haijafanikiwa kumaanisha uwakilishi bora kwa wananchi.
Pili, je kujitokeza kwa idadi hiyo kubwa ya makada wa CCM kunachangiwa na kile kinachodaiwa kuwa urais wa Jakaya Kikwete umeshusha ‘bar’ ya wadhifa huo kiasi kwamba kila mtu anapata ujasiri wa kuitaka nafasi hiyo? Japo ni vigumu kupata mwafaka wa jumla kuhusu miaka kumi ya utawala wa Rais Kikwete, kumekuwa na hisia za mara kwa mara kwamba utawala wake umekuwa wa kirafiki zaidi, au ‘kishkaji’ kama wanavyosema huko mtaani. Teuzi mbalimbali zimekuwa zikitazamwa kama za kirafiki na sio kutokana na sifa stahili za wateuliwa. Na hili linadaiwa kuchangia mabadiliko kadhaa ya kabineti ya kiongozi huyo.
Tumeshuhudia mara kadhaa jinsi Rais Kikwete alivyopatwa na kigugumizi kuchukua hatua stahili dhidi ya watendaji wake, kikwazo kikidaiwa kuwa ni urafiki uliopo kati yake na watendaji hao walioshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Sasa, urais sio uongozi wa nchi tu bali ni ulezi wa viongozi wajao ikiwa ni pamoja na marais wajao. Na ndio maana tumesikia baadhi ya watangaza nia wakijisifu kuwa wamekuwa wasaidizi wa Rais Kikwete kwa muda fulani, wakimaanisha wamejifunza mambo kadhaa kutoka kwake. Kwa hiyo ni wazi ubora au upungufu wake unawagusa walio chini yake, na katika harakati hizi za kupatikana mrithi wake, yawezekana umechangia kutuletea rundo hili la wanaotaka kumrithi.
Lakini iwe ni kukua kwa demokrasia au urais wa Kikwete umeifanya nafasi hiyo kuwa ya ‘kawaida’ kiasi kwamba mwanasiasa yeyote anaweza kujiona anaweza kuimudu, ukweli unabaki kuwa waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hawajavunja kanuni yoyote, na Katiba yetu inawaruhusu kufanya hivyo. Hata hivyo, sisi kama wananchi pia tuna haki ya msingi ya sio tu kuwaunga mkono au kuwapinga wanaojitokeza kuwania nafasi hiyo bali pia kuwachambua, kuwapongeza au kuwakosoa. Na makala hii inajikita zaidi katika kuchambua kwa ujumla zoezi hilo la kutangaza nia ya kuwania urais miongoni mwa makada kadhaa wa CCM waliokwishajitokeza hadi sasa.
Kimsingi, ukiondoa Makongoro Nyerere ambaye aliweka bayana kuwa hawezi kutangaza ajenda zake binafsi ilhali mgombea atakayepitishwa na CCM atapaswa kuuza sera zake kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho, makada wengine wote waliotangaza nia wameongelea masuala yale yale ambayo takriban kila Mtanzania anayafahamu. Nisingependa kuyaorodhesha hapa kwa vile ninaamini kila mmoja wetu anatambua tunachohitaji, tunachostahili kuwa nacho lakini hatuna na kwa nini hali iko hivyo.
Labda jambo moja la wazi ni kwamba nchi yetu ina utajiri mkubwa wa wanasiasa wenye uelewa wa hali ya juu wa matatizo yanayoikabili Tanzania yetu, sambamba na mbinu za kuyatatua matatizo hayo. Takriban kila mtangaza nia ya kuwania urais amejitahidi kwa undani kuyachambua matatizo yetu, wengine wakienda mbali zaidi na kuelezea vyanzo vya matatizo hayo, na kutoa ufumbuzi wa kuyatatua.
Swali la msingi ni hili: walikuwa wapi siku zote na ‘utaalamu huo wa matatizo yetu’ hadi nchi yetu kufikia katika hali hii mbaya tuliyo nayo sasa? Je, yawezekana licha ya takriban wote kuwa walipewa nafasi na Rais Kikwete kuwa mawaziri au manaibu waziri katika kabineti zake, walimhujumu kwa kuficha uwezo wao ili baadaye waje kutumia upungufu uliopo kama mtaji wa kuomba nafasi hiyo ya urais?
Haiingii akilini kabisa kusikia mtu akielezea lundo la matatizo yetu ikiwa ni pamoja na yale ambayo hata baadhi ya wananchi hawayafahamu, na kutoa majibu mengi zaidi ya matatizo hayo, lakini mtu huyo huyo amekuwa serikalini kwa miaka kadhaa pasipo kutumia japo asilimia 0.1 ya ujuzi anaotueleza anao kuhusu matatizo yetu.
Je, wanaotaka kutueleza kuwa haikuwa rahisi kwao kuweza kututumikia kwa uwezo wao wote kwa vile tu hawakuwa marais? Nauliza hivyo kwa sababu ghafla, hata baadhi ya mawaziri ambao waliishia kutimuliwa kwa skandali za ufisadi wanamudu kutueleza kuwa wana ufumbuzi wa matatizo yetu. Ninahitimisha kuwa huu ni utapeli wa kisiasa, kwa kimombo wanasema political conmanship.
Nadhani wanaohisi kuwa Rais Kikwete ameishusha sana ‘bar’ ya urais wanapata nguvu ya hoja hiyo kutokana na wanasiasa kama hao, ambao umaarufu wao hautokani na nyadhifa walizoshika bali skandali zilizosababisha wang’olewe madarakani. Inakera na kuchukiza kuoina wanasiasa ambao pasi kuambiwa na mtu yeyote yule wanajitambua kuwa hawafai lakini leo wanapata ujasiri wa kutaka wapewe urais. Hivi URAIS umekuwa URAHISI kiasi hicho?
Lakini hata tukiweka kando maswali hayo ya msingi, hizi hadithi tamu za kuleta matumaini kwa kila anayezisikia zitawezekana vipi ilhali pindi wakipitishwa na chama chao hawatojinadi kwa ahadi hizo bali zitakazobainishwa kwenye ilani ya chama chao?
Sawa, labda watasema kuwa ukiwa mgombea una fursa ya kushiriki uandaaji wa ilani hiyo, lakini ukweli mchungu ni kwamba CCM haitoafikiana na mgombea atakayekuja na sera za kukiua chama hicho. Ninasema ‘sera za kukiua’ kwa sababu kwa kiasi kikubwa chama hicho kimeachana kabisa na misingi yake ya asili ya kuwa mtetezi wa wanyonge na badala yake kimetekwa na mafisadi. Chama kinachojigamba kuwa ni cha wakulima na wafanyakazi kimekuwa chama cha matajiri na wasomi wasiotaka kutumia usomi wao kwingineko, bali katika siasa (kwa minajili ya ulaji).
Kibaya zaidi, wengi wa makada waliotangaza nia wamekuwa wezi wa sera za vyama vya upinzani, sera ambazo makada hao wamekuwa wakizikejeli mara kadhaa lakini ghafla wameziona zinafaa kwa vile wanaotaka tuwaamini kuwa wanaweza kutuongoza. Ninarejea tena, huu ni utapeli wa kisiasa.
Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu maendeleo ya harakati hizo za kutangaza nia ya kuwania urais, kupitia mitandao ya kijamii. Japo Watanzania waliopo kwenye mitandao hiyo ni wachache lakini kwa kuzingatia kanuni za tafiti, wanaweza kuwa sampuli nzuri kuwakilisha mitizamo mbalimbali ya Watanzania wengi kwa ujumla. Nimebaini masuala kadhaa katika ufuatiliaji wangu: kwanza, angalau Watanzania wengi wanafahamu wanasiasa wa aina gani wasiotakiwa katika urais. Lakini hapo hapo kuna tatizo: wanajua wasiyemtaka lakini hawajui wanayemtaka.
Katika hili ninawatumia lawama nyingi ndugu zetu wa vyama vya upinzani hususan UKAWA. Hivi watu hawa wana maelezo yoyote ya maana zaidi ya uzembe kwa kushindwa kutumia fursa hii ambapo ‘CCM wanakabana makoo wenyewe kwa wenyewe’ kumnadi mgombea wao laiti wangekuwa wameshampata? Watetezi wao wanadai UKAWA wapo ‘bize’ kuhangaikia suala la uandikishaji wapiga kura. Hilo ni suala muhimu lakini lisiloweza kuwazuia wao kukamilisha mchakato wa kumpata mgombea wao.
Jingine nililogundua katika ufuatiliaji wangu ni wepesi wa Watanzania kuhadaiwa na maneno matamu yasiyoambatana na uthibitisho wowote ule kuwa ni ya kweli. Mara baada ya hotuba utasikia watu wakidai “aisee huyu jamaa anatufaa haswa…” kisa katoa hotuba nzuri. Tangu lini uwezo wa kutoa hotuba nzuri unamaanisha uwezo wa kivitendo? Kimsingi, Tanzania yetu haijawahi kuwa na uhaba wa watoa porojo. Sisi ni wazuri kweli kwa maneno ila tatizo letu ni kwenye kutafsiri maneno kuwa vitendo.
Ukitaka kujua uwezo wetu katika porojo nenda kwenye vikao vya harusi, au hata kwenye vijiwe vya kahawa. Huko kuna watu wanaongea sio tu kama wamemeza santuri au CD nzima bali pia wana uelewa na utaalamu wa hali ya juu wa fani ambazo wala hawakukanyaga darasani kuzisomea. Sasa kama hayo yanawezekana vijiweni, kwa nini nikiamua kuwania urais nisitumie uwezo wangu wote wa upigaji porojo kuwahadaa watu kuwa mimi ndiye yule waliyekuwa wakimsubiri miaka nenda miaka rudi? Pengine kufikia hapa, ninakuomba msomaji mpendwa tafuta wimbo wa ‘Ndio Mzee’ wa msanii wa muziki wa Bongofleva, Joseph Haule (Profesa Jay) kisha rejea ninachokieleza hapa.
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu, uchaguzi mkuu ujao haupo kwa manufaa ya chama au mgombea fulani. Ni kwa ajili yetu sisi wananchi. Sisi ndio wanufaika wa uamuzi bora utakaotupatia mtu wa kuikomboa Tanzania yetu kutoka hapa ilipo na kuifikisha inapostahili kuwepo, na sisi ndio waathirika iwapo tutafanya uamuzi fyongo kama tulivyofanya huko nyuma hadi kujikuta tulipo sasa. Mtaani wanasema ‘akili za kuambiwa changanya na za kwako.’ Ninawasihi Wtaanzania wenzangu kutokuwa wepesi kuhadaiwa na hizi porojo ambazo tumekuwa tukizisikia miaka nenda miaka rudi na nchi yetu inazidi kuangamia kwa umasikini, ufisadi na mabalaa mengine.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.