20 Aug 2015

KAMA nilivyoahidi katika makala iliyopita, wiki hii ninaendelea na uchambuzi wangu kuhusu Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Na kama ilivyokuwa katika makala kadhaa zilizotangulia, uchambuzi wangu utaelemea kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya urais.
Wakati katika makala iliyopita nilijadili fursa na vikwazo kwa wagombea ‘wakuu’ wawili, yaani Dk. John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema/UKAWA, wiki hii nitaingia kwa undani zaidi, huku lengo likiwa kuitumia makala hii kufanya uchambuzi kwa mgombea mmoja, na makala ya wiki ijayo itamwangalia mgombea mwingine.
Nianze na Lowassa wa Chadema/UKAWA. Kati ya makala iliyopita na hii, si siri kuwa habari inayotawala zaidi ni kile kinachoitwa ‘mafuriko ya Lowassa’. Shughuli zote zilizomhusisha mwanasiasa huyo katika kipindi hicho kimeandamana na umati mkubwa mno wa watu, kuanzia alipochukua fomu za kuwania urais jijini Dar es Salaam hadi katika mikutano ya kutambulishwa huko Mbeya, Arusha na Mwanza.
Wingi wa watu wanaojitokeza katika shughuli zinazomhusu Lowassa, iwe ni kwa kuandamana au kuhudhuria mikutano, kumewapa matumaini makubwa wafuasi wake kwamba njia ya Waziri Mkuu huyo wa zamani kuelekea Ikulu ni nyeupe.
Sambamba na mahudhurio hayo makubwa, wanachama kadhaa wa CCM wamehama chama hicho tawala na kujiunga na Chadema. Lakini kubwa zaidi ni kuhama kwa baadhi ya viongozi ‘ waliokuwa na majina’ ndani ya CCM.
Kwamba maandamano na mikutano ya Lowaasa inajaza watu wengi mno, hilo halina mjadala. Kwamba matukio yajayo ya mwanasiasa huyo yataendelea kujaza watu pia si suala la mjadala. Kadhalika, kwamba kuna wanachama na viongozi zaidi wa CCM watamfuata Lowassa huko Chadema pia ni jambo la kutarajiwa.
Tusichoweza kuhitimisha kwa uhakika muda huu ni iwapo hamahama hiyo ya baadhi ya wana-CCM na viongozi wao kumfuata Lowaasa huko Chadema itaweza kutafsiriwa katika ushindi katika uchaguzi mkuu ujao hapo Oktoba 25, takribani miezi mawili kutoka sasa.
Licha ya uwepo wa hamasa kubwa kuhusu kujiandikisha katika daftari za wapigakura lililoboreshwa na teknolojia ya kuhifadhi rekodi kwenye kompyuta (Biometric Voter Register kwa kifupi BVR), hadi muda huu Tume ya Taifa ya Uchaguzi haijatoa idadi kamili ya watu waliojiandikisha.

Lakini licha ya hilo, tayari kuna dalili za kasoro katika suala la BVR ambapo zimepatikana taarifa kadhaa za waliojiandikisha kutoyaona majina yao wakati wanaofanya uhakika. Ukubwa au udogo wa kasoro hiyo bado haujafahamika kwa vile Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijalitolea ufafanuzi suala hilo.
Hapa nitaunganisha masuala hayo mawili ya hapo juu, yaani idadi kubwa ya watu wanaojitokeza katika shughuli za Lowassa na zoezi la kujiandikisha BVR.
Yayumkinika kuhitimisha kuwa ili wingi wa watu wanaojitokeza katika shughuli za mwanasiasa huyo ziwe na manufaa kwake na chama chake kwa ujumla, basi, kwanza wengi wa watu hao, kama si wote, lazima wawe wamejiandikisha kupiga kura. Bila hivyo wingi wao utabaki kuwa historia tu.
Lakini kwa uzoefu tulionao wengi, kujiandikisha kupiga kura ni suala moja, kufanikiwa kupiga kura ni suala jingine, na kumpigia kura mgombea fulani na kura hiyo kumsaidia ashinde ni suala jingine kabisa.
Nimeshazungumzia katika makala zangu zilizotangulia kuwa moja ya faida kubwa kwa CCM ni mahusiano ya upendeleo kati yake na taasisi mbalimbali za umma. Na ninatarajia wengi wenu ndugu wasomaji mmekuwa mkisikia vilio vya wanasiasa wa upinzani takribani tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi kwamba wanaohisi kura zao zinahujumiwa na chama tawala kwa kusaidiwa na taasisi za umma ‘zinazokipendelea’ chama hicho.
Japo mara zote tuhuma hizo zimeendelea kubaki kuwa tuhuma tu, ushahidi wa kimazingira unaelekea kuzisapoti tuhuma hizo.
Binafsi, nimekuwa nikifuatilia pilika za uchaguzi mkuu kupitia mtandaoni, hususani kwenye mitandao ya kijamii (social media). Majuzi, niliwatahadharisha mashabiki wa Lowassa kuhusu furaha yao inayotokana na wingi wa wahudhuriaji katika shughuli za hadhara zinazomhusu mwanasiasa huyo.
Niliwakumbusha kuhusu chaguzi zilizopita, hususan ‘kasi ya (Agustino Lyatonga) Mrema,’ aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 kupitia chama cha NCCR-Mageuzi, jinsi alivyokuwa maarufu na kujaza halaiki ya watu kwenye mikutano yake, lakini akaishia kubwagwa na mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa.
Niliwakumbusha pia kuhusu wingi wa watu waliojitokeza katika mikutano ya kampeni za Dk. Willibrord Slaa, aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi mkuu uliopita, mwaka 2010, lakini akishindwa na mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete.
Katika chaguzi zote hizo, pamoja na ule wa mwaka 2000 na 2005, kulikuwa na malalamiko kdhaa kuwa ‘CCM iliiba kura,’ lakini tuhuma hizo zilijifia zenyewe kutokana na kutokuwepo ushahidi halisi, sambamba na vikwazo vya kikatiba kupinga matokeo ya Urais.

Lakini kukumbushia yaliyojiri katika chaguzi hizo kulipelekea mimi kushambuliwa vikali, nikituhumiwa kuwa na ‘chuki binafsi’ dhidi ya Lowassa, huku wengine wakinituhumu kuwa nimenunuliwa na CCM. Na nikakumbushwa kuwa “nenda na wakati, hii ni 2015, achana na habari za 1995”.
Siwezi kuwalaumu watu ambao hawataki kusikikia lolote ‘baya’ kuhusu Lowassa, au jambo linaloweza kuwa kikwazo kwake kupata urais.
Kwa bahati mbaya, ujio wa mwanasiasa huyo huko Chadema unaoonekana kuwabadili wana-Chadema wengi, angalau huko mtandaoni, ambapo watu waliokuwa wakijadili hoja kiungwana, sasa wamekuwa mahiri wa matusi kwa kila anayeelekea kumpinga Lowassa.
Nitawalaumu kwa matumizi ya matusi badala ya kujenga hoja za kistaarabu, lakini sintowalaumu kwa kuwa ‘desperate.’ Wanasema mtu akielemewa na mafuriko basi atang’ang’ania hata unyasi ili ajiokoe.

CCM imewafikisha Watanzania wengi katikia hali hii tunavyoshuhudia. Sapoti kubwa kwa Lowassa sio kwa vile ni mchapakazi au anatarajiwa kuleta ‘miujiza’ bali ni kukata tamaa miongoni mwa Watanzania wengi, Tunasikia watu wakisema “ukiiweka CCM na jini, nitapiga kura yangu kwa jini”.
Lakini wakati kuwa na matumaini yanayotokana na kukata tamaa si tatizo sana, ni muhimu kuzingatia hali halisi. Kuna wanaodai ‘safari hii CCM haiwezi kutuibia kura’ Je kuna tofauti gani ya kimazingira ya uchaguzi katika ya mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwaka 1995,2000,2005 na 2010? Tume ya uchaguzi ni ileile, taasisi mbalimbali za umma zinazoshughulikia uchaguzi huo bado zipo vilevile, na vyombo vyetu vya dola bado vina ‘mentality’ ileile ya kuwaona Wapinzani kama wahaini, na hata Lowassa amekiri kuwa alipokuwa CCM alidhani vyombo vya dola vyalaumiwa bure tu na Wapinzani…hadi alipoonjeshwa ‘jeuri ya polisi’ hivi majuzi.
Lakini tukiweka kando kuhusu tatizo hilo ambalo niliona kama la kimfumo, yaani mfumo unaoipendelea CCM, kuna tatizo jingine ambalo pengine halijawa kubwa sana. Hili ni uwezo mdogo wa Lowassa katika kujieleza.
Unapofanikiwa kukusanya umati wa maelfu ya watu, kisha ukahutubia kwa dakika tano, na katika muda huo mfupi usiseme lolote la maana la kuwafanya waliohudhuria wakumbuke si ukubwa wa umati bali uzito wa hotuba ya aliyewajaza kwa wingi mahala husika, basi hapo kuna tatizo.
Na tatizo hili laweza kuwa turufu kwa mgombea wa CCM, Dk. Magufuli, ambaye anasifika kwa umahiri si tu wa kuongea bali kutoa takwimu nyingi kichwani kana kwamba ni mashine yenye kumbukumbu (memory) kubwa.
Ukizungumzia hilo kwa wana-Chadema/UKAWA, wanasema “nani anataka hotuba? Sisi tunachotaka ni kuondoa CCM tu”. Ninabaki ninajiuliza, “hivi wakifanikiwa ukiondoa CCM, nini kitafuata?” Sipati jibu.
Kwa kifupi, kinachowapa matumaini wana-Chadema/UKAWA na mashabiki wa Lowassa ni hayo ‘mafuriko.’ Iwapo yataweza kujitafsiri katika kura, muda utatupatia jibu (time will tell).
Na iwapo ‘mafuriko’ hayo yatamwezesha Lowassa kuingiza Ikulu, ninadhani hata wana-Chadema/UKAWA wengi hawajui jinsi gani atakavyowezesha kubadili kile kinachowafanya Watanzania wengi wachukizwe kuhusu CCM.

Kwa upande mmoja, kuahidi mabadiliko ni kitu kimoja, kutekeleza ahadi hiyo ni kitu kingine. Kwa upande mwingine, kuwa na nia ya kuleta mabadiliko ni kitu kimoja, uwezo wa kufanikisha nia hiyo ni kitu kingine, na hata pale nafasi ya kuleta mabadiliko inapopatikana, nyenzo na mazingira vyaweza kuwa kikwazo cha kutimiza azma hiyo.
Nihitimishe makala hii kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi huu katika toleo lijalo ambapo nitamzungumzia mgombea wa CCM, Dk. Magufuli kama nilivyomjadili Lowassa katika makala hii.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube