28 Nov 2015


Makala hii imechapishwa katika jarida la Raia Mwema toleo la wiki hii lililotoka tarehe 25/11/2015, lakini kwa sababu nisizoelewa tovuti ya jarida hilo haijawa-updated kwa wiki kadhaa sasa. Kwa vile makala ninazotuma gazetini hufanyiwa uhariri kabla ya kuchapishwa, yawezekana makala iliyopo gazetini ikawa na tofauti kidogo na hii.

MAKALA YA RAIA MWEMA TOLEO LA NOVEMBA 25, 2015

Hotuba hii ya Rais Magufuli ni moja ya hotuba bora kabisa katika historia ya siasa za Tanzania.” Hili lilikuwa hitimisho langu katika mtandao wa kijamii wa Twitter mara baada ya Rais John Magufuli kumaliza kulihutubia Bunge wiki iliyopita, huko Dodoma.

Na kwa hakika watu kadhaa waliafikiana na hitimisho hilo.  Kilichovutia wengi waliosikia hotuba hiyo, katika shughuli ya ufunguzi wa Bunge la 11, sio tu mpangilio wa hotuba yenyewe bali pia jinsi kila alilotamka lilivyoonyesha bayana kuwa lilitoka moyoni mwake kwa dhati kabisa.

Rais alianza hotuba yake hiyo kwa kuorodhesha matatizo mbalimbali aliyobaini wakati wa kampeni zake Urais ambapo alizunguka takriban Tanzania nzima. Alitoa uchambuzi wa kina wa matatizo hayo kabla ya kuelezea kwa undani ni kwa jinsi gani serikali yake itayashughulikia. Ilikuwa ni zaidi ya hotuba ya kisiasa, na pengine ingeweza kabisa kuwa mhadhara wa kitaaluma uliofanyika katika lugha nyepesi na ya kueleweka.

Moja ya vitu vilivyonivutia sana katika hotuba hiyo ni jinsi Rais Magufuli alivyoweza kutupatia jibu la swali ambalo kwa miaka kadhaa lilionekana kuwatatiza viongozi wetu mbalimbali: “Kwanini Tanzania ni masikini licha ya utajiri lukuki wa raslimali ilionao.” Alieleza bayana na kwa kirefu jinsi ufisadi, rushwa na uhalifu vinavyochangia kukwamisha maendeleo ya taifa letu. Kadhalika, alifafanua, kwa kutumia takwimu halisi, jinsi mabilioni ya fedha yalivyotumika visivyo kwa matumizi yasiyo muhimu na yaliyo nje ya uwezo wa taifa letu masikini.

Kwa hakika ilikuwa hotuba ya kihistoria iliyofunika kabisa utovu wa nidhamu wa hali ya juu ulioonyeshwa awali na wabunge wa upinzani ambao walitumia muda mwingi kabla ya hotuba hiyo kuzomea na baadaye kuamiriwa  kutoka nje ya ukumbi huo.

Lakini kwa vile sio rahisi kumridhisha kila mtu, baadhi ya wenzetu waliosikiliza  hotuba hiyo walidai kuwa eti “haina tofauti na hotuba nyingine kadhaa zilizokuwa nzuri kuzisikiliza lakini zikaishia kuwa maneno matamu tu.” Wengine walikwenda mbali zaidi na kudai kuwa hata mtangulizi wa Rais Magufuli, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete naye pia alianza urais wake kwa hotuba za kutia moyo kama hizo lakini mengi ya aliyoahidi, hususan lile la ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania,’ yaliishia kuwa ahadi tu.

Sikubaliani kabisa na wakosoaji hao, japo hoja zao zinaweza kuwa na mantiki kidogo. Ni kweli kwamba ukosefu wa hotuba za kuvutia si moja ya matatizo yanayoikabili nchi yetu. Wengi wa wanasiasa na viongozi wetu ni mahiri sana wa maneno lakini tatizo huwa katika kutafsiri maneno yao kuwa vitendo.
Wakosoaji hao hawapo sahihi kwa sababu, kama nilivyoeleza awali, hotuba hiyo ilikuwa ya kutoka moyoni.Ilikuwa hotuba ya kiongozi anayeguswa na yanayoisibu nchi yake, kiongozi mwenye uelewa wa changamoto zinazoukabili uongozi wake, na mwenye dhamira thabiti ya kukabiliana na changamoto hizo.

Kuna mbinu moja muhimu ya kubaini iwapo mtu anaongea ukweli au anahadaa, nayo ni kumwangalia usoni. Tangu kuanza kwa kampeni zake za urais na hadi wakati wa hotuba hiyo ya wiki iliyopita, uso wa Rais Magufuli wakati anaongea unaonyesha bayana kuwa kila neno linalotoka mdomoni mwake ni la dhati, linatoka moyoni na si sehemu ya porojo tulilozowea kutoka kwa wengi wa wanasiasa na viongozi wetu. Mtaalam yeyote wa kubaini ukweli na uongo hatoshindwa kuafikiana nami kuwa uthabiti wa kauli za Magufuli upo wazi kwa yeyete anayemwangalia usoni wakati anaongea.

Lakini pia, hotuba hiyo ilikuwa mwendelezo wa ishara nzuri zilizoanza kujitokeza siku moja tu tangu Rais Magufuli aingie ofisini, ambapo alifanya ziara ya kushtukiza Wizara ya Fedha, kabla ya kufanya ziara nyingine kama hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Na siku ya uzinduzi wa Bunge, alitukumbusha enzi za (Waziri Mkuu wa zamani) hayati Edward Sokoine, aliyesifika kwa uchungu wa mali za umma, baada ya kuamuru zaidi ya shilingi milioni 200 zilizochangwa kwa ajili ya hafla ya mchapalo ya sherehe za uzinduzi wa Bunge jipya zielekezwe kwenye ununuzi wa vitanda katika hospitali ya Muhimbili, na kiasi kidogo tu kitumike kwa ajili ya hafla hiyo.

Kimahesabu, chini ya wiki tatu tangu aingie madarakani, Rais Magufuli ameshaokoa jumla ya shilingi milioni 900 kutokana na hatua alizochukua dhidi ya matumizi yasiyo ya lazima. Kwa kasi hii, tuna kila sababu ya kutarajiwa kuiona nchi yetu ikipaa kiuchumi, na hatimaye Watanzania kunufaika na neema lukuki ambayo nchi yetu imejaaliwa kuwa nayo.

Sina shaka kuhusu uwezekano wa mafanikio ya hatua za Rais Magufuli huko serikalini. Licha ya kuwa na Waziri Mkuu mchapakazi mzoefu, Majaliwa Kassim Majaliwa, kuna kila dalili kuwa baraza la mawaziri ambalo hadi wakati ninaandaa makala hii lilikuwa halijatangazwa, litasheheni wachapakazi kama yeye. Kwahiyo, kazi ya kurejesha nidhamu serikalini, kupunguza matumizi yasiyoendana na umasikini wetu na kupambana na ufisadi ina dalili kubwa za mafanikio.

Eneo ambalo Rais Magufuli hawezi kufanikiwa peke yake pasipo ushirikiano wa Watanzania wote ni nje ya serikalini na huko ‘mtaani.’ Mara kadhaa nimekuwa nikisisitiza umuhimu wa wananchi kujenga kasumba ya kudai haki na stahili zao badala ya kuona haki/stahili hizo ni kama fadhila au upendeleo flani. Wenzetu huku Ughaibuni wamejenga desturi ya kutokubali huduma au bidhaa inayotolewa chini ya kiwango wanachostahili. Haki na stahili za mpokea huduma ni miongoni mwa vitu vinavyopewa umuhimu mkubwa huku tulipo.

Haitokuwa rahisi kwa Rais Magufuli au wasaidizi wake kwenda kila sehemu kuwezesha au kuharakiasha upatikanaji wa huduma. Jukumu hilo linapaswa kusaidiwa na wananchi wenyewe ambao mara nyingi ndio wahanga wakubwa wa huduma mbovu. Kadhalika, watoa huduma nje ya serikali wanapaswa kutambua kuwa hizi ni zama mpya, na asiyeweza kuendana na kasi ya Rais Magufuli na ajiweke kando.

Lakini mchango mkubwa zaidi wa wananchi wote unahitajika zaidi katika kupambana na ufisadi, rushwa na uhalifu mwingine nje ya serikali. Wakati Rais ameahidi kukabiliana na ‘mapapa’ wa uhalifu kama kwenye biashara hatari ya madawa ya kulevya, pasipo wananchi kumsaidia kwa kuwatenga wahusika na kuwaripoti -  badala ya kuwasujudia na kuwapa majina ya heshima kama ‘wazungu wa unga’ au ‘mapedejee’ – basi tutamkwamisha, na nchi yetu itaendelea kuumizwa na vitendo hivyo viovu.

Kadhalika, ili kauli-mbiu ya ‘Hapa Ni Kazi Tu’ iweze kuleta matokeo kusudiwa na kuwa ya ufanisi ni muhimu kwa kila Mtanzania kuachana na dhana fyongo ya kusaka mafanikio kwa njia za mkato, turejee zama za Ujamaa na Kujitegemea ambapo waliokula bila kuvuja jasho tuliwaita ‘kupe.’ Sote tuchape kazi, tuache kufanya ‘ujanja ujanja,’ tuone fahari kuwa na shughuli halali badala ya kuamini kuwa ufisadi, rushwa, uhalifu,nk ndio njia rahisi na sahihi za kufikia mafanikio kwa haraka.

Baada ya kumpoteza Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliyetujengea misingi imara ya taifa letu, japo sasa inamong’onyoka kwa kasi, na mzalendo wa daraja la kwanza, Marehemu Sokoine, sala/dua zetu katika wimbo wetu wa taifa katika maneno “Mungu Ibariki Tanzania…” zimesikika, na Mwenyezi Mungu ametuletea ‘Nyerere na Sokoine mpya’ kupitia kwa Rais wetu mpya Dkt Magufuli. Tusijiangushe wenyewe kwa kutotumia ipasavyo fursa hii adimu.

Nimalizie makala hii kwa wito ‘wa kitaalamu’ kwa ndugu zangu wa Idara ya Usalama wa Taifa, ambao pamoja na majukumu mengine, wana dhamana ya ulinzi wa Rais wetu na viongozi wengine wakuu kitaifa. Kama alivyosema mwenyewe, vita aliyoanzisha dhidi ya kila vitendo na kasumba zinazolikwaza taifa letu ni nzito na inawagusa watu wazito. Kwa vile yayumkinika kusema kuwa vitendo vya rushwa,ufisadi na uhalifu vimefikia hatua ya ‘kimafia,’ basi ni muhimu kuimarisha ulinzi wa Rais wetu (na viongozi wengine wanaopatiwa ulinzi) kwa sababu ‘tupo vitani.’

Simaanishi kuwa ulinzi uliopo una mapungufu lakini angalizo hili linazingatia ukweli kwamba ‘vita’ hiyo inagusa maslahi ya wengi, maslahi ya ‘kupe’ lukuki walioigeuza Tanzania yetu kuwa ni ‘shamba la bibi,’ la kuvuna wasichopanda, sambamba na wahalifu wanaoingiza, kuuza na kusafirisha madawa ya kulevya kana kwamba ni bidhaa iliyoidhinishwa na Shirika la Viwango la Taifa (TSB), majangili wanaoshindana kuua wanyamapori wetu na kusafirisha nyara za serikali, na wahalifu wengineo.

Rais Magufuli ameahidi kutotuangusha, basi nasi tusimwangushe.

Hapa Ni Kazi Tu!

Barua-pepe: [email protected] Tovuti: www.chahali.com Twitter: @chahali2 comments:

  1. Raia mwema halipatikani mtandaon labda wameona mapato yanapungua kwenye hard cpy......mawazo ni yangu binafsi

    ReplyDelete
  2. Raia mwema halipatikani mtandaon labda wameona mapato yanapungua kwenye hard cpy......mawazo ni yangu binafsi

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube