4 Dec 2015


KWA wanaofuatilia safu hii, watakumbuka kuwa mara baada ya CCM kumpitisha Dk. John Magufuli kuwa mgombea wake wa kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu uliopita, niliandika makala iliyoonyesha kukata tamaa na kutotegemea lolote jipya. Licha ya kutojutia kuwa na mtizamo huo ambao ulitokana na mwenendo wa chama hicho tawala kwa miaka kadhaa sasa, pia wakati huo nilikuwa na matumaini makubwa kuwa vyama vya upinzani, hususan Chadema vingetupatia mbadala wa CCM.

Hata hivyo, baada ya Chadema na vyama vingine vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumpokea Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, na baadaye kumteua kuwa mgombea wao, sambamba na ‘kumpa kisogo’ mwanasiasa aliyeifanyia makubwa Chadema, Dk. Willbrord Slaa, ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, nilitafakari upya msimamo wangu.


Awali, nilielekeza nguvu zangu katika kupingana na uamuzi wa Chadema/Ukawa kumpokea Lowassa na kumfanya kuwa mgombea wao wa kiti cha urais. Lakini kwa vile kwa vyovyote vile, ilikuwa lazima Rais wa Tano wa Tanzania angetoka aidha CCM au Ukawa na tayari nilishatafsiri kuwa uamuzi wa Lowassa kupokelewa na Upinzani na kufanywa mgombea wao ni usaliti, hatimaye nililazimika kumwangalia mgombea wa CCM, Dk. Magufuli, kwa jicho la tatu.


Baada ya kusikiliza hotuba yake siku ya uzinduzi wa kampeni za CCM na hotuba zilizofuatia alipozunguka sehemu mbalimbali za nchi yetu kuomba kura, niliamua kumuunga mkono kwa asilimia 100. Japo uamuzi huo haukuwa mgumu kwa vile kadri siku zilivyoenda ilionyesha bayana kuwa Dk. Magufuli angekuwa kiongozi mwafaka kwa Tanzania yetu, hofu yangu kuu haikuwa endapo angeshindwa bali iwapo angeshinda na kuendeleza yale yale yaliyonifanya kuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa CCM. Kadhalika, uamuzi huo, ulisababisha kurushiwa maneno makali na tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na madai kuwa nimenunuliwa na CCM.


Urahisi wa kumuunga mkono Dk. Magufuli ulichangiwa zaidi na kiburi kilichowapata wafuasi wa Lowassa ambao kwa kiasi kikubwa walikataa katakata kuweka mantiki mbele ya hisia. Wimbo uliotawala kwao ulikuwa ni mabadiliko tu, na kila aliyejaribu kuhoji kuhusu mabadiliko hayo alirushiwa maneno makali, na wakati mwingine kutukanwa. Kwa hiyo ilifikia wakati wa kuamua liwalo na liwe. Waingereza wana msemo ‘the end justifies the means,’ yaani, kwa tafsiri isiyo rasmi, matokeo huhalalisha njia iliyotumika kuyafikia.


Kwa hiyo, nilijipa matumaini kuwa iwapo Dk. Magufuli angeshinda na kutimiza ahadi zake basi sio tu itamaliza kelele za waliotuona wasaliti dhidi ya mabadiliko yaliyoahidiwa na Lowassa bali pia itatimiza ndoto ya kila Mtanzania kuiona nchi yetu ikipata kiongozi wa kutufikisha mahala tunapostahili kuwepo.


Bahati nzuri, sio tu kuwa Dk. Magufuli alishinda bali muda mfupi tu tangu aingie madarakani ameweza kufanya mambo makubwa zaidi ya matarajio ya wengi kwake. Kwa hiyo, tuliomuunga mkono sio tu tuna furaha ya ushindi wake lakini pia tuna furaha kubwa zaidi ya kupata mtu wa watu, anayetambua matatizo yanayoikabili nchi yetu, mwenye uamuzi stahili, na anayetupa matumaini kwamba hatimaye nchi yetu itaweza kuangamiza janga la kitaifa la rushwa na ufisadi, hatua itakayosaidia kutuondoa kwenye umasikini mkubwa licha ya rasilimali lukuki tulizonazo, na hatimaye kuwa na Tanzania tunayoweza kujivunia.


Binafsi, nimejijengea utaratibu wa kuanza siku yangu kwa kuangalia kilichojiri huko nyumbani, kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari mtandaoni. Mara nyingi utaratibu huo wa kila siku uliishia tu kutibua siku yangu kwani kila kukicha ilikuwa ni mlolongo wa habari mbaya baada ya habari mbaya. Ilikuwa nadra kwa wiki kupita bila kukumbana na habari za ufisadi, ujangili, ahadi za porojo, na kadhalika.


Lakini hali sasa ni tofauti tangu Magufuli aingie madarakani. Yaani ni raha mtindo mmoja, kwani kila siku ni habari njema juu ya habari njema. Na si vigumu kuwa na matumaini makubwa ikizingatiwa kuwa hadi wakati ninaandika makala hii, Rais Magufuli amekuwa madarakani kwa takriban wiki tatu tu. Yayumkinika kubashiri kuwa siku 100 za kwanza za urais wake zitashuhudia Tanzania ikiwa nchi ya mfano wa kuigwa.


Na hilo limeshaanza kutokea. Tayari vyombo mbalimbali vya habari, hususan barani Afrika, vimekuwa vikiripoti kwa wingi kuhusu hatua mbalimbali anazochukua Rais Magufuli. Lakini kivutio zaidi ni jinsi baadhi ya wananchi katika nchi kama Kenya, Uganda, Malawi, Afrika Kusini, Nigeria na kwingineko walivyofikia hatua ya kutamani Magufuli awe Rais wao. Hii inatukumbusha zama za Baba wa Taifa ambaye alionekana machoni mwa Waafrika wengi kama mmoja wachache wa bara zima.


Taratibu, hisia kuwa kasi ya Magufuli ni nguvu ya soda zinaanza kufutika huku wananchi wengi wakiahidi kumpa ushirikiano katika jitihada zake za kuikomboa Tanzania yetu. Hata baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani sasa wanamkubali baada ya kuridhishwa na uchapakazi wake.


Hata hivyo, kuna takriban makundi matatu ya wapinzani wa Dk. Magufuli. Kundi la kwanza ni la wapinzani wa asili, linalojumusiha wenzetu waliojitoa ufahamu na kuamini iwe isiwe lazima Lowassa angekuwa rais. Hawa hawashangazi na huenda baada ya muda ndoto ya urais wa Lowassa itawatoka na watakubaliana na hali halisi. Lakini kwa vile upinzani si uadui, na kimsingi upinzani wa kisiasa waweza kuwa chachu nzuri ya kumsaidia Rais wetu na chama chake kuibua uovu dhidi ya taifa letu, basi kundi hili si tatizo sana.


Kundi la pili ni la watu walioigeuza Tanzania yetu kuwa shamba la bibi, waliozoea kuvuna wasichopanda, watu ambao zama za Ujamaa tuliwaita kupe. Kundi hili lajumuisha mafisadi na wanufaika wa ufisadi, wahalifu (kwa mfano wauza dawa za kulevya, majangili). Hawa wanatambua kuwa arobaini za mwizi zimewadia. Kundi hili ni hatari kwani miongoni mwao kuna wenye tabia za kimafia. Hawa si wa kufumbiwa macho hata kidogo, na ni muhimu kwa taasisi za usalama kuwabaini na kuwadhibiti mapema. Si rahisi kwa kundi hili kumkubali Magufuli au kuunga mkono jitihada zake kwa sababu kimsingi jeuri yao mtaani inafikishwa kikomo.


Kundi la tatu ni la wenzetu waliozowea kupata wasichostahili. Kuna ugonjwa mmoja unaitwa Stockholm Syndrome, ambao kwa kifupi ni hali inayomfanya mtu anayenyanyaswa au kuteswa kuyakubali manyanyaso/mateso hayo na kuyaona kama stahili yake. Mara kadhaa tunashuhudia mwanandoa anayeteswa na mwenza wake akitokea kuwa mtetezi wake mkuu. Katika kundi hili kuna wenzetu wanaoamini kuwa mapambano dhidi ya rushwa au ufisadi hayawezi kufanikiwa kwa vile, kwa mtizamo wao, ni hatima (destiny) ya taifa letu. Uzuri ni kwamba kadri jitihada za Magufuli zitakavyozidi kuzaa matunda, taratibu watu wa aina hii wataanza kutambua kuwa imani yao ni fyongo.


Nimalizie makala kwa kukumbushia kuwa hakuna safari isiyo na kona au milima na mabonde. Jitihada za Magufuli kuikomboa Tanzania yetu hazitokuwa nyepesi lakini la muhimu ni imani kuwa zitafanikiwa. Hata hivyo, ili jitihada hizo zifanikiwe ni wajibu wetu sio tu kumuunga mkono au kumsifia tu bali nasi wenyewe tunapaswa kubadilika kwa kuchukia ufisadi, rushwa, uzembe na vitu vingine vinavyolikwaza taifa letu.


INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO

- Se

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube