
‘HAPPY
birthday Tanzania…happy birthday me.” Naam, leo ni sikukuu ya Uhuru na Jamhuri,
siku ya kuzaliwa kwa Tanganyika (sasa Tanzania Bara), siku ambayo pia ni ya
kuzaliwa kwangu.
Nilizaliwa
Desemba 9, miaka kadhaa baada ya uhuru wa nchi yetu, na kila ninapoadhimisha
siku ya kuzaliwa, ninaadhimisha pia siku ya kuzaliwa kwa nchi yetu.
Kwa
kawaida, maadhimisho yangu ya siku ya kuzaliwa huwa sio sherehe bali hutumia
siku hiyo kumshukuru Mungu, sambamba na kufanya tafakuri ya nilipotoka, nilipo
na niendapo. Sherehe pekee ilikuwa kuimbiwa wimbo wa ‘Happy Birthday’ na
marehemu baba, ambaye kwa bahati mbaya hayupo nasi sasa. Kwa hiyo hii itakuwa
birthday yangu ya kwanza kukosa ‘sherehe’ hiyo iliyoambatana na sala za
kumshukuru Mungu na kuniombea mafanikio.
Lakini
wakati wa kusherehekea siku ya kuzaliwa pamoja na ‘birthday-mate’ (mtu
mliyezaliwa naye siku moja) Tanzania imekuwa kama tukio la kihistoria na la
kujivunia, kwa upande mwingine kila ninapofanya tafakuri kuhusu ‘mwenzangu’
huyo alipotoka, alipo na aendako huishia kupatwa na maumivu.
Si
kwamba nimefanikiwa sana kuliko ‘mwenzangu’ huyo bali angalau kwa upande wangu
kila nikiangalia nilipotoka, nilipo na niendako, nimekuwa naona mwanga zaidi.
Kwa ‘mwenzangu’ Tanzania, wakati huko alikotoka kulileta matumaini, alipo na
aendako (kwa miaka ya hivi karibuni) kulinipa shaka.
-Lengo
la kupata uhuru halikuwa kumwondoa tu mkoloni bali pia kujenga jamii yenye
amani na usawa, pamoja na mambo mengine. Japo katika miaka 54 ya uhuru wetu,
Tanzania imeendelea kuwa nchi ya amani kwa maana ya kutokuwepo vita, lakini
katika miaka ya hivi karibuni amani kwa maana ya kuwa na uhakika wa mlo wa
kesho, au wanafunzi kuwa na hakika ya ajira wanapomaliza masomo au wakulima
kuwa na uhakika wa mauzo ya mazao yao, au wagonjwa kuwa na uhakika wa huduma
wanayostahili katika vituo vya afya na uhakika katika maeneo mengine, vimekuwa
ni mgogoro.
Kadhalika,
amani yetu imeonekana kuwanufaisha zaidi ‘mchwa’ wachache walioigeuza Tanzania
yetu kuwa shamba la bibi, wenzetu ambao miaka michache iliyopita tuliwaita
kupe, wanaovuna wasichopanda, wanaoneemeka kwa jasho la wengine.
Mara
kadhaa, maadhimisho ya sikukuu ya uhuru wetu yameambatana na swali gumu, je
kweli tupo huru? hasa ikizingatiwa kuwa kwa kiasi kikubwa nchi yetu imeendelea
kuwa tegemezi kwa wafadhili, miongoni mwao wakiwa watu walewale tuliowafukuza
mwaka 1961.
Kuna
wenzetu wengi tu wanaodhani kuwa uhuru wetu ulifanikiwa kumtimua mtu mweupe
lakini miaka kadhaa baadaye huku tukiwa huru tumeshuhudia ukoloni mpya
unaofanywa na mtu mweusi. Na japo wakoloni hawawezi kuwa na kisingizio cha
kututawala, lakini walipoinyonya nchi yetu walikuwa na malengo ya kunufaisha
nchi zao na sio watu binafsi. Kadhalika, hawakuwa na uchungu na nchi yetu kwa
vile sio yao.
Kinyume
chake, wakoloni weusi sio tu ni wenzetu bali wengi wao aidha walisomeshwa bure
au kwa fedha za Watanzania wenzao, lakini badala ya kurejesha fadhila kwa
kulitumikia taifa kwa uadilifu, wameishia kuwa wanyonyaji wasio na huruma.
Tofauti na wakoloni weupe, wenzetu hawa hawana kisingizio japo kimoja kwani
wanainyonya nchi yao wenyewe.
Moja
ya vikwazo vya kutuwezesha kufaidi matunda ya uhuru ni ukosefu wa uzalendo.
Licha ya jitihada kubwa za Mwalimu Nyerere kuhamasisha mapenzi na uchungu kwa
nchi yetu – uzalendo- tawala zilizofuatia baada ya yeye kung’atuka zikawekeza
katika kuboresha maslahi binafsi badala ya maslahi ya taifa. Japo mabadiliko
yaliyoikumba dunia wakati Mwalimu anataka madaraka yalisababisha haja ya
mageuzi katika itikadi ya ujamaa, lakini kilichofanyika si mageuzi tu bali kuua
kabisa mfumo wa ujamaa.
Kuna
wanaodai kuwa isingewezekana kufanya mageuzi ya kisiasa na uchumi huku
tukikumbatia mfumo wa ujamaa. Hilo sio sahihi, kwani tunashuhudia taifa kubwa
kama China ambalo limefikia hatua ya juu kabisa ya ujamaa yaani ukomunisti,
likimudu kuendelea kuwa taifa la kijamaa huku likijihusisha pia na sera za
uchumi wa kibepari kama vile uwekezaji.
Nikirejea
kwenye siku ya kuzaliwa Tanzania Bara, na yangu, Ninaomba kukiri kuwa baada ya
muda mrefu, mwaka huu sikukuu yetu ya kuzaliwa mie na ‘mwenzangu’ inaleta
furaha na matumaini.
Na
yote hayo ni matokeo ya ninachokitafsiri kama kusikilizwa kwa dua/sala zetu kwa
Mwenyezi Mungu kuturejeshea Nyerere na (Waziri Mkuu wa zamani marehemu Edward)
Sokoine wengine. Tumejaaliwa kumpata Rais mpya, Dk. John Magufuli, ambaye mwezi
mmoja tu tangu aingie madarakani ameweza kwa kiasi kikubwa kurejesha matumaini
yaliyopotea.
Na
pengine kuashiria kuwa Nyerere amerudi kupitia Dkt Magufuli, mwaka huu
tunaadhimisha siku ya uhuru na Jamhuri kwa shughuli za usafi wa mazingira, na
hii inakumbusha dhana ya Mwalimu ya Uhuru na Kazi. Na kwa hakika hatuwezi kuwa
huru kwa kuwafanyia kazi wenzetu wanaotuibia kila kukicha.
Majuzi
akiwahutubia wafanyabiashara wakubwa huko nyumbani (Tanzania), Rais Dk.
Magufuli alieleza bayana jinsi tunavyoweza kutoka kundi la nchi masikini na
ombaomba na kuwa miongoni mwa nchi wafadhili iwapo tutatumia raslimali zetu
vizuri, sambamba na kupambana na ufisadi. Uhuru wa bendera pekee, wa kumwondoa
mkoloni mweupe huku tukisumbuliwa na mkoloni mweusi ni tatizo kwani suala si
rangi ya mkoloni bali ukoloni wenyewe. Tukimudu kuboresha uchumi wetu na kuweza
kujitegemea, tutakuwa na uhuru kamili.
Kadhalika,
kama Mwalimu alivyotufundisha, uhuru bila nidhamu ni uwendawazimu. Hatuwezi
kuwa na uhuru kamili kama hatuna nidhamu ya matumizi na tuliowapa dhamana ya
kutuongoza hawana nidhamu kwa maadili ya taifa.
Ni
matumaini yetu wengi kuwa maadhimisho haya ya siku ya uhuru na Jamhuri kwa njia
ya uhuru na kazi, sambamba na kasi kubwa ya Dk. Magufuli kutumbua majipu ni
ishara njema kuwa Tanzania tuliyoitarajia Desemba 9, 1961 na kufaidika nayo
zama za Mwalimu, ipo mbioni kurejea.
Nimalizie
makala hii kwa kusema tena ‘Happy birthday Tanzania, happy birthday to me.’
Mungu
Ibariki Tanzania.
Mungu
mbariki Rais wetu Dk. John Magufuli.
Mungu
tubariki Watanzania.
0 comments:
Post a Comment