26 Feb 2016

WIKI mbili zilizopita nilishiriki katika mjadala maalumu ulioendeshwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani kuhusu siku 100 za utawala wa Rais John Magufuli.
Lengo la makala hii sio kuzungumzia mjadala huo bali mada ya hiyo muhimu kwa Dk. Magufuli na serikali yake ya Awamu ya Tano, pamoja na Watanzania kwa ujumla.
Katika baadhi ya makala za hivi karibuni nilieleza kuhusu kitabu nilichochapisha kuhusu Dk. Magufuli na safari yake ya kuelekea Ikulu, sambamba na mafanikio na changamoto kwa urais wake. Lakini nilikosolewa na watu kadhaa waliodai ni mapema mno kuzungumzia mafaniko ya kiongozi huyo katika muda mfupi aliokaa madarakani.
Hata hivyo, wakosoaji hao walikerwa na mafaniko tu na si changamoto kwake, ikiashiria bayana kuwa wangependa zaidi kuona Dk. Magufuli akikosolewa kuliko kupongezwa.
Mshiriki mmoja katika mjadala huo naye aligusia hoja hiyo na alitumia muda mwingi kukumbusha kuwa hata watangulizi wake (Dk. Magufuli) walianza urais wao kwa kasi kama hii tunayoshuhudia hivi sasa.
Sina tatizo sana na wanaodhani ni mapema mno kusherehekea ufanisi mkubwa unaoendelea kuonekana katika uchapakazi wa Magufuli na serikali yake. Kimsingi, hofu waliyonayo wanaodhani ni mapema mno ina mantiki, hasa kwa vile yalishatukumba huko nyuma.
Kwa mfano, katika awamu yake ya kwanza, Rais Benjamin Mkapa alifanikiwa kurejesha nidhamu ya matumizi na takwimu za uchumi wetu zilipaa. Hata hivyo, awamu ya pili ya uongozi wake ilikuwa na mengi yaliyoathiri mazuri mengi aliyofanya katika awamu yake ya kwanza.
Kadhalika, katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, mwanzoni ilonekana kuwa Tanzania imempata kiongozi ambaye sio tu anayajua matatizo yanayoikabili nchi bali pia mwenye nia ya dhati ya kuyatatua. Kaulimbiu ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania ilileta matumaini kwa kila Mtanzania. Vile vile, maelezo yake kwamba sio tu anawafahamu wala rushwa bali pia anawafahamu kwa majina ilileta hisia kuwa arobaini ya wala rushwa imewadia. Sote tunafahamu kilichojiri katika miaka 10 ya utawala wake.
Kwa mantiki hiyo, wenye kumbukumbu hizo zisizopendeza wana haki ya kuwa na hofu ya mwenendo wa kuridhisha wa utawala wa Dk. Magufuli na serikali yake inayoendeshwa kwa kuzingatia kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu.
Hata hivyo, nilitumia mfano huu katika mjadala huo wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani, timu mbovu ya soka, ambayo miaka nenda rudi imekuwa ikiboronga, itakapokuwa na mechi muhimu, ikafunga goli la kwanza tu, basi mashabiki hawawezi kuacha kushangilia kisa huko nyuma ilikuwa kichwa cha mwendawazimu.
Mashabiki wataishangilia na kuihamasisha, ambapo hamasa hiyo ikichanganywa na goli moja walilokwishafunga, vyaweza kuipa nguvu timu hiyo ya kichovu kupata bao jingine na pengine mengi zaidi.
Kwa mashabiki wa soka wa ligi kuu ya hapa Uingereza, ni nani alidhani timu ya kawaida tu ya Leicester City ingekuwa miongoni mwa timu zenye nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa kuliko wakongwe kama Manchester United?
Mfano huo unamaanisha kwamba kwa vile mwenendo wa Tanzania yetu katika awamu zilizopita ulianza kwa matumaini na kisha matumaini hayo kuyeyuka haimaanishi kuwa lazima iwe hivyo milele. Tukumbuke kuwa penye nia pana njia, pasipo na nia pana visingizio.
Pengine kabla ya kumhukumu Magufuli kama Rais ni vema kuangalia utendaji wake huko nyuma katika nyadhifa mbalimbali alizoshika. Kimsingi, moja ya ugumu mkubwa niliokumbana nao wakati naandika kitabu kinachomhusu ni uhaba wa maelezo kutoka kwake mwenyewe. Yaani machache yaliyo kwenye vyombo vya habari yanaelezea zaidi kuhusu aliyokuwa akitenda kuliko aliyoongea.
Wakati pekee ambapo kauli za Magufuli zilisikika zaidi ni wakati wa kampeni za kuwania urais. Na kauli hizo ndizo zilizotupatia ushawishi sisi wengine kuamini kuwa huyo ndiye kiongozi ambaye Tanzania inamhitaji. Sio tu alionyesha kujua kwa undani matatizo yanayoikabili nchi yetu bali pia alikuwa na mwelekeo kuhusu jinsi ya kuzikabili na kuzitatua.
Na kama ilivyokuwa kwenye zama za uwaziri, Magufuli tangu aingie Ikulu amekuwa mwingi wa vitendo kuliko maneno. Anapozungumza, unatamani aendelee maana hazungumzia kama kiongozi tu bali pia kama Mtanzania ambaye amechoshwa na mwenendo wa taifa letu na amedhamiria kubadilisha mwelekeo kwa uzuri.
Changamoto si lazima ziwe kikwazo kwa kiongozi. Kimsingi, changamoto ni kipimo kizuri kwa kiongozi kwa sababu kadri anavyozishughulikia zinaonyesha uwezo wake wa kiuongozi. Na itakuwa sio kumtendea haki kama akili yetu itaelekezwa kwenye changamoto tu (na ambazo baadhi amekuwa akizishughulikia vema) na kupuuzia mafaniko ya kihistoria aliyokwishapata.
Vile vile ni muhimu kutambua hali ya nchi yetu ilivyokuwa wakati Magufuli anaingia madarakani. Takriban kila eneo lilikuwa shaghalabaghala. Angeweza kabisa kujipa kisingizio kwa hotuba mfululizo kutueleza mlolongo wa matatizo na changamoto zilizopo huku akihitaji muda wa kuanza kuzishughulikia.
Lakini kama tunavyoshuhudia, na kwa vile sote tunamfahamu kama mtu wa vitendo zaidi kuliko maneno, anashughulikia matatizo na changamoto hizo zaidi ya kuongea tu.
Kuna tatizo kuhusu Zanzibar, ambalo kwa hakika linatia doa kuhusu Awamu ya Tano. Hata hivyo, kumlaumu Magufuli kwa vile ni Rais wa Tanzania nzima ni kupuuza mkanganyiko wa kikatiba kati ya ile ya Muungano na hiyo ya Zanzibar. Tunapoambiwa kuwa Magufuli hawezi kutatua mgogoro huo ni ukweli, na kama tunavyofahamu, ukweli una sifa moja kuu: hata ukiwa mchungu, hauwi uongo bali unabaki ukweli. Tungependa afanye kitu fulani kuhusu mgogoro huo lakini Katiba inambana.
Kuhusu ushauri wa nini kifanyike baada ya siku hizo 100 za urais, nafasi katika makala hii haitoshi kuelezea kwa kirefu lakini machache ni haya: mosi, asiingie mtego wa kutanguliza maslahi ya kisiasa badala ya maslahi ya nchi (na historia yaonyesha kuwa amekuwa akiongozwa na utaifa kuliko itikadi za kisiasa.
Pili, sambamba na mapambano endelevu kuhusu ufisadi, rushwa na uhalifu mwingine, aweke mkazo katika kuhamasisha uzalendo ambao umepotea kwa kiasi kikubwa. Hii itasaidia pia kupata uungwaji mkono kwenye mapambano yake dhidi ya ufisadi na uhalifu mwingine.
Tatu, kuhamasisha kilimo kwa vitendo badala ya sera mfululizo zilizoishia kuwa sera tu pasi mafanikio. Vile vile, aweke kipaumbele kuhakikisha kuwa licha ya kuwa mkombozi wa kiuchumi kwa wakulima, kilimo kinakuwa chanzo cha ajira.

Nne, haja ya kuyaangalia maendeleo ya sayansi na teknolojia kama mahitaji muhimu (basic needs) na sio anasa (luxury), kwa sababu katika miaka michache ijayo, tunapopuuza maendeleo ya sayansi na teknolojia tutabaki kuwa kama kisiwa.
Tano, kuendeleza mabadiliko ya Katiba ambayo yatazingatia maslahi ya nchi badala ya chama, na hili linaweza kutoa ufumbuzi wa migogoro isiyoisha kila kunapofanyika uchaguzi mkuu huko Zanzibar.
Sita, tumbua majipu ihamie kwenye chama tawala, hasa kwa vile huko ndiko kunakoweza kumkwaza zaidi kuliko vyama vya upinzani. Inakera mno kuona mwanasiasa mwenye lundo la tuhuma za ufisadi akichaguliwa kushika nafasi muhimu kwenye taasisi kama Bunge, kwa vile tu amepigiwa debe na wana-CCM wenzake.
Saba, hatujawa na mfumo wa kuthamini mchango wa Watanzania wenzetu, walio ndani au nje ya nchi yetu, wanaojitoa mhanga kupigania maslahi ya nchi yetu. Ifike mahala michango yao itambuliwe, si kwa kupewa vyeo bali hata kutambua rasmi (acknowledge) jitihada zao kwa pongezi tu.
Nane, kubwa zaidi ni mageuzi kwenye Idara ya Usalama wa Taifa (nimeyaeleza kwa kirefu katika kitabu nilichochapisha majuzi kuhusu taaluma hiyo nyeti).
Mwisho, kama alivyoeleza katika hotuba yake kwa wazee wa Jiji la Dar es Salaam, wakati tunajadili siku zake 100 tangu aingie aingie madarakani, je, sisi wenyewe kama wananchi tumefanya nini kwa nchi yetu katika siku hizo 100?
Tusijadili tu Magufuli ameifanyia nini Tanzania, tujiulize pia nasi tumeifanyia nini nchi yetu. Tusitarajie tu Magufuli atafanya nini, tutafakari nasi tunafanya au tutafanya nini kwa nchi yetu.
Hongera Magufuli kwa kutimiza siku 100 za urais wako kwa ufanisi wa kupigiwa mstari. Mungu akuongoze uendelee kuwa mtumishi bora wa umma, na atuongoze nasi wananchi kukuunga mkono na kutimiza wajibu wetu wa kiraia.
Mungu mbariki Rais Magufuli
Mungu Ibariki Tanzania yetu.
Mungu tubariki Watanzania

ANGALIZO: Makala hii ilipaswa kuchapishwa Jumatano mbili zilizopita lakini haikuchapishwa kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu. Iliandikwa maalum kwa ajili ya tathmini ya siku 100 tangu Rais Dokta Magufuli aingie madarakani.0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube