4 Mar 2016

MWISHONI mwa wiki iliyopita, mitandao kadhaa ya kijamii ilitawaliwa na shutuma dhidi ya tabia inayotoa mizizi kwa majirani zetu wa Kenya kutumia vivutio vya Tanzania kujitangaza kana kwamba vipo katika nchi hiyo.

Katika tukio la majuzi, video moja ilisambaa mtandaoni ikimwonyesha binti mmoja wa Kenya akihutubia mkutano mmoja wa kimataifa, huku akieleza bila aibu kuwa miongoni mwa vivutio vilivyopo nchini Kenya ni Bonde la Olduvai (Olduvai Gorge).


Tukio hilo ni moja tu katika mlolongo mrefu wa majirani zetu hao ‘kutupora’ umaarufu wetu, huku ‘uongo’ maarufu zaidi ukiwa kuutangaza Mlima Kilimanjaro kuwa upo Kenya. Hata Jumapili wiki hii nilipotembelea mtandao wa kijamii wa Twitter, nilikutana na ‘tweet’ moja inayodai kuwa Mlima huo unaonekana vizuri zaidi nchini Kenya (kuliko Tanzania).


Pamoja na lawama kadhaa zilizoelekezwa kwa majirani zetu hao, baadhi ya Watanzania walikwenda mbali zaidi na kuhoji kwa nini nchi jirani inapata ujasiri wa kujinadi kwa kutumia vivutio vyetu. Ukweli mchungu ni kwamba sisi wenyewe tumekuwa wazembe kwa kiasi kikubwa.


Uzembe huo unaonekana katika sura nyingi lakini pengine ya wazi zaidi ni katika ukweli mchungu kuwa licha ya madini ya Tanzanite kupatikana Tanzania pekee, nchi zinazoongoza kwa mauzo ya madini hayo ni India ikifuatiwa na Kenya. Hiki ni kichekesho kinachokera mno.


Binafsi, ninaona udhaifu katika kunadi vivutio vyetu na nchi yetu kwa ujumla unachangiwa na sababu kuu tatu. Ya kwanza, ni uhaba wa uzalendo. Mara kadhaa nimekuwa nikiandika kuhusu suala hili. Moja ya vitu muhimu alivyotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni kuthamini Utanzania wetu. Na thamani hiyo ya asili yetu haikuwa kwa sababu tu ni nchi yetu bali pia katika mambo kadhaa ya kujivunia kama vile mchango wa taifa letu katika mapambano ya ukombozi kusini mwa bara la Afrika.


Leo hii baadhi yetu tukikutana na Waafrika Kusini au Wazimbabwe, kwa mfano, wanaikumbuka Tanzania kama nchi iliyoshirikiana nao katika mapambano ya kudai haki yao ya kujitawala. Hata hivyo, baadhi hutuhoji kwa nini Tanzania imepoteza umaarufu mkubwa wa enzi za Mwalimu Nyerere.


Sababu ya pili, inayoshabihiana na hiyo ya kwanza ni ubinafsi. Watanzania wengi wamekuwa wakiweka mbele zaidi maslahi yao binafsi kuliko maslahi ya taifa letu. Umaarufu binafsi umekuwa ukipewa kipaumbele zaidi kuliko umaarufu wa nchi yetu. Kibaya zaidi, wachache tunaojitahidi kuitangaza nchi yetu kwa namna moja au nyingine huishia kuzodolewa kuwa tunafanya hivyo kwa minajili ya kujikomba au kusaka ukuu wa wilaya.


Katika hilo la ubinafsi, kunapojitokeza mawazo ya kuitangaza nchi yetu kimataifa, badala ya kuangalia taasisi au watu wenye uwezo wa kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, fursa huelekezwa kwa ndugu, jamaa na marafiki wasio na uwezo. Kipaumbele huwa kwenye fedha zilizotengwa kwa shughuli hiyo na wala sio matokeo chanya.


Sababu ya tatu ni kutowatumia vema Watanzania walio nje ya nchi. Kimsingi, kuwa Mtanzania nje ya nchi ni kama laana ya aina fulani. Kwa kiasi kikubwa tu, baadhi ya Watanzania wenzetu wanatuona sisi tulio nje ya nchi kama Watanzania vipande, yaani tusio kamili, na hatupaswi kujihusisha na masuala yanayohusu nchi yetu.


Baadhi yetu tunapojaribu kushiriki ujenzi wa taifa letu kwa njia kama hizi za maandiko huishia kukatishwa tamaa na kauli kama acha kutukebehi. Shida tunazopata hapa wazijua? Kana kwamba mtu akiwa nje ya Tanzania ndio amepoteza kila mawasiliano (connection) aliyonayo na nchi yetu, kuanzia ndugu, jamaa na marafiki hadi uraia.


Kama kuna nchi mbili barani Afrika ambazo zimenufaika sana kuwatumia raia wake wanaoishi nje ya nchi, nchi hizo ni Rwanda na Nigeria. Kwa Rwanda, takriban kila mwaka nchi hiyo hufanya makongamano katika nchi mbalimbali duniani, hususan hapa Uingereza na Marekani. Wiki iliyopita, Rais Paul Kagame yupo nchini Marekani, ambapo pamoja na mambo mengine anahamasisha Wanyarwanda walio nje ya nchi kushiriki katika ujenzi wa taifa lao.


Katika makongamano yaliyopita ya Rwanda hapa Uingereza, Rais Kagame alifanikiwa kuwashawishi Wanyarwanda kadhaa waliokuwa wanaishi hapa kurejea nyumbani na kuwapatia fursa mbalimbali zilizoendana na sifa, ujuzi na uzoefu wao walioupata walipokuwa hapa.
Kwa Nigeria, kabla ya kuunda serikali yake, na wakati huu ambapo nchi hiyo inapitia mageuzi makubwa ya kiuchumi, Rais Muhammad Buhari amekuwa akifanya jitihada kubwa kuwashawishi raia wa nchi yake waliotapakaa sehemu mbalimbali duniani kurejea katika taifa hilo ili kushiriki katika kulijenga na kuliboresha.


Sambamba na hatua hizo, badala ya kutumia fedha nyingi katika tenda za kuzipromoti nchi hizo nje ya nchi, kipaumbele kimekuwa katika kuwatumia raia wake kadhaa waliopo nje ya nchi hizo.


Licha ya kuvunjwa moyo, baadhi yetu tumeendelea na jitihada hizo za kuitangaza Tanzania yetu kwa kutumia njia mbalimbali. Kwa mfano, kwa muda sasa, binafsi nimekuwa nikijaribu kuitangaza Tanzania yetu kwenye mtandao wa kijamii wa twitter kwa mabandiko (tweets) yanayoambatana na hashtag #VisitTanzania (kwa kila habari au picha inayohusu vivutio vyetu) na #InvestInTanzania (kwa habari au picha zinazohusiana na fursa za uwekezaji huko nyumbani. Hata hivyo, mapokeo yamekuwa sio ya kuridhisha japo hainivunji moyo.


Kwa upande mwingine, licha ya uandishi wa vitabu kwa lugha ya Kiswahili kuchangia jitihada za kuitangaza Tanzania yetu kupitia lugha yetu ya taifa, ninaitumia pia fursa niliyoipata hivi majuzi ya kufundisha Kiswahili kwa kundi la wanafunzi wa shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Glasgow, (wanaotarajia kuja huko nyumbani kwa ajili ya tafiti zao) kuitangaza nchi yetu kwa namna moja au nyingine.


Nihitimishe makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuhusu busara hii: “…usipoeleza mazuri yako wewe mwenyewe, wenzako wataeleza mabaya yako au kuyapora mazuri yako hayo.” Hicho ndio kinachofanywa na majirani zetu wanaojinadi kwa kutumia vivutio vyetu. Sisi wenye vivutio hivyo tumejisahau/tunazembea, wenzetu wanaojua umuhimu wa kujinadi wanatumia vyema kujisahau kwetu/uzembe wetu kwa manufaa yao.
Kadhalika, ninatoa wito kwa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kutumia vyema Watanzania wenye uwezo na fursa za kuinadi nchi yetu, ndani na nje ya Tanzania.


Mungu Ibariki Tanzania

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube