17 Jun 2016


Wanaofuatilia vema siasa za Tanzania watakumbuka vizuri enzi za ‘ugaidi’ wa Chadema. Kwa bahati mbaya, mmoja wa makada wa CCM ‘walioshikilia bango’ tuhuma hizo za ugaidi alikuwa Mwigulu Nchemba, ambaye kwa sasa ndiye Waziri wa Mambo ya Ndani. 



Pengine ni kutokana na hali hiyo, inawezekana kujitokeza hisia, miongoni mwa wafuasi wa vyama vya upinzani kuwa “wasiyempenda kaja.”


Kwa kuzingatia historia yake huko nyuma, Mwigulu kama waziri mwenye mamlaka ya utendaji katika Jeshi la Polisi anaweza kutumia fursa hiyo kudhibiti vilivyo vyama vya upinzani na kibaya zaidi, uteuzi wake umekuja katika wakati ambao uhusiano kati ya Serikali ya Rais Magufuli na CCM, kwa upande mmoja, na wapinzani kwa upande mwingine, si mzuri.

Katika makala yangu ya wiki iliyopita niliyataja makundi mawili yanayofanya kila jitihada kustawisha siasa za mfarakano, ambayo ni kundi la viongozi wa vyama vya siasa na baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo.

Kwa mfano, uamuzi wa Bunge kuwafungua baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani ni dhahiri uamuzi huo utaathiri wananchi na si wabunge wanaowawakilisha. Kwa nini busara haikutumika hapa angalau kuwaonya wabunge hawa?

Baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani na kulifanya suala la vita dhidi ya ufisadi kuwa ajenda yake kuu, kulianza kujitokeza hisia kuwa upinzani utadhoofika kwa sababu suala hilo ndilo limekuwa turufu yao kuu. Sasa sijui ni kitu gani kimetokea, ghafla inaonekana kama CCM inawatafutia wapinzani hoja. Na hoja inayoonekana sasa ni kama kuna unyanyasaji dhidi ya vyama vya upinzani.

Kuanzia suala kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge na baadaye kupiga marufuku maandamano na mikutano ya siasa ya vyama vya upinzani ni mambo yaliyochangia kubadili hali ya awali ya wapinzani kukosa ajenda.

Tumeona Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akikamatwa lakini pia Kiongozi Mkuu wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe, naye akihojiwa polisi kwa madai kuwa ametoa hotuba ya kumkashifu Rais Magufuli. 


Na wakati nikijiandaa kuandika makala hii, sio tu kuwa kongamano la chama hicho kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 lilizuiliwa na Jeshi la Polisi lakini pia polisi wanaendelea kumfuatilia Zitto. Kwa lipi hasa?


Sina hakika kama ni uamuzi wa Rais Magufuli au kuna watu wanaojaribu kumkosanisha na vyama vya upinzani, lakini lililo wazi ni kwamba CCM inawapatia wapinzani hoja za kuibuka kisiasa.

Tukirejea kuhusu Mwigulu, ni muhimu kutambua kuwa hapa katikati ‘amebadilika’ kwa kiasi kikubwa. Ukimlinganisha Mwigulu ‘mrusha’ tuhuma za ugaidi na Mwigulu ‘mwomba’ ridhaa ya urais kwa tiketi ya CCM ni kama kuzungumzia watu wawili tofauti. Wakati yule wa mwanzo alikuwa akiendeshwa kwa mihemko ya kiitikadi na ukada, huyo mpya aliweka mbele maslahi ya taifa.

Wanaomfahamu vema wanadai kuwa ni mchapakazi hasa. Na ni katika hilo, majuzi nilimrushia pongezi na kumweleza matumaini kuwa sasa tumepata mtu anayeweza kumudu tatizo sugu la biashara ya dawa za kulevya. Ni wazi kuwa Mwigulu anaweza kujitengenezea mazingira mazuri ya kisiasa huko mbele (bado kijana na anaweza kuwania tena urais) iwapo atachapa kazi kwa kuwa mtumishi wa Watanzania wote na kutorejea zama za kuwazushia tuhuma za ugaidi wapinzani.

Nimalizie makala hii kwa kutoa rai kwa Rais Magufuli kuwa Watanzania wengi wanaridhishwa na jitihada zake za kuwatumikia kwa dhati huku akichukia kwa dhati ufisadi. Kadhalika, Watanzania wamechoshwa na siasa za uhasama ambazo zinawaathiri zaidi wananchi kuliko vyama vya siasa au viongozi wao. 


Tukusanye nguvu zetu, wananchi na viongozi wa vyama vya siasa, tujenge Tanzania ya neema na tunayostahili kuwa nayo. Tuna mengi ya kunufaika nayo katika umoja na ushirikiano wetu kuliko kuendekeza siasa za visasi, uhasama na uadui.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.