11 Jun 2016

NI takriban miezi minane sasa tangu Tanzania ilipofanya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, Oktoba 25, 2015. Uchaguzi huo ndio uliotupatia Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli. Ni vema nikatanabaisha mapema kuwa, kwa kutumia haki yangu ya kidemokrasia, ‘nilimpigia debe’ mgombea huyo wa chama tawala, CCM. Na hadi muda huu, sijajilaumu kuchukua uamuzi huo.

Hata hivyo, kwa upande wangu – na pengine kwa watu wengine wengi tu – baada ya uchaguzi huo kumalizika na hatimaye kupata serikali ya awamu mpya, masuala ya kampeni nayo yalihitimishwa. Zile tofauti tulizokuwa nazo wakati huo, za “Magufuli anafaa, Lowassa (aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema) hafai” au “Lowassa anafaa, Magufuli hafai” zimebaki kuwa historia. Tumekwishapata rais, sio wa CCM pekee, sio wa waliompigia kampeni na kura pekee, bali ni rais wa Watanzania wote.


Lakini kuna baadhi ya wenzetu, wengi tu, bado wapo katika kile tunachoweza kukiita mkao wa kikampeni (campaign mode) au kwa tafsiri isiyo rasmi). Kuna makundi makuu mawili: wanasiasa na wafuasi wa kambi kuu mbili katika uchaguzi huo, yaani CCM na Ukawa. Katika kundi la kwanza, kuna wanasiasa ambao kwa kiasi kikubwa wanaonekana kutamani kampeni za uchaguzi ziendelee. Hawa wanajitambulisha kwa lugha na matendo yao ambayo yameelemea kwenye kuzidisha uhasama wa kisiasa kuliko mwafaka wa kitaifa.


Na kama kuna sehemu nzuri ya kubaini hilo ni huko bungeni ambapo masuala mbalimbali ya maslahi ya taifa yanaonekana ya kipuuzi kwa sababu tu ya uhasama huo wa kisiasa. Wabunge wa CCM wenye nia ya kufanya kazi na wenzao wa Ukawa kwa ajili ya taifa letu wanakwazwa na hofu ya kuonekana wasaliti kwa chama chao. Na huenda hali ni hiyo kwa wale wa upinzani.


Kundi la pili ni la wafuasi wa kambi hizo, yaani CCM na Ukawa. Wakati upinzani baina yao unaokera, na kwa hakika unakwaza mijadala muhimu kuliko mustakabali wa taifa letu, kinachoudhi zaidi ni kasumba inayojitokeza ndani ya makundi hayo, ambapo wana-CCM wanaodhani kuna haja ya kukikosoa chama chao au Magufuli wanaonekana ni ‘mbwa mwitu kwenye ngozi ya kondoo,’ wasaliti. Hali ni hivyo hivyo kwa wana-Ukawa. Ukimkosoa Lowassa basi wewe ni kibaraka wa CCM.


Majuzi, nilikumbana na mkasa baada ya kukosoa uamuzi wa serikali kuwafukuza wanafunzi wa stashahada maalumu ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Mtu mmoja ‘alinivaa’ na kunilaumu kuwa ninashindwa kutumia uandishi wangu kumtetea Rais Magufuli. Ni baada ya kumwonyesha makala mbalimbali nilizoandika huko nyuma ‘kumnadi’ Magufuli na ‘kumtetea’ baada ya kuwa rais, sambamba na kitabu nilichoandika kuhusu urais wake, ndipo akadiriki kunitaka radhi. Huyu ni mmoja kati ya wengi wasiotaka kusikia lolote zaidi ya pongezi kwa vyama au viongozi wao.


Nimeanza makala hii kwa kuelezea suala hilo kwa sababu sio tu linakwaza mijadala muhimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu taifa letu lakini pia linaweza kuathiri dhamira nzuri ya Rais Magufuli kulitumikia taifa letu. Yeye mwenyewe alituomba tumsaidie katika uongozi wake na moja ya njia za kumsaidia mtu ni kumkosoa pale anapokosea.


Na bila kuuma maneno, na licha ya mimi binafsi kuwa ‘shabiki wa Magufuli,’ jinsi alivyoshughulikia suala la wanafunzi waliofukuzwa UDOM sio sawia. 

Kwanza, kilicholalamikiwa na wengi kuhusu hatua ya serikali kuwafukuza wanafunzi hao sio kwamba walistahili kuendelea na kozi hiyo au la bali namna walivyofukuzwa bila chembe ya ubinadamu. Na angalau basi wangekuwa wamefanya kosa fulani. Hawakuwa na kosa lolote kwa sababu hawakujidahili wenyewe wala kujiundia kozi hiyo au kujiunga wenyewe bila kuitwa chuoni.

Baadhi ya wanafunzi hao waliojitoa mhanga, wakaacha kwenda kidato cha tano huku alama walizopata zikiwaruhusu kuchaguliwa na kujiunga na kozi hiyo. Hawa sio ‘vilaza’ hata kidogo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mbunge kutoka Chama cha ACT, Zitto Kabwe, ni wanafunzi 88 tu ambao sifa zao zina mushkeli kuendelea na kozi hiyo. Hivi kulikuwa na ugumu gani wa kuchuja waliostahili kuendelea na kawaondoa hao wenye upungufu wa sifa stahili? Kilichokosekana ni busara tu.


Kwa heshima na taadhima, ninaomba pia kutoafikiana na kauli ya Rais Magufuli kuhusu vilaza. Hivi kweli tumesahau jinsi mpango kama huo wa stashahada maalumu ya ualimu, enzi hizo ukiitwa UPE (Universal Primary Education), ambao licha ya matatizo kama hayo ya stashahada ya Chuo Kikuu cha Dodoma, ulivyoweza kuiweka Tanzania yetu katika ramani ya kimataifa kwa mafanikio makubwa ya kielimu?


Sawa, kulikuwa na kasoro katika mpango huo wa stashahada maalumu ya ualimu, lakini mtoto hazaliwi akitambaa, kwa maana ya kwamba kila mwanzo ni mgumu. Kwa hiyo, kwa kutumia uzoefu wa UPE – kwa mfano vitu gani vilisababisha ‘kifo’ chake – tungeweza kabisa kuboresha stashahada hiyo maalumu ili itusaidie kukabili uhaba mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi, ambapo kwa mujibu wa takwimu za Zitto, ni walimu zaidi ya 20,000.


Kauli za Rais Magufuli zinakinzana na waziri wake Profesa Joyce Ndalichako. Lakini hilo sio muhimu kwa sasa. Wenye uelewa tunafahamu kwamba kuna makosa yamefanyika. Na badala ya kuendelea kunyoosheana vidole, ni vema serikali ikafanya utaratibu wa haraka wa kurekebisha kasoro hiyo. Sitarajii wanafunzi hao kuombwa msamaha wala kusikia hotuba ya kiongozi kukiri kwamba ushughulikiaji wa suala hilo haukuwa sahihi. La muhimu sio kuombana msamaha bali kurekebisha kosa husika.


Nimalizie makala hii kwa kuwasihi Watanzania wenzangu kwamba tuna mengi ya kunufaika kwa kuwa wamoja kuliko kuruhusu tofauti za kiitikadi au upinzani wa kisiasa au kimtazamo kututenganisha. Ifike mahala tuweke kando siasa kwenye masuala yanayohitaji busara au utaalamu.


Pamoja na kasoro kadhaa zilizojitokeza katika Awamu ya Nne, wazo hili la stashahada maalumu ya ualimu lilipaswa kuwa moja ya alama muhimu kiuongozi (legacies) za Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Nia yake ilikuwa nzuri, na kwa vile miongoni mwa walioridhia sera hiyo ni pamoja na Rais Magufuli (wakati huo akiwa mbunge na waziri), basi hakuna haja ya ‘kuwatesa’ vijana hao wazalendo ambao kufanikiwa kwao katika kozi hiyo kungesaidia kupunguza uhaba wa walimu ya masomo ya sayansi. 

Nihitimishe kwa msemo kwamba, kukosea ni ubinadamu lakini kujirekebisha ni utukufu (To err is human but to correct is greatness)0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube