2 Jun 2016

NINAANDIKA makala hii nikiwa na uchungu mkubwa. Uchungu huo unatokana na habari niliyoiona mtandaoni lakini sikuitilia maanani mwanzoni hadi nilipoisoma muda mfupi kabla ya kuandika makala hii.

Habari hiyo ni kuhusu uamuzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuwarudisha nyumbani wanafunzi 7,000. Hilo la kuwarudisha nyumbani tu sio jambo dogo lakini kibaya zaidi ni namna ya utekelezaji wa uamuzi huo.


Katika mazingira ya kawaida, na nikiamini kuwa wanafunzi hao wanatoka sehemu mbalimbali za nchi yetu, kuwaamuru waondoke chuoni hapo mara moja pasipo maandalizi ya kutosha sio tu ni kukosa ubinadamu bali pia kunahatarisha usalama wao.

Kwa mujibu wa maelezo kidogo yaliyopatikana hadi sasa, uamuzi huo wa kuwatimua wanafunzi hao umetokana na kinachoelezwa kuwa ni matatizo ya ufundishaji wa stashahada ya kozi maalumu ya ualimu wa sayansi.


Sitaki kabisa kuamini kuwa matatizo hayo yalijitokeza ghafla kiasi cha kusababisha uongozi wa chuo hicho kuchukua uamuzi huo wa ghafla. Haiwezekani kwamba uongozi wa chuo ulilala na kuamka na kukutana na matatizo hayo. Lazima uongozi huo ulikuwa ukifahamu kuhusu suala hilo muda mrefu na ulipaswa kutafuta njia mwafaka za utatuzi.

Waingereza wana usemi kwamba, “mipango mibovu huleta matokeo mabovu.” Kozi husika haikujitengeneza yenyewe, iliandaliwa na kuangaliwa ufanisi wake ungepatikanaje. Mambo kama hayo huchukua miezi kama sio miaka. Sasa iweje ghafla uongozi wa chuo ukurupuke na kueleza kuwa kuna matatizo?


Kwa mujibu wa gazeti moja la kila siku la huko nyumbani, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula alipotakiwa kufafanua kuhusu suala hilo alikiri uwepo wa tatizo hilo na kuelekeza kuwa atafutwe afisa uhusiano wa chuo hicho kwa maelezo zaidi.

Kwa upande wake, afisa huyo, Beatrice Baltazar, alieleza kwamba kusimamishwa kwa wanafunzi hao kulitokana na agizo la serikali na chuo hicho kimetakiwa kulitekeleza.


Ninapata shida kuamini kuwa serikali hii inayotumia kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” inaweza kufanya uamuzi wa kukurupuka kiasi hiki bila kujali mustakabali wa wanafunzi hao.


Taarifa za magazeti mbalimbali zinaonyesha kuwa wanachuo waliofukuzwa wamejikuta katika wakati mgumu, huku ikidaiwa kuwa baadhi ya wanachuo wa kike wameamua kujihusisha na ukahaba ili kujikimu. Ni rahisi kulaumu pindi msichana au mwanamke anapoamua kuutumia mwili wake kukidhi mahitaji yake ya fedha lakini moja ya sababu zinazoweza kumshawishi mtu kujiingiza kwenye vitendo visivyofaa kama ukahaba ni pamoja na kusaka ufumbuzi wa matatizo yanayomkabili.

Katika mazingira ya kawaida tu, mwanafunzi wa kike anapojikuta hana pa kulala wala kula, na ikizingatiwa kuwa mafisadi wa ngono wametapaa kila kona, kilichotokea huko Dodoma kinawaweka wanachuo wa kike katika mtihani mgumu ambao unaweza kuwa na athari za muda mrefu kisaikolojia.


Cha kusikitisha zaidi ni kwamba tukio hilo lisilopendeza limetokea wakati Bunge likiendelea na vikao vyake huko Dodoma. Kila mwanachuo aliyetimuliwa ana mwakilishi hapo bungeni, kwa maana ya mbunge wa jimbo lake. Na katika mazingira ya kawaida, wabunge walipaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa njia mwafaka zinatumika kutatua suala hilo sambamba na kuwapatia misaada wanachuo hao.


Lakini kama ilivyo kwenye kero nyingine majimboni, wabunge wengi wamekuwa na ufanisi mdogo katika kuelezea shida zinazowakabili wana-jimbo wao. Yayumkinika kuhisi kuwa laiti kila mbunge ambaye mwana-jimbo wake ni mwathirika wa uamuzi huo usio na busara na usio wa kibinadamu angeamua kupigana ‘kufa na kupona’ basi huenda serikali kupitia uongozi wa chuo hicho ungebadili uamuzi huo.


Tukio hili ni mwendelezo tu wa mazingira magumu yanayowaandama wasomi wa kesho. Kwa kiasi kikubwa, upatikanaji wa elimu nchini umekuwa kama adhabu, kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu.


Japo tunatambua kuwa uwezo wa serikali yetu ni mdogo kumudu gharama za elimu, na pia ikizingatiwa kuwa kuna vipaumbele vingine lukuki vinavyoikabili serikali yetu, lakini wakati mwingine kinachohitajika sio fedha bali busara tu.


Katika suala hili ninalozungumzia, ni dhahiri kuwa laiti uwepo wa matatizo husika ungebainika mapema na kutafutiwa ufumbuzi kwa njia stahili, basi tusingejikuta tuna kundi la maelfu ya wanafunzi wanaohangaika kurudi majumbani huku hawajui hatma yao kielimu na kimaisha ikoje.


Kuna wanaodhani kuwa jeuri za maofisini au katika sehemu za huduma huchangiwa na mazingira magumu ya elimu huko nchini. Kwamba, mtu baada ya kuhitimu masomo au kozi yake, na kuteseka vya kutosha, anakuwa na ‘hasira’ kiasi kwamba fursa ya kuitumia elimu yake kazini yaweza kuambatana na ‘kisasi’ kwa yeyote aliye mbele ya uso wake. Haipaswi kuwa hivyo lakini tutarajie nini kwa watu waliopata elimu kana kwamba wapo jela?


Sitarajii makala hii kubadili chochote kwa sababu tayari uamuzi umekwishafanyika na hatua zisizo za kiungwana zimekwishachukuliwa, yaani kuwafukuza wanachuo husika. Hakuna uwezekano wa fulani kusoma makala hii na kubadili uamuzi huo. Hata hivyo, bado kuna fursa ya busara kutumika kulitatua suala hilo.


Ni muhimu kwa serikali na uongozi wa chuo hicho kuandaa utaratibu wa kuwasiliana na wanafunzi hao kuwafahamisha kuhusu hatma yao. Na kama ambavyo mwajiri anavyolazimika kumfidia mwajiriwa anayesimamishwa kazi ilhali hajafanya kosa lolote, utaratibu mahsusi uandaliwe kufidia gharama walizoingia wanachuo hao kutokana na uamuzi huo wa ghafla.


Nimalizie makala hii kwa kuiomba Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kuanza jitihada za makusudi za kuyatengeneza mazingira ya elimu kuwa rafiki, yenye kumvutia mwanafunzi au mwanachuo kujiona ananufaika kwa ajili yake na taifa na sio kama amefanya kosa kujiunga au kuwepo kwenye taasisi ya elimu. Elimu sio ukombozi kwa mtu binafsi tu bali taifa kwa ujumla. Kama tunaandaa wasomi wa kulitumikia taifa letu kwa ufanisi na uzalendo basi maandalizi hayo yaambatane na kuwajengea mazingira mwafaka.0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube