Showing posts with label UDOM. Show all posts
Showing posts with label UDOM. Show all posts

11 Jun 2016

NI takriban miezi minane sasa tangu Tanzania ilipofanya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, Oktoba 25, 2015. Uchaguzi huo ndio uliotupatia Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli. Ni vema nikatanabaisha mapema kuwa, kwa kutumia haki yangu ya kidemokrasia, ‘nilimpigia debe’ mgombea huyo wa chama tawala, CCM. Na hadi muda huu, sijajilaumu kuchukua uamuzi huo.

Hata hivyo, kwa upande wangu – na pengine kwa watu wengine wengi tu – baada ya uchaguzi huo kumalizika na hatimaye kupata serikali ya awamu mpya, masuala ya kampeni nayo yalihitimishwa. Zile tofauti tulizokuwa nazo wakati huo, za “Magufuli anafaa, Lowassa (aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema) hafai” au “Lowassa anafaa, Magufuli hafai” zimebaki kuwa historia. Tumekwishapata rais, sio wa CCM pekee, sio wa waliompigia kampeni na kura pekee, bali ni rais wa Watanzania wote.


Lakini kuna baadhi ya wenzetu, wengi tu, bado wapo katika kile tunachoweza kukiita mkao wa kikampeni (campaign mode) au kwa tafsiri isiyo rasmi). Kuna makundi makuu mawili: wanasiasa na wafuasi wa kambi kuu mbili katika uchaguzi huo, yaani CCM na Ukawa. Katika kundi la kwanza, kuna wanasiasa ambao kwa kiasi kikubwa wanaonekana kutamani kampeni za uchaguzi ziendelee. Hawa wanajitambulisha kwa lugha na matendo yao ambayo yameelemea kwenye kuzidisha uhasama wa kisiasa kuliko mwafaka wa kitaifa.


Na kama kuna sehemu nzuri ya kubaini hilo ni huko bungeni ambapo masuala mbalimbali ya maslahi ya taifa yanaonekana ya kipuuzi kwa sababu tu ya uhasama huo wa kisiasa. Wabunge wa CCM wenye nia ya kufanya kazi na wenzao wa Ukawa kwa ajili ya taifa letu wanakwazwa na hofu ya kuonekana wasaliti kwa chama chao. Na huenda hali ni hiyo kwa wale wa upinzani.


Kundi la pili ni la wafuasi wa kambi hizo, yaani CCM na Ukawa. Wakati upinzani baina yao unaokera, na kwa hakika unakwaza mijadala muhimu kuliko mustakabali wa taifa letu, kinachoudhi zaidi ni kasumba inayojitokeza ndani ya makundi hayo, ambapo wana-CCM wanaodhani kuna haja ya kukikosoa chama chao au Magufuli wanaonekana ni ‘mbwa mwitu kwenye ngozi ya kondoo,’ wasaliti. Hali ni hivyo hivyo kwa wana-Ukawa. Ukimkosoa Lowassa basi wewe ni kibaraka wa CCM.


Majuzi, nilikumbana na mkasa baada ya kukosoa uamuzi wa serikali kuwafukuza wanafunzi wa stashahada maalumu ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Mtu mmoja ‘alinivaa’ na kunilaumu kuwa ninashindwa kutumia uandishi wangu kumtetea Rais Magufuli. Ni baada ya kumwonyesha makala mbalimbali nilizoandika huko nyuma ‘kumnadi’ Magufuli na ‘kumtetea’ baada ya kuwa rais, sambamba na kitabu nilichoandika kuhusu urais wake, ndipo akadiriki kunitaka radhi. Huyu ni mmoja kati ya wengi wasiotaka kusikia lolote zaidi ya pongezi kwa vyama au viongozi wao.


Nimeanza makala hii kwa kuelezea suala hilo kwa sababu sio tu linakwaza mijadala muhimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu taifa letu lakini pia linaweza kuathiri dhamira nzuri ya Rais Magufuli kulitumikia taifa letu. Yeye mwenyewe alituomba tumsaidie katika uongozi wake na moja ya njia za kumsaidia mtu ni kumkosoa pale anapokosea.


Na bila kuuma maneno, na licha ya mimi binafsi kuwa ‘shabiki wa Magufuli,’ jinsi alivyoshughulikia suala la wanafunzi waliofukuzwa UDOM sio sawia. 

Kwanza, kilicholalamikiwa na wengi kuhusu hatua ya serikali kuwafukuza wanafunzi hao sio kwamba walistahili kuendelea na kozi hiyo au la bali namna walivyofukuzwa bila chembe ya ubinadamu. Na angalau basi wangekuwa wamefanya kosa fulani. Hawakuwa na kosa lolote kwa sababu hawakujidahili wenyewe wala kujiundia kozi hiyo au kujiunga wenyewe bila kuitwa chuoni.

Baadhi ya wanafunzi hao waliojitoa mhanga, wakaacha kwenda kidato cha tano huku alama walizopata zikiwaruhusu kuchaguliwa na kujiunga na kozi hiyo. Hawa sio ‘vilaza’ hata kidogo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mbunge kutoka Chama cha ACT, Zitto Kabwe, ni wanafunzi 88 tu ambao sifa zao zina mushkeli kuendelea na kozi hiyo. Hivi kulikuwa na ugumu gani wa kuchuja waliostahili kuendelea na kawaondoa hao wenye upungufu wa sifa stahili? Kilichokosekana ni busara tu.


Kwa heshima na taadhima, ninaomba pia kutoafikiana na kauli ya Rais Magufuli kuhusu vilaza. Hivi kweli tumesahau jinsi mpango kama huo wa stashahada maalumu ya ualimu, enzi hizo ukiitwa UPE (Universal Primary Education), ambao licha ya matatizo kama hayo ya stashahada ya Chuo Kikuu cha Dodoma, ulivyoweza kuiweka Tanzania yetu katika ramani ya kimataifa kwa mafanikio makubwa ya kielimu?


Sawa, kulikuwa na kasoro katika mpango huo wa stashahada maalumu ya ualimu, lakini mtoto hazaliwi akitambaa, kwa maana ya kwamba kila mwanzo ni mgumu. Kwa hiyo, kwa kutumia uzoefu wa UPE – kwa mfano vitu gani vilisababisha ‘kifo’ chake – tungeweza kabisa kuboresha stashahada hiyo maalumu ili itusaidie kukabili uhaba mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi, ambapo kwa mujibu wa takwimu za Zitto, ni walimu zaidi ya 20,000.


Kauli za Rais Magufuli zinakinzana na waziri wake Profesa Joyce Ndalichako. Lakini hilo sio muhimu kwa sasa. Wenye uelewa tunafahamu kwamba kuna makosa yamefanyika. Na badala ya kuendelea kunyoosheana vidole, ni vema serikali ikafanya utaratibu wa haraka wa kurekebisha kasoro hiyo. Sitarajii wanafunzi hao kuombwa msamaha wala kusikia hotuba ya kiongozi kukiri kwamba ushughulikiaji wa suala hilo haukuwa sahihi. La muhimu sio kuombana msamaha bali kurekebisha kosa husika.


Nimalizie makala hii kwa kuwasihi Watanzania wenzangu kwamba tuna mengi ya kunufaika kwa kuwa wamoja kuliko kuruhusu tofauti za kiitikadi au upinzani wa kisiasa au kimtazamo kututenganisha. Ifike mahala tuweke kando siasa kwenye masuala yanayohitaji busara au utaalamu.


Pamoja na kasoro kadhaa zilizojitokeza katika Awamu ya Nne, wazo hili la stashahada maalumu ya ualimu lilipaswa kuwa moja ya alama muhimu kiuongozi (legacies) za Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Nia yake ilikuwa nzuri, na kwa vile miongoni mwa walioridhia sera hiyo ni pamoja na Rais Magufuli (wakati huo akiwa mbunge na waziri), basi hakuna haja ya ‘kuwatesa’ vijana hao wazalendo ambao kufanikiwa kwao katika kozi hiyo kungesaidia kupunguza uhaba wa walimu ya masomo ya sayansi. 

Nihitimishe kwa msemo kwamba, kukosea ni ubinadamu lakini kujirekebisha ni utukufu (To err is human but to correct is greatness)



2 Jun 2016

NINAANDIKA makala hii nikiwa na uchungu mkubwa. Uchungu huo unatokana na habari niliyoiona mtandaoni lakini sikuitilia maanani mwanzoni hadi nilipoisoma muda mfupi kabla ya kuandika makala hii.

Habari hiyo ni kuhusu uamuzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuwarudisha nyumbani wanafunzi 7,000. Hilo la kuwarudisha nyumbani tu sio jambo dogo lakini kibaya zaidi ni namna ya utekelezaji wa uamuzi huo.


Katika mazingira ya kawaida, na nikiamini kuwa wanafunzi hao wanatoka sehemu mbalimbali za nchi yetu, kuwaamuru waondoke chuoni hapo mara moja pasipo maandalizi ya kutosha sio tu ni kukosa ubinadamu bali pia kunahatarisha usalama wao.

Kwa mujibu wa maelezo kidogo yaliyopatikana hadi sasa, uamuzi huo wa kuwatimua wanafunzi hao umetokana na kinachoelezwa kuwa ni matatizo ya ufundishaji wa stashahada ya kozi maalumu ya ualimu wa sayansi.


Sitaki kabisa kuamini kuwa matatizo hayo yalijitokeza ghafla kiasi cha kusababisha uongozi wa chuo hicho kuchukua uamuzi huo wa ghafla. Haiwezekani kwamba uongozi wa chuo ulilala na kuamka na kukutana na matatizo hayo. Lazima uongozi huo ulikuwa ukifahamu kuhusu suala hilo muda mrefu na ulipaswa kutafuta njia mwafaka za utatuzi.

Waingereza wana usemi kwamba, “mipango mibovu huleta matokeo mabovu.” Kozi husika haikujitengeneza yenyewe, iliandaliwa na kuangaliwa ufanisi wake ungepatikanaje. Mambo kama hayo huchukua miezi kama sio miaka. Sasa iweje ghafla uongozi wa chuo ukurupuke na kueleza kuwa kuna matatizo?


Kwa mujibu wa gazeti moja la kila siku la huko nyumbani, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula alipotakiwa kufafanua kuhusu suala hilo alikiri uwepo wa tatizo hilo na kuelekeza kuwa atafutwe afisa uhusiano wa chuo hicho kwa maelezo zaidi.

Kwa upande wake, afisa huyo, Beatrice Baltazar, alieleza kwamba kusimamishwa kwa wanafunzi hao kulitokana na agizo la serikali na chuo hicho kimetakiwa kulitekeleza.


Ninapata shida kuamini kuwa serikali hii inayotumia kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” inaweza kufanya uamuzi wa kukurupuka kiasi hiki bila kujali mustakabali wa wanafunzi hao.


Taarifa za magazeti mbalimbali zinaonyesha kuwa wanachuo waliofukuzwa wamejikuta katika wakati mgumu, huku ikidaiwa kuwa baadhi ya wanachuo wa kike wameamua kujihusisha na ukahaba ili kujikimu. Ni rahisi kulaumu pindi msichana au mwanamke anapoamua kuutumia mwili wake kukidhi mahitaji yake ya fedha lakini moja ya sababu zinazoweza kumshawishi mtu kujiingiza kwenye vitendo visivyofaa kama ukahaba ni pamoja na kusaka ufumbuzi wa matatizo yanayomkabili.

Katika mazingira ya kawaida tu, mwanafunzi wa kike anapojikuta hana pa kulala wala kula, na ikizingatiwa kuwa mafisadi wa ngono wametapaa kila kona, kilichotokea huko Dodoma kinawaweka wanachuo wa kike katika mtihani mgumu ambao unaweza kuwa na athari za muda mrefu kisaikolojia.


Cha kusikitisha zaidi ni kwamba tukio hilo lisilopendeza limetokea wakati Bunge likiendelea na vikao vyake huko Dodoma. Kila mwanachuo aliyetimuliwa ana mwakilishi hapo bungeni, kwa maana ya mbunge wa jimbo lake. Na katika mazingira ya kawaida, wabunge walipaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa njia mwafaka zinatumika kutatua suala hilo sambamba na kuwapatia misaada wanachuo hao.


Lakini kama ilivyo kwenye kero nyingine majimboni, wabunge wengi wamekuwa na ufanisi mdogo katika kuelezea shida zinazowakabili wana-jimbo wao. Yayumkinika kuhisi kuwa laiti kila mbunge ambaye mwana-jimbo wake ni mwathirika wa uamuzi huo usio na busara na usio wa kibinadamu angeamua kupigana ‘kufa na kupona’ basi huenda serikali kupitia uongozi wa chuo hicho ungebadili uamuzi huo.


Tukio hili ni mwendelezo tu wa mazingira magumu yanayowaandama wasomi wa kesho. Kwa kiasi kikubwa, upatikanaji wa elimu nchini umekuwa kama adhabu, kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu.


Japo tunatambua kuwa uwezo wa serikali yetu ni mdogo kumudu gharama za elimu, na pia ikizingatiwa kuwa kuna vipaumbele vingine lukuki vinavyoikabili serikali yetu, lakini wakati mwingine kinachohitajika sio fedha bali busara tu.


Katika suala hili ninalozungumzia, ni dhahiri kuwa laiti uwepo wa matatizo husika ungebainika mapema na kutafutiwa ufumbuzi kwa njia stahili, basi tusingejikuta tuna kundi la maelfu ya wanafunzi wanaohangaika kurudi majumbani huku hawajui hatma yao kielimu na kimaisha ikoje.


Kuna wanaodhani kuwa jeuri za maofisini au katika sehemu za huduma huchangiwa na mazingira magumu ya elimu huko nchini. Kwamba, mtu baada ya kuhitimu masomo au kozi yake, na kuteseka vya kutosha, anakuwa na ‘hasira’ kiasi kwamba fursa ya kuitumia elimu yake kazini yaweza kuambatana na ‘kisasi’ kwa yeyote aliye mbele ya uso wake. Haipaswi kuwa hivyo lakini tutarajie nini kwa watu waliopata elimu kana kwamba wapo jela?


Sitarajii makala hii kubadili chochote kwa sababu tayari uamuzi umekwishafanyika na hatua zisizo za kiungwana zimekwishachukuliwa, yaani kuwafukuza wanachuo husika. Hakuna uwezekano wa fulani kusoma makala hii na kubadili uamuzi huo. Hata hivyo, bado kuna fursa ya busara kutumika kulitatua suala hilo.


Ni muhimu kwa serikali na uongozi wa chuo hicho kuandaa utaratibu wa kuwasiliana na wanafunzi hao kuwafahamisha kuhusu hatma yao. Na kama ambavyo mwajiri anavyolazimika kumfidia mwajiriwa anayesimamishwa kazi ilhali hajafanya kosa lolote, utaratibu mahsusi uandaliwe kufidia gharama walizoingia wanachuo hao kutokana na uamuzi huo wa ghafla.


Nimalizie makala hii kwa kuiomba Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kuanza jitihada za makusudi za kuyatengeneza mazingira ya elimu kuwa rafiki, yenye kumvutia mwanafunzi au mwanachuo kujiona ananufaika kwa ajili yake na taifa na sio kama amefanya kosa kujiunga au kuwepo kwenye taasisi ya elimu. Elimu sio ukombozi kwa mtu binafsi tu bali taifa kwa ujumla. Kama tunaandaa wasomi wa kulitumikia taifa letu kwa ufanisi na uzalendo basi maandalizi hayo yaambatane na kuwajengea mazingira mwafaka.



22 Dec 2010



Picha kwa Hisani ya Mjengwa

Japo haipendezi kuona jeshi la polisi likitumia nguvu kubwa kuzuwia haki ya kikatiba ya wananchi kuandamana au kugoma kwa amani,lakini nashawishika kutowaonea huruma wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kufuatia kichapo walichopewa na askari wa FFU.Hivi sio hawa wana UDOM waliochangisha fedha kwa ajili ya kampeni za Jakaya Kikwete?Na sio hawa waliotoa tamko la kukemea haki ya kikatiba ya wabunge wa Chadema kususisa hotuba ya Kikwete huko Bungeni?

Najua si vyema kutoa lawama za jumla kwani si kila mwana-UDOM aliafiki wazo la kujikomba kwa Kikwete lililopelekea wanafunzi hao kuchangia fedha zao za ngama ili kumwezesha mwanasiasa huyo aliyekuwa mgombea wa CCM arejee madarakani.

Na kama tulivyoandika baadhi yetu wakati wa kampeni za uchaguzi wakati tunaonya madhara ya kuirejesha CCM madarakani,haijachukua muda kwa  Kikwete na serikali yake kuwalipa fadhila wasomi hao wa Dodoma.

Majuzi nilimsuta mwanahabari mkongwe Dunstan Tido Mhando baada ya kupata taarifa kuwa serikali imemtosa ubosi wa TBC.Nilimsuta kwa vile naamini wakati Tido anaombwa na WALIOMUOMBA kuja kuendesha TBC alikuwa anafahamu fika kuwa aidha anapanda mchicha au bangi,na mavuno yangekuwa mchicha au bangi,respectively.Ukikubali kutumiwa lazima ukubali kitachotekea itapojiri "expiry date" yako.

Sasa tunashuhudia kundi jingine la walioingizwa mkenge.Hawa wasomi watarajiwa wa UDOM walijikomba kwa Kikwete na CCM na kuchangia kampeni zake,sijui wakitarajia kuwa pindi mwanasiasa huyo akirejea Ikulu angewapatia muujiza gani sijui!

MLIPANDA BANGI SASA MNATARAJIA KUVUNA MPUNGA?

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.