16 Aug 2016


NDOTO yangu ya muda mrefu utotoni ilikuwa utabibu. Moja ya sababu zilizonipa ndoto hiyo ni uuguzi (unesi) wa dada yangu, ambao ulinifanya nimtembelee kazini kwake (hospitalini) mara kwa mara. Kila nilipomtembelea, nilishuhudia wagonjwa mbalimbali wakiwa wamekabidhi afya na uhai wao mikononi mwa madaktari na manesi. Nikanuwia kuwa nitakapomaliza elimu ya msingi na kufanikiwa kuingia sekondari, nitasoma masomo ya sayansi ili baadaye niwe daktari.
Kwa bahati nzuri nilifaulu darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga sekondari ya kutwa ya Kilombero, Ifakara. Mimi na wanafunzi wenzangu tuliofaulu mwaka huo ndio tulikuwa wanafunzi waanzilishi wa shule hiyo maarufu kwa jina la Kilombero Day.
Kujiunga na shule hiyo kuliisogeza karibu ndoto yangu ya udaktari, sio tu kwa vile nilipata fursa ya kusoma masomo ambayo yangeweza kunisaidia kusomea udaktari lakini pia shule hiyo ilikuwa jirani tu na chuo cha waganga wasaidizi (MATC), kilichokuwa katika hospitali ya Mtakatifu Francis.
Hata hivyo, nilikabiliwa na vikwazo viwili. Kwanza, shule hiyo mpya ilikuwa na uhaba mkubwa wa nyenzo mbalimbali za kitaaluma, vitabu vya kiada na maabara. Kikwazo cha pili kilikuwa katika uwezo wangu binafsi. Somo la hisabati lilikuwa ‘mgogoro’ tangu siku ya kwanza, na somo la Fizikia likatokea kuwa gumu kuliko yote. Wakati huo, nilishafahamu kuwa mkondo wa udaktari ni Fizikia, Kemia na Baiolojia (PCB) na Hisabati kidogo.
Kufupisha simulizi, nilipohitimu kidato cha nne nilipata Daraja la Kwanza huku nikiwa na alama A ya Kemia, C ya Baiolojia na F ya Fizikia. Ukichanganya na D ya Hisabati, mkondo wa PCB uligoma.
Nilipochaguliwa kidato cha tano, nikataka kuikwepa Fizikia kwa kusoma Kemia, Baiolojia na Jiografia (CBG), ambayo ingeweza kunifikisha katika azma yangu ya kusomea udaktari. Nikakumbana na kikwazo cha kuchukua tena Hisabati (Basic Mathematics) kama somo la ziada na kumbe Kemia ya Kidato cha Tano na Sita haikuwa nyepesi kama ile niliyopata alama A kidato cha nne. Kipengele cha Physical Chemistry kilikuwa ni kama Fizikia zaidi kuliko Kemia na hisabati juu. Nikaamua kuzika ndoto yangu ya udaktari, nikachukua mkondo wa Historia, Jiografia na Kiingereza (HGL) na somo la ziada la Siasa.
Lengo la simulizi hiyo sio kuelezea safari yangu ya kitaaluma au ndoto yangu hiyo ya udaktari iliyokufa kifo cha asili bali kama kielelezo mwafaka cha kukosoa uamuzi wa serikali kulazimisha masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne.
Sitaki kujigamba kuhusu kiwango changu cha elimu, lakini ukweli ni kwamba licha ya kufanikiwa kuhitimu shahada tatu nikisaka ya nne kila ninapokutana na hata mhitimu wa kidato cha sita tu wa mkondo uliohusisha Fizikia na Hisabati (kwa mfano PCB au PGM), ninampa heshima zote. Sababu nyepesi ni kwamba ameweza kile kilichonishinda.
Na hadi muda huu, nikiwaona wanafunzi wa shahada ya kwanza katika masomo ya sayansi kama vile uhandisi, ninawaheshimu mno. Kwa kifupi tu, masomo ya sayansi yanahitaji mtu mwenye akili zaidi. Japo haimaanishi tunaosoma kozi zisizo za sayansi ni ‘patupu kichwani,’ ukweli ni kwamba angalau kozi zetu zina ahueni fulani.
Sasa serikali inapokurupuka na uamuzi wa kulazimisha masomo ya sayansi kwa wanafunzi wote, kinyume cha utaratibu uliopo ambapo wanafunzi wa sekondari wanaingia kidato cha tatu wanapewa uhuru wa kuchagua mkondo wanaotaka (hasa kwa kuzingatia ndoto zao kitaaluma na uwezo wao kimasomo).
Huu ni udikteta wa kitaaluma, kumlazimisha mwanafunzi kusoma kitu asichotaka. Na hapa suala sio kutaka tu bali pia kuna suala la uwezo wa kumudu masomo ya sayansi. Na kingine ni kuwabebesha wanafunzi mzigo wasiostahili.
Sababu iliyotolewa na serikali kupitia Waziri wa Elimu, Teknolojia, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kuwa hivi sasa Tanzania imedhamiria kuingia kwenye uchumi wa kati ambao ni wa viwanda, na hivyo suala la sayansi haliwezi kuepukwa (kwa sababu ni wakati sasa wa kuwa na wataalamu wengi wa fani za sayansi watakaoweza kutosheleza mahitaji ya sekta ya viwanda nchini) haina mashiko.
Nihitimishe makala hii kwa kumshauri waziri huyo msomi kurejea mada kama ‘reactance’ na ‘boomerang effect’ kwenye saikolojia na kuzihusisha na uamuzi huo wa serikali na athari zake.
Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube