30 Sept 2016

TANZANIA ina matatizo kadhaa, lakini tatizo ambalo sikuwahi kulitambua awali ni hili linalozidi kupanuka la chuki ya baadhi ya Watanzania wenzetu dhidi ya nchi yetu.
Naam, hakuna neno stahili zaidi ya chuki, pale unapokutana na Mtanzania anafurahi kusikia kuwa majirani zetu wa Malawi wameanza chokochoko kuhusu mpaka kati yetu na nchi hiyo.
Au unakutana na mtu anayefurahia taarifa za kuyumba kwa uchumi wetu, anakenua meno yote 32 huku akidai eti “si mliichagua CCM, mnaisoma namba sasa.”
Lakini kama kuna kitu kimenikera zaidi ni hizi kebehi za watu hao dhidi ya jitihada zilizofanywa na Serikali ya Rais Dk John Magufuli kununua ndege mbili kama mkakati wa kulifufua shirika letu la ndege.
Wenye chuki hao wanaendelea kukosoa kila kitu kuhusu ndege hizo, kuanzia yule twiga kwenye nembo (baadhi wanadai eti huyo twiga anaonekana kama ameteguka miguu), rangi ya ndege na kila kitu kuhusu ndege hizo.
Wanataka serikali ingenunua ndege kubwa zaidi, wengine wanataja kabisa aina ya ndege waliyotaka, wengi wao wakitamani ndege kubwa zinazotengenezwa na kampuni za Boeing au Airbus.
Ni watu hawa hawa ambao laiti serikali ingetumia fedha nyingi zaidi kununua ndege kubwa zaidi wangeishia kuilaumu kuwwa ndege sio muhimu zaidi ya mahitaji mengine mbalimbali muhimu kwa taifa letu.
Jitihada za kuwaelimisha kuwa ndege hizo mbili za aina ya Bombardier zina ufanisi zaidi kwa maana ya bei yake na gharama za uendeshaji zinagonga ukuta kwa sababu watu hawa hawataki kusikia habari yoyote njema kuhusu Tanzania.
Wataalamu wa usafiri wa anga wanaeleza kuwa ndege hizo zilizonunuliwa na serikali zinatumia mafuta kidogo zaidi kulinganisha na ndege nyingine, lakini wenye chuki hao hawataki kabisa kusikia maelezo hayo ya kitaalamu.
Na kwa kuonyesha kuwa watu hawa wana chuki kali dhidi ya nchi yao, hawataki kabisa kuzungumzia habari nyingine njema ya ujio wa mabehewa kwa ajili ya kuboresha huduma za usafiri wa Reli ya Kati.
Hawazungumzii sio kwa sababu hawafahamu kuhusu habari hiyo njema bali wameishiwa na hoja za kuwawezesha kukosoa kuhusu mabehewa hayo.
Sote tunatambua kuwa kwa miaka kadhaa nchi yetu ilikuwa ‘shamba la bibi’ kwa genge la mafisadi. Kuibadili hali hiyo sio kitu cha siku moja. Na Rais Magufuli ameshatukumbusha mara kadhaa kwamba itachukua muda kabla mambo hayajanyooka, akatuomba tumsaidie.
Lakini tatizo la wenzetu hao na chuki yao sio ununuzi wa ndege hizo, zingekuwa kubwa wangelalamika na sasa sio kubwa sana wanalalamika. Tatizo la wenzetu hao ni chuki dhidi ya nchi yetu. Wanatamani sana kuiona nchi ikiwa kwenye wakati mgumu ili wapate fursa ya kutuambia “mnaisoma namba.”
Kibaya zaidi kuhusu wenzetu hawa ni kwamba sasa wamefika mahala kuwa hoja za kuikosoa serikali pale inapostahili ni haki yao pekee. Nilishuhudia hali hiyo ya kuchukiza mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo niliweka bandiko kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook nikieleza upungufu ya Muswada wa Huduma za Habari (Media Services Bill) ambao licha ya kupingwa na wadau wengi, upo katika mchakato wa kuwa sheria kamili.
Badala ya kujadili mada husika, wenye hatimiliki ya kuikosoa serikali ‘wakanikalia kooni’ wakinituhumu kuwa nilimpigia kampeni Dk. Magufuli na sasa baada ya kukosa nilichotarajia ndio najifanya kumkosoa. Kimsingi wala sikumkosoa rais bali serikali kwa ujumla hasa ikizingatiwa kuwa mchakato wa muswada huo ulianza wakati wa Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.
Na kabla ya hapo, nilitoa pongezi zangu za dhati kwa aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, kutokana na ziara yake mkoani Kagera kuhusu janga la tetemeko la ardhi. Lakini watu wenye hatimiliki ya kumpongeza Lowassa wakanijia juu wakidai kuwa ni unafiki kumpongeza sasa wakati sikumuunga mkono kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Wengi wao wanaishi kama tupo katika kipindi cha kampeni za uchaguzi huo. Kwao ni kama rais halali hajapatikana. Pengine kwa vile walijiaminisha mno kuhusu mgombea wao, basi hawataki kabisa kukubali ukweli ambao upo kinyume cha matarajio yao.
Nihitimishe makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa hatuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania na ni wazi tusipoipenda wenyewe, tusitarajie wasio Watanzania kuipenda. Mafanikio ya nchi yetu ni yetu sote na kukwama kwake kunatuathiri sote. Tuweke mbele maslahi ya nchi yetu badala ya maslahi binafsi au ya kiitikadi.
Mungu ibariki Tanzania

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube