7 Oct 2016


NIMEKUWA mfuatiliaji mkubwa wa habari na eneo moja ninalolipa umuhimu mkubwa ni habari za teknolojia.
Ufuatiliaji huo wa habari za teknolojia umenifanya niwe na wasiwasi, kwa upande mmoja na matumaini kwa upande mwingine. Wasiwasi wangu mkubwa ni hatma ya Bara la Afrika ambalo kwa kiasi kikubwa linaichukulia teknolojia kama anasa ilhali wenzetu hususan nchi zilizoendelea wanachukulia teknolojia kama sehemu ya mahitaji muhimu kwa binadamu kama ilivyo chakula, makazi na mavazi.
Matumaini yangu katika teknolojia yanatokana na ukweli kwamba licha ya kutelekezwa kwa kiwango kikubwa, matumizi japo kidogo ya teknolojia katika sehemu mbalimbali za dunia inayoendelea, kwa mfano huko nyumbani Tanzania, yanaleta mabadiliko makubwa. Angalia jinsi mfumo wa kusafirisha fedha wa m-pesa unavyofanya kazi, ‘apps’ kama Whatsapp zinavyowezesha watu mbalimbali kuepuka gharama kubwa za simu na ujumbe wa maneno, barua-pepe zinavyotuwezesha kuwasiliana papo kwa papo bila kwenda posta kutuma au kupokea barua na maendeleo mengine mbalimbali.
Nimebahatika kushuhudia zama kabla ya ujio wa intaneti na mitandao ya kijamii, televisheni, simu za mkononi na takriban kila aina ya teknolojia ya kisasa inayoifanya dunia kuwa kama kijiji. Kadhalika, nilikuwa miongoni mwa Watanzania wa awali kukumbatia teknolojia mpya (nilikuwa miongoni mwa Watanzania wa kwanza kabisa kufungua blogu Aprili 2006).
Jumamosi iliyopita niliweza kuangalia mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga, kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook. Hii ilinikumbusha miaka kadhaa huko nyuma ambapo tegemeo pekee la kusikia matangazo ya mpira lilikuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo wakati mwingine iliwalazimu wasikilizaji kupanda juu ya miti ili kudaka vema mawimbi ya radio.
Lakini pengine lililo kubwa zaidi kuhusu teknolojia ni jinsi uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulivyoandika historia ya kuwa wa kwanza kabisa ‘kujenga ndoa’ kati ya teknolojia na siasa. Tulishuhudia jinsi mitandao ya kijamii, hususan Facebook na Twitter, ‘apps’ kama Whatsapp na Instagram, na majukwaa ya uchapishaji kama vile blogu na ‘webforums’ (kama Jamii Forums) zilivyotumika kwa ufanisi mkubwa katika kampeni za urais, ubunge na udiwani.
Na kwa hakika, ushindi wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais wa sasa Dk. John Magufuli, ulichangiwa na kampeni zilizofanyika kwenye mitandao ya kijamii, apps na webforums. Kama kuna Rais wa Tanzania anayepaswa kuthamini mno mchango wa teknolojia kwenye siasa basi ni Magufuli.
Hata hivyo, katika mazingira ya kushangaza kabisa, Dk. Magufuli alisikika akieleza kuwa anatamani malaika washuke na kusimamisha mitandao ya kijamii kwa mwaka moja na itaporudi hewani (baada ya mwaka huo mmoja) ishuhudie maendeleo yaliyofikiwa.
Watetezi wa rais wanadai kuwa kauli hiyo ni ya utani tu, lakini nikiwa miongoni mwa watu walioshiriki kikamilifu kumpigia kampeni Magufuli nikiwa maili kadhaa kutoka huko nyumbani lakini nikawezeshwa kufanya hivyo kwa kutumia maendeleo ya teknolojia kama vile matumizi ya mitandao ya kijamii na blogu, nilisikitishwa na kauli hiyo ya Magufuli.
Ni kweli kwamba baadhi ya wenzetu wamekuwa wakiyatumia vibaya maendeleo ya teknolojia, kwa kujenga chuki miongoni mwa Watanzania, upinzani dhidi ya kila kitu hata chenye manufaa kwa taifa, kugeuza mitandao ya kijamii kuwa uwanja wa matusi, na kadhalika.
Hata hivyo, wanaotumia vibaya teknolojia ni wachache kulinganisha na sisi tunaoitumia kwa nia nzuri. Hivi kama kosa la wachache linafanya wote kuwa wabaya, je itakuwa sahihi kudai kuwa malaika washuke na kuifunga serikali kwa muda fulani kwa vile ilikuwa na watumishi hewa zaidi ya 10,000 na watumishi kadhaa wasio hewa lakini ni majipu?
Na hata kama kuna haja ya kuifunga mitandao hiyo, Dk. Magufuli hahitaji malaika bali sheria dhidi ya makosa ya mitandao ya kijamii (Cyber Crime Act 2015) iliyokwishawatia hatiani watu 10 kwa tuhuma za “kumtukana rais kwenye Facebook au Whatsapp?”
Wito wangu kwa Rais Magufuli ni kwamba awe mstahimilivu. Kazi anayofanya ni nzuri na inawapendeza Watanzania wengi. Sasa kuna haja gani asumbuliwe na hizo kelele za hapa na pale ilhali anayofanya ni makubwa zaidi ya kelele hizo?
Kadhalika, kwa vile tu rais wetu hapendezwi na kitu fulani haimaanishi kitu hicho sio halali kikatiba. Kama ambavyo wengi wetu tunatumia uhuru na haki yetu kikatiba kumpongeza Magufuli, katiba yetu inatoa haki na uhuru pia kwa wenzetu kumkosoa rais wetu alimradi wasitumie lugha isiyokubalika kisheria.

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.