7 Dec 2016

ANGALIZO: Makala hii ilipaswa kuchapishwa katika toleo la wiki iliyopita la gazeti la Raia Mwema lakini haikuchapishwa kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Rais Dokta John Magufuli alitimiza mwaka kamili tangu aapishwe kuwa Rais wa tano wa nchi yetu. Nyingi ya tathmini mbalimbali zilizofanyika kuhusu mwaka wake mmoja wa urais zilionyesha anafanya kazi nzuri.

Hata hivyo, tukifuatilia kwa karibu utendaji kazi wa Rais, twaweza kubaini kuwa baadhi ya mawaziri wake hawaendani na kasi yake. Katika mazingira ya kawaida, Rais angelazimika kuchukua hatua pale tu hatua stahili zisingewezekana kufanywa na mawaziri wake.

Japo wanachohitaji wananchi ni kuona serikali inachukua hatua stahili, lakini suala la mtendaji gani wa serikali anayechukua hatua husika linaweza kueleza kiwango cha ushirikiano na uchapakazi kwa pamoja.

Na kwa ‘kusubiri hadi Rais achukue hatua’ kuna uwezekano wa kujengeka taswira kuwa ‘Rais anaingilia kazi za watendaji wake,’ au mbaya zaidi ni pale maagizo yake yatapokutana na upinzani wa namna flani.

Mfano mzuri ni hatua ya majuzi ambapo Rais aliitumbua Bodi ya Mamlaka ya Mapato (TRA).  Baadaye alieleza kuwa Bodi hiyo iliyokuwa na watendaji hao wakuu wa idara na taasisi za Serikali ilifanya dhambi ya kuidhinisha uamuzi wa menejimenti kuweka mabilioni ya shilingi katika benki za binafsi.

Juzi hapa tumekuta Sh26 bilioni zilizokuwa zimetolewa TRA kwa ajili ya matumizi ya TRA zikapelekwa kwenye mabenki matatu kama ‘fixed deposit account’ na bodi ikapitisha. Ndiyo maana nilipozipata hizo hela; hela nikazichukua na bodi kwaheri,” Rais alikaririwa

Swali hadi hapo ni je Waziri husika na wasaidizi wake walikuwa wapi wakati hayo yanatokea? Je inawezekana maamuzi hayo ya menejimenti na Bodi ya TRA yalikuwa na baraka za Waziri husika, na ndio maana hakuna hatua zilizochukuliwa hadi Rais alipoingilia kati?

Miongoni mwa wajumbe wa Bodi iliyotumbuliwa ni Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, ambaye wiki iliyopita alinukuliwa akitoa kauli inayokinzana na msimamo wa Rais. Gavana Ndulu alidai kuwa TRA kuweka fedha kwenye fixed accounts sio kosa kisheria, na hakuna hasara kiuchumi kuweka fedha kwenye akaunti ya aina hiyo.

Kwa tunaojua ‘kusoma katikati ya mistari’ Tunaelewa bayana kuwa Gavana Ndulu alikuwa anamjibu Rais Magufuli. Na pengine sio kumjibu tu bali kumkosoa. Na hii si mara ya kwanza kwa ‘kiongozi huyo wa benki kuu kupishana lugha na Rais.’ Mwezi Machi mwaka huu Dkt Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza huko Benki Kuu, ambapo pamoja na mambo mengine, alitoa agizo kwa Gavana Ndulu kupitia upya orodha ya wafanyakazi wa Benki hiyo, na kuwaondoa mara moja wale wote ambao hawana ulazima wa kuwa wafanyakazi katika benki hiyo.

Siku chache baadaye, Gavana huyo alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa orodha yenye majina 14 ya ‘watoto wa vigogo’ iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ‘haina jipya.’ Hata hivyo alieleza kuwa agizo la Rais kuhusu kupunguza wafanyakazi lingejadiliwa kwenye vikao vya taasisi hiyo na taarifa rasmi ingetolewa. Kwa kumbukumbu zangu, hadi leo hakujatolewa taarifa yoyote.

Wakati akieleza kuhusu sababu zilizopelekea kuvunja Bodi ya TRA, Rais pia aliionya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwamba imepewa zaidi ya shilingi bilioni 30 na “badala ya kuzipeleka kwenye miradi ya elimu kama kujengea madarasa na kusaidia masuala mengine ya elimu nchini lakini wameamua kuweka kwenye fixed account wakati kuna miradi ya elimu imesimama kwa kukosa pesa.

Na hapa tena tunapaswa kujiuliza, Waziri husika (na wasaidizi wake) yupo wapi? Au hapa pia, uamuzi huo wa Mamlaka hiyo una baraka za Waziri husika ndio maana haikuchukua hatua hadi Rais alipoingilia kati?

Tukiweka kando hilo la ‘kila jambo kusubiri hadi Rais achukue hatua,’ maamuzi ya baadhi ya mawaziri yanaweza ‘kumgombanisha’ kiongozi huyo mkuu wa nchi na sie wananchi anaotuongoza. 

Wiki mbili  zilizopita, Waziri wa Sheria na Katiba, Dokta Harrison Mwakyembe, ‘alilipuka’ kwa kutangaza kuwa serikali ina mpango wa kuwatimua kazi mahakimu wote wa mahakama ya mwanzo wenye elimu ya cheti na diploma. Waziri huyo ambaye ni mwanasheria kitaaluma, alisema, “Tunahitaji mahakimu wenye uwezo wa sheria ambao wamehitimu shahada ya kwanza, hivyo serikali itawafuta kazi mahakimu wote wenye elimu ya cheti na diploma.”

Tungetegemea kuwa kiongozi msomi kama Dkt Mwakyembe angetambua bayana athari za tamko hilo kwa ari na tija wa mahakimu wa mahakama za mwanzo, wengi wao wakiwa wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi. Tamko hilo la Mwakyembe linaweza kupelekea mahakimu kuamua “serikali inataka kumwaga ugali, basi nasi tutamwaga mboga.”

Lakini hata tukiweka kando athari za tamko hilo kwa ari na tija ya mahakimu wa mahakama za mwanzo, kwanini Mwakyembe na wenzake hawakuzingatia busara kwamba elimu pekee sio kigezo cha ufanisi wa mwajiriwa bali pia uzoefu ni muhimu kwenye utaalamu.

Kwahiyo, serikali yenye busara ingeandaa mazingira ya kuwahamasisha mahakimu hao kujiongezea viwango vya elimu wakiwa kazini, hususan kwa kusaka shahada ya sheria kupitia Chuo Kikuu Huria.

Tukio jingine linaloashiria kuwa baadhi ya watendaji wa Dkt Magufuli 'wanamwangusha' ni sakata kati ya serikali ya jiji la Mwanza na wamachinga. Kwa mara nyingine tena, tumeshuhudia ikilazimu Rais kuingilia kati na kumuru kuwa wamachinga waliokuwa wakibughudhiwa huko Mwanza wasisumbuliwe tena.

Hapa pia waweza kujiuliza kuhusu Waziri husika. Alikuwa usingizini kiasi cha kutofahamu kilichokuwa kinaendelea Mwanza hadi imlazimu Rais kuingilia kati? Au Waziri huyo aliridhia kuhusu unyanyaswaji wa wamachinga na ndio maana hakuchukua hatua stahili?

Kuna suala la kiwanda cha Dangote. Kauli za mawaziri husika na watendaji wengine wa serikali zimekuwa sawa na 'kujiumauma.' Sio ngumu kuhisi kuwa 'kuna namna' katika sakata hilo ambalo miongoni mwa atahri zake ni pamoja na kupotea kwa ajira za Watazania wenzetu zaidi ya 1,000.

Kwa jinsi mazingira yalivyo ambapo 'kila kitu lazima kimsubiri Rais,' yayumkinika kuhisi kuwa ufumbuzi pekee wa sakata hilo a Dangote utapatikana kwa Rais kuingilia kati. 

Wakati watendaji 'wanaomwangusha' hawawezi kuwa na kisingizio zaidi ya aidha uzembe wao au hujuma dhidi ya Rais, kwa uapnde mwingine Rais naye anaweza kubeba lawama kwa kuyavumilia majipu yanayomzunguka.


Nihitimishe makala hii kwa kutarajiwa kuwa Rais Magufuli atawakumbusha watendaji wake majukumu yao ili kuondoa taswira ya ‘kila kitu mpaka aje Rais,’ sambamba na kuwakumbusha kutumia busara hasa pale wanapotoa kauli zinazoweza kujenga chuki kati ya ‘waathirika’ wa kauli hizo na serikali


Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  
0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube