8 Dec 2016


KESHOKUTWA, Desemba 9, Tanzania itatimiza miaka 55 tangu ipate uhuru. Siku hiyo hiyo, nami nitatimiza miaka kadhaa tangu nizaliwe. Naam, mimi na nchi yangu ‘tulizaliwa tarehe inayofanana’ japo katika miaka tofauti.
Nijiongelee mwenyewe kwanza. Wakati kwa watu wengi, siku zao za kuzaliwa huandamana na sherehe na chereko mbalimbali, maadhimisho ya siku yangu ya kuzaliwa huwa ni ibada – kumshukuru Mungu kwa kuniweka hai na baraka nyingine anazonijalia – na kufanya tafakuri ya wapi nimetoka, nilipo na ninapoelekea.
Moja ya mafanikio makubwa kwangu kwa mwaka huu ni uamuzi niliouchukua Aprili Mosi kuachana na moja ya tabia hatari kabisa maishani ya uvutaji wa sigara. Hadi nilipochukua uamuzi huo, tabia hiyo hatari kiafya na kiuchumi ilikuwa na ‘umri’ wa miaka ishirini na ushee.
Katika kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa, nimeamua kugawa bure kitabu changu cha kielektroniki, kinachoitwa “Mwongozo wa Kitabibu wa Jinsi ya Kuacha Sigara na Ushauri wa Mvutaji Mstaafu.” Ni mwendelezo wa utamaduni mpya, ambapo zamani tulizoea kuona wanaosherehekea siku za kuzaliwa wakizawadiwa, lakini sasa namna maarufu ya kuadhimisha sherehe hiyo ni kutoa zawadi.

Hiyo ni kwa upande wangu. Sijui ‘mwenzangu’ Tanzania atakuwa na ‘zawadi’ gani ya kutupatia katika maadhimisho yake ya siku ya kuzaliwa. Hata hivyo, siku chache kabla ya siku hizo, kuna jambo moja ambalo linaonekana kugusa hisia za wengi. Nalo ni uteuzi wa mabalozi wapya ulifanywa na Rais Dk. John Magufuli wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa baadhi ya vyombo vya habari, uteuzi wa makada waandamizi wa chama tawala CCM umetafsiriwa kuwa ni ‘hesabu za kisiasa.’ Sina hakika hesabu hizo zina malengo gani, lakini nahisi labda ni Magufuli analenga kujiimarisha katika uongozi wake kama Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.
Kama hilo ni kweli, basi uteuzi huo wa makada sio habari njema kwetu sisi wenye matarajio ya kuona teuzi mbalimbali zikifanywa kulingana na uwezo wa kutekeleza majukumu au uchapakazi na sio ukada.
Pengine nitumie fursa hii kukumbusha kuwa kuna wimbi kubwa la mabadiliko linaloendelea duniani, hususan huku nchi za Magharibi. Muda mfupi kabla sijaanza kuandika makala hii, Austria imenusurika kuwa taifa la kwanza kurejea kuwa chini ya utawala wa mrengo mkali kabisa wa kulia. Hofu kuwa mgombea urais Norbert Hofer wa chama chenye mrengo mkali wa kulia cha Freedom Party angeshinda ilipotea baada ya mchakato wa kupiga kura kumalizika, na mgombea binafsi Alexander Van der Bellen kushinda kwa asilimia 53. Lakini muda mfupi baada ya habari hiyo njema kutoka Austria, mambo hayakwenda vizuri nchini Italia, ambapo Waziri Mkuu Matteo Renzi alishindwa kwenye kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo, na kulazimika kujiuzulu. Wapinzani wake katika kura hiyo walikuwa ni pamoja na chama chenye mrengo mkali wa kulia cha Northern League na kile cha upinzani wa tabaka tawala (anti-establishment) cha Five Star Movement (F5S).
Sasa macho yanaelekezwa huko Ufaransa na baadaye Ujerumani na Uholanzi ambako kwa nyakati tofauti watakabiliwa na kazi ya upigaji kura. Mtihani mkubwa katika nchi hizo ni jinsi ya kukabiliana na wimbi linalozidi kukua la upinzani dhidi ya tabaka tawala na mfumo wa utawala unaoonekana kutosikiliza sauti za wananchi wa kawaida. Kwa bahati mbaya, wimbi hilo lipo mikononi mwa vyama vya siasa za mrengo mkali wa kulia na vya kibaguzi.
Katika mazingira kama hayo tunahitaji mabalozi wanaoelewa kwa nini wametumwa kutuwakilisha huko nje, na sio wanaojua wameteuliwa kutokana na nafasi zao za kisiasa nchini.
Na wiki chache kabla ya maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru wetu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi Dk Mohammed Ali Shein alisaini sheria inayofanya masuala ya mafuta na gesi ya Zanzibar kuwa sio suala la Muungano, hatua ambayo ni uvunjifu wa Katiba mchana kweupe. Hilo limefanyika kwa vile Shein na SMZ wanajua hakuna mwanasiasa kutoka Bara mwenye jeuri ya kugusia suala hilo, ikiwa ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Magufuli.
Lakini pamoja na hayo, Tanzania yetu itasherehekea miaka 55 ya kuzaliwa kwake ikiwa nchi yenye amani, angalau amani kwa maana ya kutokuwa vitani au kwenye machafuko. Kazi kubwa kwa watawala wetu ni kutumia nguvu zao zote kuhakikisha kuwa amani hiyo inadumishwa kwa nguvu zote.
Happy birthday Tanzania.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube