23 Feb 2017


MOJA ya sababu zilizosababisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kifikie hatua ya kuwa chama kikuu cha upinzani ni msimamo mkali ambao chama hicho ulikuwa nao dhidi ya ufisadi.
Kadhalika, Chadema sio tu kilionyesha dalili za kuweza kuwa mbadala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali pia kiliweza kujijengea hadhi kubwa ya ‘sauti ya wasio na sauti’ (voice of the voiceless) na chenye kupigania haki za wanyonge.
Chadema hawakuuchukia ufisadi kwa maneno matupu bali kwa vitendo, ambavyo mara nyingi vilisababisha viongozi wakuu wa chama hicho kuchukuliwa hatua na Bunge au serikali/vyombo vya dola. Katika harakati za kuwapigania wanyonge, baadhi ya wafuasi wa chama hicho walipoteza maisha na wengine kuachwa na ulemavu wa kudumu.
Japo kwa kiasi kikubwa, mafanikio ya Chadema kisiasa yalichangiwa na ‘madudu’ ya chama tawala CCM takriban katika kila eneo, hiyo sio kusema kuwa chama hicho cha upinzani ‘kilidondoshewa’ mafanikio hayo.
Kupitia viongozi wake makini, chama hicho kiliwekeza vya kutosha katika upatikanaji wa taarifa sahihi, ambazo japo kila zilipotolewa zilikutana na vitisho vya “nitawaburuza mahakamani,” hakuna mmoja wa waliotoa vitisho hivyo aliyethubutu kwenda mahakamani.
Orodha ya ufisadi ulioibuliwa na Chadema ni ndefu, lakini matukio muhimu kabisa, na yatakayobaki katika historia ya taifa letu ni pamoja na skandali nzito kama ile ya Richmond, EPA, Buzwagi, Meremeta, Tangold, ‘Minara Pacha’ ya Benki Kuu na Deep Green Finance.
‘Dream team’ ya Dk. Willbrord Slaa, Zitto Kabwe na Freeman Mbowe ilikuwa ‘moto wa kuotea mbali’ kiasi kwamba ingekuwa ni ushirikiano wa ushambuliaji katika soka basi ni sawa na ‘MSN’ ya Messi, Suarez na Neymar huko Barcelona.
Ilifika mahala ambapo mstari ulichorwa bayana kwamba Chadema kilikuwa chama cha kutetea maslahi ya wanyonge wa Tanzania, hususan kwa kupambana na kila aina ya ufisadi, ilhali chama tawala CCM kikionekana kama kichaka cha kuhifadhi mafisadi, huku kikiandamwa na skandali moja baada ya nyingine.
Kwa hakika, tukiangalia jinsi Tanzania yetu ilivyotafunwa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, ni maajabu makubwa kushuhudia Mahakama Maalumu ya Ufisadi ikiwa haina kesi huku waziri husika, Dk. Harrison Mwakyembe akituhadaa kuwa kukosekana kwa kesi ni ishara ya mafanikio ya mahakama hiyo. Nchi yetu haiishiwi vituko.
Laiti dhamira nzuri ya Rais Dk. John Magufuli kuanzisha mahakama hiyo ya ufisadi ingeambatana na utashi wa kisiasa ili kuifanya iwe na ufanisi, basi kazi kubwa iliyofanywa na Chadema huko nyuma ingekuwa imeirahisishia kazi mahakama hiyo.
Sogeza mbele (fast-forward) hadi mwaka 2015 na kuendelea (hadi muda huu ninapoandika makala hii), Chadema ile iliyowanyima usingizi mafisadi na kuwapa matumaini walalahoi imegeuka kuwa kama taasisi inayoendeshwa na matukio. Kimsingi, sidhani kama hata uongozi wa juu – achilia mbali wananchama na wafuasi wa kawaida wa chama hicho – wanaofahamu chama hicho kinasimamia nini kwa sasa.
Kwa tunaofahamu ‘yanayoendelea nyuma ya pazia’ ya siasa za Tanzania, Chadema ilihujumiwa vya kutosha, huku miongoni mwa waliokihujumu chama hicho wakiwa watu muhimu walioshiri kukifikisha chama hicho katika umaarufu wa kisiasa. Tamaa ya madaraka kwa baadhi ya viongozi muhimu wa chama hicho ilitoa fursa mwafaka kwa hujuma hizo kufanikiwa.
Lakini kosa kubwa kabisa walilofanya Chadema, na ambalo linaweza kuwa na madhara makubwa zaidi yenye utata unaoendelea hivi sasa ni kumpokea aliyekuwa kada maarufu wa CCM, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, sio tu kujiunga na chama hicho bali pia kuwa mgombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Uamuzi wa Chadema kumpokea Lowassa na kumfanya mgombea wa urais ulikuwa ni kioja cha kihistoria, hasa ikizingatiwa kwamba Chadema hiyo hiyo ilitumia takriban miaka tisa mfululizo kumtambulisha Lowassa kama kinara wa ufisadi nchini Tanzania. Sasa kwa busara japo ‘kiduchu’ tu, huwezi kumchafua mtu kwa miaka tisa mfululizo kisha ukajaribu kumsafisha kwa miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.
Ninakumbuka wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka juzi, kada mmoja wa ngazi za juu wa CCM alinieleza kuwa “kwa kumpokea Lowassa, Chadema wameturahisishia safari yetu ya Ikulu,” akibainisha kuwa ajenda ya ufisadi ingeweza kuiangusha CCM katika uchaguzi huo. Hata hivyo, kwa Chadema kumkumbatia ‘mwanasiasa waliyemwita fisadi miaka nenda miaka rudi,’ chama hicho kilijinyima uhalali wa kushikilia hoja ya ufisadi dhidi ya CCM.
Kibaya zaidi, Chadema haijaona umuhimu wa kufanya sio tu tathmini ya kina ya ‘athari za ujio wa Lowassa,’ bali pia jitihada za kuwarejesha wafuasi wa chama hicho ‘walioondoka na Dk. Slaa (yaani waliokerwa na ujio wa Lowassa na kuamua kujiweka kando)
Nimalizie makala hii kwa kuikumbusha Chadema kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa chama hicho kujitathmini upya, na kifanye jitihada za kurudi zama zile za ‘List of Shame,’ EPA, Richmond, nk – yaani kuwa sauti ya wasio na sauti na wapigania haki za wanyonge. Ukimya wa Lowassa katika kipindi muhimu kama hiki cha vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya huku Mwenyekiti Freeman Mbowe akitajwa kuwa mtuhumiwa wa biashara hiyo ni ishara mbaya kwa chama hicho kilichowahi kuwa mbadala wa CCM.

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube