16 Feb 2017


KATIKA nchi nyingi za huku Magharibi, kila mwanzoni mwa mwaka Idara zao za Usalama wa Taifa huchapisha ripoti inayoelezea kwa kina maeneo yanayoonekana kuwa yanaweza kuwa tishio kwa usalama wa mataifa husika.
Kwa ‘akina siye’ kwa maana ya nchi nyingi za Afrika na Dunia ya Tatu kwa ujumla, kila chapisho la Idara ya Usalama wa Taifa ni siri kuu isiyopaswa kuonekana kwa mwananchi wa kawaida.
Na ni katika mazingira haya ya kufanya ‘kila taarifa ni siri’ hata zile ambazo zingepaswa zifahamike kwa wananchi, ndio tunashuhudia uhusiano kati ya Idara zetu za Usalama wa Taifa na wananchi wa kawaida sio mzuri, uliojaa shaka na kutoaminiana, kwa kiasi kikubwa wananchi kuziona taasisi hizo kama zipo dhidi yao.
Na hiyo ndio moja ya sababu kuu zilizonifanya, mwaka jana, kuchukua uamuzi wa kuandika kitabu kuhusu taaluma ya uafisa usalama wa taifa, si kwa Tanzania pekee, bali duniani kwa ujumla. Na kama nilivyotarajia, wasomaji wengi wamenipa mrejesho kuwa kitabu hicho kimewasaidia mno kutambua kuwa Idara za Usalama wa Taifa ni ‘rafiki mwema’ kwao na ni taasisi muhimu mno kama moyo au ubongo kwa nchi husika.
Kadhalika, wasomaji wengi wamekiri kuwa kabla ya kusoma kitabu hicho walidhani kuwa kazi kuu za watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa ni kutesa watu, u-mumiani (kunyonya damu) na vitu vingine vya kuogofya, na kwamba hakuna lolote jema kwa masilahi ya wananchi.
Sitaki kujipongeza lakini ninaamini kuwa kitabu hicho kimesaidia sana, pamoja na mambo mengine, kujenga taswira nzuri kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa, hasa ikizingatiwa kuwa kutokana na wananchi wengi kutofahamu umuhimu wa taasisi za aina hiyo, imekuwa ikibebeshwa lawama nyingi isizostahili.
Lakini lengo la makala hii sio kuongelea kitabu hicho au shughuli za Idara za Usalama wa Taifa, bali kuzungumzia maeneo ambayo kwa utafiti, uchambuzi na mtazamo wangu yanaweza kuwa tishio kwa usalama wa taifa letu.
Eneo la hatari zaidi ni kuminywa kwa kile kinachoitwa kwa kimombo ‘political space,’ yaani mazingira ambayo shughuli za kisiasa hufanyika pasi kuingiliwa na dola. Bila hata haja ya kuingia kiundani kwenye hili, ukweli ni kwamba kuminya ‘political space’ sio tu kunajenga chuki ya wananchi kwa dola bali pia kunazuia fursa ya wananchi kujadiliana kuhusu manung’uniko yao, ambayo sote tunafahamu kuwa ‘yakijaa sana bila kuwepo upenyo wa kuyapunguza, yatapasuka pasipotarajiwa.’
Suala jingine ni hisia za ukabila/ukanda. Kuna kanuni moja inasema ‘ni silika ya mashushushu kuongea na kila mtu.’ Naam, kwa kuongea na kila mtu, inakuwa rahisi kusikia ‘mazuri’ na ‘mabaya,’ na pia mitazamo ya watu mbalimbali hata ile tusioafikiana nayo.
Na katika kuongea na watu mbalimbali, nimebaini manung’uniko ya chini chini kuhusu ukabila na ukanda, huku baadhi ya watu wakienda mbali na kutamka bayana kuwa wanaona kama eneo fulani analotoka kiongozi fulani linapendelewa zaidi.
Sambamba na ukabila ni udini. Hili ni tatizo kubwa pengine zaidi ya kuminywa ‘political space’ na hilo la ukanda/ukabila, kwa sababu tatizo hili limekuwepo kwa muda mrefu huku kila awamu ya serikali iliyopita ikipiga danadana kwenye kusaka ufumbuzi wa muda au wa kudumu.
Wakati angalau kuna jitihada za makusudi za kupunguza pengo kati ya walio nacho na wasio nacho, umasikini bado ni tatizo kubwa, ni muhimu kwa serikali kuwa ‘honest’ kwa wananchi kwa kuepuka kutilia mkwazo takwimu za kupendeza (na lugha ya kitaalamu) zinazokinzana na hali halisi mtaani. Rais Dk. John Magufuli awaagize watendaji wake wawe wakweli kwa wananchi, wawafahamishe taifa linapitia hatua gani muda huu, na matarajio ni yapi, na waongee lugha inayoeleweka kirahisi.
Sambamba na umasikini ni janga la ukosefu wa ajira. Japo kilimo kinaweza kutoa fursa kwa vijana wengi wasio na ajira, bado hakuna dhamira ya dhati ya kisiasa ya kukifanya kilimo kiwe kweli uti wa mgongo wa taifa letu.
Wakati jitihada za serikali kupambana na ufisadi na uhalifu zinaleta matumaini, kasi ya kushughulikia watuhumiwa ni ndogo huku mahakama ya mafisadi ikiwa kama kichekesho fulani kwa kukosa kesi, japo waziri husika anajaribu kutueleza kwamba kukosekana kesi ni mafanikio kwa mahakama hiyo. Ikumbukwe kuwa wahusika wa ufisadi, biashara ya dawa za kulevya, ujangili na uhalifu kama huo ni watu wenye uwezo mkubwa, na wanaoweza kuunganisha nguvu za ndani na nje ya nchi ili kuliyumbisha taifa. Kibaya zaidi ni kwamba baadhi ya majina maarufu ya wahalifu, kwa mfano ‘wauza unga,’ yanahusisha familia maarufu kisiasa, na hiyo inakuwa kama kinga kwao. Sheria haipaswi kubagua kati ya ‘huyu mtoto wa fulani’ na yule ni mtu wa kawaida.
Kimataifa, kama kuna kitu kinanipa wasiwasi sana ni kinachoonekana kama uhusiano wetu mzuri na nchi moja jirani, uhusiano ambao ulichora picha ya kudorora katika miaka ya hivi karibuni. Kiintelijensia, hao sio marafiki zetu hasa kwa kuzingatia historia na siasa za ndani za nchi hiyo. Naamini wahusika wanatambua changamoto kutoka kwa majirani zetu hao. Mbali na nchi hiyo jirani, hali ya shaka huko Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni tishio kwa usalama wa nchi yetu pia. La muhimu zaidi ni kuimarisha usalama wa mipaka yetu ili kudhibiti uhamiaji haramu kutoka nchi hizo.
Binafsi, ninauona ushirikiano wa Afrika Mashariki kama urafiki wa shaka. Tatizo kubwa linaloukabili ushirikiano huo ni kuendekeza zaidi siasa na kupuuzia kabisa ukweli kuwa nchi zinazounda ushirikiano huo zinajumuisha watu wa kawaida, na sio wanasiasa pekee. Ili ushirikiano huo uwe na manufaa ni lazima uwe na umuhimu kwa watu wa kawaida katika nchi husika.
Mwisho ni tishio la ugaidi wa kimataifa. Japokuwa hakuna dalili za kutokea matatizo hivi karibuni, masuala kadhaa niliyokwishayagusia yanaweza kutoa fursa kwa tishio hilo. Kwanza, kuminya ‘political space,’ udini, umasikini na ukosefu wa ajira. Utatuzi wa matatizo haya utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tishio la ugaidi wa kimataifa.
Angalizo: Huu sio utabiri, kuwa hiki na kile kitatokea. Hii ni tathmini ya jumla ya maeneo yanayoweza kuhatarisha usalama wa taifa letu. Tathmini hii imetokana na ufuatiliaji wangu wa masuala mbalimbali, hasa ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiusalama kuhusu Tanzania yetu.

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.