13 Apr 2017


WANASEMA “wiki nzima katika siasa ni sawa na uhai mzima wa mwanadamu.” Maana ya msemo huo ni kwamba katika siasa, tunaweza kushuhudia matukio mengi katika muda mfupi tu. Kwa lugha nyingine, katika siasa, hata wiki tu ni ndefu kama uhai mzima.
Sasa kama “wiki tu ni uhai mzima” je hali ikoje kwa mwaka mzima? Pengine jawabu lipo kwenye kuiangalia Tanzania yetu, katika kipindi cha takriban mwaka na nusu sasa, kutoka zama za “tumbua majipu” na “hapa kazi tu” hadi muda huu ambapo kila kukicha ni “Bashite hili, Bashite lile,” “Bashite hiki, Bashite kile,” na mengineyo mengi.
Ni vigumu kuandika makala hii ili ifikishe ujumbe unaokusudiwa, kwa sababu takriban kila anayejihusisha na uandishi amekwishapewa angalizo kuhusu nini anatarajiwa kuandika kuihusu Tanzania yetu: habari nzuri tu.
Kwa hiyo inabidi ujuzi wa ziada utumike kuandika habari mbaya lakini ionekane kama nzuri, kwa mujibu wa matakwa ya watawala wetu.
Muda huu ninaandika kitabu kinachofanya tathmini ya “Tanzania: tulikotoka, tulipo, na tuendako” (ndio jina la kitabu husika). Na humo ninajaribu – kwa uhuru mkubwa – kujiuliza kwa mifano hai, nini hasa kimeikumba nchi yetu hadi kufikia hali hii tuliyonayo sasa?
Majuzi nilikuwa nazungumza na mtu mmoja, mzalendo anayefanya kazi kwenye taasisi moja nyeti. Ni maongezi na watu kama hawa yanayonifanya kufahamu yanayojiri nyuma ya pazia. Akanieleza kitu ambacho tangu nilipokisia kimekuwa kikinisumbua sana.
Kwa mujibu wa mzalendo huyo, kuna kikundi hatari ambacho kazi yake kuu ni aidha kunyamazisha watu kwa nguvu au kuepesha mijadala muhimu kitaifa. Kwamba kikundi hicho ambacho ni vigumu kukielezea kwa undani bila kuliingiza gazeti hili matatizoni kinahusika na “utata” wote unaoendelea huko nyumbani muda huu.
Niwatoe pembeni kidogo na kugusia kitu ambacho Rais Donald Trump amekuwa akikiongelea mara kwa mara katika siku za hivi karibuni. Kinaitwa ‘Deep state.’ Jina jingine ni ‘a state within a state’ (dola ndani ya dola).
Deep state anayoilalamikia Trump inaweza kuwa tofauti na inayowezekana kuwepo huko nyumbani. Trump anadai kuwa kuna ushirikiano kati ya taasisi za kiintelijensia za nchi hiyo na baadhi ya watendaji wa serikali, vyombo vya habari, wafanyabiashara na makundi mengine katika jamii, kwa pamoja wakiazimia kumkwamisha Rais huyo mpya wa Marekani.
Tatizo la Trump ni kwamba amekwishaongea upuuzi mwingi mno kiasi kwamba ni vigumu kuchukulia matamshi yake kwa umakini. Na pengine anachokiita ‘deep state’ hakina lengo la kumdhuru kwa kumwonea bali kushughulikia ukweli kwamba tajiri huyo alifanikiwa kushinda urais katika mazingira ya kutatanisha.
Katika Tanzania yetu tumekwishawahi kuwa na mazingira karibu na hiyo ‘deep state.’ Katika siku hizo (mazingira hayaruhusu kubainisha kwa undani kuhusu waliohusika), tulishuhudia watu wakitekwa na kuteswa katika mazingira ya kutatanisha. Nadhani sote tunakumbuka yaliyowasibu Dk. Emmanuel Ulimboka na waandishi wa habari Absalom Kibanda na Saed Kubenea.
Sasa ‘deep state’ imerejea tena, angalau kwa mujibu wa huyo mzalendo ambaye sina sababu ya kutomwamini. Na taarifa zinadai kuwa kuna angalau watu 10 wanaotakiwa “kushughulikiwa.” Baadhi ni wanasiasa wa upinzani na wa chama tawala, na wengine ni watu wenye ushawishi au nafasi muhimu au umaarufu kwenye jamii.
Kwa bahati mbaya, hadi wakati ninaandika makala hii, msanii “Roma Mkatoliki” ambaye pamoja na wenzake walikuwa “wametekwa” kabla ya kupatikana katika mazingira ya kushangaza, alikuwa hajaeleza kuhusu nini hasa kiliwasibu. Hata hivyo, maelezo ya awali yaliyokwishapatikana yanazua utata kuhusu suala hilo.
Msanii anapotekwa, kisha kundi la wasanii wenzake linakwenda kwa kiongozi fulani kuomba awasaidie kumpata mwenzao, na kiongozi huyo anasema kabla ya muda fulani msanii aliyepotea atapatikana, na kweli anapatikana kabla ya ‘deadline’ iliyotajwa na kiongozi huyo, ni wazi “kuna namna” hapo.
Nihitimishe makala hii kwa kutoa ushauri mrefu kwa ndugu zangu wa moja ya idara nyeti nchini Tanzania. Ninyi ndio tegemeo pekee kwenye mazingira kama haya. Kama mimi niliye mbali na huko nyumbani “ninasikia ninachosikia” ni wazi nanyi mtakuwa mnasikia pia. Kuna “uhuni unaofanyika huko mtaani,” na unachafua taswira ya taasisi yenu muhimu na nyeti.
Nafahamu kuwa jukumu lenu ni kushauri tu, lakini ninafahamu pia kuwa mnafahamu cha kufanya pindi ushauri wenu unapopuuzwa na pale zinapofanyika jitihada za waziwazi ku- “undermine” umuhimu wenu. Hivi kweli hizo “rogue elements” zinazohusishwa na “deep state” hazifahamiki? Msipochukua hatua mtahisiwa kuwa mmebariki hayo “yanayoendelea huko mtaani.”
Naomba isitafsiriwe kuwa ninawafundisha kazi. Laiti nisingekuwa na imani nanyi nisingepoteza muda wangu kutoa ushauri huu. Kama ilivyo kwa Watanzania wengi, nina imani kubwa nanyi. Hata hivyo, kuna haja ya haraka ya kuzuia kukua na kushamiri kwa hiyo “deep state.” Ikiachwa, itasababisha madhara makubwa.
Mungu Ibariki Tanzania

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube