5 Apr 2017


Habari iliyotawala mno jana ni taarifa kutoka Ikulu kuwa Rais John Magufuli amemteua kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo, kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji.
[​IMG]
Kwa tathmini ya haraka haraka, taarifa hiyo imepokelewa kwa mitazamo miwili: wanaounga mkono hatua hiyo na wanaoipinga. Wanaoiunga mkono wanaona hatua hiyo ya Magufuli kama mwafaka katika kujenga umoja wa kitaifa na ushirikiano bila kujali tofauti za kiitikadi.


Wanaopinga wanaona uteuzi huo umelenga kuidhoofisha ACT-Wazalendo, mtego ambao haijulikani una malengo gani, na unafiki wa baadhi ya wanasiasa wa upinzani - katika suala hili ni Profesa Kitila na bosi wake Zitto Kabwe ambaye tayari amepongeza uteuzi huo.Kwa sie tunaoliangalia suala hili 'kwa jicho la tatu,' tunabakiwa na  maswali mengi yasiyo na majibu. Swali mojawapo ni hili: katika hotuba yake moja huko Zanzibar, Rais Magufuli aliapa kutowashirikisha wapinzani kwenye serikali yake (msikilize mwenyewe kwenye video hii hapa chini)Je Prof Kitila alikuwa 'mpinzani feki kwenye chama feki cha upinzani?'

Na ukiangalia 'upendeleo' aliopewa Profesa Kitila katika wadhifa wake kama mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, kisha ukalinganisha na sababu zilizoplekea Profesa Mwesiga Baregu asiongezewe mkataba chuoni hapo, utahisi ipo namna. Hadi wakati Profesa Kitila anapewa 'ulaji' na Magufuli, ushiriki wake kwenye siasa haukuwa tatizo kwa serikali, hiyohiyo 'iliyomkalia kooni' Profesa mzoefu Barefu. 

Lakini pengine unafiki mkubwa wa Profesa Kitila ni ukweli kwamba alishaweka msimamo wake huko nyuma, alipokemea teuzi zinazofanywa na Rais Magufuli kuwachukua wahadhiri pasipo kuandaa wa kurithi nafasi zao. 


Kwahiyo, sidhani kama kuna neno stahili kuhusu Profesa Kitila zaidi ya unafiki. Ndio, alikuwa mtumishi wa serikali, lakini pia alikuwa kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo. Na hili la unafiki linahusu kotekote, kwenye kazi yake kama mhadhiri - aliyekwishakemea tabia ya serikali kupora wasomi kwenye taasisi za elimu - na kama mwanasiasa ambaye baadhi yetu tulikuwa tukimwona kama tegemeo japo kiduchu kwenye siasa za upinzani. Leo hii, Profesa Kitila ameibuliwa kutoka UDSM na ACT-Wazalendo katika namla ileile BASHITE alivyoibuliwa kwenye u-DC na kupewa u-RC.

Kuhusu Zitto, mie kitambo nimekuwa nikimwona kama mwanasiasa mnafiki. Nani asiyekumbuka ahadi yake ya kutaja majina ya mafisadi walioficha pesa za umma huko Uswisi? Na ni Zitto huyu huyu aliyewahi kurushiwa tuhuma za kuisaliti Chadema baada ya gazeti moja kudaka kile ilichodai kuwa mawasiliano kati ya mwanasiasa huyo na kiongozi mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa. Unaweza kuisoma stori husika HAPA.

Hivi majuzi tu, kulikuwa na tetesi kuwa "Zitto amepotea"

Baadaye "akapatikana" na "akamwashia moto" Rais Magufuli akidai kuwa atakuwa rais wa muhula mmoja tu. Mwanasiasa huyo machachari alilaani kile alichoita "tabia za kidikteta za Magufuli," na kwamba "Watanzania hawatamvumilia (Magufuli) kuwatawala kwa kuwaburuza kidikteta."

Muda si muda, kukajiri 'drama nyingine' kuhusu Zitto, ambaye inaelezwa kuwa alilazimika kujificha ndani ya jengo la Bunge ili asikamatwe na polisi.

Leo Magufuli kamteua Profesa Kitila kuwa katibu mkuu, katika moja ya miujiza ya kisiasa nchini Tanzania, na tayari Zitto 'amebadilika.' Hebu msikie hapa chini


Uzuri mmoja wa unafiki huu ni kwamba Magufuli kawarushia kitanzi Profesa Kitila na Zitto, wajifunge wenyewe au wakikwepe. Kwa sababu wanazozijua wenyewe wamejifunga wenyewe. Nasema hivyo kwa sababu kwa sasa haitowezekana kwa Profesa Kitila kuikosoa serikali kutokana na wadhifa wake huo mpya.

Kadhalika, Zitto na ACT- Wazalendo yake watakuwa na wakati mgumu kuikosoa serikali ambayo "nao wamo" kupitia uwepo wa Prof Kitila. 

Lakini pengine ni vema kukumbuka historia ya wawili hawa katika siasa za upinzani Tanzania. Mie ni mmoja wa watu wanaoamini kwa dhati kuwa laiti wawili hao - Zitto na Kitila - wasingefanya chokochoko ambazo baadaye zilipelekea kufukuzwa kao huko Chadema, basi huenda leo hii Chadema ingekuwa chama tawala. 

Nimaliie makala hii kwa kutahadharisha kuwa si ajabu katika siku chache zijazo mtamskia tena Zitto huyuhuyu anayemwagia sifa Magufuli akielezea kuhusu ishu moja nzito. Baadhi yetu twafahamu kuhusu mkakati fulani dhalimu unaomhusisha Bashite dhidi ya watu flani. Ninatarajia Zitto ataufahamu hivi karibuni. Tuliache hilo, muda utaongea.

Nawatakia siku njema

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.