15 Apr 2017



Nianze makala hii kwa kutoa salamu za rambirambi kwa familia za askari wanane wa Jeshi letu la Polisi waliouawa kinyama wilayani Kibiti, Mkoani Pwani. 

Huu ni msiba wa kitaifa, japo hakuna maombolezo ya kitaifa - sijui kwa vile hatuthamini uhai wa Watanzania wenzetu au tushazowea sana vifo kama vile vya ajali, nk.

Jambo moja lililonikera mno jana ni ukimya wa wahusika, na mpaka wakati ninaandika makala hii sijasikia kauli yoyote kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi. Labda kuna watakaosema "aanasubiri taarifa kamili." Hapana. Uongozi hauko hivyo. Sie huku Ulaya sasa ni kama "tumeshaanza kuzowea"  matukio ya kigaidi, maana yanatuandama mno, hasa Ufaransa, Ubelgiji na Ujerumani, na majuzi hapa Uingereza.

Katika kila tukio, bila kujali idadi ya waathirika, takriban ndani ya saa moja tangu kutokea tukio husika, Rais au Waziri Mkuu wa nchi husika huongea na wananchi katika runinga mubashara, kutoa pole kwa waathirika, kuwahakikishia usalama wananchi, na kuwaonya wahusika kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao. Huu ndio uongozi.

Je sie hali ikoje? Sana sana ni taarifa ya salamu za rambirambi kutoka kwa Rais, kama inavyoonekana hapa chini



Hadi wakati salamu hizo za rambirambi zinatolewa, hakukuwa na tamko lolote kutoka kwa uongozi wa jeshi la polisi. Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alithibitisha kutokea kwa tukio hilolakina akadai "hana taarifa" kuhusu tukio hilo hadi atakapowasiliana na IGP. 


Baadaye, Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani, aliongea na waandishi wa habari, ambapo pamoja na mambo mengine alinukuliwa akisema kuwa jeshi hilo "halitokuwa na mzaha wala msamaha" katika operesheni maalum kuhusiana na tukio hilo


Je, kulikuwa na mzaha na msamaha kabla ya tukio hilo, ambao sasa hautokuwepo wakati wa operesheni husika?

Tukiweka kando kasoro hizo, jambo moja lililonigusa mno ni ukweli kwamba matukio makubwa mawili ya hivi karibuni - uvamizi uliofanywa na RC Makonda kwenye kituo cha Clouds na "kutekwa" kwa msanii wa bongofleva, Roma Mkatoliki - yalipewa uzito mkubwa na Watanzania kuliko mauaji hayo ya polisi hao wanane.

Inasikitisha lakini haishangazi. Sababu moja kuu ya "wananchi wengi kutoonekana kuguswa na mauaji hayo ya polisi wanane" ni ukweli kwamba mahusiano katika ya Jeshi la Polisi na wananchi wengi sio mazuri. Polisi wetu wamekuwa wakisifika kwa unyanyasaji dhidi ya raia wasio na hatia. 

Na kama kuna kitengo cha Polisi wetu "kinachochukiwa mno" ni hicho cha FFU (Kikosi cha Kuzuwia Ghasia) ambacho askari hao wanane walikuwamo.

Japo siungo "chuki" hiyo, lakini naelewa jinsi gani Watanzania wengi wasivyopendezwa na utendaji kazi wa jeshi la polisi. 

Kwa upande mwingine, Jeshi hilo limekuwa likionekana kama "adui wa kudumu" dhidi ya vyama vya upinzani, huku likifanya upendeleo wa wazi kwa chama tawala CCM.

Kwahiyo, wakati tunaomboleza vifo hivyo vya polisi hao wanane, ni muhimu mno kwa wahusika kuchukua hatua za makusudi kuondoa "uhusiano wa chuki na mashaka" uliopo kati ya jeshi la polisi na asilimia kubwa ya Watanzania.

Kana kwamba uhusiano bora kati ya jeshi la polisi na wananchi sio muhimu "kihivyo," moja ya nyenzo muhimu ya kujenga na kuimarisha ushirikiano huo, mpango wa 'Polisi Jamii,' ulifutwa kwa sababu wanazozijua wahusika. Polisi jamii ilikuwa kiungo muhimu kati ya polisi wetu na jamii.

Kioperesheni, japo tukio hilo la mauaji ya polisi wanane linaelezwa kuwa ni la kijambazi, binafsi ninahisi kuwa kuna tatizo zaidi ya ujambazi. Na kwa tafsiri ninayoelewa kuhusu ugaidi, basi tukio hilo linastahili kabisa kuitwa la kigaidi. Ni majambazi gani wenye ujasiri wa kuwavizia polisi na kuwaua kufuatia 'ambush' kama hiyo iliyotokea eneo la tukio?

Halafu, hilo sio tukio la kwanza. Na hao polisi wanane sio polisi wa kwanza kuuawa katika eneo hilo, sambamba na wakazi wengine. Yayumkinika kuhitimisha kuwa jeshi la polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani hawawezi kukwepa lawama, kwa kushindwa kukabili kushamiri kwa mauaji katika eneo hilo. Sijui Rais Magufuli ameishiwa na zile sindano zake za kutumbulia majipu, au kaishiwa pumzi ya #TumbuaMajipu lakini ni wazi kuna matatizo ya msingi katika uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani na jeshi la polisi kwa ujumla. Ukimya wa polisi katika uvamizi huko Clouds, na "kutekwa" kwa Roma, na sasa hili la Kibiti, vilipaswa kumfanya Rais Magufuli achukue hatua.

Moja ya sababu maarufu ya polisi wetu wanapozuwia mikutano au maandamani ya vyama vya upinzani huwa "intelijensia." Sasa kama intelijensia ipo kwenye kudhibiti shughuli halali za vyama vya siasa, kwanini intelijensia hiyo isitumike kwenye kukabiliana na "magaidi" hao wanaotikisa Mkoa wa Pwani?

Nihitimishe makala hii kwa kurejea salamu zangu za rambirambi kwa familia za askari hao waliouawa kinyama. Pamoja na mapungufu yote niliyotanabaisha katika makala hii, hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha unyama waliofanyiwa askari hao.

Lakini pia wakati tunaomboleza vifo vyao, ni vema tukatafakari kama Taifa kuhusu mahusiano kati ya jeshi la polisi (na vyombo vyote vya dola kwa ujumla) na raia, ambayo yakiwa bora, yanaweza kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na taifa kwa ujumla

1 comment:

  1. Kwenye hili mm nalaumu sana njia wanazotumia polisi ku enforce law ziko biased sana na pia hata hao walio uliwa wanne kama majambazi watakua wameonekana wanafaa tuu kuingizwa hapo ili wasionekane kushindwa ....Polisi wanaweza kukuwekea hata Bangi wakupe kesi sembuse kukuua ili watu wasielewe kitu? Inakuaje eti watu wanne Wana silaha alafu wawaue wote kwenye majibizano ya risasi akosekane hata polisi aliejeruiwa Kama si kuvamia watu wasio na hatia na kuwaua au Kama Ni kweli hawakujiandaa basi walikua wanaweza kuwakamata na kuwafikisha mahakamani ili watoe ushahidi na kutoa muongozo WA matukio yao na hata kugundua Ni Nani yuko nyuma ya hayo Ni gaidi au jambazi? Mwisho Ni kuhusu taarifa nlizozisikia zinasema jambazi hao waliwaua wenzao waliokua wakiwapeleka polisi eneo walipojificha, hii Ni uongo kwa kuzingatia taarifa za awali ambazo zilisema polisi walikua wanaenda kubadilisha LINDO na hizi za pili zinazosema polisi walikua wanaeatafuta majambazi...Hizo roho za hao wawili zitakua zimeunganishwa tuu na hao hao polisi lkn wakaona wajitetee na Hilo Kwasababu ilishatendeka ndio maana taarifa zao hazieleweki kabisa...
    Nitoe pole kwao waliokutwa na msiba ila wakumbuke kuwa sahihi ili haya yadijirudie tuna ndugu zetu wadogo alafu police eti chaa wasije wakauwawa na wao, wawatume Kazi sahihi kulingana na ethics zao na waepuke upendeleo
    R.I.P

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.