11 May 2017


NIANZE makala hii kwa salamu za pole na rambirambi kwa ndugu, jamaa, na marafiki wa wanafunzi zaidi ya 30 waliopoteza maisha kufuatia ajali ya basi dogo la abiria, huko Karatu Arusha.
Nimeandika “zaidi ya mara 30” kwa sababu wakati ninaandika makala hii, zimepatikana taarifa kuwa inawezekana idadi ya abiria kwenye basi lililopata ajali ilikuwa kubwa kuliko iliyoripotiwa. Taarifa rasmi zinatajwa idadi ya waliofariki kuwa ni wanafunzi 33, walimu wawili na dereva mmoja.
Mungu awapatie marehemu wote pumziko la milele, na mwanga wa milele awaangazie, wapumzike kwa amani. Amina. Bwana ametoa, Bwana ametwaa. Wenzetu wametutangulia tu, lakini sote tupo safari moja, kwani kila nafsi huonja mauti.
Salamu nyingi za pole kwa wafiwa, maana uchungu wa mwana aujuaye mzazi. Wanafunzi hao wamekumbwa na mauti wakati wanaelekea kwenye mitihani yao. Kwa hiyo, tunaomboleza sio kifo tu bali pia kukatishwa kwa ndoto za kielimu za wanafunzi hao. Hili ni pigo kubwa sio kwa ndugu, jamaa na marafiki tu wa wanafunzi hao, bali taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa mila na desturi zetu, si vema kuanza kulaumiana kuhusu msiba kabla hata mazishi hayajafanyika. Lakini kama kuna kasumba mbaya inayojitokeza katika kila majanga makubwa kitaifa, basi binafsi sioni haja ya kuwa na subira.
Kama kuna kitu kinanisumbua mno kila yanapojiri majanga ya kitaifa kama ajali hii ya Karatu ni ile hali kwamba “wenzetu huku nilipo wanathamini mno uhai uliopotea, pengine kuliko sisi. Hili nimekwishaliongelea mara kadhaa, na kuna mifano lukuki ya kuthibitisha hisia hizo zisizopendeza.
Nashindwa “kupata picha” hali ingekuwaje hapa Uingereza laiti kungetokea ajali kama hiyo ya Karatu. Naandika hivyo kwa sababu “ajali ndogo tu” kwa maana ya idadi ya vifo au majeruhi, hupewa uzito mkubwa mno kiasi kwamba takriban kila mkazi wa nchi hii anaguswa na janga husika.
Nabaki ninajiuliza, “je wenzetu wanathamini mno uhai kuliko sisi?” Sipati jawabu. Najiuliza tena, “labda wenzetu ni ‘wazima’ lakini sisi tumerogwa?” Siambulii jibu. Lakini kilicho wazi ni kwamba tuna upungufu mkubwa katika kuguswa kwetu na majanga makubwa kitaifa.
Mifano ya karibuni zaidi ni janga la tetemeko la ardhi lililoyakumba maeneo ya Kanda ya Ziwa, na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa na uharibifu mkubwa wa mali; mauaji dhidi ya askari polisi wanane huko Kibiti, mkoani Pwani, na sasa janga hili ambalo limeripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari duniani.
Kitu kimoja kisichopendeza katika matukio yote hayo matatu ni kwamba serikali haikuona haja ya kutangaza maombolezo ya kitaifa. Katika udadisi wangu, nimesikia utetezi usio na mashiko kuwa “ili kuwe na maombolezo ya kitaifa, na bendera ipepe nusu mlingoti basi msiba husika shurti uwe wa kiongozi wa kitaifa.” Maana yake kwamba uhai wa viongozi wetu una thamani zaidi ya uhai wa wananchi wa kawaida. Ama?
Kitu kingine ambacho sio tu hakipendezi lakini pia kinashangaza ni Rais wetu, John Magufuli kutoungana na waombolezaji wakati wa kuaga miili ya marehemu. Hakuwepo katika tukio la kuaga miili ya waliofariki kwenye ‘Tetemeko la Kagera,’ hakuwepo kwenye tukio la kuaga miili ya askari polisi wanane waliouawa huko mkoani Pwani. Na hadi wakati naandika makala hii, mgeni rasmi kwenye kuaga miili ya wanafunzi hao wa Karatu ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Kuna wanaoweza kusema “kwani rais akiwepo atarejesha uhai wa waliofariki?” Hoja hiyo ni ya kukosa ubinadamu. Ni muhimu kutambua kuwa licha ya kuwa “commander-in-chief” wa majeshi yetu ya ulinzi na usalama, Rais pia ni “comforter-in-chief.” Rais ni kama baba, mlezi, na mtu ambaye taifa zima linamuangalia katika nyakati kama hizi.
Tukiweka kando ‘sintofahamu’ hiyo, Shirika la Utangazaji la taifa TBC, limeonyesha kasoro kwa kuendelea na ratiba za vipindi vyake badala ya kuongoza vyombo vingine vya habari katika maombolezo ya vifo vilivyotokana na ajali hiyo ya Karatu.
Nitumie fursa hii kuipongeza Clouds Media Group kwa uzalendo na ubinadamu wao mkubwa uliowasukuma kubadili ratiba za vipindi vyao ili kuungana na wafiwa na Watanzania kwa ujumla kuomboleza vifo hivyo.
Mwisho, japo ajali haina kinga, uzoefu unaonyesha kuwa ajali nyingi zinazotokea huko nyumbani huchangiwa na uzembe wa madereva ikiwa ni pamoja na kukiuka kwa makusudi kanuni za usalama barabarani, sambamba na ubovu wa vyombo vya usafiri wa abiria.
Japo sina maana kuwa sababu hizo ndio zilizochangia ajali hiyo ya Karatu, lakini ni muhimu sasa kama taifa kuliangalia balaa la ajali kama janga la kitaifa. Kwa kiasi kikubwa, madereva wazembe wapo barabarani huku wengine wakiendesha magari yasiyopaswa kuwa barabarani kwa sababu moja kuu, ugonjwa sugu wa rushwa kwenye kitengo cha polisi wa usalama barabarani. Pasipo kukabili rushwa kwenye kitengo hicho, uhai wetu utazidi kuwa mashakani kwa janga la ajali.
Poleni sana wafiwa, poleni Watanzania kwa ujumla. Njia mwafaka ya kuomboleza msiba huu mkubwa ni kwa kuwakumbuka marehemu katika dua/sala zetu

1 comment:

  1. Labda hapendi kukutana uso kwa uso na wapinzani....labda...

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.