4 May 2017

MAKALA yangu wiki hii inahusu maoni yangu kuhusu hatua ya serikali ya Rais John Magufuli kufukuza watumishi wa umma takriban 10,000 kwa tuhuma za kugushi sifa zao kielimu/ujuzi.
Kwanza, nitanabaishe mapema kuwa sisi ambao tumetumia sehemu kubwa ya uhai wetu kusaka elimu – na tunaendelea kuisaka – hatua yoyote dhidi ya ‘wahalifu wa kielimu’ inastahili pongezi.
Kwa hiyo, hatua ya serikali dhidi ya watumishi wake walioghushi vyeti/ujuzi ni ya kupongezwa. Haipendezi kuona wadogo zetu wanahitimu kihalali katika ngazi mbalimbali lakini wanakosa ajira kwa vile baadhi ya nafasi za kazi zimekaliwa na watu walioghushi vyeti.
Hata hivyo, licha ya hatua hiyo inayostahili pongezi, kuna kasoro kadhaa. Kwanza, kama ilivyokuwa kwa wanafunzi kadhaa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambao sio tu walikatishwa masomo yao lakini pia waliiitwa "vilaza" kwa kosa lisilo lao la kuingizwa katika kozi ya ualimu, japo alama za ufaulu za baadhi yao zilikuwa za chini.
Lengo la serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kuwachukua wanafunzi hao lilikuwa zuri, kwa maana ya mkakati wa kukabiliana na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi, lakini pia kutoa fursa ya pili kwa wanafunzi hao baada ya matokeo yao kutowaruhusu kuendelea na masomo ya kidato cha tano
Kama ambavyo wanafunzi hao hawakujichagua wenyewe, ndivyo ilivyokuwa kwa watumishi wa umma waliofukuzwa kwa ‘kufoji vyeti.’ Hawakujiajiri wenyewe. Waliajiriwa. Tumepasua jipu kwa kuwafukuza kazi lakini hatujashughulikia kiini cha jipu hilo. Na kwa kiasi kikubwa, kiini ni wanasiasa, ambao kama mzaha vile, hawakuguswa na zoezi la uhakiki wa vyeti vyao/elimu zao.
Uzoefu wangu katika utumishi wa serikali unaonyesha kuwa kwa kiasi kikubwa, ajira serikalini zimekuwa zikitolewa sio kwa kuzingatia elimu au uzoefu bali kujuana.
Nimeandika kuhusu hilo katika kitabu changu cha #Shushushu (kinachozungumzia kuhusu taaluma ya uafisa usalama wa taifa) kuwa moja ya changamoto kubwa kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa ni mfumo mbovu wa ajira unaotoa fursa ya ajira za kujuana/kubebana. Utumishi katika taasisi kama hiyo unahitaji utiifu kwa taifa, lakini ukiajiri mtu kwa vile ni mtoto wa fulani, sio tu anakuwa na utiifu zaidi kwa huyo "fulani" kuliko taifa, bali pia kunakuwa na dharau ya "ah watanifanya nini wakati fulani aliyeniingiza kazini yupo?"
Sasa tumeanza kuwafahamu kwa majina baadhi ya watumishi hao waliofukuzwa kazi. Hata hivyo, ni mapema mno kufahamu iwapo hatua hiyo iliwahusu watumishi wote wa umma au wale tu "wasio ndugu, jamaa au marafiki wa akina fulani"?
Je, wale watoto wa vigogo pale Benki Kuu nao waliguswa na zoezi hilo? Je, ndugu, jamaa na marafiki wa watawala wetu waliojazana kwenye balozi zetu za nje nao waliguswa? "Kitengo" je?
Ila jambo moja ninalohisi linaweza kuwa "matokeo yasiyotarajiwa" (unintended consequences) ni uwezekano wa baadhi ya waliofukuzwa kazi kufungua kesi dhidi ya serikali. Kuna kasoro kadhaa za kisheria katika utekelezaji wa amri hiyo ya rais lakini hapa sio mahala pake kuyajadili.
Japo siwezi kubashiri matokeo ya kesi hiyo iwapo itafunguliwa, vitu viwili vinavyoweza kuongeza uzito wa hoja za watumishi hao ni pamoja na kauli ya Rais Magufuli kwamba "wafungwe miaka saba." Ni kazi ya mahakama kutoa hukumu, sio Rais. Na kwa Rais katamka hivyo, ni kama anaiamuru mahakama itekeleze matakwa yake badala ya kufuata sheria.
Pili, ni wazi kuwa serikali imefanya ubaguzi kwa kuendesha zoezi hili kwa kuangalia “watumishi wasio vigogo” huku ikifumbia macho viongozi mbalimbali, ambao baadhi yao wanaendelea kuandamwa na tuhuma sio za kughushi vyeti vya elimu tu bali hata majina (ni nani asiyejua kuhusu suala la “Bashite”?)
Yayumkinika kuituhumu serikali kuwa imekwepa kwa makusudi kuhakiki sio elimu tu bali hata uraia wa viongozi wa kisiasa. Tuna wanasiasa wengi tu wenye elimu au uraia tata.
Kwa hiyo japo hatua ya kuhakiki elimu ya watumishi wa umma inastahili pongezi, ubaguzi wa makusudi uliofanyika katika zoezi hilo unapaswa kulaaniwa vikali. Lengo halikuwa kumnusuru ‘Bashite’ pekee bali pia baadhi ya wabunge, Wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, na viongozi wengine wa kisiasa ambao baadhi yao sio tu wana walakini kielimu bali pia uraia wao ni tete.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube